UKUTA wa CHADEMA hautakuwepo Oktoba Mosi

Freeman Mbowe
Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe ametangaza kuwa operesheni UKUTA iliyokuwa ifanyike Oktoba Mosi haitafanyika tena.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mbowe amesema hayo leo baada ya kimya cha muda mrefu tangu kuahirishwa kwa mikutano na maandamano hayo Septemba Mosi. Aidha, Mbowe amesema kuwa hawatataja tarehe ya kufanya maandamano ili kutompa adui nafasi ya kujipanga. Amesisitiza kuwa maandamano yapo, ila tarehe hawataiweka hadharani.

Operesheni hii ilikuwa ifanyike Septemba Mosi mwaka huu lakini iliahirishwa ili kuwapa nafasi viongozi wa dini kuweza kukutana na kujadiliana na Rais Dkt Magufuli juu ya mustakabali wa hali ya kisiasa nchini kufuatia kuzuiwa kwa shughuli mbalimbali za kisiasa.

Hadi leo viongozi wa dini bado hawajakutana na Rais Magufuli licha ya wao kueleza kuwa Rais Magufuli hajakataa kukutana nao kama inavyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Wakati huo huo, Mbowe amewataka wanachama wa chama hicho na watanzania kwa ujumla kupuuza taarifa za utafiti za wa taasisi ya Twaweza, anaandika Pendo Omary via MwanaHALISI Online.

Tamko la Mbowe limekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya Twaweza, kutangaza matokeo ya utafiti wake uliopewa jina la ‘Demokrasia, Udikteta na Maandamano.’

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mbowe amesema Twaweza ni wapiga zumari wanaochaguliwa wimbo na watawala wa kiimla ili kujaribu kufunika aibu inayolikabili taifa letu kwa sasa.
“Hatua zinazochukuliwa na Rais John Magufuli zimeporomosha uchumi wa nchi yetu kwa kiasi cha kutisha. Mapato ya wananchi yameanguka. Uwekezaji wa ndani na nje ya nchi umepungua. Ajira zimepungua kwa kiasi kikubwa na umasikini umeongezeka,” amesema Mbowe.
Ripoti ya utafiti wa Twaweza iliyokusanywa kutokana na wahojiwa 1,602 kati ya tarehe 23 na 29 Agosti, mwaka huu kwa njia ya simu Tanzania Bara, imesema kwamba watu 6 kati ya 10 wamepinga madai kuwa nchi ya Tanzania inaongozwa kidikteta.

Hata hivyo Mbowe amesisitiza kuwa, kwa sasa mifumo ya kikatiba na kisheria ya uendeshaji wa nchi na serikali imevurugwa kwa kiasi ambacho nchi inaendeshwa kwa amri na vitisho vya mtu mmoja.


Aidha, Mbowe amesema Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya CHADEMA inatambua mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi - CUF, unaomhusisha aliyekuwa Profesa Ibrahim Lipumba unachochewa na Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Jaji Mutungi anaivuruga CUF kwa kujaribu kumrudisha madarakani Prof. Lipumba, ambaye alijiuzulu madarakani katika mazingira yanayoashiria kununuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa lengo la kusaliti vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi.
CHADEMA hatumtambui Prof. Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF Taifa au Mwenyekiti mwenza wa UAWA, tunamtambua kama adui wa demokrasia na msaliti wa harakati za kudai haki katika nchi yetu,” amesema Mbowe.
Mbowe ameongeza kuwa, Jaji Mutungi pia ni adui wa demokrasia ya vyama vingi na kwamba CHADEMA haitampa ushirikiano wowote isipokuwa ule tu unaolazimishwa na matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa.