Taarifa ya hatua ya TMAA dhidi ya waliotorosha, na biashara haramu ya madini


UDHIBITI WA UTOROSHAJI NA BIASHARA HARAMU YA MADINI 

Moja ya majukumu ya Wakala wa Ukaguzi wa madini Tanzania (TMAA) ni kufuatilia na kuzuia utoroshaji/magendo na biashara ya madini unaopelekea ukwepaji wa ulipaji mrabaha kwa kushirikiana na taasisi nyingine husika za Serikali zikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji.

Taarifa za matukio ya udhibiti wa utoroshaji na biashara haramu ya madini zilizopo zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2015 mpaka Januari 13, 2016 kulikuwepo na jumla ya matukio 14 ya utoroshaji wa madini ambapo madini yenye thamani ya Dola za Marekani 1,474,194 milioni (zaidi ya Shilingi bilioni 3,235,856,181) yalikamatwa na wakaguzi wa Wakala kupitia Madawati ya Ukaguzi yaliyopo katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam (JNIA), Kilimanjaro (KIA) na Mwanza.

Katika matukio ya hivi karibuni ya ukamataji wa madini katika viwanja vya ndege, madini yenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni 11,217,300 yalikamatwa na wakaguzi wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola.

Raia mmoja wa kigeni na mwingine wa Tanzania walikamatwa wakiwa na madini hayo bila kuwa na kibali chochote cha usafirishaji kulingana na Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Raia wa kigeni (jina limehifadhiwa) ambaye alikuwa anasafiri kwenda Bangkok alikamatwa akiwa na madini aina mbalimbali ikiwemo almasi, aquamarine, sapphire, green tourmaline, quartz na rhodolite.

Tukio la pili, mtuhumiwa mwingine ambaye ni raia wa Tanzania aliyekuwa akisafiri kwenda Ujerumani alikamatwa akiwa na madini mbalimbali ikiwemo amethyst, moonstone cabochon, rulilated quartz (cabochon), rulilated quartz(faceted), chrysoprase, green tourmaline, ruby, red garnet, green quartz, zircon na rhodolite.

Kufuatia Matukio hayo wahusika wote wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufunguliwa kesi mahakamani.

Wakala unatoa rai kwa Umma kujiepusha na shughuli za utoroshaji/magendo na biashara haramu ya madini, kwani hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa yeyote atakayebainika/kukamatwa akijihusisha na shughuli hizo. Aidha, madini yatakayokamatwa yakisafirishwa kinyume cha sheria na taratibu zilizopo yatatafishwa na Serikali.

Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini inatoa wito kwa yeyote atakayetoa taarifa za utoroshaji/magendo na biashara haramu ya madini kwa Kamishna wa Madini au Wakala ambazo zitawezesha ukamataji wa madini, atazawadiwa fedha taslimu ambazo ni sawa na asilimia 5 ya thamani ya madini yatakayokamatwa na kunadiwa. Kwa mawasiliano ya haraka, wananchi watumie barua pepe [email protected] na simu 022-2137142 au 022-2601819.

IMETOLEWA NA
DOMINIC RWEKAZA
MTENDAJI MKUU
WAKALA WA UKAGUZI WA MADINI TANZANIA
15 JANUARI, 2016

Waziri Muhongo asimamisha kazi na kukamata vifaa vya kampuni ya Off Route Technology kwa ajili ya uchunguzi

Serikali imesimamisha shughuli za uchimbaji wa Makaa ya Mawe ya Kampuni ya Off Route Technology iliyopo Kyela ikiwemo kukamata vifaa vya uchimbaji na kuhakikisha kuwa vinakuwa chini ya uangalizi wa Mkoa wa Mbeya hadi hapo uchunguzi dhidi ya uhalali wa kampuni hiyo kuchimba makaa utakapokamilika.

Hatua hiyo inafuatia ziara ya Waziri wa Nishati na Madini, Prof Sospeter Muhongo kutembelea mgodini hapo na kubaini kuwa, kampuni hiyo inachimba makaa bila kuwa na leseni halali ya uchimbaji madini.

Aidha, Prof. Muhongo ameitaka kampuni hiyo kulipa kodi zote za Serikali ikiwemo inazodaiwa na Halmashuri tangu ianze kufanya shughuli za kuchimba. Aidha, ili kujua undani wa suala hilo, Prof. Muhongo ameitisha kikao kifanyike kati ya mgodi huo, Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania ( TMAA), Ofisi ya Madini Kanda ya Kusini Magharibi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyela, tarehe 18 Januari, 2016 chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini.

