"Overview" ya gharama ya kumsomesha mtoto shule za binafsi Tanzania


Wakati Serikali ikihaha kuandaa mwongozo kwa vyuo na shule binafsi za msingi na sekondari ili kudhibiti viwango vya ada, hali ni tofauti kwenye shule za kimataifa ambazo zinaonekana kama zinachuana kwa kuwa na ada kubwa.

Wakati ada ya juu kwa shule zinazotumia Kiingereza kuanzia elimu ya msingi ni kati ya Sh2 milioni na Sh3 milioni, ada ya shule za kimataifa zilizopo nchini inafikia hadi Sh60 milioni mwa mwaka, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwenye shule mbalimbali za jijini Dar es Salaam na baadhi ya mikoa.

Uchunguzi huo unaonyesha kuwa mwanafunzi wa chekechea hutakiwa kulipa hadi Sh35 milioni kwa mwaka na fedha hizo hulipwa kwa kutumia dola ya Marekani.

Baadhi ya shule zinapokea wanafunzi wenye asili ya Asia, nyingine hupokea wanafunzi kutoka nchi tofauti bila ya kubagua na ni dhahiri kuwa hata wazazi wa watoto ni wale wa kipato kikubwa.

Shule nyingi zinatumia Kiingereza katika kufundisha masomo yote darasani kwa mitalaa ya kimataifa na walimu wa kigeni ambao wanalipwa mishahara kwa viwango vya kimataifa.

Wanafunzi wanaosoma katika shule hizo wanaishi mazingira tofauti na wanaosoma katika shule za kawaida. Mwananchi lilishuhudia baadhi ya wanafunzi wa kike wakiwa wamevaa kaptura, bukta na sketi zinazoacha wazi mapaja, kufuga rasta huku wavulana wakiwa huru kufuga nywele, na kuvaa hereni bila kubanwa na sheria.
Kwa kuzingatia nyaraka za kujiunga na shule ya International School of Tanganyika (IST) iliyoko Masaki, ada ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili wa chekechea ni Sh35.9 milioni; darasa la tatu hadi la tano ada ni Sh 39.8 milioni na kwa wale wanaoingia darasa la sita, la saba na la nane ni Sh46. 3 milioni huku darasa la tisa na la kumi ada ni Sh49.2 milioni.

Mchanganuo wa ada kwa mwanafunzi anayeingia darasa la 11 na 12 ni Sh 59.4 milioni. Mbali ya ada hiyo, mwanafunzi hutakiwa pia kulipiwa gharama za ujenzi, ada ya dharura, fomu ya kujiunga shuleni pamoja na michango mingine ambavyo jumla ni Sh 19.8 milioni.

Shule nyingine ambayo tozo zake - ada na michango mingine – imefuata mkondo huo Braeburn iliyoko barabara ya Bagamoyo, Africana. Ada ya mwanafunzi wa chekechea ni Sh 12.7 milioni kwa mwaka.

Mwaka wa kwanza na wa pili ambao ni sawa na darasa la kwanza na la pili hulipa Sh19.3 milioni. Darasa la tatu hadi la sita Sh21.1 milioni na darasa la saba hadi la tisa (sekondari) ni Sh25.4 milioni. Mwanafunzi anayejiunga na shule ya msingi ya Readers Rabbit iliyoko Masaki hutakiwa kulipa kiasi cha Sh24.1 milioni kwa mwaka.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco), Benjamin Nkonya alitetea ada hizo.

“Zinatumia mitalaa ya kimataifa ambayo Tanzania haina walimu wanaoweza kuitumia katika kufundisha. Pia, walimu hao wanalipwa kwa mishahara ya viwango vya kimataifa,” alisema
Nkonya ambaye wanachama wake wanapambana na Serikali dhidi ya uamuzi wa kuweka ada elekezi, alisema sababu nyingine za shule hizo kutoza ada kubwa ni gharama kubwa za vibali vya kufanya kazi na kuishi nchini ambavyo hufikia Sh7 milioni kwa miaka miwili, na pia huduma zake.

“Gharama zake lazima zitakuwa juu kuliko za kwetu. Kwa mfano, mwanafunzi wa shule za kimataifa anatakiwa akaone Mlima Alps au Everest,” alisema.

Lakini lengo la shule hizo kufundisha kwa kutumia mitalaa ya nje ni kuepuka kuwavuruga wanafunzi wa mataifa mengine ambao tayari walishaanza kutumia mitalaa hiyo.

Kadhalika, Nkonya alisema shule hizo hazina madhara kwa wanafunzi wa Kitanzania kwani wanajifunza tamaduni za kigeni na kuchangamana na mataifa mengine.

Sababu nyingine ya shule hizo kutoza ada kubwa alisema ni masomo ya ziada kama kuogelea (lazima), kareti na muziki.

Shule ya Aga Khan Tanzania (AKES, T) iliyoko Upanga ni ya kimataifa na inafundisha kwa kutumia mitaala ya Uingereza. Shule hii inatoza ada ya Sh 7.4 milioni kwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili wa chekechea na mwaka wa tatu analipiwa Sh 8.2 milioni.

Darasa la kwanza hadi la sita ada ni Sh 9.4 milioni; sekondari ambayo ni darasa la saba hadi la tisa ada ni Sh 9.9 milioni. Kwa wanafunzi wa darasa la 10 hadi 11 ada ni Sh 10.4 milioni wakati kidato cha tano ni kati ya Sh 20milioni hadi Sh22 milioni kwa mwaka.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Shule ya Kimataifa ya St Constantine yenye sekondari na msingi, inatoza ada ya Sh7 milioni kwa wanafunzi wa chekechea, wakati darasa la kwanza na la pili ni Sh9.5 milioni kwa mwaka na darasa la tatu ni Sh11.7 milioni.

Wanafunzi wa darasa la nne ni Sh12 milioni, la tano (Sh13 milioni), la sita (Sh13.5 milioni) na darasa la saba ambayo ni masomo ya sekondari ada hupanda hadi Sh19.2 milioni, huku darasa la nane na tisa (Sh19.4 milioni) na kidato cha tano na sita ni Sh 21. 7 milioni.
Pia, fedha za dharura, chakula cha mchana na safari ambazo jumla yake ni Sh3.6 milioni.

Shule ya Haven of Peace (Hopac) iliyoko Mbezi Beach, mwanafunzi wa msingi hulipiwa Sh17.2 milioni na sekondari ni Sh20.5 milioni. Gharama nyingine mbali ya ada ni fedha za usaili, ukarabati na ada ya maendeleo ambavyo jumla yake ni Sh 4.9 milioni.

Nyaraka za kujiunga na shule ya msingi Genesis iliyopo Masaki zinaonyesha ada ni Sh6.3 milioni kwa wanafunzi wa chekechea ambao husoma kwa miaka mitatu. Kwa darasa la kwanza hadi la sita, ada ni Sh8.8 milioni na darasa la nane ni Sh9.4 milioni.

