Mwasisi wa TRA ‘ajilipua’ namna vigogo walivyovuruga na ufisadi wa viongozi waandamizi serikalini

Mmoja wa waasisi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mushengezi Nyambele,  hatimaye amejitokeza kueleza namna vigogo walivyoshiriki kuvuruga Mamlaka hiyo na vitendo vya ufisadi vilivyofanywa na baadhi ya viongozi waandamizi serikalini.

Nyambele ni Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi na Mshauri wa Sheria wa TRA wa kwanza.

Anaeleza matukio kadhaa yaliyofanywa na wakubwa serikalini, yakiwamo ya ukwepaji kodi, uptevu wa kontena zima lenye dawa za kulevya; na TRA ilivyoingiliwa na ukabila na upendeleo.

Juni 20, mwaka huu, TRA ilitimiza miaka 20 tangu ilipozinduliwa na Rais Benjamin Mkapa.

Nyambele ameliambia JAMHURI: “Ni lazima nikiri kwamba hata kufifia kwa maadili ya watumishi wa umma katika Serikali nzima hakukutokana na kukosa ‘code of conduct’.
“Viongozi wa juu, hasa wale wa kisiasa walikuwa chanzo kikuu cha uozo katika utumishi wa umma. Nitatoa mifano michache ya mambo niliyoyashuhudia mimi binafsi.”
Anarejea nyuma kidogo mwaka 1992 kabla ya kuanzishwa kwa TRA na kusema, mwaka huo akiwa Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya katika Idara ya Forodha walikamata kontena la futi 20 lililojaa dawa za kulevya.

Kwa sasa anasita kumtaja mtu au watu walioingiza dawa hizo na baadaye kuziiba kwa kukata kontena, lakini anasema ni watu wakubwa serikalini.
“Enzi hizo kazi hiyo ilikuwa jukumu la Idara ya Forodha ingawa tulishirikiana na Jeshi la Polisi katika operesheni kubwa.
“Baada ya kukamatwa katika Bandari ya Dar es Salaam, kontena hilo lilihifadhiwa kwenye bohari la Mamlaka ya Tumbaku Kurasini. Bohari lilifungwa na funguo kuwekwa katika mikono salama huku askari wa FFU wakililinda.
“Siku kontena lilipofunguliwa kwa ajili ya Jaji aliyekuwa anasikiliza kesi dhidi ya watuhumiwa wa kuliingiza nchini ili kuona vielelezo, iligundulika kwamba kontena lilikuwa limekatwa sehemu ya juu na dawa kuondolewa!
“Baada ya dawa kutolewa, sehemu iliyokatwa bati lake lilichomelewa upya. Hadi leo hakuna mtu yeyote aliyewahi kukamatwa kwa uhalifu huo uliofanyika ‘chini ya ulinzi wa FFU’”.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) wa wakati huo alikuwa Harun Mahundi; na Mkuu wa Upepekezi katika Jeshi hilo alikuwa Arthur Mwaitenda.

Anasema wakati wakipeleleza jinsi kontena hilo lilivyoingia nchini, walipata taarifa za kuaminika kuwa kontena la pili lilikuwa limeteremshwa kwenye Bandari ya Zanzibar.
“Niliamua kwenda mwenyewe kufuatilia taarifa hizo. Baada ya kufanya kazi hiyo kwa siku kadhaa huku nikichunguza pia juu ya upatikanaji na matumizi ya dawa za kulevya Kisiwani humo, ilitolewa amri ‘kutoka juu’ kwamba niondoke Zanzibar katika muda wa saa tatu na nisirudi wakati wowote ‘bila kuomba na kupata kibali kutoka juu’”.
Nyambele anasema aliyemjulisha uamuzi huo wa Serikali alikuwa ni Waziri wa Fedha wa wakati huo. Ingawa hamtaji kwa jina, Waziri wa Fedha kipindi hicho alikuwa Profesa Kighoma Malima.
“Ilikuja kufahamika kuwa ni vinara wa uingizaji wa dawa za kulevya ndio walijenga hoja iliyosababisha nifukuzwe mithili ya prohibited immigrant!,” anasema.
Katika tukio jingine, Nyambele anasema: 
“Mwaka 1993 nikiwa Kaimu Kamishna wa Upelelezi na Uzuiaji wa Magendo katika Idara hiyo hiyo niliamua kukagua viwanda vya wafanyabiashara waliokuwa wanaingiza walichoita mafuta ghafi ya kula ili kuhakiki iwapo walikuwa na mitambo ya kusindika mafuta hayo.
“Nilitaka kufanya hivyo ili kulinda mapato ya Serikali kwa vile kwa muda mrefu mafuta ghafi yalikuwa hayatozwi ushuru wa forodha wala kodi ya mauzo. Tuliamini kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wanaingiza mafuta yaliyokuwa yamesindikwa, lakini ili kukwepa kulipa kodi waliamua kuyaingiza kama mafuta ghafi.
“Siku tulipokwenda kukagua kiwanda cha kwanza, tulicheleweshwa mlangoni wakati walinzi wakiwasiliana na wenye kiwanda.
“Baada ya muda kupita huku tukisubiri, tuliitwa sehemu ya mapokezi ambako niliombwa kuzungumza na mtu aliyekuwa anasubiri kwenye ‘line’. Huyo hakuwa mwingine, bali Kamishna wangu ambaye aliniamuru kusitisha zoezi hilo (kazi hiyo) baada ya kupokea maelekezo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu.”
Waziri Mkuu wa kipindi hicho alikuwa John Malecela.

