Barua ya wazi kwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Barua ya Wazi kwa Mh Januari Makamba, Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Mheshimiwa January Makamba, waziri unayehusika na mazingira,

Sisi wakazi wa Kitongoji cha Teema, Kijiji cha Ngyani, Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha tunakuandikia barua hii ya wazi baada ya jitihada zetu za kukufikia kushindikana. Kwa muda wa miezi kama saba sasa tumekua waathirika wakubwa wa mradi wa mgodi wa uchimbaji mchanga unaofanywa na Kampuni ya Kichina katikati ya makazi yetu na kupanuliwa kwa kasi kubwa na sasa umefikia eneo la zaidi ya hekari 10. Eneo hili liko umbali wa takribani kilometa 3 kutoka barabara kuu ya Arusha – Moshi unapoandisha vijiji vya Meru kwa barabara inayoanzia eneo la Leganga na kama mita 600 kutoka mji mdogo wa Juakali.

Figure 1:Ulipo Mgodi kutoka barabara kuu ya Arusha- Moshi
Kama unavyojua hali ya vijiji karibu vyote vilivyo chini ya Mlima Meru, haya ni maeneo ambayo yana idadi kubwa ya watu na ni kati ya maeneo nchini yenye uhaba mkubwa wa ardhi kutokana na msongamano wa watu. Vijiji vingi vilivyokua vimejaa mashamba makubwa ya kahawa, migomba na mazao mengine kama mahindi, kwa sasa vimejaa makazi ya watu na maeneo mengine ile mandhari ya kijiji inabadilika kuwa kama miji midogo inayoanza. Kitongoji chetu ni kati ya maeneo yaliyojaa makazi ya watu wengi (nyumba) na pia kina chanzo cha maji ya chemechem ambacho kwa miaka mingi tangu kuanzishwa kwa kimekua ni tegemeo kubwa la maji kwa kijiji.

Katika hali ya kushangaza, miezi saba iliyopita kampuni inayofanya upanuzi barabara kuu ya Arusha kwenda Moshi ilinunua eneo la mkazi mmoja wa kitongoji chetu kwa lengo la kulifanya kuwa mgodi wa mchanga. Jambo hili lilifanyika bila sisi wanakijiji au majirani wa karibu na eneo hili kutaarifiwa na tulifahamu pale tulipoona mitambo mikubwa ya kuchimba mchanga ikifanya kazi usiku na mchana na malori yakifanya kazi ya kusomba. Ndani ya muda wa kama mwezi mmoja, mwenekano (landscape) wa sehemu kubwa ya kitongoji chetu ulibadilika kwani walishusha kilima na kuchimba eneo kubwa huku wakiingia chini sana. Jambo hili lilileta usufumbu mkubwa sana kwetu wakazi wa eneo hili. Kwanza tulishangaa imekuaje serikali imekubali eneo la makazi libadilike kuwa mgodi wa mchanga na bila kujulisha wakazi. Pili tumepata madhara makubwa sana ya vumbi majumbani kwetu litokanalo na uchimbaji huu. Tatu, kutokana na uzito wa mitambo inayotumika na upasuaji wa miamba, baadhi ya nyumba zimeathirika na kupata nyufa. Nne, kwa kua kazi hii inafanyika usiku na mchana, imekua vigumu sisi kulala usiku kutokana na kelele za uchimbaji huu na watoto kuathirika kimasomo kwa kulazimika kwenda shule asubuhi huku wakiwa hawajalala vema usiku. Tano, kelele hizi za usiku kucha imewasaidia sana wezi kwani wanakuja na kuvunja majumbani mwetu na kuiba kwa kuwa mtu huwezi kuwasikia. Sita na linalotupa hofu zaidi, ni ukweli kwamba tunakwenda kupata athari kubwa ya muda mrefu kutokana na uharibifu huu unaoendelea.

Figure 2: Eneo la Mgodi katika ya makazi
Tulitoa taarifa katika serikali ya kijiji kuhusu tatizo hili lakini hakuna kilichofanyika. Baadaye tulitoa taarifa kwa diwani na tuliona maafisa kadhaa wa serikali waliokuja kutembelea eneo hili na kupiga picha lakini hakuna kilichofanyika. Baadaye tukaamua kuandika barua kwa mkuu wa wilaya na sasa mwezi mzima umekwisha na hatujawahi kupata majibu huku uchimbaji ukiendelea. Kwa bahati mbaya, jitiihada zetu za kumpata Mbunge wa Arumeru Mashariki Mh Joshua Nassari hazijazaa matunda na hatujawahi kusikia kaluli yake kuhusu uharibifu huu.

Mheshimiwa waziri, baadhi ya majirani wa eneo uliupoanzishewa mgodi huu waliposikia kwamba aliyeuza amelipwa fedha nyingi sana kwa uchimbaji huu, wakaanza kushawishika kupitia mawakala wa kampuni hii maeneo yao mmoja baada ya mwingine yatumike kama migodi na hivyo uchimbaji ukapanuliwa zaidi. Hadi tunapoandikia barua hii, uchimbaji unaendelea na maeneo mengine yanazidi kununuliwa hivyo makazi yetu yaliyokua katika madhari ya kuvutia na kupendaza kwa enzi na enzi sasa yamebadilika kuwa mashimo makubwa ambayo hatujui yatakuja kujanzwa na kitu gani. Uchimbaji huu umehatarisha sio nyumba/makazi yetu tu bali nguzo za umeme zinazokuja maeneo yetu kwa sasa zimeegeshwa kwa zimezungukwa na mashimo. Kama vile haiotshi wachimbaji wamefikia hatua ya hatua kufukua makaburi ya familia na imetulazimu kuzika upya watu wengine ambao tuliwazika zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Ndugu Mheshimiwa Waziri, tunakuomba ufike katika eneo kwa haraka na kushuhudia uharibifu huu na kuchukua hatua stahiki kabla maisha yetu hajaingia kwenye hatari kubwa zaidi. Kinachofanyika kwenye kitongoji chetu sio uharibifu mkubwa wa mazingira tu bali ni kinyume kabisa na sheria za mazingira na uanzishwaji wa migodi. Hatuelewi kibali cha uchimbaji huu kilitolewa na nani na kwa misingi gani kwani kila jitihada za kutafuta kauli ya serikali za mitaa na wilaya ya kusimamishwa machimbo haya zimekwama na majibu tuliyopewa mara ya mwisho na kampuni husika ni kwamba hii ni kazi ya serikali. Tunaomba usitume maafisa bali ufike wewe mwenyewe kwani tumeona makundi kadhaa ya maafisa wa serikali wakija hapa na kuondoka bila kutuambia chochote na bila kuona mabadiliko. Jambo hili linatupa hofu hata ya ufuatiliaji kwani hatuna hakika na usalama wa maisha yetu kwa vile hatujui ni mamlaka ipi inatutendea haya. Wachina hawa wanaharibu makazi yetu bila huruma na uchimbaji huu unafanyika kwa kasi sana.

Pamoja na barua hii, naambatanisha picha za baadhi ya maeneo yuchimbaji ulipofanyika ujionee mwenyewe jinsi ambavyo kijiji chetu kimebadilika kuwa mashimo. Tuna nakala za barua tulizotuma kuhusu swala hili na kumbukumbu ya vikao vya wakati na tutakupatia kwa uthibitisho juu ya kukwama kwetu kupata kiongozi wa kutusaidia

Tunatanguliza shukrani kwa msaada wako wa hara katika hili.

NI SISI WAKAZI WAATHIRIKA WA KITONGOJI CHA TEEMA, KIJIJI CHA NGYANI, WILAYA YA ARUMERU.