Baba'ke Mbwana Samata aeleza "siri" ya mafanikio ya mwanaye


Viiongozi wa UKAWA wakutana Dar

Aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania, Edward Lowassa wakati viongozi wa UKAWA walipokutana jijini Dar es Salaam, Januari 19, 2016. 


  • Picha: Francis Dande

Mtizamo wa Rais Wa Chama Cha Walimu kuhusu "elimu bure"


The science behind Internet trolls


Taasisi kufanya maombi kwa Mungu apunguze joto kali katika pwani ya mwambao wa Tanzania


Taasisi ya Kidini ya Good News for All Ministry inatarajia kufanya maombi ya kumuomba Mungu kupunguza joto kali linaloendelea kuongezeka katika maeneo ya Dar es Salaam, Pwani na Visiwa vya Zanzibar.

Akizungumzia maombi hayo, Mwenyekiti wa Good News for All Ministry, Askofu Dk Charles Gadi alisema wanatarajia kufanya maombi siku ya Jumatano, Januari, 20 katika eneo la Feri jijini Dar es Salaam kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa sita mchana.

“Wastani wa joto ambalo kwa sasa lipo jijini Dar es Salaam, Tanga na Visiwa vya Zanzibar linakadiriwa kufikia nyuzi joto 35 ambazo kiafya inaweza kuwa na athari kwa binadamu na sasa tunataka kumuomba Mungu kuliondoa joto hili,” aliongeza.

Askofu Gadi alisisitiza kuwa joto hili linaweza kusababisha matatizo kwa wananchi na hivyo kuamua kuliombea kwa Mungu kusudi aliondoe kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza hapo mbeleni kwani tayari baadhi ya watu wanaugua mapele na joto bahari linaongezeka kwa kasi kiasi cha kuweza kusababisha mafuriko.

Aidha, aliwamba wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika maombi hayo ili kuomba kwa pamoja ili Mungu asikie sauti zetu na kuweza kupunguza joto katika mikoa iliyoathirika.
Wito wa Lowassa kuhusu "bomoa bomoa"


Rais Magufuli azungumza na Balozi wa Israel


Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akimkaribiusha Ikulu, Balozi wa Israeli nchini Mhe Yahel Vilan alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Januari 19, 2016.Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiongea na Balozi wa Israeli nchini Mhe Yahel Vilan
alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Januari 19, 2016


Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akipeana mikono na Balozi wa Israeli nchini Mhe Yahel Vilan alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Januari 19, 2016

Taarifa ya habari ChannelTEN, 19.01.2016Mwili wa marehemu Laeticia Nyerere wapokelewa Tanzania kwa mazikoAskari wa Bunge wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Laeticia Nyerere (aliyefariki nchini Marekani alikokuwa akitibiwa) mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam leo jioni. Mwili huo kesho utaagwa nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, Msasani kabla ya kusafirishwa kwenda Butiama mkoani Mara kwa mazishi yatakayofanyika kesho kutwa.


Mwili huo ukiingizwa kwenye gari maalumu katika uwanja huo.


Ndugu jamaa na marafiki wakijadiliana jambo wakati wa kuupokea mwili huo.


Ndugu, jamaa, marafiki na watoto wa marehemu wakisubiri kuupokea mwili wa mpendwa wao.


Madaraka Nyerere, aliyekuwa mume wa marehemu Laeticia, akizungumza na wanahabari baada ya kuupokea mwili huo uwanjani hapo.


Mtoto wa marehemu (kulia), Julius Nyerere Jr., akifarijiwa na mmoja wa ndugu wakati wakienda kupanda gari kabla ya kuondoka uwanjani hapo.

