Akamatwa kwa kutapeli mke wa mmiliki wa shule mil 600/= ili wanafunzi wafurike shuleni

Jeshi la Polisi limefanikiwa kumtia mbaroni mkazi mmoja wa jijini Dar es Salaam, anayetuhumiwa kujifanya mganga wa kienyeji na kumtapeli mke wa mmiliki wa shule moja ya sekondari Sh600 milioni.

Mtuhumiwa huyo alifanikiwa kutapeli fedha hizo baada ya mwanamke huyo kukataa ushauri wa awali kuwa ili dawa ya kufanya wanafunzi wafurike shuleni hapo ifanye kazi, waue mwanafunzi mmoja kimazingara. Alipokataa ushauri huo ndipo alipoambiwa atoe fedha ili atengenezewe dawa mbadala.

“Yuko hapo kituo kikuu cha Mkoa wa Kilimanjaro. Mimi nilimuuliza ilikuwaje akasema ni kweli alichukua fedha hizo lakini kwa makubaliano ya uganga. Inaonekana kuna zaidi ya uganga,” alidokeza polisi mmoja.

Kamanda wa polisi wa mkoa, Ramadhan Mungi aliomba apewe muda hadi leo atakapotoa taarifa sahihi, lakini wiki iliyopita aliyekuwa kaimu kamanda wa mkoa, Koka Moita alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo.

Waziri asimamisha kazi Mkurugenzi na Maafisa Misitu wa Mikoa yote

Sehemu ya wajumbe wa kikao hicho wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe.

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Mohammed Kilongo na Maofisa wa Misitu wa Mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi wa upotevu wa mapato ya Serikali.

Akizungumza leo na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya Wizara hiyo Dar es Salaam, Prof. Maghembe amesema agizo hilo limekuja kutokana na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.

Ameagiza pia maofisa hao wote wanaokusanya maduhuri ya Serikali katika Wilaya watumie muda wa siku kumi kuanzia leo kuhakikisha maduhuri yote yaliyokusanywa yanapelekwa benki ikiwa ni pamoja na kukabidhi vitabu vya kukusanyia mapato kinyume cha hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Wale district forestry officers wote wapeleke vitabu vyao wanavyokusanyia maduhuri ya Serikali kwenye ofisi za Kanda, Naibu Katibu Mkuu tusaidie kuwasiliana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali ifanye ukaguzi wa vitabu hivyo ndani ya siku kumi tuhakikishe fedha zinazotakiwa zinaingia kwenye mfuko wa Serikali, Mtu anakusanya fedha ya Serikali toka mwaka 2004 mpaka leo hajapeleka benki ananeemesha hali yake ya nyumbani, hili hapana”. Alisisitiza Prof. Maghembe.

Kwa mujibu wa Waziri Maghembe Bw. Mohammed Kilongo ambaye Idara yake ndiyo inatoa vitabu kwa ajili ya kukusanya maduhuri ya Serikali katika Mikoa yote na Wilaya zote nchini analazimika kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi ambapo ukikamilika sheria itachukua mkondo wake bila uonevu wowote.

Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amewaagiza pia Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kutumia muda wa siku saba kurudi katika jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii maarufu kama Mpingo House ambalo walihama mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka jana na kwenda kupanga katika jengo la NSSF Mafao House lililopo Ilala.

“Wakati tunajenga nyumba hii hapa, tumejenga jengo hili ni kama jengo la misitu ndio maana linaitwa Mpingo House kwa maana ni jengo la Misitu, ninyi wenyewe mmejenga jengo kubwa hili mmemaliza mmehama, Naagiza jumatatu Desemba 11 muwe mmesharudi katika jengo hili, ghorofa ya tatu nikija kukagua niwakute, haiwezekani mueleze matatizo yote mliyonayo muhame nyumba ya Serikali mkapange jengo hapo jirani” Alisema Prof. Maghembe.

Katika hatua nyingine ya kuboresha uhifadhi wa Misitu nchini Waziri Maghembe ameiagiza Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili kuhakikisha inajiimarisha katika lengo lake kuu la uhifadhi kwa kushirikiana na wadau wanaohusika kuhakikisha Mamlaka iliyolengwa ya Uhifadhi Misitu inakamilika.

“Tunataka tutoke kwenye Wakala wa Huduma za Misitu (Tanzania Forestry Services Agency) twende kwenye Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu (Tanzania Forestry Services Authority) ili tuweze kufanya vizuri zaidi kwenye eneo la uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini, Katibu Mkuu tunaomba pia usaidie kufanikisha hili” Alisema Prof Maghembe.

Aliongeza kuwa wakati wa kuundwa Mamlaka hiyo ni vizuri pia Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili ikatenganishwa na kila moja kuwa Idara kamili kutokana na umuhimu wa kila sekta katika kujenga uchumi wa nchi kwa kutoa fursa ya kuboresha maeneo hayo na kuongeza pato la taifa.

