[video] Maelezo ya JWTZ kuhusu Rais Magufuli kuvaa magwanda ya jeshi


Mdau anaomba mawasiliano ya Mustafa Sabodo

Ninaomba kupata anwani binafsi ya Mzee Mustafa Jaffer Sabodo, kwani tuna huduma ya WAJANE na YATIMA kwa Nyanda za Juu Kusini bila kubagua itikadi za Kidini, tuna mikakati mikubwa kwa ajili ya makundi haya mawili, tunaomba atuunge mkono katika huduma hii.

Natanguliza shukrani nyingi kwako kunisaidia nipate anwani yake.

Mungu akubariki sana.

Ndimi
Bishop Mike Basil Mtweve
Full Salvation Christian Church,
(Nyanda za Juu Kusini)
Box 1032,
Iringa
Tanzania.

[email protected]

Kilichosababisha Mwl. Nyerere kuanza kuwatumia watumbuizaji kwenye shughuli maalumu

Huyu ni mchezaji mashuhuri wa ngoma ya Ekesa na Bwenga, Warioba Kebarata wa Ikizu.

MWAKA 1978, wakati Majeshi ya Ukombozi ya Tanzania yakirejea Nchini, baada ya kumfukuza mvamizi nduli Iddi Amin Dadaa wa Uganda, aliyevamia ardhi ya Tanzania akidai kuwa sehemu ya Kyaka, iliyoko Ziwa Magharibi, Mkoani Kagera ni sehemu ya Uganda, baada ya kupata kipigo kikali kutoka kwa majeshi yetu, vikundi mbalimbali vya ngoma za asili vya makabila ya Tanzania, viliongeza hamasa ya mapokezi kwa wapiganaji wetu walipokuwa wakirejea nyumbani.

Kitime asimulia wimbo wao uliopigwa marufuku, "Bomoa Tutajenga Kesho"


BOMOA TUTAJENGA KESHO- Orchestra Mambo Bado, Mtunzi -Tchimanga Assossa


Bendi yangu kubwa ya kwanza kujiunga ilikuwa Orchestra Mambo Bado. Baada ya kukamilisha filamu ya Wimbo Wa Muanzi, ikalazimika kurekodi muziki kwa ajili ya filamu hiyo. Mimi nikiwa na wenzangu William Maselenge, Ally Lashku, Hashim Kasanga tulifika studio za TFC Mikocheni, pale ilipo Cine Club, tukiambatana na Kick Van De Heuvel ambaye ndiye alikuwa producer wa filamu hiyo (Huyu Kick ndiye aliyekuja kuanzisha bendi ya Tatu Nane). Pale studio tulimkuta Tchimanga Assossa akiwa na wanamuziki wengine wakiwa wanarekodi wimbo wa tangazo la TANPAX pads.

Hivyo tulizungumza nao ili kushirikiana kupiga nyimbo ambazo tulikuwa tumeshazitunga. Tulifanya mazoezi na hatimaye kurekodi nyimbo nane. Baada ya hapo ndipo Assossa akatuambia ana mpango wa kuanzisha bendi. Mimi na William Maselenge tulijiunga na wale wanamuziki tuliowakuta na Assossa katika kuanzisha bendi ya Orchestra Mambo Bado. Bendi hii iliweka makao yake makuu Mabibo nyuma ya Ubungo Maziwa. Pale kulikuwa na mfanyabiashara mmoja alikuwa anataka kufungua bar na restaurant, hivyo ikawa mpango kuzindua bendi na kuzindua bar na restaurant ile uwe siku moja. Bar ilikuwa na geti kubwa la chuma na hata ikapata jina la Lango La Chuma.

Siku chache kabla ya ufunguzi mfanyabiashara yule alipita kuangalia mazoezi na mmoja ya wanamuziki akamtania kuwa tayari kulikuwa na ufa kwenye geti hivyo siku ya uzinduzi ukuta utabomoka kwa kujaa watu. Jibu la yule mfanyabiashara lilikuwa. ‘Bomoa tutajenga Kesho’. Wanamuziki wakalipenda lile neno, na Assossa akatunga wimbo ukaitwa Bomoa Tutajenga Kesho, hata staili ya uchezaji wa show ikaitwa Bomoa. Wimbo uliporekodiwa ukatokea kupendwa sana na kuwa nembo ya bendi.

