Mbele na nyuma magazetini leo Jumanne, Januari 12 "Mapinduzi Day", 2016


Salam za CHADEMA-USA kwa msiba wa Leticia Nyerere

SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA ALIYEWAHI KUWA MBUNGE WA VITI MAALUM CHADEMA, MHESHIMIWA LETICIA NYERERE

Napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya Viongozi, wanachama na wapenzi wa Chadema wa Tawi la Washington DC, Marekani, kutuma salamu za pole kwa familia ya aliyekuwa Mbunge wa viti maalum Chadema Kupitia Jimbo la Kwimba Mheshimiwa Leticia Nyerere kilichotokea baada ya kuugua kwa muda mfupi hapa Maryland, Marekani, siku ya Jumapili Tarehe 10 Januari 2016. 

Kwa hakika tumepokea taarifa ya msiba wa mheshimiwa Leticia Nyerere kwa mshtuko mkubwa kutokana na kumbukumbu ya mchango mkubwa aliyotoa kwenye kufungua Tawi letu la Chadema hapa Washington DC, Marekani. Pia kwa mchango wake aliyotoa akiwa kama mbunge wa Viti Maalum kupitia Chadema. Kwa kweli bado tulikuwa tunahitaji sana mchango wake lakini mpango wa mungu hauna makosa.

Mungu ailaze roho ya Marehemu Leticia Nyerere mahali pema peponi, Amin.
Mwenyekiti wa chadema Washington DC, Marekani
Kalley Pandukizi

Kauli ya Serikali ya Tanzania kuhusu raia wa kigeni nchini


Waziri Lukuvi apiga marufuku Halmashauri kuchukua mashamba ya wananchi bila kuwalipa


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi ameziagiza Halmashauri zote nchini kuacha tabia ya kuchukua mashamba ya wananchi bila kuwalipa fidia na kisha kupima viwanja na kuviuza kwa bei kubwa, huku wanunuzi wa viwanja hivyo majina yakijirudia nchi nzima, kwa lengo la kufanya biashara ya ardhi.
WM mstaafu Sumaye 'ashangazwa' na Rais Magufuli kumjulia hali hospitalini

Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akimpa pole Waziri Mkuu Mstaafu Mhe Freredick Sumaye
alipokwenda kumjulia hali katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam leo Jumatatu Januari 11, 2016Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiongea na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe Freredick Sumaye na Mama Esther Sumaye alipokwenda kumjulia hali katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam leo Jumatatu Januari 11, 2016


Taarifa ya habari ChannelTEN, Jumatatu, 10.01.2016
Maalim Seif azungumza kuhusu hali ya kisiasa nchini Zanzibar

Maalim Seif Sharif Hamad
Maalim Seif Sharif Hamad
  • video imepachikwa hapo chini
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ametoa msimamo wake na chama chake kufuatia mazungumzo ya siri ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa unaotokana na tangazo la kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.

Akizungumza leo na waandishi wa habari katika hotel ya kitalii ya Serena jijini Dar es Salaam, Maalim Seif amesisitiza kuwa hoja ya kurudia uchaguzi wa Zanzibar kama inavyoelezwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), haina msingi, haikubaliki na sio halali kikatiba.

“Hoja ya kurudia uchaguzi haina msingi, haina uhalali, ni hoja ambayo inaweza kuzaa fujo na vurugu na inaweza kuleta mzozo mkubwa wa kikatiba wa kisheria. Sidhani kama tunataka kuwapeleka huko watanzania,” alisema Maalim Seif.

Makamu huyo wa kwanza wa rais wa Zanzibar ameeleza kuwa tayari wameshafanya vikao nane vilivyowashirikisha wagombea urais pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar lakini hawakukubaliana kurudia uchaguzi kama baadhi ya viongozi wa CCM walivyoeleza.

Aidha, Maalim Seif amekanusha kilichoelezwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd baada ya kukutana na Rais John Magufuli, kuwa rais alisema warudie Zanzibar kujiandaa na marudio ya uchaguzi kwani rais hakusema hivyo alipokutana naye.

Maalim Seif amesema kuwa ana imani kubwa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika kuleta maridhiano na ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar kutokana na mazungumzo aliyofanya naye hivi karibuni katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa endapo uchaguzi mkuu utatakiwa kurudiwa, zipo changamoto nyingi za kikatiba ambazo zitakwamisha zoezi hilo hivyo uchaguzi huo hautawezekana.

Ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupitishwa kwa fedha za kugharamia uchaguzi na baraza la wawakilishi ambalo hivi sasa halipo kwa kuwa limefikia ukomo wake.

Mbali na hilo, Maalim Seif alieleza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu kwa kutoa tamko lisilo halali la kufuta uchaguzi huo huku akifahamu dhahiri kuwa hana nguvu hiyo kikatiba.

Ameitaka ZEC iongozwe na makamu mwenyekiti wake kwa mujibu wa katiba pamoja na wajumbe wengine kukamilisha utaratibu wa kuhakiki matokeo ya uchaguzi na kumtangaza mshindi.

Maalim Seif ameeleza kuwa anafahamu dhahiri kuwa kuna mpango wa kutangaza kwa nguvu marudio ya uchaguzi Februari 28 mwaka huu, lakini yeye pamoja na chama chake hawatakubaliMahakama yafuta kesi ya Kiwia (CHADEMA) ya kupinga matokeo ya Ubunge Ilemela

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza jana ilifuta rasmi Kesi ya madai ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Angelina Mabula (CCM) baada ya mlalamikaji aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya Cha Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Haighness Kiwia kushindwa kulipi kiasi cha Sh 10 milioni ili kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Kesi hiyo hiyo Namba 2 ya mwaka 2015 ilifunguliwa na mgombea Kiwia ambaye alikuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa miaka mitano kabla ya kushindwa na Mabula katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka 2015, ambapo awali kesi hiyo ilifunguliwa Novemba 25 mwaka 2015 na Wakili wa kujite Agrey Labani ambaye alikuwa akimtetea Kiwia.

Akitoa uamuzi wa kufutilia mbali kesi hiyo, Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Eugenia Rujwahuka, alieleza mahakama hiyo imekubaliana na Hati iliyowasilishwa na Wakili wa kujitegemea Paul Kipeja kutoka Kampuni ya Goldstone Chamber akiwa upande wa mlalamikaji kuwa mteja wake Kiwia ameshindwa kumudu kulipia gharama za kufunguliwa kesi hiyo kiasi cha Sh 10 milioni ambazo zilitakiwa kulipwa kwanza kabla kesi ya msingi kusikilizwa.

Rujwahuka alieleza kwamba kutokana na mlalamikaji kushindwa kulipia gharama za ufunguaji wa kesi ambapo Mahakama hiyo ilimtaka kulipa kiasi cha Sh 10 milioni ikiwa ni kutokana na kushitakiwa Mbunge Mabula na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao kwa pamoja walitajwa katika madai ya kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu jimbo la Ilemela.

“Mahakama haina pingamizi na uamuzi uliofikiwa na mlalamikaji wa kuliondoa shauri hili, leo hii asubuhi upande uliokuwa ikilalamika uliwasilisha Hati ya kuomba kuifuta kesi hii lakini pia mlalamikaji Kiwia alishindwa kulipia gharama ya ufunguaji wa kesi kwa watu aliotajwa kwenye madai yake ndani ya muda pamoja na kuomba kupunguziwa na Mahakama gharama hiyo ambapo Mahakama ilimtaka kulipa,”alieleza.

Rujwahuka alimhoji Wakili wa kujitegemea, Mutabaazi Lugaziya, kutoka Kampuni ya M.J. Lugaziya aliyekuwa akimtetea Mbunge Mabula kama anakubaliana na Hati hiyo ya kufuta kesi ambaye alikubaliana na hatua hiyo na kudai hana kupingamizi, lakini akiomba Mahakama hiyo kukubali ombi la mteja wake Mabula kufungua kesi ya madai ya kwa Kiwia ambazo walitumia wakati wa kufatilia kesi hiyo.

Wakili Kipeja alisema kwamba kutokana na mteja wake kushindwa kumudu gharama za kufungua kesi naye amekubaliana na uamuzi huo kwa madai kuwa Kiwia alimuomba kupeleka Hati hiyo ili kutoendelea na kesi hiyo ngazi yoyote ile ambapo uamuzi huo anakubaliana nao kwa asilimia 100 na anaishukuru Mahakama hiyo kulikubali ombi hilo na kutoa uamuzi.

