Vitambue vyeo vya askari wa Jeshi la Polisi TanzaniaImenukuliwa kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Road Safety Ambassadors (RSA)

Mwananchi atoa hadhari ya daraja la Sikonge


WAHUSIKA WA BARABARA MNASUBIRI MAAFA HAPA MTO KASISI SIKONGE ROAD?

Mto Kasisi ni mto wa msimu wa mvua, ambao ni mpaka wa Wilaya ya Uyui (Tabora vijijini) na Wilaya ya Sikonge. Daraja hili ambalo unaliona kwenye picha hizo, hapa ndipo yanapita Magari ya mizigo na Mabasi ya Abilia yanayokwenda Sikonge, Mpanda ( Katavi ) na Mbeya. Pia yanayotoka mikoani Mbeya, Katavi, Rukwa n.k kuelekea Tabora, Shinyanga, Mwanza n.k yanapita juu ya daraja hili hatari.

Sisi tunaopita hapa kwa baiskeli, pikipiki na miguu, ndio tunaona vizuri hatari inayowakabiri wapitaji wa Magari kama wahusika hawatachukua hatua za haraka bila kuchelewa.

Mto huu kwa sasa umejaa maji tofauti na mwaka jana ambapo ulikuwa na maji madogo sana. Udongo katika daraja umeanza kubomolewa na kasi ya maji! Wahusika ( viongozi wa serikali ) wanayaona haya, maana njia yao ni i hii!
Jambo la ajabu hapa hata alama za Barbara za kuonesha uwepo wa daraja hakuna!

Wahusika wasipochukua hatua, TCRA mjiandae

kunidaka nikiripoti tukio.

MWISHO WA KUTOA TAHADHARI!!Mchanganuo wa Wabunge katika Kamati Mpya za Bunge la XI

Anatafutwa kwa kumbaka na kumlawiti binti yake na kutishia kumuua

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamsaka Mohamed Said Mkazi wa Mjimwema katika halmashauri ya manispaa ya Songea kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa kike ambaye anasoma darasa la sita katika shule ya msingi Samola iliyopo katika manispaa hiyo.

Habari zilizopatikana jana mjini hapa ambazo zimezibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi zimesema kuwa mwanafunzi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, inadaiwa amekuwa akilawitiwa na kubakwa na baba yake mzazi tangu Oktoba mwaka jana.

Malimi alifafanua kuwa inadaiwa Saidi alikuwa akimtishia mtoto wake kuwa asiseme kwa mtu yeyote na kwamba taarifa hiyo ikisikika atamuua kwa kuwekewa sumu kwenye chakula au kumchinja kwa kutumia panga.

Alisema kuwa kufuatia vitisho hivyo Saidi, anadaiwa kuwa alikuwa akifanya kitendo hicho cha kufanya mapenzi na binti yake mara kwa mara kwani mke wake alikuwa ameachana naye miaka mingi iliyopita. Alifafanua zaidi kuwa taarifa za awali zinaonyesha kuwa mtuhumiwa alikuwa ameachana na mke wake tangu mwaka 2009 na kumuachia mtoto huyo mama yake Hadija Mohamed Hitima mkazi wa Tunduru.

Alieleza zaidi kuwa Oktoba mwaka jana, Saidi alimfuata mtoto wake alikokuwa anaishi Tunduru na mama yake mzazi kisha kumleta Songea ili aendelee kuishi naye. Kamanda Malimi alieleza zaidi kuwa Saidi alipofika Songea Mjini alianza kumueleza mtoto wake kuwa anapokwenda kulala usiku asiwe anafunga mlango wa chumba chake. Baadaye alianza kuingia kwenye chumba hicho na kuanza kumrubuni na alipoona mtoto anamkataa ndipo alipoanza kumpa vitisho kisha kufanikiwa kumbaka.

Malimi ambaye pia ni Afisa Upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Ruvuma alisema kuwa inadaiwa mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu, baba mzazi wa mwanafunzi huyo aliaga anaenda shambani ambako binti huyo hakufahamu ndipo mtoto huyo alipata nafasi ya kutoa taarifa kwa majirani ya hali halisi aliyokuwa anafanyiwa ya kubakwa na kulawitiwa na baba mzazi. Majirani walimsaidia kumpeleka kwenye kituo kikubwa cha polisi cha Songea Mjini.

Alisema kuwa taratibu za uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo zimefanywa licha ya kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa msichana huyo ameingiliwa sehemu zake za siri na mzazi wake kama alivyojieleza yeye mwenyewe na polisi inaendelea kumsaka mtuhumiwa ili afikishwe mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.

