Rais Magufuli amepatwa na nini?


NINI kilichomsibu Rais John Magufuli akafika hadi ya kutamka aliyoyatamka katika hotuba zake za karibuni Pemba na Unguja? Alikuwa akifikiri nini alipokuwa akizitoa hotuba hizo ambazo wengi wanaamini zilimshushia hadhi na zikionyesha dalili kwamba taifa linaelekea pabaya?

Kama ilikuwa bahati mbaya iliyomfanya ateleze Pemba kwa nini washauri wake wasimtanabahishe ajizuie asiteleze tena alipohutubia Unguja? Au hana wa kumuonyesha njia anapokuwa anapotea?

Magufuli ana nini? Kwa sababu hiyo inatubidi tujiulize alifikwa na nini akajikuta ameanguka hivyo? Labda akionyesha ubabe wa wenye nguvu za dola na kibri cha wanaolewa madaraka. Ubabe huo ndio unaowafanya baadhi ya wachambuzi wamuone kuwa ni kiongozi mwenye muelekeo wa kidikteta.

Sidhani kama kuna aliyetarajia kwamba angezungumza alivyozungumza Pemba na Unguja. Hotuba zake zote mbili ziliwashangaza wengi, kuwahuzunisha wengine na ziliwatia haya hata baadhi ya viongozi wenzake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) .

Hizo hazikuwa hotuba za kutolewa na kiongozi anayeishi katika zama hizi za intaneti na za ustawi wa mitandao ya kijamii yenye kusambaza habari kwa haraka. Hata watu wanaoishi nje ya miji mikuu siku hizi huwa na uwezo wa kuziona habari za nje ya nchi mubashara, yaani papo kwa papo, zinapotokea. Ni taabu katika zama hizi kwa kiongozi yeyote, awe Magufuli au nani, kuweza kuwadanganya watu mchana kweupe.

Juu ya hayo, Magufuli alijaribu kufanya hivyo. Kwa mfano, alithubutu kujivunjia heshima kwa kudai kwamba Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alijifungia chumbani Dar es Salaam huku akijidai kwamba alikwenda Ulaya.

Bila ya shaka kuna mengi ya Maalim Seif yaliyomuudhi Magufuli. Miongoni mwayo ni hatua yake ya kuukataa hadharani mkono wa Dk. Ali Mohamed Shein katika mazishi ya Aboud Jumbe, Rais wa pili wa Zanzibar na aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania. Mengine ni hizo ziara alizofanya katika nchi kadha wa kadha za Ulaya, Marekani na Canada.

Ni taabu kufahamu kwa nini Magufuli alijaribu kumkadhibisha Maalim Seif ilhali kwa kufanya hivyo inakuwa ni yeye anayesema uongo. Katika nchi zote alizozitembelea huyo Katibu Mkuu wa CUF alipokewa na wakuu wa serikali wa ngazi mbalimbali, alihojiwa na vyombo vya habari vya baadhi ya nchi hizo na alihutubu katika vikao mahususi alivyopangiwa yeye, hususan katika miji ya Washington na London.

Inashangaza kumsikia Magufuli akisema kwamba Maalim Seif alijifungia chumbani Dar ilhali katika baadhi ya mikutano aliyoandaliwa Washington na London walikuwako wanabalozi wa Tanzania. Ule wa Chatham House, London, ulihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dk. Asha-Rose Migiro, aliyezungumza kuitetea serikali yake.

Sasa Magufuli akijaribu kumbabaisha nani?

Kuna ushahidi pia kwamba Maalim Seif na wenzake walifika mjini Hague, Uholanzi, kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ambako walichukua hatua za mwanzo katika mchakato wa kuwashtaki baadhi ya wakuu wa serikali ya Zanzibar na wa ile ya Muungano kwa ukiukwaji wa haki za binadamu, matumizi ya vyombo vya ulinzi dhidi ya wananchi kuanzia kipindi kilichoelekea uchaguzi wa Oktoba 25, 2015, na baadaye.

Pia yameshutumiwa makundi ya “Mazombi”, “Janjaweed” na mengineyo kama hayo ambayo yanasemekana kuwa yanaratibiwa na wakuu fulani wa serikali ya Zanzibar.

Magufuli anaziona shutuma zote hizo kuwa ni adha tupu.

Ilishangaza pia kumsikia Magufuli akiwaambia Wazanzibari kwamba alikwenda kwao kuwashukuru kwa kura nyingi walizompigia ilhali sote tunajua kwamba Unguja na Pemba alishindwa kwa idadi za kura na mpinzani wake mkuu Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyekuwa mgombea wa vyama vilivyo chini ya mwavuli wa Ukawa.

Hotuba alizozitoa Magufuli visiwani Zanzibar zilifanana katika maudhui yao na ukali wao. Aidha zilituonyesha jinsi Rais huyu alivyo tayari kuikiuka Katiba ya nchi na kutumia mabavu kupambana na wapinzani wake. Zote hizo ni dalili za hali mbaya inayoweza kuivaa Tanzania.