Shule ya kimataifa ya Laureate iliyoko Mikocheni inashika nafasi ya nane kwa ada kubwa kwani katika mwaka wa kwanza na wa pili wa chekechea mwanafunzi hutozwa Sh3.5 milioni kwa mwaka. Wanaoingia elimu ya msingi hadi darasa la sita hulipa Sh4.7 milioni.

Sekondari, yaani darasa la saba hadi la tisa ada ni Sh5.6 milioni na darasa la 11 na 12 ni Sh6.6 milioni. Kidato cha tano na sita ni Sh7.6 milioni kwa mwaka na kila mwanafunzi hulipia usafiri Sh1.7 milioni kwa mwaka.

Katika Shule ya Academic International, ada imechanganuliwa kwenye mfumo wa mihula mitatu ambayo mwanafunzi anaweza kuilipa kwa mafungu. Jumla ya ada hiyo kwa mwaka wa kwanza kwa chekechea ni Sh3.4 milioni na kwa wa pili hupungua hadi Sh2.8 milioni.

Wanaoingia darasa la kwanza hadi la sita ada ni Sh2.7 milioni kwa mwaka na darasa la saba hutakiwa kulipa Sh3 milioni. Mchanganuo wa ada kwa kidato cha kwanza na cha pili ni Sh3.8 milioni, kidato cha tatu wasiosoma sayansi ni Sh3.9 milioni na wa masomo ya sayansi hulipa Sh 4.1 milioni.

Kidato cha nne wasiosoma mchepuo wa sayansi ni Sh4.6 milioni na wanaosoma sayansi ni Sh5.1 milioni. Kwa masomo ya kidato cha tano wasiosoma sayansi ada ni Sh5.7 milioni wakati wanaosoma sayansi ni Sh5.9 milioni.

Masomo ya kidato cha sita kwa wanaosoma sayansi ada ni Sh5.9 milioni na wasiosoma sayansi ni Sh6.2 milioni. Pamoja na ada hiyo, kila mwanafunzi ni lazima alipe fedha ya usajili Sh550,000, fomu ya maombi Sh150,000 na usafiri kwa kila mwanafunzi Sh1.1 milioni kwa mwaka.

Tozo za ada kwa shule ya East Africa International ni nafuu ikilinganishwa na shule nyingine za kimataifa zinazofundisha kwa kutumia mitalaa na mihtasari ya Uingereza. Kwa mwanafunzi wa shule ya msingi, ada ni Sh2.7 milioni na shule za sekondari ni Sh3.0 milioni. Ada hii inajumuisha pia usafiri, kuogelea, kifungua kinywa na fedha ya kujisajili.

Shule za Feza International za chekechea, msingi na sekondari zilizoko Kawe, Mikocheni, na Tegeta kwa wasichana na wavulana hutegemea ngazi ya elimu.

“Mtoto wa shule ya msingi analipiwa Sh4 milioni kwa mwaka na yule anayeanza sekondari analipia zaidi ya Sh7 milioni. Kwa shule ya msingi ada pekee ni Sh2.9 milioni bila kuhusisha gharama nyingine kama chakula, malazi, vifaa na usajili,” alieleza mmoja wa wazazi ambaye ana mtoto wake anasoma moja ya shule hizo.

Ada ya Sh60 milioni yatetewa Dar


Tofauti ya ubora wa elimu, mazingira ya kufundishia, mishahara kwa walimu na miundombinu ndicho chanzo cha kuwapo matabaka kati ya shule za kimataifa na za kawaida, kwa mujibu wa wadau waliohojiwa na Mwananchi.

Gazeti la Mwananchi lilihoji wadau mbalimbali wa elimu baada ya kuchapisha habari iliyoonyesha ukubwa wa viwango vya ada vinavyotozwa na shule za kimataifa ikilinganishwa na ada za shule binafsi za kawaida ambazo wanafunzi wake hutahiniwa na Baraza la Taifa la Mitihani la Taifa (Necta).

Katika habari hiyo iliyochapishwa jana, gazeti hili lilionyesha ada za baadhi ya shule hizo za kimataifa kufikia hadi Sh60 milioni kwa mwaka huku chekechea ikitoza hadi Sh35 milioni kwa kipindi hicho.

Pamoja na viwango hivyo vikubwa, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Hakielimu, James Kalaghe alisema shule hizo zinatoza ada kubwa kwa sababu zinatumia mfumo wa kimataifa, mazingira mazuri ya kusomea na walimu bora.

Kalaghe alisema matabaka yaliyopo katika elimu yanasababishwa na uduni wa shule za umma ambazo zinachukua asilimia 94.7 ya wanafunzi wote nchini.

Pia, alisema shule za kimataifa zinawalenga raia wa kigeni waliopo nchini, kama mabalozi na wale wanaofanya kazi katika taasisi za kimataifa zikiwamo za Umoja wa Mataifa.

“Sisi wadau wa elimu na Serikali tushughulike na shule za umma ambazo zina wanafunzi wetu. Usawa katika elimu hauwezi kupatikana kama hatutaboresha mazingira ya shule za umma,” alisema.

Alisema inaonekana shule binafsi zina viwango bora vya elimu, walimu wenye taaluma ya kutosha na wasimamizi wazuri.

“Walimu wa shule za umma wana msongo wa mawazo, hawana hela ya likizo, hawapewi stahiki zao hata wakihamishiwa vijijini. Ili usawa uwepo, shule za umma ziimarishwe ili zitoe elimu bora, tuwasimamie stahiki zao, tuwalipe vizuri,” alisema.

Mkuu wa Kituo cha Elimu (Duce), Dk Joviter Katabaro alisema kama shule si ya kimataifa inatoza ada hadi Sh60 milioni, basi mfumo huo unajenga matabaka.

“Ni bahati mbaya kwamba bado tunasubiri wizara kutoa mchanganuo wa ada elekezi katika shule binafsi.

“Ni sawa na hoteli, kila mtu anatoa bei yake kwa sababu hakuna mtu wa kumwambia,” alisema.

Hata hivyo, alisema iwapo shule inayoitwa ya kimataifa inatoza ada kubwa basi aghalabu wanaopeleka watoto hapo wanataka wafuate mitalaa ya kimataifa na wanapanga ada hizo kwa utaratibu wa kimataifa.

“Lakini tujue kuwa hiyo shule imewekwa kwa ajili ya watu gani, mabalozi au watu wengine kutoka nje, kwenye ngazi za kimataifa, labda UNDP, UNHCR. Huenda watoto wao wanatakiwa kupelekwa. Kwa hiyo matabaka hayo yameanzia kwenye aina ya kazi na utaifa,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Chris Maina alisema ni vyema kusubiri kwanza Serikali itakachozungumza kuhusu ada elekezi ili kuwasikia wenye shule hizo za kimataifa na watakachosema. “Nasubiri Serikali itatumia vigezo gani kuweka ada elekezi na wamiliki wa shule binafsi watachukua uamuzi gani. Inashangaza kuona mwanafunzi wa chekechea analipa ada kubwa kuliko mwanafunzi wa chuo kikuu,” alisema.