Membe azungumza: Alichofanya Rais Magufuli ni kubadili form na siyo content


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali iliyopita, Bernard Membe ameungana na waziri mwenzake wa zamani, Dk Makongoro Mahanga kukosoa sera ya kubana matumizi ya Rais John Magufuli ya kudhibiti safari za nje na kuteua baraza dogo la mawaziri.

Kama ilivyokuwa kwa Dk Mahanga, waziri huyo aliyedumu kwa miaka tisa kwenye Wizara ya Mambo ya Nje amesema kiuhalisia, Rais hajapunguza idadi ya wizara kama alivyosema bali amepunguza “idadi ya mifuko”, huku akisisitiza kuwa mkuu huyo wa nchi atalazimika kutoka nje “atake asitake”.

Membe amekuwa waziri wa pili wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kukosoa sera ya kubana matumizi ya Serikali ya Awamu ya Tano baada ya Dk Mahanga, ambaye sasa amehamia Chadema, kumkosoa akisema idadi ya wizara inapimwa kwa kuangalia makatibu wakuu na si wizara na hivyo ukubwa wa Baraza la Mawaziri bado uko palepale.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi mapema wiki hii, Membe alikuwa na maoni kama hayo na akaenda mbali zaidi kuzungumzia hata sera ya kudhibiti safari za nje na Rais kujizuia kusafiri, akisema “Tanzania haiwezi kuishi kama kisiwa” katika dunia ya leo.

Kubana matumizi 

Membe, ambaye alikuwamo kwenye kinyang’airo cha urais na kufika hadi tano bora, alisema Rais hajabana matumizi yoyote kwa kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri, bali alichofanya ni kupunguza idadi ya mawaziri na siyo wizara.

“Alichofanya ni sawa na kuwa na mayai kumi halafu ukaamua kuyaweka kwenye mifuko kumi, maana yake ni kwamba utakuwa na mifuko kumi yenye mayai,” alisema Membe.

“Lakini unaweza kuwa na idadi hiyo hiyo ya mayai na ukaamua kuyagawanya; mayai matatu unayaweka kwenye mfuko mmoja, mawili kwenye mfuko mwingine na yaliyobaki kwenye mfuko mmoja.

Maana yake ni kwamba utaendelea kuwa na mayai kumi lakini idadi ya mifuko imepungua. Hapa sasa utakuwa hujapunguza gharama za kuyatunza hayo mayai.”

Rais aliahidi kwenye kampeni na hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge kuwa atapunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri ili kubana matumizi. Alitekeleza ahadi yake kwa kuunda baraza lenye mawaziri 34 tofauti na lililopita ambalo lilikuwa na mawaziri 55.

Upunguzaji huo wa baraza ulifanywa kwa kuunganisha wizara na hivyo kufanya makatibu wakuu, ambao ni maofisa masuhuli wa wizara kuwa zaidi ya mmoja kwenye baadhi ya wizara.

“Ameendeleza wizara zilezile, lakini akaamua kuzikusanya pamoja. Hiyo haimaanishi kuwa atakuwa amepunguza gharama za uendeshaji wake,” alisema Membe.

“Hilo tutaliona kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka huu. Tuone kama bajeti itaongezeka au itapungua? Kwa sababu kama wizara zimepungua kama tunavyoamini, lazima bajeti ipungue, sasa bajeti ikiongezeka au ikibaki vilevile maana yake hakuna kilichofanyika.”

Membe alitoa mfano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo sasa inaitwa “Wizara ya Mambo ya Nje, Kikanda na Ushirikiano wa Afrika Mashariki”, akisema itapaswa kuwa na bajeti mbili; ya Mambo ya Nje na Bajeti ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kinyume chake ni vigumu kuiendesha.

Membe alikiri kuwa hata yeye angeingia kwenye mtego wa kupunguza idadi ya wizara kama angefanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais kama ilivyokuwa nchini Namibia ambako wizara zilipunguzwa kutoka 32 hadi 20.

“Baadaye nikagundua kuwa hata Namibia yenyewe inajuta,” alisema.

