SUA - Taarifa: Usajili wa Wafanyakazi katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya


Adha ya mvua ilivyoonekana Mwanza leo Januari 14, 2016


Barabara ya Nyerere

Kesi ya Kafulila: Mahakama yatupilia maombi ya wakili wa serikali

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora Chini ya Jaji Sam Rumanyika leo Januari 14, 2016 imetupilia mbali mapingamizi ya Wakili wa serikali yaliyowasilishwa na kujadiliwa Januari 11, 2015 katika mahakama hiyo.

Katika mapingamizi ya serikali Wakili wa serikali kwa niaba ya msimamizi wa uchaguzi na Mwanasheria wa serikali aliweka mapingamizi na kutaka mahakama itupilie mbali kesi ya Kafulila David kwa madai kwamba;
  1. Hati ya mashtaka haina vifungu vya sheria vinavyoipa mahakama mamlaka ya kusikiliza kesi hii
  2. Ombi la Kafulila kutangazwa mshindi halimo ndani ya uwezo Wa mahakama kwakuwa mamlaka hayo ni ya Tume ya uchaguzi
  3. Kwamba ombi la Kafulila kwamba mahakama ipitie fomu za matokeo haitambuliki kisheria.
Katika uamuzi wa MAHAKAMA, Jaji Rumanyika amesema baada ya kusikiliza na kuchambua mapingamizi na utetezi wa Wakili wa Kafulila imeamua kuwa;
  1. Hoja kwamba hati ya mashtaka haina au haijaweka sheria I nayoipa mamlaka mahakama kusikiliza na kuamua KESI hii haina msingi kwakuwa kwanza kesi ya uchaguzi sio sawa na maombi ya kawaida na zaidi sheria ya uchaguzi ya 2015, kifungu110 kimesisitiza wazi kuwa mahakama kuu ndio yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za uchaguzi na hivyo haikuwa na ulazima kutaja ukweli ulio hayana.
  2. Hoja kwamba mahakama haina uwezo wa kutangaza mshindi haina msingi kwasababu sheria ya uchaguzi ya 2015 kifungu112 kimeweka wazi mamlaka ya mahakama kuwa ni pamoja na kutangaza mshindi alochaguliwa na hivyo Kafulila Ana haki kuomba ombi hilo.
  3. Kuhusu pingamizi kuwa ombi la Kafulila la kuomba kupitiwa fomu 21B za kila kituo, MAHAKAMA imelekeza kuwa dhana ya ombi hilo inamezwa na ombi la kutangazwa mshindi hivyo halina sababu kuwepo.
Baada ya maelekezo na maelezo hayo, Mahakama haioni sababu ya kufuta kesi ya Kafulila David Kama ilivyombwa na wakili wa serikali na badala yake Kesi itaendelea Januari 28, 2015.

Wageni 20 wakamatwa Mbeya kwa makosa kadha wa kadha

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya Ndugu Asumsyo Achacha akizungumza ofisni kwekwe juu ya zoezi linaloendelea la kuwasaka wahamiaji haramu mkoani humo.

Zoezi la kuwasaka wahamiaji haramu na wageni wanaofanya kazi bila kibali limeendelea kufanikiwa mkoani Mbeya ambapo jumla ya wageni 20 wamekamatwa mkoani humo kutokana na makosa mbalimbali likiwemo la kuingia nchini kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwakwe Afisa uhamiaji Mkoa wa mbeya Ndugu Asumsyo Achacha amesema hatua hiyo imefanyika ikiwa ni kutekeleza majukumu yao ya kila siku sanjali na kutekeleza agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani Dkt Charles Kitwanga alilotoa hivi karibuni.

Aidha amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa sheria mpya ya kuratibu ajira za wageni ,Sherii Na.1 ya mwaka 2015 ambayo inawataka wageni wote walioajiliwa hapa nchini kuwa na vibali vya kazi na hati za ukaazi nchini.

Afisa uhamiaji huyo amewataja raia hao waliokamatwa katika msako huo ni pamoja wakenya watatu (3)wamalawi 14 pamoja na wakongo watatu (3).

Aidha amesema kuwa mwaka 2015 jumla ya wahamiaji haramu 478 kutoka mataifa mbalimbali walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo kufikishwa mahakamani pamoja na kufukuzwa nchini.

