Mkuu wa Mkoa ashitukiza shule; Aunga foleni kupokea na kula nao chakula chao

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Mstaafu, Zelote Stephen akipatiwa ugali na maharage.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Mstaafu, Zelote Stephen alijiunga kwenye foleni ya wananfunzi wa Shule ya Sekondari ya Miangalua iliyopo katika kijiji cha Miangalua kata ya Miangalua, wilaya ya Sumbawanga ili kula pamoja nao chakula cha “boarding”.

Mkuu wa Mkoa alifanya kitendo hicho baada ya kufika katika shule hiyo bila ya taarifa ili kufahamu mazingira halisi ya maisha ya wananfunzi hao wanaoishi katika shule ya bweni yenye mchanganyiko wa wasichana na wavulana kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

Kabla ya kujiunga kwenye foleni ya chakula, Mkuu wa Mkoa aliingia kwenye madarasa matatu ambayo yanaandaliwa kuwa maabara ya shule hiyo na kisha kuangalia upatikanaji wa maji katika shule hiyo ndipo Makamu Mkuu wa Shule wa Shule hiyo Josephat Mwakasitu alipomwambia kuwa maji hutoka kwa saa maalum.

Wakati Mkuu wa Mkoa akiendelea kula ugali na maharage, wanafunzi wengi walimshangaa, ndipo alipowauliza maswali mbalimbali yaliyohusiana na lishe inayopatikana katika shule hiyo.
“Wanafunzi huwa mnakula mboga za majani?... Nyama?... Wali?...” 
Mkuu wa Mkoa aliuliza, na maswali yote hayo majibu yake yalikuwa, “Hapana.”

Baada ya kumaliza kula Mkuu wa Mkoa aliyatembelea mabweni ya wasichana na wavulana na kisha kukagua ubora wa vyoo vinavyotumika na wananfunzi hao kisha alihitaji kuonana na wanafunzi pamoja na waalimu na kuweza kuwapa nasaha juu ya namna ya kuboresha chakula pamoja na mazingira ya hapo shuleni.

Pamoja na hayo Mkuu wa Mkoa hakusita kusisitiza juu ya ulinzi wa mabweni kutokana na matukio ya moto yaliyokithiri na kuwasihi wanafunzi na waalimu kuwa waangalifu na matumizi ya mishumaa, taa za fanusi (chemli), vibatari, viberiti pamoja na wanafunzi wa kiume wenye tabia za kuvuta sigara.
“Katika Shule ya Nkomolo huko Nkasi kulitokea moto katika mabweni na baada ya kufika pale usiku niliwauliza wale wanafunzi kama walikuiwa wanatumia vibatari au mishumaa, wakanikatalia katakata, lakini baada ya polisi kufanya msako katika yale mabweni walikuja kugundua taa nne za chemli, ndipo walipotajana.” Mkuu wa Mkoa alielezea tukio hilo.
Katika kuwachangamsha wanafunzi, Mkuu wa Mkoa aliuliza maswali kwa wanafunzi na kutoa zawadi kwa kila aliyejibu swali vizuri, kitendo ambacho kiliwaacha wanafunzi wakiwa na furaha.