Alisema siku ya kuapishwa Rais Magufuli, alikutana na Makamu wa Rais wa Namibia, Nickey Lyambo na baada ya kusalimiana na kumpongeza kwa hatua ya kupunguza wizara, kiongozi huyo wa Taifa hilo la kusini mwa Afrika alimweleza kuwa uamuzi huo umewasababishia matatizo makubwa bungeni

“Aliniambia katika Bunge la Namibia kuna mjadala mkali wa kutaka wizara ziongezwe,” alisema Membe akimnukuu makamu huyo wa rais wa Namibia.

Membe alibainisha kuwa kwa Tanzania, mfumo huo mpya wa wizara pia unaweza kuathiri uwasilishaji wa bajeti bungeni kwa kuwa mawaziri sasa watahitaji muda mwingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali ili kuzungumzia wizara kadhaa zilizounganishwa, jambo ambalo lililalamikiwa pia na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu.

“Kila kitu kina form na content (muundo na maudhui). Alichofanya Rais Magufuli ni kubadili form na siyo content ya wizara, wizara ni zilezile na mzigo ni uleule,” alisema.

Safari za nje 

Mbunge huyo wa zamani wa Mtama mkoani Lindi, pia alikosoa udhibiti wa safari za nje, akisema Tanzania si kisiwa.

Alikuwa akijibu swali lililomtaka aeleze uhalisia wa mpango wa Rais Magufuli kubana matumizi kwa kufuta safari za nje za mawaziri na watumishi wengine wa umma.

Mara tu baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alifuta safari zote za nje ya nchi kwa watendaji na watumishi wa umma, isipokuwa zile tu ambazo zingepata kibali cha Ikulu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kubana matumizi ya Serikali.

Rais Magufuli alisema katika hotuba yake ya kuzindua Bunge kuwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2015, safari hizo ziliigharimu Serikali Sh356.3 bilioni na kwamba kati ya fedha hizo, Sh183.1 bilioni zilitumika kwa ajili ya tiketi za ndege, Sh68.6 bilioni kwa ajili ya mafunzo na Sh104.5 bilioni kwa ajili ya posho.

Bila kugusia madhara ya kufuta safari hizo, Rais Magufuli alijielekeza zaidi kwenye matumizi ya fedha ambazo angeokoa.

“Lakini tujiulize fedha hizo zingeweza kutengeneza zahanati ngapi? Zingeweza kutengeneza nyumba za walimu ngapi? Zingeweza kutengeneza madawati mangapi? Zingeweza kununua dawa hospitalini tani ngapi?” alihoji Rais Magufuli katika hotuba yake iliyotoa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Lakini Membe, ambaye wizara yake iliwahi kutetea safari za Jakaya Kikwete nje ya nchi baada ya wapinzani kusema ziligharimu zaidi ya Sh4 trilioni, alisema safari za nje zina umuhimu kwa taifa lolote.

“Tanzania si kisiwa, hata ukiwa tajiri namna gani lazima utoke nje ya nchi yako,” alisema Membe ambaye ana shahada ya umahiri ya uhusiano wa kimataifa aliyoipata Marekani.

“Lazima utakwenda mwenyewe au mawaziri wako na hasa Waziri wa Mambo ya Nje kwa sababu kuna vikao nje ya nchi ambavyo mabalozi hawaruhusiwi kuingia.

“Ukijaribu kujifanya kisiwa utakuwa kama Zimbabwe. If you isolate yourself you will be isolated (ukijitenga, utatengwa).”

Membe alisema nchi ina mabalozi 36 tu duniani kote kati ya nchi 194 zinazohitaji uwakilishi huo na kibaya zaidi, mabalozi hawaruhusiwi kuingia kwenye baadhi ya vikao, na hata wakiingia wakifika kwenye hatua ya uamuzi watazuiwa kushiriki.

“Kwa mfano, Uturuki hatuna ubalozi, sasa unapoona ndege inaleta watalii kutoka Uturuki, unadhani Bunge la Uturuki liliketi kutuletea watalii Tanzania? Hapana. Tulitoka nje na kuwashawishi wakaja,” alisema Membe aliyewahi kueleza kuwa wakati wa awamu ya Rais Jakaya Kikwete mawaziri walikuwa wanapishana angani kana kwamba kuna moto ardhini.

“Pia, leo unaposikia gesi, gesi, gesi nayo imepatikana nje ya ubalozi. Mawaziri walitoka nje ya nchi wakatafuta wawekezaji.

Ni kazi ya wizara kufanya yote hayo.” Membe alirudia kauli aliyoitoa siku chache kabla ya kuanza mchakato wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana kuwa lazima waziri wa mambo ya nje awe nje ya nchi kwa muda mwingi na ikitokea yuko ndani ya nchi kwa mwezi mmoja mfululizo, lazima ni mgonjwa.