Amesema mbali na changamoto zilizojitokeza ikiwemo upungufu wa vitendea kazi ,fedha pamoja na rasilimali bado shughuli za uhamiaji mkoani humo ziliendelea kufanyika kama kawaida na kwa ufanisi mkubwa.

Pia Afisa Uhamiaji huyo amebainisha kuwa zoezi hilo ni endelevu hivyo ofisi yake itahakikisha kila mtu aliyevunja sheria anakamatwa hivyo ametoa wito kwa waajiri kuacha tabia ya kuwapa ajira wafanyakazi wa kigeni wasio na vibali vya kazi na ukaazi kwani msako huo utaendelea katika viwanda ,migodi mashuleni na mahotelini.

Mwisho.
  • Tumeshirikishwa taarifa hii na JamiiMoja blogu, Mbeya

Kitime: Imani za kishirikina katika tasnia ya muziki

Imani ya uchawi ni utamaduni ambao umekuweko katika jamii zote za binaadamu kwa maelfu ya miaka. Historia na maandiko ya dini mbalimbali yanatukumbusha hilo katika masumilizi mbalimbali. Kwa kawaida unaweza kudhani kuwa kadri maendeleo na elimu yanavyoongezeka, na majibu ya kisayansi yanavyopatikana kuhusu mambo mbalimbali, ndipo imani ya uchawi ingepungua na kupotea, lakini ni wazi safari bado ni ndefu kwani ukipita katika mitaa mingi utaona vibao vikiashiria imani hiyo bado iko na inawezekana inaongezeka zaidi. Matangazo ya waganga wanaoweza ‘kusafisha nyota’, ‘kuondoa majini’ , kusaidia watu kupanda vyeo kazini, kupasi mitihani na kadhalika, sasa yamekuwa kitu cha kawaida mitaani.

Tasnia ya muziki kwa kuwa ni sehemu ya jamii,haijakwepa kuguswa na tatizo hilo. Uzoefu nilionao kwa kuwa katika tasnia ya muziki kwa zaidi ya miaka 40 nimekwisha kuona na kusikia vituko vingi vilivyoashiria kuwa imani ya uchawi iko hai katika tasnia hii pendwa. Mara ya kwanza kuanza kuona vitimbi hivi ‘live’ ni nilipojiunga na bendi moja ambayo ilikuja kuwa maarufu sana wakati wake. 

Kwa mara ya kwanza nilishuhudia kiongozi wa bendi yangu akiwa na katibu wake wakiwa wanafukiza radio kwa moshi wa majani fulani wakati kipindi cha nyimbo tulizorekodi muda mfupi kabla ya hapo kikiwa hewani. Siku hiyo vibao ambavyo tulikuwa tumerekodi siku chache kabla, vilikuwa vikirushwa hewani kwa mara ya kwanza, ndipo viongozi wangu hawa nikawakuta wakiwa katika shughuli hiyo ya kishirikina kwa imani kuwa kwa kufanya hivyo, vibao hivyo vitatikisa wasikilizaji wote. Baada ya hapo vituko vingi viliendelea hatimae tulimzoea kiongozi wa bendi yetu kuwa ni mshirikina. Kuna wakati aliletwa mganga ambaye alidaiwa aliwahi kuifanya timu moja maarufu ya soka, ishinde kikombe na kuwa bingwa wa Taifa na alichukuliwa kwa mkataba na bendi na kazi yake ikawa ni kukaa mlangoni akijifanya ni muuza machungwa. Yeye alidai kila anapomenya chungwa kwa kuunganisha maganda basi na wateja nao wataingia katika ukumbi kwa kuunganika, huyu alikaa kiasi katika bendi na tukaweza hata kusafiri nae kwenda mikoani. 

Harakati za bendi kutafuta umaarufu kwa uchawi zilipeleka mpaka bendi ikasafiri hadi kwenda Mpanda, ambako viongozi wa bendi walikwenda kwa mganga na kufanya mambo yao yalioyohusisha na hata kumchinja mbuzi ambaye nadhani masharti yalikuwa ni sisi wanamuziki wote tule kipande cha mbuzi yule wa kafala. Sijajua hatima ya nyama ya mbuzi yule maana wanamuziki walifanya mgomo wa kumla yule mbuzi. Kiongozi wa bendi katika safari hiyo, alichanjwa shingo yote na akawa na mikrofon ambayo wengine wote tulikatazwa kuitumia kasoro yeye tu, na sikuona mtu akiigusa mpaka nilipoacha bendi. Ushirikina una matatizo ya kufanya watu wasiaminiane hata kwenye bendi yenyewe, haikuchukua muda mrefu bendi ilipoanza kupoteza umaarufu, Kiongozi wa bendi akaaitisha mkutano na kutuambia kuwa kuanguka kwa bendi kunatokana na mmoja wetu kuiloga bendi, hapo ikatolewa tishio kuwa mtuhumiwa asipojitaja mwenyewe na kuomba msamaha mganga atamfanya awe kichaa. Jambo ambalo liliungwa mkono na wote kuwa kama ni kweli kuna mtu namna hiyo basi apate uchizi. Hakuna aliyekumbwa na tatizo hilo mpaka leo.