Ameitaka pia Idara ya Misitu na nyuki kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuhakikisha kuwa inaongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuziba mianya yote ya ubadhilifu pamoja na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vyanzo vilivyopo.

Akizungumzia mchango wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwenye pato la taifa Mtendaji Mkuu, Bw. Juma Mgoo amesema katika mwaka huu wa fedha TFS imeweka makisio ya kukusanya Tsh. Bilioni 88 ambapo mpaka hivi sasa wameshakusanya zaidi ya asilimia 20 na makisio hayo.

Waziri Maghembe akizungumzia kuhusu uvamizi kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba amewataka wananchi wote waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa kwa ajili ya kuchunga mifugo waondoke ndani ya siku saba zijazo, na wale walivamia mapori ya akiba kwa shughuli za kilimo na ufugaji waondoke ndani ya miezi mitatu ijayo.

"Serikali itawaondoa kwa nguvu wasipotekeleza agizo hili la kuondoka katika maeneo ya hifadhi za taifa na kwenye mapori ya akiba yaliyohifadhiwa” Alisisitiza Prof. Maghembe.

Akizungumzia kuhusu biashara ya Mkaa, Prof. Maghembe amewaagiza wataalamu wa Idara ya Misitu kusimamia biashara ya mkaa kwa kuzingatia taratibu na sheria ikiwa ni pamoja na kuzuia usafirishaji wa Mkaa nje ya nchi.

Ameongeza kuwa nishati ya Mkaa ni muhimu lakini Tanzania ina hifadhi kubwa ya makaa ya mawe ambapo ameitaka Idara ya Misitu kwa kushirikiana na wadau wengine kuona ni namna gani ya kuweza kutumia mbadala huo kwa kuzalisha makaa hayo ya mawe kwa matumizi ya kawaida ili kuokoa misitu nchini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Waziri yatafanyiwa kazi kwakuwa lengo lake ni kuona dhamira ya msingi ya Serikali ya awamu ya tano inafikiwa ya kubana matumizi, kuongeza mapato ya Serikali na kuhifadhi maliasili za taifa ikiwemo misitu.
  • Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii 

Msaada wa Mbunge uliokataliwa - Katibu Mkuu Wizara ya Afya azungumzia

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza na waandishi wa habari kuhusu watumishi wa wizara hiyo nchini kote kupokea misaada inayotolewa na taasisi mbalimbali na watu wenye moyo wa kusaidia jamii bila kujali itikadi za siasa au dini isipokuwa wahakikishe misaada hiyo inakidhi viwango vinavyotakiwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema misaada inayotolewa na watu mbalimbali kwa ajili ya kusaidia jamii ni lazima iwe imekidhi viwango vya ubora, hivyo haitakiwi kuangaliwa kwa vigezo vya dini, itikadi wala siasa.

Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake baada kituo kimojwapo nchini kukataa misaada iliyotolewa na Mbunge wa Bukoba Mjini (CHADEMA), Wilfred Lwakatare hivi karibuni.

Dkt. Ulisubisya alisema hivi karibuni gazeti moja la kila siku la hapa nchini liliripoti kwamba misaada iliyotolewa na Mbunge huyo, katika baadhi vituo afya Zahanati kwa ajili ya wajawazito kukataliwa.“Serikali ina sera ya kusaidia jamii hususan misaada inayotolewa kwenye huduma za afya, ambayo inakidhi viwango vya ubora kulingana Sheria , kanuni na taratibu za Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA),” alisema Katibu Mkuu huyo.

Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari kiliripoti kwamba baadhi ya wakuu wa vituo vya afya na zahanati katika Manispaa ya Bukoba, wamegoma kupokea misaada kwa ajili ya wajawazito uliotolewa na kwa madai ya kupewa maelekezo na Serikali.Dkt. Ulisubisya aliwataka watendaji wa afya wa vituo hivyo kuwa wasiangalie misaada hiyo kwa misingi ya dini, itikadi na kisiasa.

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo aliwataka watu mbalimbali wenye lengo la kutoa misaada katika vituo vya afya kuhakikisha kwamba imekidhi viwango viliyowekwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA). Katika hatua nyingine aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Donan Mmbando alikabidhi ofisi hiyo kwa Katibu Mkuu huyo mpya.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akikabidhiwa nyaaraka muhimu na aliyekuwa katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk Donan Mmbando.
  • Taarifa ya Magreth Kinabo – Maelezo

AWALI GAZETI LA MWANANCHI LILICHAPISHA HABARI IFUAFAYO...