Hata hivyo, Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa alisema amesikia taarifa za shule za kimataifa kutoza ada kubwa na kuzungumza na timu yake kwa ajili ya kufuatilia.

“Ingawa hatuhusiki moja kwa moja na shule za kimataifa, lakini lazima tukisikia taarifa kama hizo tuzifuatilie. Kimsingi tunafahamu shule chache zinazotoza ada kubwa,” alisema Bhalalusesa.

Alisema ingawa yupo likizo, amesoma taarifa hizo kisha kuzungumza na msaidizi wake ili kujua kwa kina kuhusu ada hizo.

Kalamu maalumu za UKAWA zilizotumika katika uchaguzi wa MameyaKila kukicha watu hubuni mbinu ili wafanikiwe kwenye jambo fulani. Hivi ndivyo ilivyotokea Januari 16, kwa Ukawa kuja na mbinu ya kununua kalamu maalumu ya kuandikia na kupiga picha wakati wa upigaji kura wa uchaguzi wa mameya wa manispaa za Kinondoni na Ilala za jijini Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo, Diwani wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob alishinda umeya wa Kinondoni kwa kura 38 dhidi ya 20 alizopata Benjamin Sitta wa CCM. Naibu Meya alichaguliwa Jumanne Mbunju wa Kata ya Tandale (CUF) aliyepata kura 38 dhidi ya 19 za John Manyama (CCM).

Kwa upande wa Ilala, aliyeshinda ni Charles Kuyeko (Chadema) aliyepata kura 31 na naibu ni Omari Kumbilamoto (CUF) ambaye pia alipata kura 31 za madiwani wa Ukawa baada ya wale wa CCM kususia.

Kabla ya uchaguzi huo, kulikuwa na vuta nikuvute na ushindani mkali, hali iliyosababisha Ukawa kuwa na wasiwasi wa kuhujumiwa na hivyo kuandaa mazingira ya kushinda, ikiwamo kununua kalamu hizo.

Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa Ukawa ambaye hakutaka kutajwa jina lake, viongozi walibuni mkakati huo uliowagharimu takriban Sh30 milioni katika ununuzi wa kalamu za kupigia kura na wakati huo huo kuwapiga picha wanaozitumia na kuandaa sehemu ya kufuatilia jinsi kura zilivyopigwa.

Kila mjumbe alipewa kalamu yenye jina lake na kuitumia katika upigaji wa kura.

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee aliliambia Mwananchi kuwa waliamua kufanya hivyo baada ya Manispaa ya Temeke ambako madiwani wawili Ukawa waliipigia kura CCM.

“Ukiumwa na nyoka lazima ukiona jani ushtuke, hiki ndiyo tulichokifanya baada ya madiwani wetu wawili kutusaliti,” alisema Mdee.

Alisema walishanusa harafu ya rushwa kwa baadhi ya madiwani wao kuhongwa fedha kupitia kwa mmoja wa maofisa wa Chadema makao makuu.

Alisema baada kusikia taarifa hizo, walikaa chini na kutafakari na kuja na mbinu hiyo ambayo imekuwa mwarobani wa kuhakikisha Ukawa wanapata kura sahihi za wajumbe wake.

“Wanakinondoni wangetushangaa kama tungekosa umeya kwa idadi ya madiwani waliotupatia,” alisema Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha).

“Kuna wajumbe mnakubaliana vizuri, lakini wakifika kwenye sanduku la kura wanabadilika. Kalamu imetusadia sana kwani tulikuwa 38, CCM 20, kura zilivyopigwa tulizipata zote kama tulivyotarajia,” alisema.

Alifafanua kuwa walimweka mtu maalumu wa kufuatilia mwenendo wa kila mjumbe wa Ukawa wakati wa kupiga kura.

“Kama nilivyosema juzi zile kalamu ukifungua tu ina kamera. Ukianza kuitumia kuna mtu maalumu aliyetarishwa kwa ajili ya kuangalia wajumbe wote wa Ukawa wanaopiga kura,” alisema.

Hata hivyo, alisema licha ya baadhi ya wajumbe wa Ukawa kuchukua fedha, lakini wametimiza wajibu wao wa kuhakikisha meya anakuwa chini ya umoja huo na iwe fundisho siku nyingine kwa wajumbe wao wengine.

Akizungumzia umeya wa Dar es Salaam, Mdee alisema wanajipanga vyema ili kuhakikisha jiji hilo linakuwa chini ya Ukawa kwa kuwa wana hazina kubwa ya madiwani wakataowawezesha kuibuka kidedea.

“Kwenye umeya wa Jiji tutakuja na staili tofauti, hizi tulizozitumia katika manispaa za Ilala na Kinondoni, tunaziboresha na tuna uhakika wa kunyakua umeya wa Dar es Salaam,” alisema Mdee.
  • via MWANANCHI

Yanayokwamisha mazungumzo ya muafaka wa kisiasa Zanzibar

Wakati hatua ya aliyekuwa mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif, ya kujitoa kwenye mazungumzo ya maridhiano yaliyokuwa yakiendelea visiwani Zanzibar ikiwa imeacha mshangao kwa wananchi, Nipashe imebaini siri ya kujiondoa kwake.

Maalim Seif alijiondoa katika mazungumzo ya kutafuta maridhiano ya muafaka katika kamati iliyowajumuisha Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Dk. Salmin Amour Juma, Amani Abeid Karume na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Katika kamati hiyo iliyowahi kukutana mara tisa kwa nyakati tofauti ili kutatua mgogoro huo bila ya kufikiana muafaka, inaelezwa kuwa kulikuwa na mvutano mkubwa kati ya wastaafu hao na Maalim Seif.

Kutopatikana kwa muafaka wa vikao hivyo, Januari 11, mwaka huu, Maalim Seif alitoa sababu kadhaa za kutotaka uchaguzi huo kurudiwa huku akimwomba Rais Dk. John Magufuli kuingilia kati mgogoro huo ili kupatikane kwa muafaka wa haraka.

KWA NINI SEIF AMEJITOA

Baada ya kuwapo kwa usiri mkubwa wa vikao vilivyokuwa vinafanyika katika kutafuta muafaka huo, Nipashe katika uchunguzi wake imebaini sababu saba zilizomfanya Maalim Seif kung’atuka kutoka katika kamati hiyo.

TOFAUTI ZA KIITIKADI 

Historia iliyokuwapo tangu miaka ya 1950 ya tafauti za kiitikadi na kisiasa, bado zinaendelea kujitokeza hadi miaka ya sasa na kusababisha kurithishana kwa chuki kwa vizazi hadi vizazi.