Miezi michache baadae, wanamuziki wawili walioamua kuacha bendi walirudisha uniform zao shati zikiwa zimechanywa kwenye kwapa na suruali kuchanywa kwenye maungio ya miguu kwa imani kuwa hizo ndizo sehemu zenye jasho kwa hiyo waliamini zingeweza kutumiwa na bendi kiuchawi kuwaharibia maisha.

Katika mizunguko kwenye bendi mbalimbali, nilikuwa katika bendi ambapo siku kukiwa na mpambano wa kupiga bendi zaidi ya moja katika ukumbi mmoja, basi hapo mganga maalumu lazima atafutwe ili kuilinda bendi isimalizwe na wapinzani. Ilikuwa inaaminika kuwa katika mpambano wa bendi, uchawi huaminika kuwa hutumika kuimaliza bendi ambayo itakuwa haina kinga.

Kwa ukweli kabisa hata wanamuziki kutembeleana zamani ilikuwa ni vigumu, kwani ukionekana mwanamuziki wa bendi nyingine katika ukumbi, basi bendi iliyo jukwaani haina raha, anaweza hata akatumwa mtu kufuatilia kila utakachofanya. Na ilikuwa vigumu kuruhusiwa kugusa vyombo vya bendi nyingine kwa wasiwasi wa kuwa unaweza ukaloga kile chombo.

Kulikuwa na hadithi nyingi kuhusu ni kiasi gani bendi ziliweza kufanya ili kupata wateja. Kuna bendi ambayo ilisifika kuwa kila ikimaliza kufanya onyesho, viongozi wake walipita katika kumbi na kuokota vizibo vya chupa, masalia ya chakula walichokuwa wanakula wapenzi wa muziki walioingia katika onyesho lao, na hata kuchota maji machafu kutoka vyooni kwenda kuloga ili wale walioingia wasiingie bendi yoyote kasoro yao. Bendi nyingine zilidaiwa kuwa ziliweka mkataba ambapo zililazimika kutoa kafala ya mtu kila baada ya kipindi fulani ili umaarufu usitetereke, hivyo viongozi wa bendi kufiwa na watoto, na hata wanamuziki wageni katika bendi hizo kukutwa na mauti ambayo, kwa chinichini yalidaiwa ni katika kutoa kafala.

Bendi mbili ambazo zilikuwa na upinzani mkubwa katika jiji la Dar es Salaam zilidaiwa hata kutaka kuweka uchawi katika chanzo kimoja cha maji cha Jiji la Dar es Salaam, na kujikuta wakitaka kuumbuana hadharani kuhusu hilo.

Kama nilivyosema imani ya uchawi huleta kutokuaminiana na hata madhara makubwa ya kutuhumiana mambo ambayo mara nyingi hayana ukweli wowote. Kuna mwanamuziki niliyejaribu kumshawishi aingie katika bendi niliyokuwa nikipigia , alikataa katakata kwa kuwa alidai mmoja wa wanamuziki katika bendi ni mchawi. Mwanamuziki mmoja aliwahi kuhadithia jinsi alivyopita uchochoro wa nyumba ya mwanamuziki mwenzake akashangaa kusikia jina lake likitajwa na mwenzie aliyekuwa chumbani kwake na kusema,’ Nyota ya …….izimike kama kaa hili’, akadai alichungulia katika ufa na akakuta mwenzie anatumbukiza kaa la moto kwenye glasi ya maji. 