Rais Magufuli afunga zoezi la Onesha Uwezo Medani, Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akijadiliana jambo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini General Davis Mwamunyange wakati akielekea kupewa maelezo ya zoezi zima la Onesha Uwezo Medani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefunga "Zoezi la Onesha Uwezo Medani" lililoandaliwa na kutekelezwa na Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ambalo ni sehemu ya Jeshi la wananchi Tanzania katika eneo la Lang'arurusu nje kidogo ya Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Mkoani Arusha.

Akizungumza na Askari na Maafisa wa Jeshi la wananchi Tanzania kabla ya kufunga zoezi hilo, Rais Magufuli amesema katika awamu yake ya tano ya uongozi amedhamiria kulitumia Jeshi la wananchi Tanzania katika kujenga uchumi, ikiwemo kuanzisha viwanda na kampuni za ujenzi ili kuharakisha maendeleo.

Ametoa mfano wa kiwanda cha Nyumbu ambacho kipo chini ya jeshi la wananchi Tanzania na kueleza kuwa wakati umefika wa kukiimarisha na kukiendeleza kiwanda hicho, ili kiweze kufanya uzalishaji mkubwa kwa manufaa ya nchi ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa.

"Zipo nchi nyingi ambazo majeshi yao yanatumika katika uchumi na yanafanya kazi nzuri ya kupigiwa mfano, wakati umefika na sisi kufanya hivyo. Hata hizi sare za jeshi na viatu, hatuna sababu ya kuvinunua kutoka nje ya nchi, tunaweza kutengeneza sisi wenyewe" Alisisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuandaa "Zoezi Onesha Uwezo Medani" ambalo limethibitisha uwezo, weledi na utayari lilionao katika jukumu lake la kiulinzi.

Ameahidi kuwa ataendeleza juhudi zilizofanywa na viongozi wenzake waliotangulia za kuliimarisha kwa vitendea kazi na maslai ya wanajeshi ili liweze kutekeleza wajibu wake bila vikwazo.

Pamoja na kuwapongeza Askari na maafisa wa Jeshi la wananchi Tanzania walioshiriki katika zoezi hilo, Rais Magufuli ameagiza Askari Mgambo na Askari wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT) walioshiriki zoezi hilo kuajiriwa na jeshi la wananchi Tanzania.

Akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba ya Rais Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Wizara yake itaongeza na kusimamia juhudi za kuliboresha jeshi hilo kwa zana, vifaa na maslai kwa wanajeshi ili kuwajengea uwezo na morali ya kutekeleza majukumu yao ya kuilinda nchi, pamoja na kutoa msaada stahiki kwa nchi zenye kuhitaji ulinzi wa amani popote duniani.

Kwa upande wake Mkuu wa majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange amemhakikishia Rais Magufuli kuwa Jeshi la wananchi Tanzania lipo imara na litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, nidhamu ya hali ya juu na uzalendo mkubwa.

Kabla ya kuwahutubia maafisa wa jeshi la wananchi, Askari na wananchi waliohudhuria ufungaji wa "Zoezi Onesha Uwezo Medani", Rais Magufuli ameoneshwa zana mbalimbali za kivita ikiwa ni pamoja na kushuhudia upigaji wa mizinga ya masafa mafupi, masafa ya kati na masafa marefu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na baadhi ya Maafisa wa jeshi katika tukio hilo la Ufungaji.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akielekea kwenye uwanja wa maonesho akiwa pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini General Davis Mwamunyange.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa ngazi za juu wa Jeshi mara baada ya kufunga zoezi la Onesha Uwezo Medani Monduli Mkoani Arusha.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini General Davis Mwamunyange wakati waufungaji wa zoezi la Onesha Uwezo Medani lililofanyika Monduli nje kidogo ya Jiji la Arusha.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katikati akishuhudia matukio ya zoezi la Onesha Uwezo Medani Monduli Mkoani Arusha.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipewa maelezo ya zana mojawapo ya Kivita katika Zoezi la Onesha Uwezo Medani Mkoani Arusha.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na wananchi wa Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha waliojitokeza kumsalimia wakati akielekea Monduli kwa ajili ya kufunga zoezi la Onesha uwezo Medani.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia wananchi wa Mbauda Mkoani Arusha hawaonekani pichani wakati akielekea Monduli kwa ajili ya kufunga zoezi la Onesha uwezo Medani.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisoma bango mara baada ya kukabidhiwa na mwananchi mmoja katika eneo la Kona ya Nairobi Mkoani Arusha.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia wananchi wa Arusha katika eneo karibu na chuo cha Arusha Tech. Wananchi hao walifunga barabara ili wapate nafasi ya kumuona Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi wa Mianzini Mkoani Arusha.