Hali hiyo imejitokeza katika sherehe za mapinduzi zilizofanyika Januari 12, mwaka huu, pale baadhi ya wanachama wa CCM walipobeba bango lenye maneno “Machotara Hizbu waondoke Zanzibar ni nchi ya Waafrika”

Chuki iliyokuwapo baina ya chama cha ZNP na ASP miaka ya nyuma hadi kufanyika kwa Mapinduzi 1964, baada ya ASP kuungana na Umma Party na kuiangusha ZPPP bado inaendelea kujitokeza sasa baina ya CUF na CCM, huku ubaguzi huo ukijitokeza CUF ikitawala Pemba na baadhi ya maeneo ya Unguja na CCM kutawala Unguja

UHAFIDHINA

Hii mi moja ya sababu zilizofanya kiongozi huyo kujiondoka katika mazungumzo kwa sababu ya dhana ya kuwapo kwa makada ndani ya CCM wasiotaka mabadiliko ndani ya nchi.

Kuwapo kwa wanachama wenye msimamo mkali ndani ya CUF na CCM wasiobadilika kimtazamo, nayo ni sababu ya Maalim Seif kujiengua katika mazungumzo hayo.

Kwa mfano baadhi ya wanachama wa CUF kumtuhumu Maalim Seif kuwasaliti inadhirisha wazi kuwapo kwa misimamo mikali ndani ya vyama hivyo.

Ndani ya CCM kuna baadhi ya wanachama ambao hawako tayari kukabidhi Zanzibar mikononi mwa CUF, wako tayari kuona CCM ikitawala milele. Hiyo nayo huenda ikawa sababu mojawapo ya kiongozi huo wa CUF kujiengua katika kamati ya mazungumzo.

Tangu kuzaliwa kwa chama cha TANU 1954 hadi kuanzishwa kwa CCM mwaka 1977, chama hicho kimekuwa kikishika dola kwa miaka yote tangu kupatikana kwa uhuru 1961 na hata Mapinduzi 1964.

Kwa mujibu wa CUF na kauli zinazotolewa na Maalim Seif ni kuwa kuanzia mfumo wa vyama vingi kuanza mwaka 1992 na uchaguzi wa kwanza mwaka 1995, CUF imekuwa ikishinda kila uchaguzi unapofanyika lakini CCM imekuwa ikiwapora ushindi huo kwa kuchakachua matokeo.

Hata katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana uliofutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), CUF wanadai kuwa walishinda uchaguzi huo, hivyo CCM wakatumia mbinu ya kufuta uchaguzi ili wapate mwanya wa kujipanga upya.

MUSTAKABALI WA MUUNGANO

Dhana ya kuwapo kuvunjika kwa Muungano kwa wananchama wa CCM endapo CUF itaongoza Zanzibar ni mojawapo ya sababu inayofanya CCM Zanzibar kutokukubali kuikabidhi nchi kwa upinzani.

Dhana hiyo pia ni sababu ya uchaguzi Zanzibar kufutwa na kutakiwa kurudiwaa, kwa dhana kuwa CUF inasimamia kuwapo kwa serikali tatu na mamlaka kamili, hivyo Muungano huenda ukavunjika.

Uwapo wa dhana hiyo na kufanyika kwa vikao mara tisa vilivyowajumuisha marais wastaafu kwa ajili ya kutafuta muafaka pasipo kuwapo kwa kiongozi mwingine zaidi ya Maalim Seif, huenda ndiyo sababu pia ya kujitoa kwake katika mazungumzo.

HAKUNA KIONGOZI WA KUKEMEA

Kutokuwapo kwa kiongozi mwenye uwezo wa kukemea mambo mabaya na maovu ambayo yanaweza kuitumbukiza nchi katika machafuko nako kumesababisha Maalim Seif kujitoa katika mazungumzo hayo.

Wakati wa uchaguzi wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi tangu baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 ulifanyika mwaka 1995 ambapo CCM ilipata asilimia 50.2 na CUF asilimia 49.8, mivutano ya kisiasa ilijitokeza.
Katika sokomoko hilo, CUF ilikataa kuyatambua matokeo hayo na kutomtambua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa wakati huo, Dk. Salmin Amour Juma.

Mivutano ya kisiasa ilijitokeza wazi wazi baina ya vyama hivyo- CUF na CCM, ambapo uhasama na chuzi za kisiasa zilishika kasi. Watu walikuwa hawashiriki hata katika masuala ya kijamii. Kama mtu amefariki dunia kwa mfano, iwapo ni wa CUF basi CCM hawatamzika na vivyo hivyo kwa CCM, CUF hawamziki.

Hatua hiyo ilimfanya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuingilia kati na kuagiza kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). kukosekana kiongozi kama Nyerere kukemea na kutoa uamuzi kumechangia Maalim Seif kujitoa katika mazungumzo hayo.

KAULI ZA CCM NA CUF

Katika kile kilichoonekana ni kuvurugika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa kisiasa visiwani Zanzibar, na kusababisha Maalim Seif kujitoa ni kauli za baadhi ya viongozi wakiwemo wakuu wa CUF, CCM na serikali za Zanzibar.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, katika hotuba yake aliyoitoa Januari 12, mwaka huu, wakati wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, aliwataka wafuasi wa CCM kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio utakaotangazwa na ZEC .

Kutolewa kwa kauli hiyo na kiongozi huyo ambaye ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya kusaka muafaka, huenda imechangia kumvunja imani Maalim Seif kuendelea kuhudhuria vikao vya kamati hiyo na kuamua kujiengua.

Kadhalika, Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, aliwahi kuwaeleza wanachama wa CCM kujiandaa na marudio ya uchaguzi wakati kamati ikiwa bado inaendelea kutafuta muafaka.

Pia aliwataka wana CCM Zanzibar kujiandaa na uchaguzi wa marudio na kuepukana na propaganda zinazotolewa na wapinzani kwamba hakuna uchaguzi mwingine, huku akieleza kuwa kwa upande wao wako katika maandalizi ya uchaguzi mwingine ikiwemo kutayarisha mawakala watakaosimamia.

Vilevile, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Ismail Jusa Ladhu, aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema uchaguzi Zanzibar hauwezi kurudiwa.

Maalim Seif naye amewahi kueleza msimamo wa CUF wa kutotaka uchaguzi urudiwe bali kuendelea kwa kazi ya kuhesabu kura.

MUUNDO WA KAMATI
Hii pia ni sababu nyingine iliyomfanya Maalim Seif kujiweka kando katika kamati ya kutafuta muafaka visiwani humo, hivyo kusababisha sintofahamu na mustakabali wa siasa za Zanzibar.

Jopo la wanakamati wanaounda kamati hiyo ni wanachama wa CCM hata mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Ali Mohammed Shein ni mmoja wa wagombea urais.

Kuwapo kwa Maalim Seif peke yake na kutokuwapo kwa wajumbe wengine kutoka vyama vingine vya upinziani, kumesababisha Maalim Seif kuitwa ‘msaliti’ na wanachama wenzake wa CUF.

