Mke wa Waziri aandika barua ya kuacha kazi ATCL baada ya kauli ya Rais Magufuli

MKE wa waziri mwandamizi katika Serikali ya Awamu ya Tano (jina tunalihifadhi kwa sasa) aliyekuwa akifanya kazi Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ameacha kazi.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya shirika hilo vililiambia Nipashe jana kuwa mke huyo ambaye amedumu ATCL kwa zaidi ya miaka 20, aliandika barua ya kuacha kazi ghafla.

Kuacha kazi kwa mtumishi huyo (jina tunalihifadhi kwa sasa) kumekuja siku chache tangu Rais John Magufuli, bila kutaja jina, kusema anashangaa kuona wake wa baadhi ya mawaziri wake wanafanya kazi katika shirika ambalo halifanyi kazi vizuri.

Rais Magufuli aliyasema hayo Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizundua ndege mbili mpya ambazo zimenunuliwa na serikali kwa ajili ya 'kulifufua' shirika hilo.