Ugonjwa wa ukimwi ulipoanza kuuwa wanamuziki kwa mara ya kwanza mara nyingi ulihusishwa na uchawi. Rafiki yangu mmoja nilipomtembelea wakati akiwa hoi kitandani akanambia,’Nikupe siri? Mi ntakufa lakini nauawa na wanamuziki wenzangu kwenye bendi. Nimepata mganga kanitajia na majina kabisa’. Miezi michache baadae mwanamuziki huyu kabla hajafariki alinambia,’Mjomba sijalogwa wala nini, udude huu, unaniua udude’. Alifariki siku chache baada ya kunambia haya. Mungu amlaze Pema peponi Mjomba.

Kitu ambacho kimenishangaza karibuni tuhuma kuwa kuna wanamuziki wa kizazi kipya wanaendeleza imani hii ya ushirikina. Producer maarufu amejitokeza na kuwakanya wasifanye mambo hayo kwenye studio yake. Na siku chache baada ya hapo tena mwanamuziki mwingine wa muziki huo kawataja ambao aliwaita wabaya wake wanaomloga.!!! Katika kipindi kilichorushwa karibuni katika luninga fulani binti mmoja alieleza kwa kirefu jinsi yeye mwenyewe anavyoshiriki katika ushirikina na kujisifia kuwa kishaoga njia panda, chini ya miti, baharini katika mapambano ya kishirikina. Siku moja rafiki yangu mmoja anaeishi Mburahati alinipigia simu usiku na kunambia niende jirani na kwakwe kwani kuna mwanamuziki mmoja maarufu sana yuko kwa mganga wanachinja ng’ombe usiku ili umaarufu usipotee.

Nikaona loh kumbe shughuli bado inaendelea.

Wafanyakazi wageni 15 wa mgodi wa Tanzanite One wafukuzwa nchiniTeresia Mhagama na Mohamed Saif

Jumla ya raia wa kigeni 15 waliobanika kufanya kazi kinyume na taratibu za kisheria katika mgodi wa Tanzanite One uliopo wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wameondoshwa nchini tarehe 25 Desemba, mwaka jana.

Hayo yalielezwa jana jijini Arusha na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro, Amos Makala wakati wa kikao chake na wajumbe wa kamati hizo pamoja na Naibu Katika Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe kilichofanyika katika Kituo cha Jimolojia jijini humo.

Alisema kuwa raia hao waliamuliwa kuondoka nchini na Idara ya Uhamiaji mkoani Manyara ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa hiyo ambazo ziliunda kikosi kazi cha wajumbe 13 kwa ajili ya udhibiti utoroshwaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi, ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni zinazoshughulika na biashara ya madini na kuchunguza raia wa kigeni wasiokuwa na sifa za kufanya kazi kwenye migodi pamoja na kampuni za madini.

“Amri hiyo ya kuondoka nchini ndani ya siku saba ilianza kutekelezwa kuanzia tarehe 17 Desemba, 2015 na raia wote hao waliofukuzwa wanatoka nchini India. Nakipongeza Kikosi kazi hiki ambacho kimeanza kutekeleza majukumu ya kamati kwa ufanisi na zoezi hili litakuwa ni endelevu,” alisema Makala.

Aidha, alisema kuwa kikosi kazi hicho kilifanya operesheni ya siku mbili katika Mikoa hiyo kwa lengo la kukamata wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite ambao hawana leseni ambapo jumla ya wafanyabiashara 15 walikamatwa mkoani Arusha wakati mkoani Manyara idadi ya wafanyabiashara waliokamatwa kwa tuhuma za aina hiyo ni Nane na madini waliyokamatwa nayo yana thamani ya takribani shilingi milioni 47.

Alisema kuwa operesheni hiyo iliyofanyika tarehe 30 na 31 mwezi Desemba mwaka jana ilijikita pia katika kuwabaini raia wa kigeni wanaofanya biashara ya madini bila vibali ambapo raia mmoja kutoka nchini Ethiopia alikamatwa kwa tuhuma za kufanya biashara ya madini kinyume na sheria na anatarajiwa kufikishwa Mahakamani mara baada ya taratibu za awali za kipelelezi kukamilika.

Awali, Mwenyekiti wa Kikosi kazi hicho, Muliro Muliro ambaye pia ni Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Arusha alisema kuwa baada ya zoezi la kuwabaini pamoja na kuwakamata wafanyabiashara wa madini wasiokuwa na vibali, jumla ya wafanyabiashara 272 ambao walikuwa wakifanya biashara hiyo kinyemela walijitokeza katika Ofisi za Madini za Arusha na Merelani ili kuomba leseni za kufanya biashara hiyo.

