Polisi yaua wanawake 3 walioshukiwa ugaidi baada ya kushambulia kwa kisuWANAWAKE watano waliovalia mabaibui na walioaminika kuvaa mikanda ya kujilipua wamevamia kituo kimoja cha polisi mjini Mombasa katika shambulio linalodaiwa kuwa la kigaidi.

Maofisa wa polisi nchini Mombasa wameeleza kuwa walitibua jaribio hilo na kufanikiwa kuwaua wanawake watatu huku wawili wakikamatwa.

Maofisa wa polisi wanasema washukiwa hao waliwasili katika kituo cha polisi cha Central ili kuripoti kuhusu simu iliyoibiwa na wakati maelezo yao yalipokuwa yakichukuliwa mmoja wao alichukua kisu na kuwadunga maofisa wawili wa polisi, huku mwingine akiwarushia polisi waliokuwa wakichukua maelezo yao bomu la petroli.

Polisi wanasema kuwa waliwafyatulia risasi na kuwaua watatu.

Maofisa wa polisi waliojeruhiwa wamepelekwa hospitali huku kituo hicho cha polisi kikilindwa ili kuhakikisha kuwa hakuna tishio jingine.

Kumekuwa na mashambulio kadhaa katika eneo la Pwani ya Kenya katika miaka ya hivi karibuni mengi yakifanywa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.