Wakili wa Lugaziya aliwashukuru walalamikaji kwa kuifuta kesi hiyo mapema ili kuwezesha mteja wake Mbunge Mabula ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi apate muda wa kuwatumikia wapiga kura wake na majukumu mengine ya kiserikali kwa kuwa ingweza kuchukua muda mrefu, lakini pia haki ya imetendeka kama tulivyokuwa tukisubiria kwa kuwa tuliamini mteja wetu alishinda kihalali kwenye uchaguzi huo wa Oktoba 25 mwaka 2015 na hakuna ubishi.
  • Taarifa ya PETER FABIAN, MWANZA via GSengo blog

Taarifa ya Bunge ya uteuzi wa Wabunge kwenye Kamati za Kudumu

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 

BUNGE LA TANZANIA

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UTEUZI WA WABUNGE KWENYE KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE.

Katibu wa Bunge anatoa taarifa kwa umma kwamba:

(a) Kwa mujibu wa Kanuni ya 116 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano amepewa mamlaka ya kuteua Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa namna ambayo itawezesha kila Mbunge kuwekwa kwenye Kamati mojawapo. Katika kufanya uteuzi huo, Spika huzingatia vigezo mbalimbali vilivyoainishwa katika Kanuni ya 116 (5);

(b) Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mhe. Job Yustino Ndugai (MB), ametekeleza mamlaka yake ya uteuzi kwa mujibu wa Kanuni tajwa hapo juu, kwa kuwateua kwanza Wabunge Kumi na Tano (15) kuwa Wajumbe wa Kamati ya Kanuni za Bunge. Kamati hiyo imeundwa na kutangazwa kabla ya Kamati zingine ili ifanye marekebisho ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge kuhusu majukumu ya Kamati zingine za Bunge kwa kuyashabihisha na majukumu ya Serikali kwa kuzingatia Muundo wa Baraza la Mawaziri lililopo sasa. Lengo kuu ni kuleta urahisi, ufanisi na tija kwa Bunge katika kuisimamia na kuishauri Serikali;

(c) Kwa msingi huo, Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ambayo Spika ndiye Mwenyekiti wake na Naibu Spika ni Makamu Mwenyekiti, Kiongozi wa Upinzani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao ni Wajumbe kwa nyadhifa zao itakutana katika Ofisi ya Bunge, Dar es Salaam siku ya Ijumaa tarehe 15 Januari, 2016 saa tano kamili asubuhi katika Ukumbi wa Spika. Wajumbe wengine ni: -
(i) Mhe. Makame Kassim Makame, MB. - Jimbo la Mwera;

(ii) Mhe. Tundu Antipas Mughwai Lissu, MB. - Jimbo la Singida Mashariki;

(iii) Mhe. Jasson Samson Rweikiza, MB. - Jimbo la Bukoba Vijijini;

(iv) Mhe. Ally Saleh Ally, MB. - Jimbo la Malindi;

(v) Mhe. Magdalena Hamis Sakaya, MB. - Jimbo la Kaliua;

(vi) Mhe. Salome Wycliff Makamba, MB. - Viti Maalum;

(vii) Mhe. Dkt. Jasmine Tiisekwa Bunga, MB. - Viti Maalum;

(viii) Mhe. Zainab Athman Katimba, MB. - Viti Maalum;

(ix) Mhe. Balozi Adadi Mohamed Rajab, MB. - Jimbo la Muheza;

(x)Mhe. Dkt. Charles John Tizeba, MB. - Jimbo la Buchosa; na

(xi) Mhe. Kangi Alphaxard Lugola, MB. - Jimbo la Mwibara.

(d) Spika atakamilisha uteuzi wa Wajumbe katika Kamati zingine za Bunge kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Pili wa Bunge tarehe 26 Januari, 2016, Mjini Dodoma ili kutoa fursa kwa Kamati zote kuchagua Viongozi wake na kuandaa Mpango Kazi kwa mwaka 2016/17; na

(e) Wabunge wote wanatangaziwa kuwa wawe wamefika Dodoma tarehe 20 Januari, 2016 tayari kwa kuanza kwa Kamati za Bunge na Mkutano wa Bunge, isipokuwa Kamati ya Wabunge (Caucus) wote wa Chama cha Mapinduzi wanatakiwa kuwa Mjini Dodoma tarehe 17 Januari, 2016 kwa Mkutano wao.

Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano,
Ofisi ya Bunge,
S. L. P. 9133,
DAR ES SALAAM.
11 Januari, 2016.

Picha za mafuriko ya mvua mkoani Mwanza

Kuna video mwishoni mwa picha zifuatazo...

Rais Magufuli ampa pole mama Maria Nyerere kwa msiba wa mkwewe Mhe. Leticia Nyerere

Leticia Nyerere
Leticia Nyerere
Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akimfariji Mama Maria Nyerere, Mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na wanafamilia alipokwenda nyumbani kwake Msasani kumfariji kufuatia kifo cha mkwe wake Marehemu Leticia Nyerere huko Maryland, Marekani.


Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akimfariji Mama Maria Nyerere, Mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na wanafamilia alipokwenda nyumbani kwake Msasani kumfariji kufuatia kifo cha mkwe wake Marehemu Leticia Nyerere huko Maryland, Marekani.

Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiagana na Mama Maria Nyerere, Mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,na wanafamilia alipokwenda nyumbani kwake Msasani kumfariji kufuatia kifo cha mkwe wake Marehemu Leticia Nyerere huko Maryland, Marekani.

Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiagana na Mama Maria Nyerere, Mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na wanafamilia alipokwenda nyumbani kwake Msasani kumfariji kufuatia kifo cha mkwe wake Marehemu Leticia Nyerere huko Maryland, Marekani.

Music video cover: Beka Ibrozama ‘Hello’ ya Adele


Muimbaji mahiri wa nchini Tanzania, Beka Ibrozama ameachia video ya cover ya wimbo maarufu wa msanii wa Uingereza, Adele ‘Hello’ uliopo kwenye albamu yake 25 iliyotoka November 20 mwaka jana.

Hello umekuwa wimbo maarufu zaidi kutoka mwaka 2015 huku hadi sasa video yake ikiwa imeangaliwa kwa zaidi ya mara milioni 940 kwenye mtandao wa Youtube huku albamu yake ‘25’ ikiuza nakala milioni 7.4 ndani ya sita tu nchini Marekani.

Hello umekuwa wimbo uliofanyiwa cover nyingi zaidi hadi sasa na wasanii kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo wakongwe kama vile Joe Thomas, Celine Dion, Demi Lovato na wengine.

Beka anadai aliamua kuwa mmoja wa waimbaji waliofanya cover za wimbo huo ili kuwaonesha wapenzi wa muziki duniani uwezo mkubwa alionao kiuimbaji.

“Ni wimbo fulani mgumu sana, ni wimbo wenye sauti za juu, una melody nzuri na ili uweze kupita kwenye hizo njia ni lazima kidogo uwe unajua muziki,” anasema Beka.

Anasema pamoja Hello kuwa na sauti ngumu kuweza kuzimudu, alipata tabu katika kuweza kutamka vizuri matamshi ya Kiingereza kutokana na kuwa lugha asiyoijua kabisa.

“Ukweli uko hivyo kwamba sijui Kiingereza lakini nimeimba wimbo wa Kiingereza kwa uwezo wangu naamini nimefanya kwa uwezo mkubwa ukizingatia kuwa sijui hata nilichokuwa nakiimba, naamini ni kipaji cha ajabu sana Mungu amenipa,” anasisitiza.

“Kwahiyo watu hata wakisikia baadhi ya maneno sijayatamka kama Muingereza mwenyewe anavyoyatamka, wajue kuwe sijui hicho kitu ila nimejitahidi kwa uwezo wangu.”

Msanii huyo ambaye kwa sasa hupenda kujiita Fundi, anadai kuwa jina hilo amepewa kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kuchezea sauti kama anavyotaka na uwezo wa kuimba aina zote za muziki kwa umahiri mkubwa.

“Nina vitu vingi sana vikubwa watu hawajavigundua kutoka kwangu.”

Amesema mwaka 2016 utakuwa mwaka muhimu kwake sababu amedhamiria kuuthibitishia ulimwengu kuwa yeye ni dhahabu iliyoanguka kwenye tope na inahitaji sikio la mtu anayejua muziki kuiona, kuikota na kuiutumia vyema ili kuitangaza Tanzania kwa kipaji kikubwa alichobarikiwa na mwenyezi Mungu.

Beka alijipatia umaarufu mkubwa kwa wimbo wake ‘Natumaini Remix’ aliouandika kwa ufundi mkubwa huku akitumia kuunganisha mantiki wa wimbo huo kwa kutumia majina na nyimbo za wasanii mbalimbali.

Mwenyekiti wa CCM ampongeza Mbwana Samatta ofisini Lumumba

Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete akiingia ukumbini na Nyota wa Soka Tanzania, aliyeshinda Tuzo ya mwanasoka Bora wa Afrika kwa Wachezaji wa ndani, Mbwana Samatta, alipokutana na mchezaji huyo leo, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam, kwa ajili ya kumpongeza kufuatia kutwaa tuzo hiyo.