"Hawa watu wamechimba makaa, wameuza bila kuwa na leseni na tunawadai kodi zetu. Uongozi hakikisheni katika kikao hicho mnakuja na madai yenu. TMAA pia mje na madai yenu", ameongeza Prof. Muhongo.

Prof. Muhongo pia amezitaka pande zote kuwasilisha nyaraka muhimu kuhusu suala hilo, ili iamuliwe kwa kufuata sheria na taratibu stahili, "hakuna mtu atakayeonewa, kila upande uje na nyaraka zote na sisi Wizarani huko ndani kwetu tutaulizana wenyewe kuhusu jambo hili halafu tutalitolea taarifa", amesema. Prof. Muhongo.

Akifafanua kuhusu suala hilo , Afisa Mfawidhi wa TMAA, Mhandisi Jumanne Mohamed amesema kuwa, awali Wakala ilifanya ukaguzi na kubaini kuwa kampuni hiyo hailipi kodi na kuwa yapo malimbikizo ya madai ambayo yalipaswa kulipwa na kuongeza kuwa baada ya mawasiliano juu ya suala hilo, kampuni iliahidi kulipa kwa awamu jambo ambalo halijafanywa hadi sasa.

Kampuni ya Off Route Technology, ipo katika Kijiji cha Ngana Wilaya ya Kyela mkoa wa Mbeya.

RCRSDS kuzindua mfumo wa kielektroniki wa taarifa za kitafiti za uwajibikaji kwa umma


Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Utafiti wa Shughuli za Maendeleo ya Jamii Tanzania (RCSDS),Abraham Shempemba (kulia) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo. Kushoto ni Meneja Uhusiano wa kituo hicho, Chrizostom Thadeo. (PICHA: RICHARD MWAIKENDA)

Celina Mathew

KITUO cha Utafiti wa shughuli za maendeleo ya jamii Tanzania (RCSDS), kinatarajia kuzindua mfumo wa kielektroniki wa kukusanya, kuhifadhi na kuweka angani taarifa za kitafiti za uwajibikaji wa taasisi za binafsi, za umma na watu binafsi serikali kuu na za mitaa na hata mtu mmoja mmoja.

Mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa mwishoni mwa mwezi huu ambapo utapelekwa katika mikoa 30 Tanzania Bara pamoja na maeneo 100 yenye wananchi wenye uhitaji mkubwa.

Akizungunza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kituo hicho, Abraham Shempemba alisema lengo la mwendelezo huo ni kutoa nafasi kwa walengwa kutambua mchango unaotolewa kwao na wadau mbalimbali pamoja na misaada kwa jamii zenye uhitaji mkubwa.

"Sisi kama RCSDS tunatambua uwepo wa makampuni, mashirika na taasisi mbalimbali za umma na binafsi zinazochangia kwa kiasi kikubwa mahitaji na hata majanga yanapotokea ili kunusuru na kuboresha maisha ya watanzania wenzetu na kuthamini michango na misaada yao,"alisema.

Alisema mfumo huo unaoaznishwa una lengo la kutambua michango na misaada mbalimbali inayotolewa na wadau kwa jamii pia wadau nao wapate fursa ya kuweka malengo yao ya uwajibikaji kwa jamii kwa kuona ni wapi wanaweza kuwekeza zaidi kiuwajibikaji na eneo lipo nani amewekeza.

Shempemba alisema utafiti walioufanya na kuutolea taarifa msimu ulipita kwa kushitikiana na taasisi ya ukaguzi ya Konsalt inayofanyika kila mwaka wapo waliosaidia jamii kwa sekta mbalimbali kama huduma za afya, maji, miundombinu, elimu, michezo, maafa na mambo mengine kwa asilimia tofauti.

Aliongeza kuwa tafiti hizo pia zimesaidia takwimu za misaada iliyotolewa kisekta, gharama zilizotumika, uwajibikaji jamii ulivyowekezwa, jamii ilivyonufaika na misaada hiyo na wadau walivyonufaika na uwekezaji wao kwa jamii hizo.

Waziri Mbarawa: Hakikisheni watumishi wote wanatumia "electronic attendance registration"

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame Mbarawa akijisajili katika mfumo wa mahudhurio wa elektoniki (kulia), ni Afisa Utumishi Bi, Elizabeth Maduhu akimwelekeza.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa amezungumzia umuhimu wa taasisi zote za Serikali kuwa na mfumo wa mahudhurio kwa njia ya kielekroniki (electronic attendance registration (EAR)).