Maalim Seif amekuwa akihudhuria vikao vyote tisa peke yake kutoka CUF wakati CCM imekuwa ikiwakilishwa na Dk. Shein, Mwinyi, Mkapa. Dk. Salmin, Karume na Balozi Iddi.

KUTOAMINIKA ZEC

Tangu Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta uchaguzi Oktoba 28, mwaka jana, siku tatu baada ya kumalizika kupiga kura kwa kile kilichoelezwa ni uchaguzi kuwa na kasoro, wanachama wa CUF walikosa imani na ZEC kwa kudai kuwa mwenyekiti huyo hakunukuu kifungu chochote cha katiba au sheria kilichompa mamlaka ya kufuta uchaguzi huo.

Toka kufutwa kwa uchaguzi huo, CUF wamekuwa wakimtaka Mwenyekiti
Jecha kujiuzulu na kuvunjwa kwa tume hiyo na kuundwa mpya.

Vilevile kuwapo kwa madai ya muda mrefu ya kuhitaji kuundwa kwa Tume huru ya Uchaguzi na CUF ni mojao ya sababu za chama hicho kutokuwa na imani na ZEC na Maalim Seif kujiondoka katika mazungumzo.

MAZUNGUMZA YA MUAFAKA ZANZIBAR

Mazungumzo ya kwanza ya kusaka muafaka wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar uliotokana na utata wa matokeo ya uchaguzi wa urais mwaka 1995, yaliyosimamiwa na Jumuiya ya Madola chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Chifu Emeka Anyaoku, aliyewakilishwa na mjumbe wake, Dk. Moses Anafu.

Licha ya makubaliano hayo yaliyotiwa saini na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin na Maalim Seif katika Ikulu ya Zanzibar Juni 1999, utekelezaji wake ulikwama kutokana na sababu ambazo hazikujulikana.

Mazungumzo ya pili ya kusaka mgogoro ulioibuka mwaka 2001 baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2000 na kusababisha mauaji ya zaidi ya wafuasi 30 wa CUF, wakati wakiandamana Unguja na Pemba kupinga matokeo hayo, yalianza Machi, 2001 chini ya makatibu wakuu wa vyama hivyo, Philip Mangula (CCM) na Maalim Seif (CUF).

Muafaka ulifikiwa na makubaliano na kutiwa saini katika Ikulu ya Zanzibar na makatibu wakuu hao mbele ya wenyeviti wa vyama hivyo, Benjamin Mkapa (CCM) na Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF pamoja na mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, Ikulu ya Zanzibar Oktoba, 2001.

Kama ilivyokuwa katika mazungumzo ya kwanza, utekelezaji wa makubaliano hayo ulikwama kutekelezwa, ikiwamo waathirika wa matukio ya mauaji yaliyofanywa na polisi kulipwa fidia kama ilivyopendekezwa na Tume ya Hashim Mbita, iliyochunguza tukio hilo.

Mgogoro uliozuka wakati na baaada ya wa uchaguzi wa mwaka 2005, ulisababisha Rais Jakaya Kikwete wakati wa kulizindua Bunge la tisa Desemba 30, 2005 kuwaelekeza makatibu wakuu wa CCM na CUF, kufufua mazungumzo ya kusaka muafaka mwingine.

Mazungumzo hayo yaliyoanza mapema mwaka 2006 kwa kusimamiwa na Yussuf Makamba (CCM) na Maalim Seif, yalikoma mwaka 2008 muda mfupi kabla ya vyama hivyo kutoa taarifa ya pamoja juu ya waliyokubaliana. Hatua hiyo ilitokana na kitendo cha Baraza Kuu la uongozi la CUF kutangaza baadhi ya makubaliano hayo kwa waandishi wa habari ikiwamo kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Baada ya mkwamo huo, mwaka 2009, Rais Karume na Maalim Seif walikutana binafsi Ikulu, Zanzibar, na kukubaliana vyama hivyo kumaliza uhasama ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Makubaliano hayo yalitekelezwa kisheria kwa kuifanyia Katiba ya Zanzibar marekebisho mwaka 2010 ikiwamo kuruhusu kura ya maoni, ambayo ilifanyika mwaka huo na wananchi wengi kukubali kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Kuundwa kwa serikali hiyo, baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 uliompa ushindi mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kulisababisha mgawanyo wa madaraka baada ya Maalim Seif kuchukua nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na nafasi ya Makamu wa pili wa Rais kwenda kwa Balozi Seif Ali Iddi huku vyama hivyo vikigawana nafasi za Baraza la Mawaziri.

Serikali ya umoja wa kitaifa ndiyo iliyoifanya Zanzibar kuwa na utulivu wa kisiasa kabla ya kuibuka kwa mgogoro wa sasa uliotokana na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.

WANASHERIA, WANASIASA Z'BAR WANENA

Baadhi ya wanasheria na wanasiasa, wamesema muafaka wa kuleta suluhu ya mkwamo wa uchaguzi mkubwa Zanzibar, unakwamishwa na kukosekana kwa ukweli na nia njema miongoni mwa viongozi wanaoshiriki mazungumzo hayo.

Walikuwa wakizungumzia uamuzi wa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif kujiondoa katika mazungumzo ya kutafuta muafaka huo.

Mazungumzo hayo yanaongozwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein na wajumbe wake akiwamo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Marais wastaafu akiwamo Dk. Salmin Amour, Dk. Amani Abeid Karume na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.

NASSOR MOYO

Mwanasiasa mkongwe Zanzibar, Hassan Nassor Moyo, alisema baadhi ya viongozi ndani ya CCM, hawana ukweli katika kutafuta muafaka wa kumaliza mgogoro huo.

“Tatizo letu viongozi wetu CCM hasa Zanzibar, waliopumzika kazi na wale wamo serikalini na nje, baadhi yao hawana ukweli na bila ya ukweli jambo lolote haliwezi kukamilika na kuleta tija kwa wananchi wake,” alisema Moyo Waziri wa kwanza wa Katiba na Sheria baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.

Alisema kabla ya mazungumzo hayo kuanza kufanyika, viongozi walitakiwa kuweka mbele maslahi ya Zanzibar na kuacha itikadi na utashi wa kisiasa wa vyama vyao, jambo ambalo halikufanyika.

Alisema Kamati ya Maridhiano ya kutafuta muafaka wa mpasuko wa kisiasa mwaka 2009, ilipata mafanikio na kuzaliwa serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya wajumbe wake sita kutoka CCM na CUF kufanya kazi bila kujali maslahi ya vyama vyao.

Moyo alisema siasa za Muungano si kikwazo kwa Zanzibar kumaliza matatizo yake ya kisiasa, isipokuwa kuna watu wamekuwa wakipandikiza siasa zisizofaa dhidi ya uhai wa Muungano kama kutatokea mabadiliko ya kiutawala na Maalim Seif kuwa Rais wa Zanzibar.