Baadhi ya wakuu wa vituo vya afya na zahanati katika Manispaa ya Bukoba, wamegoma kupokea misaada kwa ajili ya wajawazito uliotolewa na Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare kwa madai ya kupewa maelekezo na Serikali.

Mbunge huyo mwishoni mwa wiki alikuwa akisambaza vifaa tiba katika vituo vya afya na zahanati, lakini wasimamizi walikataa kuvipokea, huku wengine wakikimbia wakidai walipewa maelekezo na viongozi wao kutovipokea.

Katika hali ya kushangaza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Richard Mihayo ambaye alikuwa katika msafara wa mbunge huyo alitoweka ghafla baada ya kufika Kituo cha Afya cha Zamzam, huku Kaimu mganga, Samwel Chaba akigoma kupokea vifaa hivyo.

Baada ya mkurugenzi kutoweka, mbunge huyo alilazimika kutelekeza vifaa hivyo kituoni hapo na kwenda Zahanati ya Kashai ambako Kaimu Msimamizi wa zahanati hiyo, Emmanel Luviga alikubali kuvipokea.

Katika Kituo cha Afya Rwamishenye vifaa hivyo vilipokewa na wauguzi waliogoma kuzungumza suala lolote.

Baada ya kufika Zahanati ya Kagemu, Msimamizi wake Glory Sailo aligoma kupokea vifaa kwa ajili ya mama wajawazito kwa madai ni maelekezo ya viongozi.

Hatua ya viongozi kuweka vikwazo kwenye upokeaji wa vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh3 milioni ililalamikiwa na Lwakatare aliyedai aliandika barua manispaa na kutoa nakala hadi ngazi ya mkoa, lakini Mganga Mkuu wa manispaa hiyo, Dk Hamza Mgula alisema hajui lolote kuhusu suala hilo.

Akizungumzia suala hilo, Mihayo alisema kwa kawaida vifaa vya tiba ni lazima vikaguliwe na mganga mkuu wa manispaa ili kuthibitisha ubora, hivyo haviwezi kupelekwa bila kuthibitishwa.

Mahakama yazuia na kuruhusu 'bomoa bomoa' kwa baadhi ya makazi
Wakili wa Nemc, Manchele Suguta (kushoto) akizungumza na mawakili wa walalamikaji, George Mwalali (kulia) na Abubakar Salim mara baada Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, kuweka zuio la kusitisha ubomoaji wa nyumba zaidi ya 600 za wakazi wa mabondeni jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis Dande)

Wakili wa Nemc, Manchele Heche akizungumza na waandishi wa habari.

Wakili wa wakazi wa mabondeni, Abubakar Salim akizungumza na waandishi wa habari.

Wakazi wa mabondeni waliofungua kesi ya kupinga kubomolewa nyumba zao wakimsikiliza mbunge wao, Maulid Mtulia CUF)

Tulieni tulieni...........

Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia akizungumza na wakazi wa mabondeni mara baada ya Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kutoa uamuzi wa kuweka zuio la ubomoaji wa nyumba 681 za wakazi wa mabondeni.

Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia akiwapungia mkono wananchi waliokuwa wamefurika nje ya mahakama.

DAR ES SALAAM, Tanzania

Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi leo Januari 5 imeweka zuio la kusitisha ubomoaji wa nyumba 681 za wakazi wa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo kabla ya mahakama kutoa amri hiyo, kazi ya ubomoaji wa nyumba za wananchi hao ilikuwa ikiendelea hata kwa walalamikaji 681 ambao walikuwa wakisubiri amri ya mahakama.
Hali hiyo imetafsiriwa kuwa ni ukatili na unyama wa hali ya juu wanaofanyiwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, kwani watekelezaji wa kazi hiyo walipaswa kusubiri uamuzi wa mahakama.

Baada ya uamuzi wa mahakama kuweka zuio, tingatinga liliendelea kubomoa nyumba za wananchi hao zaidi ya 100 katika bonde la Mkwajuni, Kata ya Hananasif huku nyumba zaidi ya 5,000 zikiwekwa alama ya X tayari kwa kuvunjwa.

Uamuzi wa shauri hilo umetolewa siku moja baada ya Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF) na walalamikaji wengine wanane, wakiwakilisha wenzao 681, kufungua kesi ya kupinga ubomolewaji wa nyumba hizo.

Katika kesi hiyo namba 822 iliyofunguliwa dhidi ya Manispaa ya Kinondoni, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), chini ya Jaji Penterine Kente, juzi ilianza kusikilizwa lakini kutokana na mvutano mkali wa kisheria kutoka pande mbili baina ya serikali na walalamikaji, iliahirishwa hadi jana kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Pamoja na Mtulia, wengine walioshiriki kufungua kesi hiyo na kuwawakilisha wenzao 681 ni Alli Kondo, Agness Machalila, Sanura Abeid, Sultan Ally, Mussa Hassan, Godwin Cuthbert na Rene Duma.