Akizungumza mara baada ya kujisajili katika ofisi za sekta ya mawasiliano Prof. Mbarawa amesema kwa kuanzia utaratibu huo utaendelezwa katika sekta Uchukuzi na Ujenzi na kisha utafungwa katika taasisi zote za Serikali ili kuhakikisha watumishi wa umma wanafika ofisini kwa wakati na kupunguza utoro.

“Hakikisheni watumishi wote wanatumia mfumo huu wa kielektroniki ili kudhibiti utoro na kuwezesha wafanyakazi kufanyakazi kwa muda unaokubalika kiserikali”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Aidha Waziri Mbarawa amewataka wafanyakazi wa mapokezi kuacha kuwafungulia wafanyakazi watoro na wanaochelewa kazini kuingia ofisini ili kuwezesha mfumo kutambua watumishi watoro na hivyo kuchukuliwa hatua stahiki.

Amesisitiza kuwa mfumo huo utakapofungwa katika taasisi zote za umma utadhibiti watoro kwa kuwa unaweka kumbukumbu ya muda mtu anaokuwa kazini na hivyo kuwawezesha viongozi kupata taarifa sahihi za mahudhurio.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI,UCHUKUZI NA MAWASILIANO.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame Mbarawa akifungua mlango kwa kutumia mfumo wa mahudhurio wa elektroniki baada ya kujisajili.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame Mbarawa akisaini kitabu cha mahudhurio baada ya kujisajili katika mfumo wa mahudhurio wa elektroniki katika ofisi za sekta mawasiliano.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame Mbarawa wa (kwanza kulia), akitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano upande wa sekta ya mawasiliano Profesa Faustin Kamuzora (katikati) na kulia ni Naibu Katibu Mkuu Dakta Maria Sasabo.

Maelezo ya Wizara kuhusu tiba asilia na tiba mbadala

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Ummy Mwalimu (katikati) akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Saslaam jana, juu ya serikali kupitia wizara hiyo kutoa msamaha wa miezi mitatu kwa waganga wanaotoa huduma za tiba asili na tiba mbadala kuendelea kujisajili ili kutambulika kisheria. Kulia ni Naibu waziri wa wizara hiyo, Dk.Hamis Kigwangwallah na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Mpoki Ulisubisya

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


MAELEZO YA WAZIRI KUHUSU TIBA ASILI NA TIBA MBADALA


Ndugu Wananchi, Katika nchi yoyote ile uhuru usio na mipaka ni jambo la hatari; lakini pia hakuna haki isiyo na wajibu. Vivyo hivyo, katika huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala hapa nchini kuna Sheria, Kanuni na Taratibu za Maadili zinazoweka masharti, uhuru na mipaka; pia haki na wajibu wa kila mdau. 

Huduma za tiba asili na tiba mbadala ni huduma zinazotambulika na Jamhuri yetu, watu wake na ina thamani kubwa. Aidha, ni huduma inayotambuliwa na sayansi ya tiba ya kisasa. Hata hivyo huduma hizo zimekumbwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa watoa huduma wasiozingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali. 

Kutokana na hali hiyo na kutokana na ziara ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (Mb) kwa Tabibu Juma Mwaka Juma tarehe 14/12/2015 na kufuatia uchambuzi uliofanywa na Wizara baada ya ziara hii, Wizara imebaini changamoto zifuatazo:-

1. Huduma za tiba asili na au tiba mbadala zinatolewa na watoa huduma wasiosajiliwa na Mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria. 

2. Uwepo wa vituo vinavyotoa huduma za Tiba Asili na au Tiba Mbadala bila kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria.

3. Kutolewa dawa kwa wagonjwa bila dawa hizo kusajiliwa na mamlaka husika. 

4. Uingizaji na matumizi ya vifaa vya uchunguzi ambavyo havijasajiliwa na mamlaka zinazohusika, na
5. Utoaji wa matangazo bila ya kufuatwa kwa matakwa ya sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo. Aidha baadhi ya matangazo hayo yamekuwa na taarifa zinazoweza kuleta madhara na kupotosha Umma wa Watanzania.

