Mcheza kikapu apata udhamini kusoma Marekani na kutakiwa aitangaze Tanzania


Na: Geofrey Tengeneza

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imemtaka kijana wa kitanzania ambaye pia ni mchezaji wa mpira wa kikapu Underson Simon (19) kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya utalii nchini Marekani kwa lengo la kuvutia watalii wengi zaidi kuitembelea Tanzania.

Underson ambaye ni tunda la kituo cha Michezo cha Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park cha jijini Dar es salaam amepata udhamini wa masomo kwenda kusoma shahada ya kwanza ya sayansi ya Kompyuta katika Chuo Kikuu cha Georgia University kilichoko Atlanta Georgia nchini Marekani.

Akizungumza wakati wa kumuaga Underson ofisini kwake jijini Dar esalaam, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Bibi Devota Mdachi mchezaji huyo anayechipukia wa mpira wa kikapu nchini anayechezea timu mpira wa kikapu ya vijana (Vijana Basketball Club) pamoja na kumtaka ajitahidi katika masomo yake, lakini pia amemtaka atumie fursa hiyo na ile ya kushiriki katika mashindano mbalimbali akiwa na timu yake ya chuo kikuu cha Georgia katika mchezo wa kikapu kuvitangaza vivutio vyetu vya utalii.
“Peperusha vema bendera ya nchi yetu na tumia kila jukwaa utakalopata ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii kuitangaza Tanzania kama eneo bora la utalii duniani” alisema Bi Mdachi na kuongeza kuwa TTB inakusudia kuanza mchakato wa kumpa heshima ya kuwa Balozi wa heshima wa Utalii wa Tanzania.
Mkurugenzi huyo wa TTB alimkabidhi mchezaji huyo wa mpira wa kikapu nchini, bendera ya Taifa na vielelezo kadhaa vinavyoelezea utalii wa Tanzania ili visaidie kumjengea uelewa zaidi kuhusu vivutio vya utalii vya Tanzania.

Kwa upande wake kijana huyo Underson Simon alielezea kufurahishwa kwake kupata nafasi hiyo lakini pia kutambuliwa na TTB kama mmoja wa wanamichezo wa kitanzania wanaoweza kuvitangaza vema vivutio vyetu vya utalii nje ya nchi na hivyo kuchangia kukuza sekta ya utalii.

Naye mwalimu mwandamizi (kocha) wa mpira wa kikapu wa kituo cha Jakaya Mrisho Kikwete Bw. Bahati Mgunda amesema kituo chake kinajivunia mafanikio hayo ya mmoja wa wachezaji wao kupata ufadhili huo wa masomo ambao umetokana hasa na umahiri wake katika mchezo huo.

Simon ameondoka saa 9.00 alfajiri ya leo kwa shirika la ndege la Uturuki kuelekea nchini Marekani tayari kujiunga na chuo kikuu hicho cha Georgia.