Akitoa uamuzi wa kubomolewa au kutokubomolewa kwa nyumba hizo jana saa nane mchana badala ya muda uliotarajiwa wa saa tano asubuhi, Jaji Kente alisema licha ya kuibuka hoja mbalimbali katika usikilizwaji wa awali wa shauri hilo, baadhi hazikuwa za msingi.

Alisema hoja kubwa ambayo inasubiriwa na watu ni ombi la kuzuia ubomoaji wa nyumba 681 ambao umewakilishwa na watu wanane, huku swali kubwa ni kwamba mahakama itaweza kutoa zuio la ubomoaji au la?

Jaji Kente alisema kuwa suala hilo limekuwa na ugumu kutokana na ukubwa wake, lakini bado anayo ya kusema, akisisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa na serikali zina nia njema, pia anakubaliana na kushawishika kwamba hatua zote zinafuata sheria.

Alisema kwa kuwa mchakato huo umekuwa na athari kubwa kwa wanaobomolewa, basi kuingilia kati kwa mahakama ni muhimu kwa sababu inawalinda watu hao.

“Sina ushahidi wa serikali wala walalamikaji kutokana na kukosa ushahidi wa kina kwa kuwa kesi haijaanza kusikilizwa, pia hata upande wa walalamikaji haujaleta majina yote,” alisema.
Licha ya hayo, Jaji Kente alisema ni vema ifikie wakati watu wakubaliane kwamba katika shauri hilo kuna watu walioguswa na hatua hizo za serikali.

“Kutokana na hayo, mahakama imesitisha kubomolewa nyumba za waombaji hao hadi hapo shauri la msingi lililofunguliwa kupinga ubomolewaji huo litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi,” alisema.

Hata hivyo, Jaji Kente alisema ili kuondoa shaka dhidi ya zuio hilo, serikali inaweza kuendelea na mchakato wa kuweka alama na kuvunja nyumba ambazo hazitambuliki mahakamani.

“Zuio hili linawahusu wale waombaji 681 waliofikisha maombi yao mahakamani na si vinginevyo. Kwa wale wasiohusika serikali inaweza kuendelea na mchakato wake kama kawaida,” alisema.
Hata hivyo, Jaji Kente aliwataka baadhi ya waombaji hao 681 kuhakikisha wanawasilisha orodha ya majina na anuani zao kwa kuwa awali yalikuwa ya watu wanane tu.

Baada ya kusema hayo, Jaji Kente alisema kuwa licha ya kutolewa kwa zuio hilo lakini kuna kesi ya msingi ambayo itaendelea kusikilizwa Januari 11, mwaka huu.

Wakili wa Nemc, Manchare Heche, alisema licha ya kutolewa kwa uamuzi huo, mchakato huo utaendelea kama ilivyopangwa ili kuhakikisha taratibu zinafuatwa.

Alisema kuwa kutokana na uamuzi huo na hadi kesi hiyo itakapoisha ni vema wananchi hao wazidi kujiweka katika hali ya maandalizi ya kuhama kabla ya kubomolewa.

“Huu mchakato unawalinda wao, ndiyo maana tunawaondoa mabondeni, lakini tutaendelea kubomoa zile nyumba zote ambazo hazikuhusika katika ufunguaji wa kesi hii kama mahakama ilivyosema,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali inasisitiza kwamba watu wa mabondeni waondoke kwa hiari yao katika maeneo hayo, licha ya kuwa kesi inaendelea.

Nje ya mahakama hiyo iliyopo maeneo ya Sokoine idadi kubwa ya wananchi ilijitokeza kwa ajili ya kushuhudia uamuzi wa kesi hiyo.

Mamia ya watu walianza kujikusanya kwa makundi kuanzia saa mbili asubuhi, ambapo wengine walikaa pembezoni mwa barabara na kusababisha magari kupita kwa shida.

Wakati idadi hiyo ikijitokeza kwa ajili ya kusikia uamuzi huo uliotarajiwa kutolewa saa tano asubuhi, lakini baadaye uliahirishwa hadi saa nane na Jeshi la Polisi liliongeza ulinzi katika maeneo hayo.

Ilipotimu saa tano asubuhi idadi kubwa ya wananchi walikuwa na shauku ya kujua nini kinaendelea, lakini walikatishwa tamaa baada ya Mbunge Mtulia kuwatangazia muda wa kesi hiyo kutolewa uamuzi umesogezwa mbele.

Kutokana na kauli hiyo, baadhi ya wananchi walisikika wakiwahamasisha wenzao kwamba hakuna kuondoka eneo hilo hadi wajue hatima yao, ikiwezekana wakanunue vyakula walie hapo hapo.