Lengo la hotuba hizo lilikuwa kuonyesha nani mwenye nguvu na pia kuwatia hofu wananchi. Lililoshtusha na kusikitisha zaidi ni kumsikia akimuagiza Shein afanye mambo ya kwenda kinyume na Katiba kwa kumshinikiza asikubali kusaini nyaraka za kuidhinisha malipo anayostahiki kupewa Maalim Seif kwa mujibu wa Katiba ya nchi kutokana na wadhifa aliokuwa nao wa umakamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Tutumai kwamba Shein hatoingia mtegoni kwa kutenda mambo anayoamrishwa ayatende ambayo endapo akiyatekeleza atakuwa anaukiuka utaratibu wa utawala wa kisheria. Na akiyatenda atakuwa anazidi kuthibitisha shtuma za kwamba hatima ya Zanzibar huamuliwa Dodoma.

Wazanzibari wamepitia misukosuko mingi hasa walipokuwa chini ya tawala za Awamu ya Kwanza na Awamu ya Tatu. Wakati wa Awamu ya Kwanza watu wakifungwa ovyo, wakiteswa na kuna waliopotea wasijulikane hadi leo wamepotelea wapi. Wakati wa Awamu ya Tatu, chini ya Dk. Salmin Amour, kuna wapinzani waliobandikizwa kesi kwa kisingizio cha uhaini na kuihujumu serikali.

Safari moja Salmin alipoulizwa kuhusu hatima ya wafungwa hao wa kisiasa alijibu kwa kejeli kwa kusema: “hawaozi hao, si mapapai.”

Wakati wa utawala wa Amani Abeid Karume hapakuwa na wafungwa wa kisiasa na huo ulikuwa mwanzo mwema kwa mustakabali wa Zanzibar, ingawa utawala huo uliingia nuksi kwa mauaji yaliyotokea Pemba muda mfupi kabla ya Karume mdogo hajakaa sawa madarakani.

Watu walianza tena kukamatwa kwa sababu ya fikra zao wakati wa utawala wa Shein hata palipokuwako Serikali ya Umoja wa Taifa walipotiwa mbaroni viongozi wa Uamsho. Ijapokuwa viongozi hao wa Uamsho wamefikishwa mahakamani lakini namna kesi yao inavyoendeshwa kunawafanya wengi wajiulize iwapo siasa za hofu hazirejelewi tena.

Tunaweza kusema kwamba alichofanya Magufuli Pemba ni kuzitumia hizo hofu pale alipowapongeza wanajeshi kwa “kulinda” amani, wanajeshi walewale ambao wananchi walikuwa wakilalamika kuhusu nyendo zao za kutumia nguvu na vitisho, Unguja na Pemba, na zaidi Pemba. Kwa kuwapongeza Magufuli amekuwa kama akiwahimiza wasiogope kitu waendelee kuwadhalilisha wananchi.

Inashangaza kwamba Magufuli huyuhuyu aliyewahi kusema kwamba hawezi kuyaingilia mambo ya Zanzibar pale uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 ulipofujwa kwa kusudi ili CCM na mgombea wake wa urais wafaidike, hivi sasa anaonekana akipiga mbizi katika maji marefu ya siasa za huko.

Kwa hakika, siku hizi hata Bara, Magufuli amezoea tabia ya kuzusha mambo ya kieneo katika hotuba zake na hata kuzungumza lugha za makabila fulani anapokuwa anahutubia. Anajisahau kuwa yeye si Rais wa eneo fulani au wa kabila fulani. Ni Rais wa Tanzania nzima.

Kuzidekeza siasa za kikabila au kieneo ni jambo la hatari kwa mustakabali wa Tanzania. Nchi nyingi barani Afrika zimeangamia kwa laana ya uhasama baina ya maeneo au makabila. Inasikitisha kwamba katika Tanzania ya leo tunawashuhudia viongozi wa serikali na wanasiasa wa chama kinachotawala wakiipandisha mizizi ya fitina hii kwa kujinasibu na makabila yao.

Ikiwa Magufuli alikuwa akifuatilia kwa makini yaliyokuwa yakisemwa juu ya hotuba zake za Pemba na Unguja katika mitandao ya kijamii, vijiweni na kwenye vyombo vya habari lazima sasa anatambua ya kuwa kama ana washauri waliomshawishi atoe hotuba hizo basi walimpotosha. Na kama hakushauriwa na mtu bali alichochewa na andasa zake basi huu ni wakati wa kuwa na washauri ataowasikiliza.

Hiyo huenda ikawa kazi kubwa kwani walio karibu naye na wanaomfahamu wanatwambia kuwa haambiliki na hakubali ushauri wa mtu. Kama ni kweli basi tabia hiyo ni hatari kwa taifa lolote lenye kiongozi mwenye hulka ya aina hiyo. Anapoteleza ndipo maamuzi yake yanapokuwa ya kiimla, ya kidikteta. Mwenyewe anaghadhibika akiitwa dikteta na anakanusha kuwa yeye si dikteta.

Tusisahau kuwa hakuna dikteta anayekubali kuwa yeye ni dikteta, kuwa ni mtawala wa kimabavu. Ni matendo yake yanayotufanya tuamue kuwa mtawala ni wa kimabavu au wa haki. Hatua za kujaribu kuwadhibiti wapinzani na wakosoaji wa mwenendo wa serikali na wa viongozi wake kwa kujaribu kuwanyamazisha kwa kuwakamatakamata na kuwatisha ni hatua zinazotufanya tumhukumu mwenye kuzitumia kuwa ni mtawala wa kimabavu.

AHMED RAJAB
SEP 15, 2016
[email protected]