“Hakuna mwanasiasa anayetafuta mabadiliko ya kiutawala Zanzibar kwa madhumuni ya kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mawazo hayo hayafai," alisema Moyo.

Moyo alisema kuwa hakuna mwanasiasa mwenye ubavu wa kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hata kama kutatokea mabadiliko ya kiutawala Zanzibar kutokana na uimara wa misingi ya Muungano.

Alisema misingi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyowekwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Karume, ipo imara katika Jamhuri ya Muungano.

Alisema wanasiasa Zanzibar lazima wakubali kubadilika kimawazo na kifkira na kuwa tayari kukubali misingi ya demokrasia ya kushinda na kushindwa katika uchaguzi.

“Tumekubali mfumo wa vyama vingi, lazima tuwe tayari pia kukubali matokeo pale unaposhinda au kushindwa hiyo ndiyo demokrasia,” alisisitiza Moyo.

RAIS WA ZLS

Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Awadh Ali Said, alisema wakati umefika kwa Rais Dk. John Magufuli, kuingilia kati mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar.

Alisema mazungumzo hayo yatafanikiwa kama watashirikishwa watu huru badala ya kuendelea na viongozi kutoka pande mbili zinazovutana.

Awadh, ambaye ni Wakili mkongwe wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, alisema mkwamo wa uchaguzi mkuu Zanzibar, unahusu Katiba na sheria na hauwezi kupata ufumbuzi kwa njia za kisiasa kutokana na kila upande kutetea maslahi yake.

Alisema Rais Magufuli kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi la Ulinzi na Usalama, bado ana jukumu kubwa la kumaliza mgogoro huo katika kuimarisha amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Zanzibar.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa zamani Zanzibar, Hamid Mbwezereni, alisema mahakama pekee ndiyo ina uwezo wa kutafsiri Katiba na kuangalia kama Mwenyekiti wa Zec alikuwa na mamlaka ya Kikatiba na sheria kufuta matokeo ya uchaguzi huo.

Alisema kama kuna watu wanapinga maamuzi ya Mwenyekiti, wanatakiwa kwenda mahakamani badala ya kuendelea kulalamika nje ya mfumo wa sheria.

NAIBU KATIBU MKUU CCM Z'BAR

Naibu Katibu CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema hawezi kutoa msimamo wa Chama baada ya Maalim Seif kujiengua katika mazungumzo ya kutafuta muafaka wa mkwamo wa uchaguzi kabla ya kutolewa rasmi taarifa na kamati ya Mazungumzo hayo.

Hata hivyo, alisema CCM bado inaamini mazungumzo ndiyo muafaka katika kumaliza matatizo ya migogoro ikiwamo ya kisiasa.

NAIBU KATIBU MKUU CUF

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Jimbo la Kaliua, Magdalena Sakaya, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu CUF Tanzania Bara, alisema kujitoa kwa Maalim Seif katika mazungumzo hayo, kutafanya watu wengine waingilie kati hali itakayofanya Zanzibar isiwe salama.

Alisema kwa uelewa wake, madhumuni ya vile vikao ilikuwa ni kutoa matunda mazuri.

“Habari ya Zanzibar kila mtu anajua ukweli ukoje hata CCM wenyewe, kilichofanyika sasa hivi ni makusudi kupindisha ukweli, Maalim Seif alikubali kuingia kwenye vikao vya maridhiano akijua wenzake watakaa wafikirie mbele ili kutoa kitu chenye manufaa kwa Wazanzibar,” alisema Sakaya.

Alifafanua kuwa Maalim Seif kwenda katika vikao hivyo peke yake, ilikuwa ni tatizo, lakini katika vikao vya chama tangu mwaka jana walitoa msimamo wao kama chama.

Naye Mhadhiri kutoka UDSM Idara ya Sayansi ya Siasa, Dk. Rasul Ahmed, alisema kujitoa kwa Maalim Seif kunaweza kuongeza au kuchochea mgogoro zaidi.

Alisema Maalim Seif angepaswa kuwa mvumilivu au kutafuta njia nyingine nzuri ya kuboresha mazungumzo hayo kuliko uamuzi aliouchukua kwa kuwa athari zake zinaweza kuwa mbaya mbele.

Hata hivyo, Profesa Mohamed Bakari, kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa UDSM, alieleza kuwa hatua ya Maalim Seif kujitoa kunamaanisha matumaini ya kupatikana kwa suluhu yamepungua.

Alisema athari za mgogoro huo endapo hautapatiwa ufumbuzi, kiwango cha misaada itapungua kutoka kwa wafadhilri, akitolea mfano Tanzania ilivyokosa fedha za MCC.

CHANZO: NIPASHE

Rais Maguguli amteua Rais mstaafu Kikwete kuwa Chancellor UDSM

Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Asha Rose Migiro akimhudhurisha Shahada ya Falsafa ya Udaktari ya Heshima, Mwenyekiti wa CC, Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, katika mahafali ya Chuo hicho yaliyofanyika jana, Kampasi ya Kinondoni, Dar es Salaam. (Picha na Bashir Nkoromo)


Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Asha Rose Migiro akimhudhurisha Shahada ya Heshima ya Udaktari ya Uhusiano wa Kimataifa, Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, katika mahafali ya 30 ya Chuo hicho, yaliyofanyika ana, Alhamisi, Januari 21, 2016, Kampasi ya Kinondoni, Dar es Salaam.


Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Asha Rose Migiro akimhudhurisha Shahada ya Heshima ya Udaktari ya Uhusiano wa Kimataifa, Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, katika mahafali ya 30 ya Chuo hicho, yaliyofanyika leo, Alhamisi, Januari 21, 2016, Kampasi ya Kinondoni, Dar es Salaam.


Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Asha Rose Migiro akimhudhurisha Shahada ya Heshima ya Udaktari ya Uhusiano wa Kimataifa, Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, katika mahafali ya 30 ya Chuo hicho, yaliyofanyika leo, Alhamisi, Januari 21, 2016, Kampasi ya Kinondoni, Dar es Salaam.


Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Asha Rose Migiro akimpongeza baada ya kumhudhurisha Shahada ya heshima ya Udaktari ya Uhusiano wa Kimataifa, Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, katika mahafali ya 30 ya Chuo hicho, yaliyofanyika leo, Alhamisi, Januari 21, 2016, Kampasi ya Kinondoni, Dar es Salaam.