Siku moja tukasoma kwenye gazeti kuwa Umoja wa Vijana wa Dar es Salaam umepiga marufuku mambo kadhaa. Ulipiga marufuku wasanii kujiita ‘aka’ zilizokuwa za lugha za kigeni, mwanamieleka mmoja alikuwa anajiita Power Savimbi akambiwa asitumie tena jina hilo, ikawa marufuku kusema shule za vidudu, ila ziitwe chekechea, stage show ilipigwa marufuku, na wimbo huo pia ulipigwa marufuku. Ikawa hausikiki tena redioni japo bendi tuliendelea kuupiga kwa wizi. Mpaka leo sijaweza kujua hasa kwa nini wimbo huo ulipigwa marufuku. Haikuwa rahisi kuulizia hilo kwani wakati huo Umoja wa Vijana ulikuwa na nguvu sana.

Wacheza show wa bendi walikuwa kati ya wacheza show maarufu nchini wakati ule Pangapanga, Chileshi Ally, Stella na Nadhifa. Bendi hii ilikuwa chini ya Tchimanga Assossa ambaye ndiye alikuwa muimbaji na mtunzi mkuu.

Wimbo huu ulikuwa na washiriki wafuatao:-
Waimbaji walikuwa Tchimanga Assossa, George Mzee, Athumani Cholilo, John Kitime, Lucas Faustin na msichana pekee Jenipher Ndesile, Solo Huruka Uvuruge, William Masilenge rhythm gitaa, Likisi Matola Bezi gitaa, Andre Milongo gitaa la Solo la pili, Sadi Mnala Drums.

WOTE- Bomoae Bomoae Bomoa mama tutajenga kesho imaa, Tujajenga kesho imaa x2

JENIFA NDESILE-Imaao enyi watoto wazuri wote, njoni tucheze leo bomoa

WOTE- Bomoae Bomoae Bomoa mama tutajenga kesho imaa, Tutajenga kesho imaaa

ASSOSSA- O betu bayai yoyoyo bomoa

WOTE- Bomoae Bomoae Bomoa mama tutajenga kesho imaa, Tutajenga kesho imaaa

SOLO GITAA

WOTE- Bomoae Bomoae Bomoa mama tutajenga kesho imaa, Tujajenga kesho imaa x2

JENIFA NDESILE-Imaao enyi watoto wazuri wote, njoni tucheze leo bomoa

WOTE- Bomoae Bomoae Bomoa mama tutajenga kesho imaa, Tutajenga kesho imaaa

ASSOSSA- O betu bayai yoyoyo bomoa

WOTE- Bomoae Bomoae Bomoa mama tutajenga kesho imaa, Tutajenga kesho imaaa

ASSOSSA-Kumbe njoni wote tucheze bomoa

WOTE- Kumbe njoni wote tucheze bomoa

ASSOSSA- O betu bayai yoyoyo bomoa

WOTE- Bomoae Bomoae Bomoa mama tutajenga kesho imaa, Tutajenga kesho imaaa

Taarifa ya habari ChannelTEN, 24.01.2016

Ufa hatimaye shimo linalokata njia ya lami Mtua barabara ya Lindi - MasasiMvua zinazoendelea kunyesha nchini Tanzania katika maeneo mbalimbali ,hapo Jana January 22, 2016 usiku imeleta madhala ya kubomoa daraja maeneo ya mtua Barabara ya Lindi – Masasi.


 • Picha kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Road Safety Ambassadors (RSA)

UKAWA yazuia uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar kwa nyaraza zilizoshitukia njama

Naibu Katibu Mkuu CHADEMA Zanzibar Salum Mwalimu akizungumza. Wengine ni wajumbe halali wanaopiga kura kwenye uchaguzi huo wakiwemo Madiwani na wabunge wa Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni.