(Imeandaliwa na mtandao wa www.habarizajamii.com - simu namba 0712-727062)

Picha za msiba kutoka nyumbani kwa marehemu George Sebo Bowie, MarekaniKushoto niAbdul Sebo mtoto wa marehemu akipewa pole na moja ya ndugu, jamaa na marafiki waliofika nyumbani kwa marehemu Bowie kutoa pole na rambi rambi zao kwa wafiwa kutokana na kifo cha mpendwa wao Mzee George Sebo kilichotokea siku ya Jumatatu asubuhi January 18, 2016 katika Hospitali ya Prince George iliyopo Maryland nchini Marekani. Utaratibu na mipango tutajulishwa leo kwa sasa imetengenezwa GOFUNDME ambayo ni www.gofundme.com/8fjvpcns

Picha na Vijimambo/Kwanza Production

Mwalimu apigwa makofi na Ofisa Elimu

MWALIMU wa shule ya msingi Ikombolinga, Peter Emma, ameeleza masikitiko yake ya kudhalilishwa na Ofisa Elimu wa shule za msingi, Mohammed Msongo, wilaya Chamwino kwa kumzaba makofi mbele za walimu wenzake.

Mwalimu Emma anasema udhalilishaji aliofanyiwa na Ofisa elimu huyo kwa kupigwa makofi mbele ya walimu wenzake unatokana na kuchelewa kufika katika semina ya mafunzo ya KKK licha ya kuwa mwalimu huyo alikuwa anatoka mbali na alikuwa hajalipwa fedha ya nauli.

Akielezea tukio hilo Mwalimu Emma amesema kwa mujibu wa ratiba ya mafunzo ambayo yalianza Januari 16, mwaka huu yalitakiwa kuanza saa mbili kamili lakini yeye na wenzake zaidi ya 20 walifika saa 2:40 asubuhi.

Akiendelea kuzungumza na waandishi wa habari mwalimu huyo amesema kwamba yeye na walimu wenzake waliochelewa na walimkuta ofisa elimu huyo na kuwazuia kuingia darasani kutokana na kuchelewa kwao.

Amesema Ofisa huyo aliendelea kuwakaripia na kuwataka waandike majina yao kwa malengo kwamba wasihudhurie mafunzo hayo KKK ambayo yalikuwa yanawahusu walimu wote wa darasa kwanza na la pili.

“Wakati najitetea kuwa tunatoka mbali na usafiri ni wa shida huku hatukuwa na fedha, ofisa elimu alinizaba makofi na kunisukuma ukutani.
“Kitendo hicho kweli kimeniumiza na kunidhalilisha sana hata hapa najifunza lakini sina amani natamani kurudi nyumbani.
“Tuliandika majina ya waliochelewa sijui tutalipwa au la maana tunatakiwa kulipwa Sh. 55,000 kwa kila siku na nauli lakini mpaka sasa hatujalipwa mimi sielewi kwa kweli nimefadhaika sana.
“Kama uongozi ni wa ubabe hivyo hakika kazi itakuwa ngumu sana kwani hali hii inavunja moyo,” amesema Mwalimu Emma.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Chamwino, Richard Masimba alipotafutwa ofisini kwake amesema taarifa hizo hawana na watazifuatilia. Masimba amesema ofisi haina taarifa ya mwalimu kupigwa vibao na kusukumwa ukutani na iwapo itathibitika hatua za kisheria na kinidhamu zitafanywa.

Mtuhumiwa wa tukio hilo, Ofisa Msongo, alipoulizwa alikana na kukataa katakata kuwa hajampiga kibao wala kumsukuma ukutani mwalimu huyo.

“Jumla ya walimu 348 wanapatiwa mafunzo kazini na mafunzo hayo ni kwa shule za msingi serikali 119.
“Ila ni kweli wapo walimu waliochelewa badala ya kufika saa 2:00 kama tulivyo kubaliana wao wamefika saa 2:40 hivyo walipoteza dakika 40 za kipindi.
“Kutokana na hali hiyo nililazimika kukaa na walimu wote waliochelewa yakiwa makundi mawili na kuwapa maelekezo ili wasiendelee kuchelewa kwani kwa kufanya hivyo hawawezi kufaidika na hayo masomo,” alijieleza Msongo.