“Hakuna kuondoka mtu hapo, nunua muhogo hapo kuleni hapa hadi kieleweka,” alisikika mmoja wa wananchi hao akisema.

Wakati wananchi hao wakihamasishana, Jeshi la Polisi liliwataka wawe watulivu ikiwezekana kuondoka eneo hilo na kurudi baadaye.

Mara baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, wananchi walisikika wakishangilia kwa mbwembwe huku wakimpongeza mbunge huyo kwa kazi nzito aliyoifanya.

Taarifa: Waziri Simbachawene amteua Lwakatare "kushika usukani" DART

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS

TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA - TAMISEMI

TAARIFA KWA UMMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb) kwa Mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 2(2) cha Amri ya kuanzisha Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), (The Executive Agencies) (The Dar Rapid Transit Agency) (Establishment) Order ) Tangazo la Serikali namba 120 la 2007, amemteua Mhandisi Ronald Lwakatare kuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) kuanzia tarehe 04/01/2016.

Uteuzi huo unafuatia kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi kwa aliyekuwa Mtendaji Mkuu Bibi Asteria L. Mlambo tarehe 23/12/2015. Kabla ya uteuzi huu, Mhandisi Ronald Lwakatare alikuwa Naibu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (Road Fund Board) akishughulikia Ufuatiliaji na Tathmini. Mhandisi Lwakatare anatakiwa kuripoti na kuanza kazi mara moja.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Januari 05, 2016

NW amsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Ilemela

NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, Suleiman Jafo, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, John Wanga kutokana matumizi mabaya ya madaraka.

Waziri Jafo amefikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa ufujaji wa fedha za ujenzi wa uzio wa halmashauli hiyo ulioghalimu Sh. 347 milioni pamoja na kukaidi kuhamia kwenye nyumba ya Serikali ya Sh. 200 milioni.

Naibu huyo wa Tamisemi alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, ambako amesema mkurugenzi huyo ameshindwa kuhamia katika nyumba hiyo ambayo inakadiliwa kughalimu Sh. 200 milioni na kusababisha Serikali kuendelea kulipia nyumba anayoishi.

Amesema kuwa licha ya Serikali kutoa agizo mkurugenzi huyo kuhamia katika nyumba hiyo lakini yeye aliendelea kupangishia nyumba nzima inayolipiwa Sh. 2 milioni kwa mwezi licha ya kukamilika kwa nyumba iliyojengwa.

Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe CCM amesema kuwa katika manispaa hiyo kuna matatizo mengi na kwamba itatumwa kikosi cha uchunguzi kutoka Tamisemi ili kufanya uchunguzi namna ambavyo fedha za ujenzi wa uzio zilivyotumika ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa watakaobainika kuhusika na suala hilo.

“Huu ukuta (uzio) hauwezi kughalimu fedha zote hizo, nyie hata kwa madai yenu mnayosema mlifanya haraka kwa sababu ya uchaguzi sio kweli hamtaweza kushawishi kwa hilo.

“Watanzania wana shida, dawa hospitalini hakuna, wakina mama wanajifungulia chini halafu, milioni 200 imekaa tu haina shughuli yeyote ile, mkurugenzi unapaswa kupisha uchunguzi kufanyika kwanza,” amesema Jafo.

Hata hivyo amesema kuwa ujenzi wa nyumba hiyo ulianza tangu mwaka 2013 lakini mpaka sasa mkurugenzi huyo amekataa kwenda kuishi kwa sababu ya kuwa chini ya kiwango na kwamba ipo katika maeneo hatarishi.

Amesema licha ya uongozi wa manispaa hiyo kujipangia kiwango cha Sh. 2 milioni kwa mwezi,kiwango hicho kipo juu ya kiwango cha serikali cha laki nane.

Kwa upande wake mkurugenzi, Wanga katika kujitetea amesema sababu zilizosababisha kushindwa kuhamia katika nyumba hiyo ni kutokana na kuwa katika eneo hatarishi ikilinganishwa na nafasi yake ya ukurugenzi.

“Waziri (Naibu Waziri Tamisemi) tunafanya kazi kubwa za wananchi na kazi zetu mnazifahamu tunafanya watu wengine hawapendi tunachokifanya, sasa nikihamia katika nyumba ile na ukilinganisha na eneo ilipo ni hatari,” amesema Wanga.

NW afuta kibali cha kazi cha mgeni:; Aviadhibu viwanda vya Lodhia na Sunflag; Aagiza wafanyakazi walipwe KCC


NAIBU Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde amevitoza faini ya zaidi ya Sh milioni 60 viwanda viwili vya Lodhia Plastic Industries Limited na Sunflag (T) Ltd kwa kukiuka taratibu za kazi na kudharau mamlaka ya usalama mahali pa kazi (OSHA).