HALMASHAURI ya jiji la Dar es Salaam imeahirisha uchaguzi wa Meya wa Jiji uliokuwa ufanyike Januari 23, 2016 mpaka hapo tarehe itakapotangazwa baadaye.

Mkuu wa Kitengo cha Itifaki na Uhusiano na Umma wa Jiji, Gaston Makwembe alisema uchaguzi huo uliokuwa ufanyike saa nne asubuhi katika ukumbi wa Mmikutano wa Karimjee, umeahirishwa.

Alisema tarehe ya uchaguzi huo itapangwa baadaye na taarifa zitatolewa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari bila kueleza sababu ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo.

Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa na mvutano wa aina yake kati ya vyama vinavyounda na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Diwani wa Kata ya Vijibweni, Isaya Mwita (CHADEMA) ndiye atapeperusha bendera ya UKAWA huku mgombea wa nafasi ya Naibu Meya akitarajiwa kutoka CUF.

Chama Cha Mapinduzi (CCM ) wakiwakilishwa na Diwani wa Kinondoni, Yusuph Omary Yenga.

Inaelezwa kuwa UKAWA wanapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho kutokana na kuwa na idadi kubwa ya madiwani ambapo wanaizidi CCM kwa jumla ya madiwani 13.

Ikiwa UKAWA watafanikiwa kutwaa jiji hilo, itakuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa wapinzani kuliongoza tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.

Awali, Ofisa Habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, alitoa mwito kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusimamia uchaguzi huo kwa amani na haki ili usifanyike kama wa kumtafuta meya wa Ilala na Kinondoni uliokuwa na mizengwe mingi.

DSC_1099

Pichani ni Naibu Katibu Mkuu CHADEMA Zanzibar Salum Mwalimu akionesha nyaraka ambazo zinadaiwa kufanyiwa ‘fojali’ (forgery) zilizoelezea kuwa zinatoka Tume. Hata hivyo UKAWA wameeleza kuwa nyaraka hizo wanatarajia kuziwasilisha Jeshi la Polisi kwani kuna baadhi ya vitu vimefojiwa huku vikibainisha kuwa vinatoka Tume hiyo ya Taifa ya Uchaguzi.

Abiria wazuia wafanyakazi wa kituo cha mizani kutoza faini basi lililodai kuzidisha uzito

Moja ya gari likishindwa kupita kwenye mizani ya Uyole baada ya kuwekewa mawe na abiria wa Basi la New Force

ABIRIA waliokuwa wakisafiri na basi la Newforce lenye namba za usajili T 520 CXE linalofanya safari kati ya Kyela na Dar es salaam walilazimika kuweka mawe kwenye kituo cha mizani Uyole wakipinga kitendo cha wafanyakazi wa kituo hicho kulitoza faini basi hilo kwa madai ya kuzidi uzito.

Waliibua tafrani wakionekana wakiwa na hasira wakibeba mawe na kuyaweka kwenye njia ya kupita kwenye mizani ili kuzuia magari mengine yasipime kwa kile walichodai hadi hapo watakapooneshwa uzito unaodaiwa kuzidi wa Basi hilo.

‘Tunataka watuoneshe uzito wa hii gari wanadai limezidi uzito wakati ndani ya Basi tupo abiria 41 na hili basi linabeba abiria 57,’alisema mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la Angelina Basiku anayesafiri kuelekea jijini Dar es Salaam.

Naye abiria aliyejitambulisha kwa jina la Ephraim Mwankenja alisema kuwa kitendo hicho ni wizi wa wazi wa baadhi ya watumishi wa mizani katika maeneo mengi ambao hutoza faini kinyume cha taratibu.

Mwankenja alisema iwapo basi linakuwa limezidisha abiria au mizigo uzito wake unaonekana na kuwa kitendo cha kusema basi hilo limezidi uzito wakati lina abiria wachache na halina mizigo ni kitendo kinachotia mashaka utendaji wa wafanyakazi hao.