Hata hivyo Msongo amesema siku ya tukio ambalo inadaiwa alimpiga mwalimu huyo alimshika shati kwa nyuma na kumvuta ikiwa ni hatua ya kutaka asijichanganye na kundi lingine lisilomuhusu lakini siyo kumpiga.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Walimu (CWT), Wilaya ya Chamwino, James Puya amesema analaani vikali kitendo cha ofisa elimu msingi kumzaba mwalimu vibao.

“Kitendo hicho kinawafanya watumishi kukosa morali wa kufanya kazi kwa ufasaha na wakati mwingine kuhamishia hasira kwa watoto.
“Mimi nimepata taarifa za mwalimu kupigwa na nasema kama kiongozi wa CWT wilaya ya Chamwino kulikotokea hili tatizo naomba tume ya Haki za binadamu, Mkurugenzi na Utumishi kuingilia kati suala hili.
“Unyanyasaji huu usipokomeshwa haraka itakuwa mwendelezo wa viongozi wa ngazi ya juu kuwanyanyasa watumishi wa ngazi ya chini jambo ambalo ni hatari,” amesema Puya.

Kashfa ya fedha na madaraka katika ofisi ya CAG


  • Imeandikwa na Masyaga Matinyi, Dar es Salaam via MTANZANIA
OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imeingia katika kashfa nzito na kudaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.

Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli inapambana na kudhibiti matumizi makubwa pamoja na vita dhidi ya ufisadi.

Ofisi hiyo ambayo inaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Profesa Juma Assad, imethibitika kufanya matumizi hayo pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.

MTANZANIA limebaini katika uchunguzi wake kuwa tangu Profesa Assad alipoteuliwa kushika wadhifa huo Novemba 5, 2014 na kuapishwa Desemba 2 mwaka huo na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ofisi hiyo imebariki mambo kadhaa kinyume na maadili na majukumu yake.

UKARABATI WA NYUMBA

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo MTANZANIA inazo, Aprili mwaka jana Ofisi ya CAG ilianza mchakato wa kukarabati nyumba ya Serikali Plot namba 973 iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam inayotumiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.

Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa kwa mujibu wa taratibu, nyumba zote za Serikali zipo chini ya Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) na taratibu zote za ukarabati hufanywa na kusimamiwa na wakala huyo.

“Lakini hapa kwetu hali ilikuwa tofauti kabisa, ofisi ya CAG iliamua kufanya yenyewe ukarabati huku ikijua kabisa inakiuka utaratibu na ikatoa kazi hiyo kwa kampuni bila hata kutangaza zabuni, hata kampuni husika haikuwa na mkataba wowote na ofisi ya CAG.

“Cha kushangaza zaidi kampuni hiyo ya M/SAfriq-Engineering and Construction Co. Ltd si ya kigeni, ni ya Waswahili wenzetu, lakini ililipwa gharama za kazi kwa dola za Marekani badala ya shilingi ya Tanzania.

“Na si kwamba ililipwa kwa wamu kama ilivyo kawaida, bali wao walilipwa jumla ya dola za Marekani 102,570 kwa mkupuo, tena hata kabla ya kuanza kazi, ambapo pamoja na gharama zikiwamo kodi za Serikali, jumla ilifika Sh milioni 281.8,” kilisema chanzo chetu.

Mtaalamu mmoja wa majengo katika Chuo Kikuu cha Ardhi jijini Dar es Salaam (jina tunalihifadhi), ameliambia MTANZANIA kuwa kiasi hicho cha fedha kinatosha kujenga nyumba nzuri ya kisasa ambayo inaweza kutumiwa na ofisa yoyote mwandamizi wa Serikali.

Kabla ya Profesa Assad kuingia katika nyumba hiyo, ilikuwa ikitumiwa na CAG aliyestaafu, Ludovick Utouh.

UNUNUZI SAMANI ZA NDANI

Pamoja na hali hiyo ofisi hiyo ya CAG ilikiuka sheria na taratibu za Serikali kutokana na kiongozi wa taasisi hiyo ya umma kulipwa posho ya Sh milioni 18 kwa ajili ya kununua samani za ndani ambazo hubadilishwa kila baada ya miaka mitano.