Mavunde alitoa adhabu hiyo jana jijini hapa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye viwanda hivyo huku akiongozana na wakuu wa idara ya kazi, idara ya uhamiaji na viongozi kutoka OSHA.

Awali alipokuwa katika kiwanda cha Sunflag, alizungumza na baadhi ya wafanyakazi na kugundua kuwa baadhi yao hawana mikataba ya ajira na wamefanya kazi zaidi ya mwaka mmoja lakini pia hawana vifaa vya kutosha vya kuzuia pamba kuingia mwilini.

Pia aliagiza menejimenti ya kiwanda hicho, kuhakikisha inalipa mishahara ya wafanyakazi kwa kima cha Serikali na si kuwalipa Sh 4,424 kwa siku. Aidha akiwa kiwandani hapo aligundua kuwa kuna wafanyakazi raia wa kigeni 41 wanaofanya kazi katika idara mbalimbali zinazopaswa kusimamiwa na raia wa Tanzania.

Akiwa katika kiwanda cha Lodhia, Mavunde alifuta kibali cha mmoja wa wageni kutoka nje ya nchi kutokana na kukiuka kibali cha kufanyakazi na kumwagiza Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Raju Sighn kupeleka vibali 38 vya raia wa kigeni ili vikaguliwe.

Kutokana na kasoro hizo Mavunde alitoza faini ya jumla ya Sh milioni 22.9 kwa kiwanda cha Sunflag na kiwanda cha Lodhia Plastic kilitozwa Sh milioni 10 kutokana na kukiuka masharti ya uendeshaji viwanda na kutoa siku 14 faini hiyo iwe imelipwa.

“Ndani ya siku saba muwe mmepeleka taarifa OSHA na hivi vibali vya wageni kutoka nje ya nchi kwa ofisi za kazi jijini Arusha. Maana mnasema mna vibali lakini nilivyoviona havijaniridhisha, pelekeni ili waone na ikithibitika mmekidhi viwango mtapunguziwa adhabu, ila heshimuni sheria za nchi,” alisisitiza.

Agizo la RC kwa wazazi, walezi: "Hata kama hana sare ya shule, mvishe nguo zake za nyumbani aende shule"

(picha: humanium.org)
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Magalulla Said Magalulla amewataka wazazi na walezi mkoani humo kuhakikisha watoto wao wenye sifa za kuanza masomo wanakwenda shule mara tu zitakapofunguliwa hata kama hawana sare.

Magalulla alisema kuwa hakuna visingizio tena vya watoto kushindwa kuhudhuria masomo kwa madai wazazi hawana uwezo kwa sababu tayari Rais John Magufuli ametangaza elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi sekondari.

“Mahitaji mengine mtoto atayapata akiwa tayari shuleni lakini sio mzazi au mlezi asubiri mpaka amtimizie mahitaji yote. Wazazi kwanza wapelekeni watoto wote waliofaulu kuanza kidato cha kwanza pia walioandikishwa kuanza darasa la kwanza,” alisema. “Hata kama hana sare ya shule mvishe nguo zake za nyumbani aende shule (na kumtafutia taratibu). Sio haki hata kidogo kumkataza au kumzuia mtoto kwenda shule kwa sababu tu hana sare kwani hilo sio kosa la mtoto,” alisisitiza Magalulla.

Aliwakumbusha wazazi na walezi kutambua kuwa kazi ya mtoto ni kusoma tu ambapo mzazi kazi yake ya msingi ni kumpelekea mtoto wake shule na kuhakikisha anahudhuria masomo na kumpa mahitaji mengine ya lazima.

Mkuu huyo wa mkoa pia amewaagiza maofisa elimu kuhakikisha watoto wanapokewa shuleni na kama kuna masharti hayajatimizwa basi wabaki wakiwadai wazazi kuyatimiza huku watoto wakiwa tayari wanaendelea na masomo.

“Pia ni wajibu wa wazazi na walezi ambao watoto wao wako shuleni wanasoma kushirikiana na walimu wao kuhakikisha kuwa kweli wanakwenda shuleni, maana baadhi ya watoto wanavaa sare lakini hawafiki shuleni, tuhakikishe watoto wana kwenda shule,” alisema.

Magalulla alisema ni kosa la kisheria kwa mzazi au mlezi kusababisha mtoto asiende shule au kumshawishi kukatiza masomo ili aweze kujihusisha na ajira.

Alionya kuwa mtu huyo akikamatwa atashtakiwa kwa sababu sheria inataka mtoto akianza shule lazima amalize. Kwa mujibu wa matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mkoa wa Rukwa mwaka jana, mkoa huo umefanya vibaya kwa kushika nafasi ya tatu kitaifa kutoka mwisho.

Halmashauri ya wilaya ya Kalambo ilishika nafasi ya 165 kati ya halmashauri 166 nchini.