“Mkoani Manyara (Mererani) ilipo migodi ya Tanzanite jumla ya wafanyabiashara 154 walijitokeza na kuwasilisha maombi ya leseni za wakala wa madini ya vito (brokers’ licence) na hivyo hadi kufikia tarehe 8 Januari mwaka huu, kiasi cha shilingi milioni 38.5 zilikusanywa kutokana na ada ya maombi ya leseni husika,” alisema Muliro.

Vilevile alisema kuwa kwa upande wa Arusha, maombi mapya ya leseni za wakala wa madini yapatayo 115 yaliwasilishwa Ofisi za Madini za kanda ya Kaskazini na hivyo kiasi cha shilingi milioni 28.7 kimekusanywa kutokana na maombi hayo.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Profesa Mdoe alizipongeza Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa hiyo kwa kazi nzuri wanayofanya kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini katika kudhibiti utoroshwaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi, kubaini wafanyabiashara wa madini hayo wasiokuwa na vibali na wanaokwepa kulipa kodi stahiki.

Alisema kuwa bado kuna kazi kubwa mbele ya kuhakikisha kuwa suala hilo linakomeshwa na kusisitiza kwamba kila mtumishi anapaswa kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo huku akieleza kuwa operesheni haitoweza kumaliza tatizo hilo kama watumishi hawatatimiza majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi ili kutotoa mianya kwa matatizo hayo kuendelea kuwepo.

Pichani juu ni Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Uchumi na Biashara katika Wizara ya Nishati na Madini, Salim Salim (aliyesimama) akitoa taarifa ya juhudi mbalimbali zilizofanywa na Wizara ya Nishati na Madini katika ya udhibiti utoroshwaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi na ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni zinazoshughulika na biashara ya madini nchini wakati wa kikao cha Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha kilichofanyika katika Kituo cha Jimolojia jijini Arusha. Wa Tano kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hizo, Amos Makala na wa nne kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe.

Malalamiko 5 ya wastaafu kwa SSRA dhidi ya mifuko ya hifadhi ya jamiiWATUMISHI wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa na idara zake wameishtaki kwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii wakiilalamikia kwa mambo makubwa matano ikiwemo ucheleweshaji wa mafao kwa wanachama wake wastaafu.

Katika kikao kilichofanyika juzi mjini hapa baina ya SSRA na watumishi hao; watumishi hao walisema uzoefu toka kwa baadhi ya wastaafu wengi unaonesha kwamba inawachukua muda mrefu kupata mafao yao.

Afisa Utumishi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa, Gasto Andongwisye alitoa mfano akisema; “baadhi ya watumishi waliostaafu kabla ya mwezi Julai mwaka jana hawajapata mafao yao hadi leo na imekuwa ni kilio kikubwa ofisini kwangu.”

Akijibu lalamiko hilo, Afisa Uhusiano wa SSRA, Sabato Kasuri alisema ucheleweshaji wa mafao ni changamoto ambayo tayari imefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa baada ya kubainika ilikuwa ikisababishwa na na ukosefu wa kumbukumbu sahihi za walengwa.

Alisema mamlaka yao imetoa miongozo mbalimbali ya kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii na katika suala la kumbukumbu kuna miongozo ya utunzaji wa kumbukumbu na takwimu ambayo kama ikitumiwa ipasavyo hakuna mstaafu atakayecheleweshewa mafao yake kwasababu zilizondani ya uwezo wa mifuko.

Ili kuondokana na lalamiko hilo wanachama hao walitaka mifuko hiyo ilipie riba fedha za mafao zinazochelewa kulipwa kwa wahusika sawasawa na waajiri wanapochelewa kuwasilisha michango ya wanachama katika mifuko hiyo.

Malalamiko mengine yaliyotolewa na watumishi hao ni pamoja na uwepo wa taarifa kwamba baadhi ya mifuko hiyo haitaki kulipa mafao ya kabla ya mwaka 1999 na inataka mzigo huo ubebwe na serikali.

Mengine yanahusu baadhi ya mifuko hiyo kushindwa kuweka kumbukumbu zake vizuri pamoja na uwepo wa miongozi ya SSRA jambo linalowafanya baadhi ya wanachama wake wawe na akaunti zaidi ya moja na wakati huo huo taarifa za baadhi ya michango yao kutoonekana.

Huduma ya bima ya afya ni eneo jingine lililotajwa na wanachama hao kuwa na changamoto kubwa kwani mbali na wanachama wake kuchangia michango yao lakini baadhi yao wameendelea kupata huduma hafifu.