Katika kutekeleza stahiki yake hiyo, Profesa Assad alikwenda mwenyewe Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kwa ajili ya kununua samani hizo za ndani Desemba 27, mwaka juzi.

Inadaiwa katika safari hiyo CAG alikiuka sheria na taratibu za Serikali kwa kutumia zaidi ya Sh milioni 18, ambazo zinaruhusiwa kwa “KUNDI A” la viongozi kwa mujibu wa waraka wa Idara Kuu ya Utumishi (Ofisi ya Rais) namba 1 wa mwaka 2014.

Baada ya kununua samani hizo, ofisi yake ililipa fedha za ziada kiasi cha Sh milioni saba kwa ajili ya kuzisafirisha, pamoja na dola za Marekani 4,265 (sawa na shilingi milioni 9) kwa ajili ya kodi, visa na gharama nyingine za usafiri.

UNUNUZIWA SHANGINGI

Mei 13, 2015 ofisi hiyo ya CAG ilimwandikia barua Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) barua yenye kumbukumbu namba FA.242/305/01 yenye kichwa cha habari; “UNUNUZI WA GARI MOJA KWA AJILI YA MATUMIZI YA CAG TOYOTA LAND CRUISER GX-V8 200 HIGH.”

Baada ya Mtendaji Mkuu wa GPSA, J. Mwambega kupokea barua ya ombi hilo, alimjibu kwa barua ya Mei 15, mwaka jana, yenye kumbukumbu Na. CAD.124/318/01/64.

Sehemu ya barua hiyo ambayo nakala ilipelekwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha inasomeka; “Napenda kukujulisha kwamba ombi lako la ununuzi wa dharura halikubaliki kwa sasa kwa sababu upo utaratibu ulioandaliwa na Serikali kwa ajili ya ununuzi wa magari ya viongozi.

“Kwa kuzingatia hilo, nakushauri ulipie gharama za ununuzi wa gari hilo US $ 84,480.05 kupitia akaunti ya GPSA – UNUNUZI WA MAGARI KWA PAMOJA yenye Na. 0250095100500 ‘US$ Account’ iliyopo benki ya CRDB Bank (Plc) Tawi la Vijana, Dar es Salaam.”

Pamoja na maelekezo hayo, ofisi hiyo ya CAG ilikiuka maelekezo ya Mtendaji Mkuu wa GPSA na kununua gari hilo kwa dharura, ambapo malipo yalifanyika Mei, 15, 2015.

SAFARI YA SEYCHELLES, CHINA

Septemba 5, mwaka jana maofisa kadhaa akiwamo Profesa Assad walisafiri kikazi kwenda nchini Seychelles, ambapo Septemba 11, waliondoka nchini humo na kwenda Dubai, Septemba 12 waliondoka Dubai kwenda Nanjing (China), Septemba 19, waliondoka Shanghai kwenda Beijing na Septemba 22, waliondoka Beijing kurejea Dar es Salaam.

Uchunguzi umebaini kuwa ukiacha safari ya Seychelles ambako kulikuwa na mkutano wa wakaguzi wa hesabu, safari ya China haikuwa na uhusiano na majukumu ya kiofisi, ambapo tiketi za ndege ziligharimu Sh milioni 26.4.

Mbali ya CAG, ofisa mwingine kutoka ofisi yake, Edwin Rweyemamu, naye alisafiri kwa mzunguko kama huo, ambapo tiketi yake iligharimu Sh mil 21.7.

Ofisa wa tatu ambaye hakwenda Seychelles, lakini aliambatana na CAG kwingineko ni Elibariki Lyatuu, ambaye tiketi yake iligharimu Sh milioni 21.4.

Wote walisafiri kwa kutumia daraja la “Business Class” ambapo jumla ya gharama za tiketi zote tatu ilikuwa Sh mil 69.6, gharama ambazo zinatajwa kuwa kubwa kulinganisha na gharama halisi za safari kwenda nchi hizo, gharama ambazo hubadilika kutegemea na msimu wa safari.

