Yanayojiri baada ya kufikisha tatizo letu kwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Rejea: MALALAMIKO YA KUHARIBIWA MAKAZI YETU NA KUHITAJI MSAADA WA WAZIRI JANUARI MAKAMBA (BOFYA HAPA)

Sisi wakazi wa Kijiji cha Ngyani kilichoko Wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha tulioathirika sana na uchimbaji haramu wa mchanga katika maeneo yetu ya makazi tangu mwezi wa sita mwaka huu unaofanywa kwa kibali kilichotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru na Mwenyekiti wa kijiji, tunazidi kumshukuru Waziri wa Mazingira Mhe. Januari Makamba kwa hatua za haraka ananzochukua kufutilia jambo.

Leo hii maafisa wa NEMC wamefika eneo la tukio na wamechukua ushahidi wote wakiwa na baadhi ya wananchi na Mhe. Diwani wa kata ya Nkoaranga ambaye amekua mstari wa mbele kupinga hili jambo tangu lilipoanza bila mafanikio (picha zinajieleza). Pia wamejionea kwa macho yao jinsi ambacho chanzo cha maji/chemchem ambayo imekua ikitiririsha maji kwa karne na karne sasa maji yameanza kukauka na wananchi wanachota kwa vikombe.

Kwa upande mwingine, baada ya habari kujulikana kwa waliotoa vibali na kampuni inayochimba kwamba tumefikisha tatizo letu kwa waziri, wananchi wameanza kupata habari za kuwatisha kwamba hawatafanikiwa na leo wachina wamefika asubuhi na mapema na kuanza kuweka nguzo upoande mmoja wa maeneno waliyochimba chini sana pembezoni na barabara ya umaa. Kwa walivyochimba, barabara hii haiwezi kuvumilia mvua kubwa bila kumomonyoka (picha zinajieleza).

Tuna imani kwamba katazo la kusimamisha uchimbaji huu litatoka leoleo baada ya NEMC kujionea kiwango cha uharibifu. Mungu akubariki Mhe. Waziri na wasaidizi wako kwa uwajibikaji wenu na tunategema haki yetu itapatikana mapema.