Dk. Kikwete akishukuru


Dk. Kikwete akingoka baada ya kuhudhurishwa
Dk. Kikwete akiwa na Rais wa Chuo Kikuu cha Choson cha Korea, Profesa Such Chae Hong, ambaye naye pia alitunukiwa Shahada ya heshima ya Udaktari katika Mahahali hayo


Dk. Kikwete na Profesa Such wakiwa wamesimama kuimba wimbo wa Taifa baada ya kutunukiwa Shahada zao za Udaktari. Kulia ni Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk. Asha-Rose Migiro


Dk. Kikwete na Profesa Such na Mama Salma Kikwete wakiwa na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk. Asha-Rose Migiro


Dk. Kikwete na Profesa Such wakiwa Dk. Asha-Rose Migiro na viongozi wengie wa Chuo Kikuu Huria. Karibu na Dk. Migiro ni Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi


Dk. Kikwete na Profesa Such wakiwa na Mama salma Kiwete na Dk. Asha-Rose Migiro na baadhi ya viongozi wa OUT


Mama Salma Kikwete akiteta jambo na Dk. Asha-Rose Migiro


Dk. Jakaya Kikwete akimpongeza mmoja wa wahitimu katika chuo hicho mwenye ulemavu wa miguu.


Dk. Jakaya Kikwete akimdodosa maswali, mtoto Novatus Salala (11), ambaye alimuona akimpiga picha kwa simu wakati wa mahafali hayo. Kulia ni Mama Salma Kikwete


Dk. Jakaya Kikwete akiwa na Mkuu wa Chuo Kikuu huria w zamani, Dk. John Malecela na Mkuu wa sasa wa Chuo hicho, Dk. Asha-Rose Migiri wakati akiondoka mwishoni mwa hafla hiyo. (Picha zote na Bashir Nkoromo).

Wamiliki wa shule binafsi wapongeza kufutwa mfumo wa GPA na kurudishwa Divisheni

Shirikisho la wamiliki wa shule na vyuo visivyo vya serikali TAMONGSO watoa pongezi kwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi kwa kuliagiza Baraza la Taifa la Mitihani kufuta mfumo unaotumika sasa wa Wastani wa Alama (GPA) na kurudi katika mfumo uliokuwa unatumika hapo awali wa Divisheni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti Taifa wa TAMONGSO Bwa. Mrinde Mzava amesema kuwa Waziri wa Elimu Ameitendea haki Sekta ya Elimu kwani mfumo huo ulileta sintofahamu kwa wananchi wengi.

“Waziri ameitendea haki sekta ya Elimu kwani mfumo wa GPA ulileta sintofahamu kwa wananchi na pia ulikuwa unaongeza ufaulu usio na mashiko kwa wanafunzi walio wengi ukilinganisha na mfumo uliokuwa unatumika awali,” aliongeza Mwenyekiti huyo.

Vilevile Mwenyekiti huyo alisema kuwa Tanzania inahitaji kuingia kwenye soko la upinzani hasa katika sekta ya Elimu ili iweze kuajiri watu wenye utaalamu na sifa stahiki na kuweza kushindanishwa kwenye soko la kimataifa hivyo kwa mfumo wa GPA ulikuwa unadidimiza elimu ya Tanzania.

Mbali na hayo Mwenyekiti huyo alitoa agizo kwa baadhi wamiliki wa shule na vyuo visivyo vya Serikali kutotumia kigezo cha pesa ili kudidimiza kiwango cha Elimu nchini.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa shirikisho hilo Bwa. Emmanueli Gwegenyeza ameshauri viongozi na wananchi kwa ujumla kutochanganya suala la Siasa na Elimu kwani kwa kufanya hivyo tutazidi kudidimiza Sekta ya Elimu nchini.

“Tusiingize suala na Siasa na Elimu kwa wakati mmoja kwani kwa kufanya hivyo tunaweza kuididimiza Sekta ya Elimu pia tunaahidi kumpa Waziri ushirikiano ili kuzidi kuinua Sekta ya Elimu nchini,” aliongeza Makamu huyo.

Waziri Mwalimu aagiza MSD kuwa na maduka ya dawa kila hospitali kabla ya Mei

WaziriMwalimu (kulia), akihutubia wakati akizindua rasmi duka la Dawa la MSD mkoani Mwanza jana ambalo liko ndani ya Hospitali ya SekouToure, nakufanya maduka ya MSD yaliyofunguliwa baada ya agizo la Rais Dk. John Magufuli kufikia mawili baada ya lile la Muhimbili lililofunguliwa mwaka jana mwishoni. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu na katikati ni Mwenyekiti wa Bodi MSD, Profesa Idrisa Mtulia.

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummi Mwalimu ameiagiza Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kujenga maduka ya dawa katika kila Hospitali ya mkoa hapa nchini kabla ya Mei na Juni mwaka huu.

Kauli ameitoa jana wakati wa ufunguzi wa duka la dawa katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure, ambako amesema MSD wanapaswa kujenga maduka ya dawa katika kila hospitali ya mkoa nchini ili kukabiliana na uhaba wa dawa.

Amesema MSD wanapaswa kutambua kwamba suala la afya ndio kipaumbele kikubwa katika wizara ya afya hivyo lazima juhudi za upatikanaji wa dawa zifanyike kwa nguvu zote, kwani tatizo la dawa limekuwa ni sugu nchini.

Waziri Ummy amesema kuwa hata kama hawashindwa kujenga kila mkoa angalau wanapaswa kufikisha asilimia 50 ya ujenzi wa maduka katika baadhi ya mikoa ili kabla ya bunge la bajeti la Juni awe amepata cha kuzungumza bungeni.

Hata hivyo amesema wizara ya afya imejiwekea malengo ya upatikanaji wa dawa nchini kutoka asilimia 70 ya sasa hadi 95 na kwamba kama hatatatua tatizo la dawa katika hospitali za Serikali yupo tayari kuwajibishwa.

“Nilishajihukumu mwenyewe kwamba kama sitaweza kutatua suala la dawa hospitalini nipo tayari kuwajibishwa na hilo sikusubiri Rais (John Magufuli) aniambie nilijihukumu mimi mwenyewe na sasa nipo tayari kuwajibika.

“Pia unakuta mgonjwa anakaa saa sita hospitalini kumsubiri daktari akishamuona daktari na unapofika muda wa anakuta dawa hakuna, ni bora akae saa sita kumsubiri mganga alafu akapata dawa na hilo ndilo lengo letu,” amesema Ummy.

Mkurugenzi wa MSD, Laulean Kunu, amesema kuwa agizo la waziri huyo litafanyiwa kazi kwani mpaka sasa tayari wameishajenga maduka mengine mawili katika mikoa ya Mbeya na Arusha na katika kila duka la MSD dawa aina zote zitapatikana.

“Mikoa mingine iliyobaki sasa hivi tupo katika mazungumzo na viongozi wa mikoa hiyo na MSD tupo tayari kupeleka dawa aina zote katika maduka ili kuondokana na tatizo la uhaba wa dawa katika hospitali za Serikali,” amesema Kunu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amesema kujengwa kwa duka hilo litahudumia zaidi ya asilimia 30 ya vituo vya afya 373 na zahanati 321 na hivyo kujengwa kwake kutapunguza tatizo la upatikanaji wa dawa.WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto. Umy Mwalimu (kushoto), akiwa na viongozi mbalimbali wa MSD wakati wa uzinduzi wa duka hilo.