Taarifa ya Serikali 11.01.2016 kuhusu ugonjwa wa kipindupindu

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari leo. Kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dkt. Rufaro Chatora

Taarifa kwa umma, kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu hapa nchini ni kama ifuatavyo; Tangu ugonjwa huu uanze, jumla ya watu 13,491 wameugua Kipindupindu, na kati yao jumla ya watu 205 wameshafariki kwa ugonjwa huu.

Katika kipindi cha wiki iliyoanza tarehe 04 hadi 10 Januari 2016, kumekuwa na jumla ya wagonjwa 615 walioripotiwa nchini kote na vifo vitatu (3). Mikoa ambayo bado imeripoti kuwa na ugonjwa huu ndani ya wiki moja iliyopita ni 11 kati ya 21 iliyokuwa imeripoti ugonjwa hapa nchini. Mikoa hiyo ni pamoja na Morogoro, Arusha, Singida, Manyara, Pwani, Dodoma, Geita, Mara, Tanga, Mwanza na Simiyu. Kati ya hiyo, mikoa inayoongoza kwa kuripoti idadi kubwa ya wagonjwa wapya ndani ya wiki moja iliyopita ni pamoja na Morogoro (Manispaa ya Morogoro 87, Halmashauri ya Morogoro 66), ukifuatiwa na Arusha (Arusha Manispaa 50), Singida (Iramba 40) na Manispaa ya Dodoma (33).

Aidha, mikoa iliyokuwa na maambukizi lakini kwa muda wa wiki moja iliyopita hakukuwa na mgonjwa yoyote wa kipindupindu ni pamoja na Mbeya, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kagera, Lindi. Vile vile mkoa wa Dar es Salaam ambako ndiko ugonjwa ulianzia na kudumu kwa muda wa miezi minne (4) haujaripoti mgonjwa wa kipindupindu kuanzia tarehe 22/12/2015.

Mikoa ambayo ilikwisha kuwa na ugonjwa huo lakini hapajakuwepo na wagonjwa wowote kwa muda wa zaidi ya miezi miwili iliyopita ni pamoja na Shinyanga, Kilimanjaro na Iringa. Pia mikoa ambayo haijawahi kutoa taarifa ya ugonjwa wa kindupindu tangu mlipuko huu uanze hapa nchini ni Njombe, Ruvuma na Mtwara.

Bado Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaendelea kusisitiza kuwa, ili kudhibiti ugonjwa huo na kuokoa vifo vinavyotokana na ugonjwa huu, wananchi wanasisitizwa kunywa maji yaliyo safi na salama, kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka:-

- kabla na baada ya kula

- baada ya kutoka chooni

- baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia

- baada ya kumhudumia mgonjwa

Aidha, jamii inaaswa kutumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, maziwa na mabwawa.

Hivyo, Mamlaka za Mikoa na Halmashauri pamoja na watendaji wake kote nchini zinaagizwa kuendeleza juhudi za kuzuia kusambaa kwa mlipuko pamoja na kuchukua hatua stahiki za tahadhari kwa kusimamia utekelezaji wa yafuatayo:

*Ushirikishwaji wa viongozi ngazi mbali mbali, hasa ngazi za Halmashauri kwa kushirikisha madiwani na viongozi wa kata, vijiji, na mitaa.

*Mamlaka husika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama ikiwa ni pamoja na uwekaji wa dawa ya klorini kwenye maji na kupima usalama wa maji mara kwa mara.

*Upatikanaji wa dawa za kutibu maji (Water Guard, Aqua Tabs) katika maeneo ya mlipuko.

*Juhudi kubwa ziongezwe kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya vyoo bora kwa kila kaya.

*Uelimishwaji wa Baba na Mama Lishe, na wauzaji wengine wa vyakula kuhusu kanuni za afya.

*Kusimamia utekelezwaji wa Sheria ya Afya ya Mazingira na Sheria ndogo ndogo (By-Laws).

*Uhamasishaji wa Wananchi wanaopata ugonjwa kuwahi kutumia maji ya chumvi chumvi (ORS) na kuripoti mapema katika vituo vya huduma.

*Uboreshwaji wa vituo vya kutolea huduma za afya.

Hitimisho

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inawashukuru wadau wote wanaoshirikiana na Serikali katika harakati za kupambana na ugonjwa huu. Aidha, Wizara inaipongeza mikoa ambayo ilikuwa na ugonjwa na sasa umetoweka au kupungua kwa kiasi kikubwa na pia kuikumbusha mikoa ambayo bado haijaathirika kuchukua hatua za tahadhari za kuzuia ili isipate mgonjwa yeyote wa Kipindupindu.