Baadhi ya picha za ziara ya Waziri Mkuu, Majaliwa mkoani Ruvuma


Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akikagua mahindi yaliyohifadhiwa nje ya majengo ya maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA mjini Songea akiwa katika ziara ya siku tatu mkoani Ruvuma Januari 4, 2016. 

Wimbi la uvamizi wa mashamba ya viongozi: Wananchi wajigawia ya Yona, Sumaye

Zaidi ya wakazi 50 wa Kijiji cha Kerege wilayani Bagamoyo wamevamia shamba la waziri zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona lililopo jirani na kijiji lakini hawakutimiza azma yao ya kugawana baada ya kukurupushwa na polisi.

Mmoja wa wanakijiji hao, Issa Hemed alisema wananchi walifika kwenye shamba hilo jana saa 12:00 asubuhi na kuanza kupimiana maeneo, huku kila mtu akiweka alama za kiwanja anachotaka.

Hemed alisema shamba hilo lililoko mkoani Pwani halijaendelezwa kwa muda mrefu na limekuwa msitu ambao alidai hutumiwa na majambazi kama sehemu ya maficho.

Alisema wanakijiji hao waliunda kamati kwa ajili ya kuchukua eneo hilo na kuwagawia kwa sababu haliendelezwi.

Hata hivyo, alisema wakati wakiendelea kugawana jana saa 5:00 asubuhi, polisi walifika na wananchi kulazimika kukimbia, huku baadhi yao wakikamatwa.

Alisema yeye ni mpangaji ambaye hana ardhi ya kujenga hata chumba kimoja, lakini sasa anashukuru kupata eneo.

Alipoulizwa kama haoni ni kosa kuchukua ardhi ya mtu mwingine, Hemed alisema haiwezekani mtu mmoja akamiliki ekari nyingi bila kuziendeleza, huku wengine wakikosa eneo dogo la kulima bustani.

Mkazi mwingine wa Kerege, Naomi Bandawe alisema Serikali inapaswa kuwagawia wananchi mashamba hayo kwa kuwa watu wengi walihodhi, lakini wameshindwa kuyaendeleza.

“Kuna faida gani ya kuwa na misitu isiyoendelezwa wakati wananchi wengi hawana ardhi,” alisema.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Pwani, Jaffer Mohamed alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema watu 10 wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kosa la uvamizi.

Alisema kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya uvamizi wa mashamba na kwamba kuna watu wengi waliokamatwa na kesi zao zinaendelea mahakamani.

“Baada ya polisi kufika eneo hilo, baadhi ya wananchi walikimbia, lakini wengine 10 walikamatwa na watafikishwa mahakamani kwa kuvamia mashamba ya watu,” alisema.

Alisema hata siku ya Uhuru wakati wananchi wanafanya usafi, wengine walikuwa wanagawana mashamba ya watu jirani na eneo hilo na walikamatwa na polisi.

“Tabia hii imeota mizizi katika Wilaya ya Bagamoyo ya watu kujichukulia sheria mkononi kwa kugawana mashamba ya watu wengine,” Kamanda Mohamed.

Wananchi zaidi ya 100, wakiwemo waliobomolewa maeneo ya mabondeni jijini Dar es Salaam, wamevamia shamba la Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye lenye ukubwa wa heka 33, lililopo Mji Mpya eneo la Mabwepande na kujikatia viwanja.

Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tano kati ya mwaka 1995 hadi 2005, amekiri wananchi kuvamia shamba hilo lakini alisema hana wasiwasi kwasababu ana hati za umiliki.

Aidha alisema atafuata mkondo wa sheria kuhakikisha wavamizi hao wanaondoka kwenye shamba lake.

Juzi Nipashe ilishuhudia wananchi kadhaa wakiendelea kujenga nyumba za miti na wengine za matofali baada ya kujigawia kila mmoja eneo lake kwenye shamba hilo.

Musa Juma, aliyekutwa kwenye shamba hilo akijenga nyumba, alisema yeye ni miongoni mwa waathirika wa bomoa bomoa iliyofanyika Kinondoni Mkwajuni na kwamba amefika hapo baada ya mwenzao aliyemtaja kwa jina moja la Ema kuwaeleza kuwa kuna pori la Sumaye alilolitelekeza.

“Mwenzetu Ema alikuja kule bondeni tulikobomolewa na kutupa habari hiyo hivyo watu kama 100 tukaamua kuja na tukawakuta wengine tuliliona shamba hili likiwa ni pori kubwa ndipo tukaanza kujigawia vipande vipande,” alisema.

“Tumefanya kazi kubwa ya kulifyeka mpaka unaliona lipo katika hali hii, kazi haikuwa ndogo dada yangu, tumekutana na nyoka wakubwa, ukishuka kule bondeni kwenye kingo za shamba utajionea mwenyewe jinsi pori hili lilivyokuwa.”

