Sasa ni UKAWA v/s Lipumba

UKAWA imeeleza kuwa itatumia wanasheria wa vyama vyote vinavyounda umoja huo (CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, kufungua kesi ili kumuondoa Ofisi Kuu za CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam.

Akitoa tamko la umoja huo mbele ya waandishi wa habari leo katika Hoteli ya Courtyard jijini Dar es Salaam, Freeman Mbowe, mwenyekiti mwenza wa UKAWA amesema, hatua hiyo itasaidia kuuweka umoja huo katika hali salama kwani Lipumba anatumiwa ili kuvuruga upinzani hapa nchini.
“Alichokifanya Lipumba mwaka jana, akiwa jemedari anayeongoza chama chake lakini akaamua kukisaliti chama na UKAWA tena katikati ya mapambano ni uhaini na katika nchi yoyote, iwe ya kidemokrasia au ya kidikteta, uhaini ni kosa ambalo adhabu yake ni kifo. Sisi siyo mahakama au majaji. Sisi ni wanasiasa na kwa alichokifanya, tunamuhukumu kifo cha kisiasa,”
amesema Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema kwa niaba ya viongozi wenzake wa UKAWA aliyekuwa ameambatana na wenyeviti wenza wa UKAWA, James Mbatia (NCCR Mageuzi), Julius Mtatiro (CUF), Oscar Emmanuel (NLD) pamoja na makatibu wakuu wa vyama hivyo akiwemo Maalim Seif Sharrif Hamad (CUF), Dk. Vincent Mashinji (CHADEMA) na wengine.
“Tumekubaliana wanasheria wetu waanze kuchukua hatua, huu ni wakati muhimu wa kushikamana kuliko wakati wowote ule kwani huyu bwana anatumiwa na serikali ya CCM kwa kazi maalum. Hana lengo la kuivuruga CUF tu bali pia kuvuruga ushirikiano wa UKAWA,” amesema.
Alisema, kwa kiwango kikubwa mgogoro huo umechangiwa na Jaji Mutungi kutokana na barua ama msisitizo wake wa kumtambua Prof. Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho licha ya kujiuzulu Agosti 2015.
“Jaji Mutungi anaivuruga CUF kwa kujaribu kumrudisha madarakani Prof. Lipumba, ambaye alijiuzulu madarakani katika mazingira yanayoashiria kununuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa lengo la kusaliti vyama vinavyounda UKAWA.
“Chadema hatumtambui Prof. Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF Taifa au Mwenyekiti mwenza wa UKAWA, tunamtambua kama adui wa demokrasia na msaliti wa harakati za kudai haki katika nchi yetu.”
Mtatiro (Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF Taifa) amesema hoja za msajili kumrudisha Lipumba madarakani hazina mashiko yoyote kisheria na ndiyo maana chama hicho kimempuuza.
“Duniani kote mtu akishaandika barua ya kujiuzulu anakuwa amejiuzulu tayari, ndiyo maana Katiba ya CUF Ibara ya 117 (1) inasema; Kiongozi yoyote anaweza kujiuzulu wakati wowote….suala la kujiuzulu ni uamuzi na utashi wa mtu binafsi.
Mtatiro amesema CUF ilichukua hatua za kisheria zinazothibitisha kujiuzulu kwa Prof. Lipumba ikiwemo kuteua Kamati ya Uongozi Taifa chini ya Twaha Taslima na kueleza kuwa hata Msajili wa Vyama Vya Siasa aliidhinisha uamuzi huo na kuliweka jina la Taslima kama kiongozi wa CUF.
“Mpaka sasa tunavyozungumza, tovuti ya ofisi ya msajili bado imemuweka Taslima katika orodha ya viongozi wa CUF taifa, hii ina maana kuwa hata yeye alitambua kujiuzulu kwake na alikubaliana na hatua zilizochukuliwa na CUF,” amesema Mtatiro.