Umati mkubwa uliojitokeza katika eneo la Mianzini Mkoani Arusha
Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dkt Magufuli akiwasikiliza wananchi kwa makini alipopita maeneno ya Sanawali kuwasalimia wakati akielekea Wilayani Monduli.


Rais Magufuli akiwa amevalia sare za kijeshi amesimamishwa na kuwasalimu wananchi katika maeneo ya Sanawali, Tekniko, Ngarenalo, Mbauda, Majengo Na Kisongo


Amiri Jeshi Mkuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na wananchi wa Arusha Mjini wakati akipita Barabarani kuelekea Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA) Monduli ambako pamoja na mambo mengine kesho tarehe 23 Januari, anatarajiwa kutunuku Kamisheni kwa Maafisa wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli kundi la 57/15.

Kamati ya kuratibu Miss Tanzania yajivua jukumu kwa kudai kuingiliwa kazi

Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu Miss Tanzania Juma Pinto akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani) leo jijini Dar-es-Salaam juu ya kujitoa kwao kama kamati ya kuratibu Miss Tanzania ambayo ilichagulia na kampuni ya Lino International Agency, kushoto ni Msemaji wa kamati hiyo Joketi Mwegelo na kulia ni Mjumbe wa kamati Gladys Shao.

Kamati ya kuratibu Miss Tanzania imejitoa rasmi kusimamia mashindano ya Miss Tanzania kuanzia leo tarehe 21/01/2016.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Juma Pinto alisema hayo leo, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dar-es-Salaam.

“Tumekuja kutoa taarifa kwamba, kama tulivyo teuliwa na kampuni ya Lino International Agency, kuandaa, kuendesha na kusimamia mashindano ya Miss Tanzania, kamati yangu imeamua kujitoa kutokana na majukumu ya kamati kuingiliwa na kampuni ya Lino,” alisema Pinto.

Pinto aliongeza kwa kusema kuwa kamati yake ilipewa jukumu la kuendesha mashindano na kuwajibika kufanya kila kitu na Lino itakuwa kama washauri, lakini badala yake Lino imetaka kuhodhi majukumu yote na kamati ikawa ni ya kutafuta wadhamini.

Kamati hiyo imefanya vikao vingi vya kuhakikisha mashindano yanaboreshwa na kubadilisha mfumo ili kuifanya Miss Tanzania kuwa na mwonekano tofauti kama ambavyo Lino ilivyoamua kuweka kamati mpya ili kuboresha mashindano hayo.

Kutokana na kutopata muafaka katika vikao hivyo vya kuboresha mashindano ya Miss Tanzania, Kamati ya kuratibu mashindano hayo kwa nia njema na wala si kwa ubaya imeamua kujitoa katika Mashindano hayo.

Aidha, Pinto amewaomba radhi wadhamini ambao wameshaongea nao kama kamati na walioonesha nia ya kuwasaidia, amewataka kuendelea kufanya mawasiliano na kampuni ya Lino kwani madhumuni ni kudhamini mashindano na sio kamati.

Msemaji wa Kamati ya Kuratibu Miss Tanzania Joketi Mwegelo akitoa maelezo kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) namna Kamati hiyo ilivyokuwa ikijitahidi kubadili mfumo ili kubadilisha muonekano wa mashindano ya urembo(Miss Tanzania) kulia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo Juma Pinto.

PICHA NA Beatrice Lyimo-Maelezo.
TAARIFA NA Lilian Lundo - Maelezo,
Dar es Salaam.

Waraka "ulioghushiwa" wa ombi la radhi kwa kufutwa uchaguzi wa Zanzibar


Taarifa ya ZEC ya tarehe mpya ya kurudia Uchaguzi Mkuu Zanzibar
Ugeni wa Balozi wa Norway, Kaarstad katika kituo cha kufua umeme Hai


Mkuu wa wilaya ya Hai, Anthony Mtaka akisalimiana na balozi wa Norway nchini Tanzania Hanne-Marie Kaarstad wakati akimpokea ofisini kwake kwa ajili ya ziara ya kutembelea kituo cha kufua umeme cha Kikuletwa.