Uchunguzi wa MTANZANIA ulibaini fedha hizo zilikopwa kutoka fungu la fedha za Umoja wa Mataifa (UN) zinazotumika katika shughuli mbalimbali ya ukaguzi wa hesabu, ambapo ofisi ya uhasibu ilisema katika dokezo.

Dokezo hilo linasomeka; “Lipa Sh 69,659,200 kwa ajili ya tiketi za safari ya CAG na ujumbe wake nchini Seychelles na China. Fedha hii ilipwe toka UN, lakini tukumbuke kuirudisha mara tutakapopokea mgawo wa fedha ujao.”

KAULI YA CAG

MTANZANIA ilipomtafuta Profesa Assad na kufanya mahojiano naye Alhamisi iliyopita ofisini kwake, alikataa kujadili au kuzitolea ufafanuzi tuhuma dhidi yake.

“Kwanza unajua ni makosa kuwa na nyaraka za ofisi ya Serikali, sasa kama ukiandika basi na sisi tutachukua hatua. Pia hayo yote uliyosema mimi sihusiki, watafute watendaji wakupe majibu,” alisema Profesa Assad.

Pamoja na kutoa majibu hayo, alisema atahakikisha anampata mfanyakazi anayetoa siri za ofisi na kumfukuza kazi mara moja.

Baada ya mwandishi kuagana na CAG na kuondoka, akiwa nje ya ofisi hizo, ofisa mmoja ambaye alihudhuria mahojiano hayo, alimwita na kumwomba nakala ya nyaraka husika, ambapo alipewa, lakini hakuna majibu au maelezo yoyote ambayo yalitoka baada ya hapo.

MAJUKUMU YA CAG

Kwa mujibu wa sheria, majukumu ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ni pamoja na kuhakikisha wizi, upotevu na ufujaji wa fedha na mali za umma unadhibitiwa mapema, kwa kufuata taratibu za uhasibu na kanuni za fedha.

Majukumu mengine ni kusaidia utendaji wa mara kwa mara kwa kutathmini taratibu za fedha, ili kuhakikisha kuwa zinafaa kwa wakati uliopo na zinakidhi makusudi ya kuwapo taratibu hizo.

Viwanja vinauzwa Arusha. Havina dalali.


Hivi viwanja vinauzwa Njiro Arusha. 
Vimepimwa.
Direct contact, Mzee Elias Mshiu - 0754339466. 
Hakuna dalali.

Anwani za makazi kuanza kutumika mwezi Machi mikoa ya Arusha, Dar, Dodoma na Unguja

Anwani za makazi zinatarajiwa kuanza rasmi kutumika ifikapo Machi mwaka huu kwa mikoa ambayo miji yake imekamilika uwekaji wa anwani hizo.

Mikoa ambayo hadi sasa imeshawekewa awuani za makazi katika miji yake ni Dar es Salaam, Dodoma, Arusha na Unguja.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Ally Simba alisema matumizi rasmi ya mfumo huo, yataanza kutumika mwezi Machi huku akisema wamejipanga kuliboresha shirika hilo ili litoe huduma zote za serikali.

Alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu kuhusu maadhimisho ya Siku ya Posta Afrika ambayo Tanzania ni mwanachama wake.

“Shirika la Posta nchini litaboresha huduma zake na kuhakikisha kuwa mbali na kusafirisha barua a vifurishi vingine lakini linatoa huduma zote za serikali kwa wananchi badala ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo mahali kwengine,” alisema Dk Simba.

Dk Simba alisema kuwa halmashauri za miji, mitaa na vijiji, zinatakiwa zitoe ushirikiano kufanikisha ulinzi wa miundombinu ya anwani za makazi na na kutenga fungu katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo wa anwani za makazi nchini kote.
via HabariLeo

Makazi Mkwajuni yabomolewa leo chini ya ulinzi wa askariPOLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia wananchi kadhaa, wakituhumiwa kufanya fujo na kufunga barabara ya Kawawa kwa muda na kuchoma matairi.