Lingine linalolalamikiwa katika mifuko hiyo ni mikopo ya nyumba ambayo kwa maelezo ya wanachama ni mzigo mkubwa kwa wastaafu kwani zinauzwa zikiwa na riba wakati zimejengwa kwa fedha za wanachama.

Katika kukabiliana na changamoto za mifuko hiyo, Kasuri aliwaambia watumishi hao kwamba SSRA inaendelea kutoa elimu kwa wadau wake, inarejea miundo na kanuni zinazogongana katika sekta ya hifadhi ya jamii, inafanya tathmini za mifuko yote ya hifadhi ya jamii na inatoa miongozo ya uwekezaji.

Alisema mamlaka yao ina wajibu pia wa kupitia vikokotoo vya mafao na mafao yanayotolewa, kutathimini afya ya mifuko yote na kushauri ipasavyo, na imeielekeza mifuko yote ya hifadhi ya jamii kufanya mikutano ya wanachama.

Kwa kutambua umuhimu wa hifadhi ya jamiii kwa kila mwananchi, Kasuri alisema sheria iliyounda SSRA imeruhusu uandikishaji wa wanachama kutoka katika sekta isiyo rasmi jambo linalowanufaisha pia wakulima na wafanyabiashara wadogo.

Alisema mpaka sasa Tanzania Bara ina mifuko sita ya hifadhi ya jamii ambayo ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni wa PPF, Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali (GEPF), Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF) huku Zanzibar ikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).

Katika kikao hicho ni mifuko miwili ya GEPF na mfuko mpya wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ilipata fursa ya kueleza majukumu yao.

Ufafanuzi wa Wizara kuhusu uhaba wa chanjo ya polioAgizo la Serikali la kukamatwa kwa waliomwozesha binti wa miaka 13

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


(PRESS RELEASE).


WIZARA YAAGIZA KUKAMATAWA KWA WALIOMWOZESHA MTOTO WA MIAKA 13 WILAYA YA KISHAPU, MKOA WA SHINYANGA


WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea kwa masikitiko makubwa na inataka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wazazi wawili tofauti wanaotuhumiwa kuwaozesha watoto wao wa umri wa miaka 13 na kuwakatisha masomo katika mkoa wa Shinyanga na Dodoma.

Imeelezwa kuwa, wakati mtoto mmoja mwanafunzi wa shule ya msingi Wishiteleja wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga ameozeshwa kwa nguvu kwa mahari ya ngombe 13 na kumkatisha masomo yake akiwa darasa la sita, mtoto mwingine wa mtaa wa Chikole, Kata ya Msalato Manispaa ya Dodoma anasemekana kuozeshwa kwa mahali ya shilingi 600,000. Kufuatia kuwepo kwa matukio haya mawili Wizara inataka vyombo vya dola kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi wa Mtoto katika mikoa yote kuhakikisha kuwa watuhumiwa wanachukuliwa hatua kali.

Tukio la kuwaoza watoto katika umri mdogo siyo tu linakinzana na haki za msingi za mtoto bali pia linamkosesha mtoto haki ya kuendelezwa ikiwa ni pamoja na kuhatarisha uhai wake kwa kupatiwa majukumu ya mtu mzima katika umri mdogo.

Wizara inawataka wazazi na walezi kubadilika na kuachana na tabia ya kuwaoza watoto wao katika umri mdogo maana vitendo hivyo ni vya kikatili. Jamii inatakiwa kutambua kuwa, vitendo vya kikatili kama hivyo vinapofanywa katika familia vinarudisha nyuma juhudi za Serikali za kupambana na ukatili maana kwa kiasi kikubwa familia inatakiwa kuwa mahala salama panapofaa watoto kuishi na kulindwa.

Aidha, Wizara inakumbusha wazazi, walezi na wadau wengine kuwa, ndoa za utotoni ni kinyume na Sheria ya Mtoto (2009) na Mikataba ya Kimataifa kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto. NIwajibu wa kila mtu kuhakikisha kuwa watoto wanaishi katika usalama na kuhakikishiwa haki zao zote za msingi ikiwemo kulindwa, kuendelezwa, kuishi na kushirikishwa katika maisha ya kila siku ili kujenga Taifa linaloheshimu maslahi ya watoto.

Erasto T. Ching’oro
Kny: KATIBU MKUU

MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZAZI NA WATOTO.