Msigwa (Mb) alikabidhi jimbo la Iringa Mjini madawati 537

MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akikabidhi madawati 537 ambayo ameyatoa kwa ajili ya Jimbo la Iringa Mjini.
NA FREDY MGUNDA, IRINGA

MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amekabidhi madawati 537 katika jimbo lake ili kuwasaidia wanafunzi waliokuwa wanakabiliwa na chanagamoto ya kusoma katika mlundikano mkubwa huku baadhi yao wakiketi sakafuni.

Aidha Msigwa katika hotuba yake amewataka viongozi wa manispaa hiyo kuachana na tabia ya kuhujumu na kuiharibu miundombinu ya shule na badala yake wahakikishe wanatunza mali zote za serikali kwa lengo la kuwasaidia watoto wengine wa vizazi vijavyo waweze kusoma katika mazingira mazuri.
“Sipendi kuona wanafunzi wanaosoma katika shule za jimbo langu wanakaa chini. Kitendo hicho huwa kinaniumiza sana, ndiyo maana nimeamua kupambana kutafuta madawati ili kufanikisha azima yangu ya kukuza elimu kwa wanafunzi wa jimbo la Iringa Mjini,” alisema Msigwa
Naye Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe alisema kwa sasa hawana upungufu wa madawati hivyo hakutakuwa na changamoto ya mwanafunzi wake kujisomea wakiwa wamekaa sakafuni.

Madawati hayo 537 yamegharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 60 na yatasambazwa katika Kata zote.

Baadhi ya wanafunzi wa shule za Halmashauri hiyo wamesema kuwa tatizo la kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika baadhi ya shule za Msingi na Sekondari katika Halmashauri hiyo lilikuwa linasababishwa na wanafunzi wengine kujisomea wakiwa wameketi sakafuni pamoja na miundombinu isiyo rafiki kwao hivyo kujikuta wanashindwa kutimiza malengo yao.

Wanafunzi hao akiwemo Ayoub Joseph, Paul Kisige pamoja na Riziki Ismail walisema kwamba kitendo cha baadhi yao kujisomea wakiwa sakafuni kimesababisha kupunguza uwezo wa kufikiri, hivyo wamempongeza Mbunge Mch. Peter Msigwa kwa juhudi anazozifanya.
“Hapo mwanzoni kwa kweli hali ilikuwa ni ngumu sana kwa sababu wanafunzi wengine walikuwa wanasoma wakiwa wanakaa chini na hii kiukweli inamwondolea kabisa uwezo wa kufanya vizuri mwanafunzi, lakini kutokana na agizo hili la Rais tumepata nafuu kubwa, na wanafunzi tuna imani tutaweza kufanya vizuri katika masomo yetu… na pia tunampongeza Mbunge wetu kwa juhudi zake za kutuletea madawati,” walisema wanafunzi hao.
Pia waliitaka serikali kutilia mkazo suala la nyumba za walimu na kuimarisha mambo ya msingi, kama kuongeza madarasa ili kuepuka mlundikano kwa wanafunzi.MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akikabidhi madawati 537 akiwa na Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe

Mch. Msigwa akikabidhi madawati 537 akiwa na Kimbe
haya ni baadhi ya madawati 537 aliyokabidhi Msingwa