Kauli ya NEC kuhusu habari iliyochapishwa na MwanaHALISI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU UPOTOSHWAJI WA TAARIFA ZILIZOANDIKWA NA GAZETI LA MWANAHALISI KUHUSIANA NA UCHAGUZI WA UBUNGE JIMBO LA KIJITOUPELE


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inapenda kutaarifu Umma na Watanzania kwa ujumla kuwa Jimbo la Kijitoupele lililoko Zanzibar ni miongoni mwa Majimbo hamsini(50) ambayo yalitegemewa kufanya uchaguzi mkuu tarehe 25, oktoba,2015.

Hata hivyo Jimbo hilo halikufanya uchaguzi wake wa Mbunge kutokana na hitilafu katika karatasi za kupigia kura badala Wapiga kura walishiriki katika kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Tume imefikia uamuzi wa kutoa ufafanuzi huu kutokana na taarifa iliyochapishwa na gazeti la MwanaHalisi toleo l Na.322 la Januari 18, 2016 katika ukurasa wake wa mbele likidai “ NEC YAIBUA MAPYA” Habari hii si sahihi na inalenga kuupotosha umma na kuleta uchochezi miongoni mwa Wananchi.

Kwa ujumla maelezo yote yaliyopo katika taarifa hiyo yanaeleza kwamba, Tume imeanzisha Jimbio jipya, kwa mujibu wa taarifa ya gazeti husika ni Jimbo la Kijitoupele – Zanzibar.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda inasisitiza kuwa taarifa zilizotolewa na Gazeti la MwanaHALISI siyo za kweli, ni za uongo, uzushi, uzandiki na uchochezi. Kufuatia taarifa hiyo,Tume inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:

• Tarehe 13 Julai, 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari ikionesha Orodha ya Majimbo yatakayofanya uchaguzi wa Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na Jimbo la Kijitoupele lipo katika Orodha hiyo. Taarifa hii ipo katika tovuti ya Tume.

• Katika Taarifa hiyo, Tume ilieleza wazi kuwa Majimbo ya Zanzibar yataendelea kuwa hamsini (50), ingawaje Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeongeza majimbo manne na kuwa Hamsini na Nne (54).

• Tulieza sababu ya kubaki na Majimbo hamsini (50) ni kutokana na matakwa ya Ibara ya 98 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo ili kuongeza idadi ya wabunge kutoka Zanzibar inahitaji theluthi mbili ya Wabunge kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge kutoka Zanzibar kuunga mkono mabadiliko hayo.

• Tulieza kuwa, kipindi hicho Tume isingeweza kuandaa na kuwasilisha Muswada Bungeni kwa kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilikuwa linamaliza muda.

• Katika taarifa hiyo, ilifafanuliwa kuwa, ili kubaki na majimbo Hamsini (50), kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, majimbo manne yaliunganishwa kwa ajili ya Uchaguzi wa Wabuge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaotoka Zanzibar.

• Majimbo yaliyounganishwa ni:

1. Jimbo la Bububu liliunganishwa na Jimbo la Mtoni, likaitwa jimbo la Bububu
2. Jimbo la Mwera liliunganishwa na Mto pepo likaitwa jimbo la Mwera
3. Jimbo la Kiembesamaki liliunganishwa na Chukwani likaitwa jimbo la Kiembesamaki
4. Jimbo la Pangawe liliunganishwa Kijitoupele likaitwa Kijitoupele

• Kwa mantiki hiyo Jimbo la Kijitoupele ni mojawapo ya Majimbo hayo (50) ambayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilisimamia na kuratibu Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge.