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Umy Mwalimu amezindua rasmi duka la Dawa la MSD mkoani Mwanza ambalo liko ndani ya Hospitali ya Sekou Toure, nakufanya maduka ya MSD yaliyofunguliwa baada ya agizo la Rais Dk. John Magufuli kufikia mawili baada ya lile la Muhimbili lililofunguliwa mwaka jana mwishoni.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa duka hilo, ameipongeza MSD kwa hatua hiyo nzuri ya kufungua maduka ili kuwawezesha wananchi kupata dawa, na kuitaka MSD kukamilisha ufunguzi wa maduka mengine mawili yaliyosalia katika mikoa ya Arusha naMbeya, kwani hicho ni moja ya kipaumbele katika uongozi waserikali ya awamu yaTano.

Waziri huyo ameeleza kuwa Wizara yake imejiwekea malengo ya upatikanaji wa dawa nchini kutoka asilimia 70 kwa sasa kufika hadi asilimia 95.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema maduka mawili ya Arusha naMbeya yamemekamilika, na yanatarajia kufunguliwa hivi karibuni, na kwamba kwa mikoa mingine wameshafanya mawasiliano na kwamba tayari MSD imefanya mazungumzo na viongozi wa mikoa Ruvuma, Rukwa, Singida, Dodoma, Geita, Kagera na Iringa kufungua maduka yao ya dawa ambapo MSD itawauzia dawa.

“Tutakachofanya, sisi (MSD) utawapa utaalamu na kuwawezesha utaalamu wa uendeshaji maduka hayo” alieleza Bwanakunu.

Polisi ACP Hussein Kashindye afariki dunia akiwa katika kazi maalum

Aliyekuwa kamishina msaidizi wa jeshi la polisi nchini Hussein Kashindye amefariki dunia katika hospitali ya Maweni mkoani Kigoma.

Taarifa tulizozipata ni kwamba Kashindye alikuwa mkoani Kigoma kwa kazi maalum ya jeshi la polisi lakini wakati akiendelea kutekeleza majukumu yake hali ilibadilika na kukimbizwa katika hospitali ya Maweni na taarifa zinadai kuwa amefariki dunia jana usiku kwa ugonjwa wa shinikizo la damu.

ACP Hussein Kashindye alikuwa akifanya kazi makao makuu ya polisi Dar es salaam.

Kabla ya kuhamishiwa jijini Dar es Salaam, Kashindye alikuwa mkuu wa upelelezi wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga.

Taarifa tulizozipata ni kwamba mazishi yanatarajia kufanyika kesho Alhamisi nyumbani kwao Lunguya wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Matokeo ya Upimaji wa Kitaifa Darasa la Nne (SFNA) 2015

Dkt. Charles Msonde

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), limetangaza matokeo ya mitihani ya kujipima ya darasa la nne huku matokeo hayo yakionyesha wanafunzi wengi wamefeli katika somo la Kiingereza kwa asilimia 65.67 katika mitihani hiyo iliyofanyika mwishoni 2015.

Akitangaza matokeo hayo leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt. Charles Msonde amesema juhudi za makusudi zinahitajika katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzia ili kuboresha kiwango cha ufaulu.

Jumla ya wanafunzi 869,057 kati ya wanafunzi 977,886 sawa na asilimia 88.87 waliofanya upimaji wamepata alama katika madaraja ya A,B,C, na D. Wanafunzi 108,829 sawa na asilimia11.13 wamepata alama za ufaulu usioridhisha.

Aidha wanafunzi wamefanya vizuri zaidi katika somo la Sayansi kwa asilimia 89.44, na baraza limewataka walimu kuweka mkazo zaidi kwa wanafunzi waliofanya vibaya ili wawasaidie kuimarika na waweze kupata ufaulu mzuri.

Mahakama yafuta kesi ya kupinga ushindi wa Lissu

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma imefutilia mbali kesi ya uchaguzi iliyofunguliwa na mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jonathan Njau kupinga ushindi wa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu (CHADEMA).

Katika madai yake ya msingi, Njau alikuwa akipinga matokeo na kutaka kura kuhesabiwa upya.

Shauri hilo lilikuwa mbele ya Jaji Berkel Sehel ambapo mgombea wa ubunge kupitia chama cha Mapinduzi CCM Jonathan Njau alishindwa kwenye uchaguzi kwenye jimbo hilo mwaka 2010 na 2015.

Njau Aliwasilisha ombi mahakamani la kutaka kesi hiyo kufutwa kwani hana haja ya kuendelea na shauri hilo.

Awali mlalamikaji aliwahi kupeleka mahakamani mara mbili maombi ya ombi la kusamehewa kwa gharama za kesi kiasi cha milioni 15 lakini maombi hayo yalitupwa

Lisu amesema Mahakama kuu ilishatamka mwaka 2010 kuwa kesi za uchaguzi si za kuendea kwa papara bila umakini wowote.

Rais Magufuli awasili ArushaNgoma za asili zikiwa zinatumbuiza katika uwanja wa KIA mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutua na ndege uwanjani hapo 

Gazeti lapewa siku 7 kukanusha habari inayoihusu familia ya mstaafu Rais Kikwete

Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simos Group na UDA, Robart Kisena akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.

GAZETI la Jamhuri lapewa siku saba kukanusha habari iliyoandikwa kwenye gazeti hilo Januari 18, 2016 toleo no. 25 lililokuwa na kichwa cha habari FAMILIA YA JK YAHUSIKA UDA habari iliyokuwa ukurasa wa mbele wa gazeti hilo.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simos Group na UDA, Robart Kisena wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo,amesekuwa hakuna uhusiano wa umiliki na familia ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne,Dk Jakaya Kikwete.

Kisena amesema kuwa Familia ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ,Dk. Jakaya Mrisho Kikwete hahusiki kabisa kwani kampuni ya UDA na kampuni ya Simon Kisena haihusiani na familia ya JK hata miradi inayofanywa na Kampuni hiyo.

Aidha amesema gazeti lililoandika habari hiyo linatakiwa kuomba radhi kwa siku hizo kwa kuwa na habari yenye uzito ule ule na ukurasa ule ule.

Kisena amesema wasipofanya hivyo watapelekwa mahakamani ili wakatoe ushaidi wa maandishi mahakamani hapo juu ya uhusikaji wa Familia ya Rais Mstaafu katika kampuni ya usafiri Dar es Salaam (UDA).

Hata hivyo amesema kuwa kampuni ya (UDA) itarudishwa kwa wananchi ifikapo Machi Mwaka huu ili iweze kuendeshwa kwani shirika hili kwa mara ya kwanza lilikua na magari 7 mpaka sasa maari hayo yameongezeka na kufikia zaidi ya magari 400.
  • via Michuzi blog