Ndugu Wananchi,

Kutokana na hali hiyo, Wizara itahakikisha kuwa huduma za tiba asili na tiba mbadala zinatolewa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo. Lengo ni kuwezesha huduma za tiba asili na tiba mbadala zinakuwa huduma rafiki na salama kwa watumiaji. Tunao wajibu wa kuwalinda wananchi, vile vile tunaowajibu wa kuweka mazingira mazuri kwa watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala ili kufanya shughuli zao vizuri.


Hivyo kwa upande wetu Wizara itahakikisha kuwa:- 

1. Baraza na sehemu inayosimamia huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala inakuwa na watumishi wa kutosha kwa mujibu wa Ikama. 

2. Kunakuwa na Mpango Mkakati wa muda mrefu kuwezesha kufanikisha uboreshaji wa huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.

3. Watoa huduma wote, vituo vyote vya kutolea huduma, dawa na vifaa na vifaa tiba vinavyotumika vinasajiliwa. 

4. Utaandaliwa mwongozo wa mafunzo kwa watoa huduma wote nchini, kuhusu namna ya kuweka kumbukumbu za wagonjwa, kutoa rufaa kwa wagonjwa na kutengeneza dawa zilizo bora. 

5. Kunakuwa na mawasiliano na Wizara zinazohusika na habari na mawasiliano ili kuboresha utoaji matangazo yanayohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala. 

6. Kunakuwa na mawasiliano na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Taasisi za Utafiti ili kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini. 

7. Tutafanya mabadiliko ya Sheria ili kuongeza kiwango cha adhabu kwa watakaokiuka, na pia tunakusudia kuondoa Kanuni inayoruhusu matangazo kwa idhini ya Baraza kwa sababu inaweka mianya ya matumizi mabaya ya fursa ndogo ya matangazo inayotolewa.
Ndugu Wananchi, Katika kufanikisha hayo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatoa maelekezo yafuatayo kwa watoa huduma na jamii:-

1. Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kutoa huduma za tiba asili na au tiba mbadala bila kusajiliwa. 

Ninalielekeza Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kuhakikisha kuwa watoaji huduma wote wanasajiliwa kwa mujibu wa Sheria: 
(a) Mijini, (Majiji, Manispaa na Miji) – usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi mitatu; kuanzia Januari 15, 2016 na 
(b) Vijijini, Halmashauri zote zilizobaki – usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi sita kuanzia Januari 15, 2016. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaye puuza kujisajili katika kipindi hicho 

2. Hairuhusiwi kuuza na au kugawa dawa yoyote ile ya tiba asili au tiba mbadala mpaka iwe imesajiliwa na Baraza baada ya kuchunguzwa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ni salama na kupewa kibali na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA). 

3. Hairuhusiwi kuendesha kituo cha kutolea huduma za tiba asili na au tiba mbadala bila kukisajili. 

4. Wizara inapiga marufuku kwa mtu binafsi au taasisi yoyote ile kutumia kifaa au kifaa tiba chochote bila kukisajili TFDA na kupewa kibali; na 5. Matangazo yote yanayohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala ambayo hayajapitishwa na Baraza yamezuiliwa kuanzia leo tarehe 15/1/2016. 

Wizara inavitaka vyombo vya Habari hasa Televisheni, Radio na Magazeti kuzingatia Sheria na Kanuni za Tiba Asili na Tiba Mbadala inayozuia matangazo ambayo hayajachunguzwa na Baraza. Ni wajibu wa vyombo vya habari kujiridhisha na Mamlaka husika yaani Baraza kabla ya kutoa tangazo lolote linalohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala. 

Wizara itashirikiana na Mamlaka zinazohusika na habari na mawasiliano kutekeleza agizo hili. Vile vile, hairuhusiwi kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara kuhusu tiba asili na tiba mbadala.

Ndugu Wananchi, Katika kuwezesha ulinzi wa afya za wananchi, kila mmoja wote alinde afya yake kwa kuhakikisha kuwa huduma anayopata ya tiba asili na tiba mbadala ni kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo inayotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. 

Ni uhakika uliowazi kuwa kwa pamoja tukiboresha huduma za tiba asili siyo tu tutaboresha afya zetu bali pia tutaweza kuuza dawa na huduma hizo nje ya nchi na kupata fedha za kigeni kupitia na hivyo kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii na nchi kwa ujumla.

Kwa pamoja tushirikiane kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini. 

INAWEZEKANA.

Ummy A. Mwalimu (Mb) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO 15 Januari, 2016