• Tarehe 28 Oktoba, 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa taarifa kwa Umma kuwa, ilishapokea Matokeo ya Kura za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa kutoka Majimbo yote ya Zanzibar na siyo “siyo Matokeo ya Ubunge”

• Tarehe 19 Desemba, 2015 Tume ilitoa orodha ya Majimbo ambayo hayajafanya Uchaguzi wa Wabunge tarehe 25 Oktoba, 2015 kutokana na hililafu mbalimbali, mojawapo ya majimbo hayo nane (8), jimbo la Kijitoupele - Zanzibar ni miongoni.

Ni vema wananchi wakafahamu kwamba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi haianzishi na haijaanzisha Jimbo jipya la Uchaguzi baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.

Hii inaonesha ni kiasi gani Mhariri wa Gazeti la MwanaHALISI alivyodhamiria kuupotosha Umma kwani katika Makala/Taarifa hiyo hiyo ambayo anadai hakuna Jimbo la Kijitoupele (Unguja); anaeleza kuwa tarehe 25 Oktoba 2015 wapiga Kura wa Jimbo la Kijitoupele walikosa fursa ya kumchagua Mbunge. Amemtaja Mhariri wa Gazeti la MwanaHALISI kuwa ni Wapiga Kura wa Jimbo la Kijitoupele, ambalo anadai eti Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeliibua miezi mitatu baada ya Uchaguzi. Huu ni uongo na upotoshwaji wa makusudi kabisa.

Tume inapenda wananchi waelewe kuwa, hata kabla Tume ya Uchaguzi haijafuta matokeo wa Zanzibar, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikuwa imesha tangaza kuahirisha Uchaguzi katika Majimbo nane (8) likiwemo la Kijitoupele kwa sababu za Vifo vya Wagombea na hitilafu mbalimbali.

Jimbo la Kijitoupele la Zanzibar ni miongoni mwa majimbo nane (8) ambayo yaliahirishwa kufanya uchaguzi wa Wabunge tarehe 25 Oktoba, 2015, ambapo majimbo sita (6) ambayo ni Lushoto, Ulanga Mashariki, Masasi Mjini, Ludewa, Handeni Mjini na Arusha Mjini yaliahirishwa kutokana na vifo vya wagombea na majimbo mawili (2) ya Kijitoupele - Zanzibar na Jimbo la Lulindi – Masasi yaliahirishwa kutokana na hitilafu mbalimbali.

Hoja nyingine iliyotolewa na gazeti hilo ilihusu uteuzi wa Uteuzi wa Wabunge wa Viti Maalum. Ifahamike kwamba katika maamuzi yake kuhusiana na viti maalum, Tume imezingatia matakwa ya Ibara ya 78 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayoeleza kuwa, ili chama kilichoshiriki Uchaguzi Mkuu kipate Viti Maalum ni lazima kiwe kimepata angalau asilimia tano (5%) ya Kura zote halali za Ubunge. Hivyo, Viti Maalum vilivyobaki haviwezi kugawanywa hadi hapo Jimbo la Kijitoupele litakapofanya Uchaguzi katika tarehe ambayo itaitangazwa na Tume hapo baadaye.

Mhariri wa Gazeti la MwanaHALISI alipaswa kufanya uchunguzi na uchambuzi wa kina kuhusu habari aliyoiachapisha ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Viongozi wa Tume ya Uchaguzi ili wapate ufafanuzi wa Majimbo ya Uchaguzi na siyo kutoa Taarifa za uongo, uchochezi na upotoshaji kama walivyofanya.

Mhariri wa Gazeti la MwanaHALISI atambue uandishi wa habari ni zaidi ya kushika kalamu na kuandika, unahusisha uwezo wa kutafuta habari pande zote mbili ili kupata mizania ya habari anayoiandika, kufanya utafiti, kujiridhisha pasipo shaka kuwa habari anayoitoa ni sahihi.

Kwa kuwa Mhariri wa Gazeti la MwanaHALISI alikusudia kuupotosha umma kwa sababu anazozifahamu yeye mwenyewe kwa kutoa Taarifa zisizo sahihi, za uongo na uchochezi Tume ya Taifa ya Uchaguzi inamtaka Mhariri wa MwanaHALISI KUIOMBA RADHI TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI, UKURASA WA MBELE WA TOLEO LIJALO KAMA ALIVYOFANYA KATIKA GAZETI HILO.