Nyambele anakumbuka tukio jingine katika mwaka huo wa 1993 kwa kusema aliamuriwa na kiongozi mwandamizi katika Wizara ya Fedha kuacha kufuatilia ulipwaji wa kodi kwenye kiasi kikubwa cha bia aina ya Stella Artois iliyokuwa imeingia nchini.
“Waziri wa Fedha akaamua kwamba waingizaji wangelipa kodi husika kwa awamu (installments); uamuzi ambao ulikuwa kinyume cha sheria.
Kila mzigo mpya ulipofika nchini, kilitoka kibali kipya chenye masharti yale yale hata kama hakuna kodi iliyokwishakulipwa kwa mzigo uliotangulia. 
“Nilipomwambia kiongozi huyo kuwa kufuatilia ulipwaji wa kodi hizo lilikuwa ni jukumu langu, alinitajia jina la mke wa kiongozi serikalini kuwa ndiye alikuwa anahusika na uingizwaji wa bidhaa hiyo. Nilipodadisi zaidi sababu za kunitaka nisitekeleze wajibu wangu, nilifukuzwa ofisini kwake na baada ya muda mfupi nilijikuta nashushwa cheo na kuhamishiwa mkoani Mwanza!”
Ingawa Nyambele hawataji viongozi hao, rekodi zinaonesha kuwa Waziri wa Fedha mwaka huo alikuwa Profesa Kighoma Malima, Waziri Mkuu alikuwa Malecela, na Rais alikuwa Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Anaongeza:
 “Hayo ni ya huko nyuma, lakini ni vielelezo vinavyothibitisha uhusika wa viongozi wa ngazi za juu serikalini na hata kwenye chama tawala katika kushuka kwa maadili ya watumishi wanaohusika na ukusanyaji kodi na wale wa umma kwa ujumla wao.”
Anasema mmomonyoko wa uadilifu katika utendaji kazi ndani ya TRA ulishika kasi baada ya Kamishna Mkuu wa kwanza kuondolewa kwa manufaa ya aliowaita ‘walafi’.

Mwaka 2003 Kamishna Mkuu wa kwanza wa TRA Melkzedeck Sanare aliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Harry Kitillya, ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha.
“Mbegu za mmomonyoko huo zilianza kupandwa baada ya ujio wa Mwenyekiti wa Pili wa Bodi ya Wakurugenzi uliofuatiwa kwa karibu na mabadiliko ya mawaziri katika Wizara ya Fedha. Wote wawili (Mwenyekiti wa Bodi ya TRA na Waziri wa Fedha walianza kukiuka misingi ya kazi iliyokuwa imewekwa na Bodi ya kwanza.
“Misingi hiyo ndiyo ilikuwa nguzo ya ufanisi katika utendaji wa TRA kati ya mwaka 1996 na 2003. Pamoja na kwamba sheria iliyoanzisha TRA ilikuwa inatambua madaraka ya Waziri wa Fedha juu ya Bodi na watendaji wakuu wa TRA, mawaziri wa fedha waliokuwapo wakati TRA inaanzishwa hadi kuanza kufanya kazi waliheshimu mipaka ya kazi iliyokuwa imeainishwa kwa kuwa walikuwa wameidhinisha wenyewe.
“Mwenyekiti wa Bodi aliyeingia madarakani mwaka 1998 alitoka serikalini na alianza kulazimisha Bodi kubadili baadhi ya uamuzi wa Bodi ya kwanza. Alikuja na hoja za usawa wa jinsia na hata ukabila katika ajira bila kujali uwezo – na hilo lilianza kuathiri utendaji katika ukusanyaji mapato ya Serikali.
“Alikiuka baadhi ya taratibu za kiutendaji kwa kushughulika na walipa kodi yeye mwenyewe huku akitoa maelekezo kwa Kamishna Mkuu juu ya viwango vya kodi vya kutoza wafanyabiashara hao.
“Kwa kufanya hivyo alikuwa anakiuka sheria ya TRA ambayo inakataza Bodi kuingilia kazi za ukadiriaji na ukusanyaji kodi.
“Hakuishia hapo. Ilifika wakati akaanza kuongoza timu za wapelelezi wa kodi kufanya doria mchana na usiku ili kukamata bidhaa za magendo au wakwepa kodi. Tuliomuonya juu ya ukiukwaji huo wa sheria ‘tulilipwa’ kama alivyoona inafaa.
“Kwa ujumla, Mwenyekiti huyo alishirikiana na Waziri wa Fedha wa wakati huo katika kukanyaga msingi imara uliokuwa umejengwa na Bodi ya kwanza pamoja na Waziri aliyekuwapo wakati huo. Wote wawili walishirikiana kuweka viongozi waliotaka na ambao wangetii maagizo yao bila kuhoji. Wigo wa fungate hilo la viongozi wapya wa TRA na wale wa wizara liliendelea kupanuka hadi kwenye ngazi za juu za uongozi wa nchi, huku wakiingiza pia viongozi wa idara nyeti kama TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia Rushwa) na Usalama wa Taifa.
“Kutokana hali hiyo, ilifika wakati ambako viongozi wa TRA walifanya wanalotaka wakijua kuwa hakuna mamlaka yoyote inayoweza kuwauliza; achilia mbali kuwawajibisha. Matunda ya hali hiyo ni pamoja na madudu machache sana yaliyoibuliwa na Serikali mwanzo kabisa wa Awamu hii ya uongozi wa nchi hii,” anasema Nyambele.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa Waziri wa Fedha anayetajwa kwa wakati huo ni Basil Mramba, aliyechukua nafasi hiyo kutoka kwa Daniel Yona. Mwenyekiti wa Bodi ya TRA wa pili alikuwa Dk. Enos Bukuku; ambaye pia kwa wakati huo alikuwa Msaidizi wa Waziri Mkuu wa Mambo ya Uchumi.

Taarifa zaidi imechapishwa uk. 12&13 wa gazeti la hili la JAMHURI.