Juma alisema walivamia shamba hilo mwezi Oktoba mwaka jana, na wengine walikuja baadaye baada ya kupata taarifa kuwa kuna shamba la bure ambalo limetelekezwa akiongeza kuwa wako pia watumishi wa serikali waliovamia shamba hilo.

“Aliwahi kuja mwanamke mmoja ambaye hatumfahamu akidai kuwa yeye ni mke wa kiongozi huyo na kutueleza kuwa tunapaswa kuondoka eneo hili eti ni mali yao lakini juzi kaja mwenyewe Sumaye; akatusalimia na kuondoka bila kusema lolote,” alisema.

“Mwamamke yule alikuja na watu wengine akiwemo mtu ambaye alikuwa akipiga picha na baadaye aliondoka hadi Alhamisi ya wiki hii walivyokuja wote na Sumaye mwenyewe ingawa hakusema lolote mpaka anaondoka hapa.

“Sumaye alikuja kwa sababu Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, aliitisha mkutano na wananchi wa hapa, lakini tukiwa tumekusanyika tukimsubiria Makonda ghafla alifika Sumaye, ambaye hakushuka kwenye gari lake, alitusalimia kwa kutunyooshea mikono na kuondoka kwasababu Makonda hakuja siku hiyo.”

Alipoulizwa sababu za kuvamia shamba hilo, alisema walimsikia Rais John Magufuli kwenye kampeni akisema kuwa mashamba yote ambayo hayajaendelezwa yarudishwe serikalini na wapewe watu wenye uwezo wa kuyaendeleza.

Juma alisema wamejigawia shamba hilo na sasa wanasubiri serikali ije kuidhinisha kwa kuwamilikisha wao.

“Mtu anahodhi shamba kubwa kama hili halafu halijapimwa, tumetafuta alama za mipaka hakuna, wakati mashamba yote yaliyolizunguka shamba hili yamepimwa,” alisema.

Sumaye alisema anamiliki shamba hilo kihalali na ana hati zote na kwamba upo utaratibu wa kuchukua mashamba yaliyotelekezwa lakini sio huo walioutumia wananchi hao.

“Shamba hatujalitelekeza kama wanavyodai hao wananchi, tuna hati na ni letu kihalali, wanasema halina alama za mipaka je, waulize hati nilipataje? Shamba lina alama labda kama wamezing’oa kwa sababu ya jeuri.”

Sumaye alisema juhudi za kuhakikisha shamba hilo linarudishwa mikononi mwake zimeanza kufanyika na mamlaka husika na kusisitiza kuwa hatatumia nguvu kuwaondoa zaidi ya kufuata sheria.

Kuhusu kuonekana eneo hilo siku ya Alhamisi, Sumaye alisema alienda huko kwa sababu Makonda aliitisha mkutano na wananchi ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo lakini hakufika baada ya kupata udhuru.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Jastine Chiganga, alisema alipigiwa simu na Makonda akimweleza kuhusu mkutano huo lakini hakuweka bayana sababu za kuuitisha, ingawa aliuahirisha baada ya kupata dharura.

Makonda alilipoulizwa kuhusu lengo la mkutano aliouitisha na baadaye kuuairisha, alisema lilitokana na ofisi yake kupokea malalamiko ya uvamizi wa mashamba unaofanywa na wananchi eneo hilo.

Alisema baada ya kupokea malalamiko hayo aliomba kukutana na viongozi wa mitaa husika, wananchi, watu wa ardhi na wamiliki wa mashamba hayo ili kujua ukweli kuhusu mgogoro huo.

“Hilo shamba linalodaiwa kuwa ni la Sumaye, sijawahi kupokea malalamiko kutoka kwake dhidi ya uvamizi huo ila niliwahi kupigiwa simu na mmoja wa Makamanda wa Polisi Mkoa ambaye alinieleza kuhusu uvamizi huo,” alisema.

Aidha, Makonda alisema mbali ya shamba hilo la Sumaye yapo mengine likiwemo la Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), marehemu Daudi Ballali ambalo nalo limevamiwa.

Alisema mkutano wake aliouitisha ulilenga kwenda kupata taarifa kamili ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Makonda alitoa wito kwa watu wanaodai ni wamiliki halali wa mashamba yaliyovamiwa wajitokeze katika mkutano atakaouitisha wiki ijayo eneo hilo ili ufumbuzi uweze kupatikana.

MUHAS call for application: Masters, PhD, Post Doc Programmes under SIDA Support 2015/2020

The Swedish International Development Agency (SIDA) has provided financial support to Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS) for the period 2015 to 2020 to support the training of 37 PhDs, 23 Masters and 6 Post-doctoral researchers (Post-docs).