Kama wasipofanya hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi italichukulia Gazeti la MwanaHALISI hatua za Kisheria.

Imetolewa na
Kailima, R.K
MKURUGENZI WA UCHAGUZI.

Kailima, R.K
Kailima, R.K

Wito wa WM Majaliwa kwa Tanzanian Diaspora alipozungumza na wanaoishi Botswana

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watanzania waishio Botswana baada ya kuhudhuria mkutano wa SADC mjini Gaborone Januari 18, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kufungua viwanda vya kusindika ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam ili kutoa soko kwa ngozi za wanyama wanaochinjwa kwenye machinjio ya mikoa hiyo.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Januari 18, 2016) wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania waishio Botswana kwenye kikao kilichofanyika kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.

Waziri Mkuu alikuwa nchini Botswana kwa ziara ya siku moja kumwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa SADC Double Troika yaani kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na Wakuu wa Nchi wanaounda Chombo cha Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics, Defense and Security Cooperation) uliofanyika kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana

Akizingumza na Watanzania hao, Waziri Mkuu alisema: “Tumeamua kufungua viwanda vya kusindika ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam (kule Pugu) ili ngozi zikishachunwa, zipelekwe moja kwa moja kiwandani,” alisema.

Alisema Serikali imeamua kuongeza viwanda nchini kama njia mojawapo ya kukuza uchumi, kuacha kuuza mali ghafi lakini pia ni fursa ya kuongeza ajira kwa Watanzania.

Akijibu hoja zilizoainishwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu alisema Serikali bado ina nia ya kuhamia Dodoma na kwamba itaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingi zijenge ofisi zao Dodoma. “Serikali ilikwishaamua kwamba Dodoma ni mji wa kiserikali na Dar es Salaam ni mji wa kibiashara. Kwa sasa kuna baadhi ya Wizara zimeshajenga ofisi Dodoma na kuna taasisi kama vile Benki Kuu nazo pia zimejenga ofisi zake Dodoma. Tutaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingine zikamilishe ujenzi wa ofisi zao,” alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) watafute fedha za mitaji ama zao ama kupitia kwa marafiki zao ili waweze kuwekeza nyumbani (Tanzania).

“Nia ya Serikali sasa hivi ni kufungua milango kwa wawekezaji hasa wenye nia ya kujenga viwanda. Njooni nyumbani muone ni eneo gani mnaweza kuwekeza, kama mna miradi huku fungueni matawi kule nyumbani. Serikali inajivunia uwepo wenu kwa sababu inatambua kwamba huku mliko kuna kitu mnajifunza na mnaweza kukirudisha nyumbani kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla,” alisema.

Mapema, akisoma risala yao kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha Watanzania waishio nchini Botswana (The Association of Tanzanians in Botswana – ATB), Bw. Neiman Kissasi alisema chama hicho kilianzishwa mwaka 1992 kikiwa na lengo la kuwaunganisha Watanzania waishio Botswana pamoja kujenga undugu wao na kusaidiana.

Katika risala yao, walishauri wafugaji wa Tanzania waelimishwe na kuwezeshwa kufuga kisasa na kuondokana na ufugaji wa kurandaranda. Pia waliiomba Serikali iongeze kasi ya mpango wake wa kuhamisha shughuli zote za Serikali mjini Dodoma, kwani itasaidia kupunguza matumizi ya Serikali kwa kuwa shughuli za Serikali zitakuwa zinafanyika eneo moja.

Vilevile, waliiomba Serikali ifungue fursa za kiuchumi kwenye mikoa mingine ya Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Arusha badala ya kuziacha ziwe Dar es Salaam peke yake. “Hii itasaidia kuibua fursa za kiuchumi na kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam”, ilisema sehemu ya risala yao.

Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam jana usiku (Jumatatu, Januari 18, 2016.)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM

JUMANNE, JANUARI 19, 2016