Hata hivyo alisema kuwa kitendo hicho mbali ya kuwa na dalili ya wizi wa wazi pia kinaleta kero na usumbufu kwa abiria wanaohitaji kusafiri kwa usalama.

Abiria mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mama Mwalukuta alisema kuwa yeye amekuwa anasafiri mara nyingi na magari kuelekea Dar es salaam na kuwa iwapo Basi limebeba mizigo mingi au kuzidisha abiria uzito huongezeka kwenye mizani na kwamba ndani ya basi hilo siti nyingi ziko wazi.

Mkazi wa Uyole aliyejitambulisha kwa jina la Michael Somo alidai kuwa kituo hicho cha Mizani kimekuwa kikilalamikiwa na madereva wengi ambapo limekuwa ni tatizo sugu kutokana na tabia ya kuongeza vipimo vya mizani kwa nia ya kujipatia fedha kwa njia isiyo halali.

‘Inawezekana huu ndio utaratibu wanaoutumia hawa wafanyakazi kujipatia fedha kwa njia isiyo halali, gari likizidi uzito linatakiwa kulipa fidia, gari letu ni tupu halina abiria huo uzito umetoka wapi,’alihoji kondakta wa Basi hilo aliyejitambulisha kwa jina la Abdul Paresh.

Paresh alisema kawaida uzito wa basi hilo unatakiwa usizidi GVM 23,000 na kuwa wafanyakazi wa mizani walipima uzito ambao ulikuwa mbele ni GVM 8,550 na nyuma GVM 11,100 na hivyo kutakiwa kulipa faini sh. 36,000 na kwamba hata hivyo walipofika kituo cha Makambako wamepima tena uzito ambao umesomeka mbele GVM 7,400 na nyuma GVM 11,100.

Kwa upande wake Yuhai Chen ambaye ni msimamizi wa mabasi ya New Force Nyanda za Juu kusini alisema kuwa Basi hilo hata kama lingekuwa na abiria 61 bado uzito usingeweza kuongezeka na kuwa kilichofanyika ni ujanja wa wafanyakazi hao kujipatia fedha kwa njia isiyo halali.

Chen aliomba ipimwe tena wafanyakazi wakakataa na kudai kuwa kompyuta yao ilikuwa mbovu na kuhoji kuwa iwapo kompyuta yao ni mbovu inakuwaje wanatoa huduma.

‘Huu ni ubabaishaji wametupimia wanakataa kurudia kutupimia wakidai kuwa kompyuta ni mbovu, inawezekana wanaibia watu kwa kutoa huduma kwa kompyuta mbovu’ alisema Chen.

Msimamizi wa kituo cha Uyole alipoulizwa tatizo hilo alisema kuwa yeye hana mamlaka ya kutoa maelezo juu ya suala hilo kwa kuwa si msemaji wa TANROAD ambapo Mkuu wa wahandisi wa TANROAD ambaye jina lake limesomeka kupitia namba yake ya simu ya mkononi jina la Boniface Mkumbo alidai kuwa yupo njiani kufika eneo la kituo.

Basi hilo liliondoka majira ya saa 5:00 katika kituo hicho cha Mizani Uyole bila masharti ambapo pia Mkuu wa wahandisi wa TANROAD Mkumbo alikuwa bado kufika eneo hilo kutolea ufafanuzi tatizo la wafanyakazi wa kituo hicho kudaiwa kuzidisha vipimo vya uzito wa magari eneo hilo.

Hata hivyo kwa mujibu wa Kondakta aliyesafiri na Basi hilo kuelekea jijini Dar es salaam Abul Paresh alisema kuwa waliruhusiwa kuondoka hapo baada ya shinikizo la abiria kutaka kurudia kupima Basi hilo ambalo katika kipimo cha kwanza lililonekana limezidi 8,550 na nyuma 11,000.

Alisema uzito huo haukuwiana na mzigo wa Basi hilo na kuwa baada ya kuondoka walipima tena katika mzani wa Makambako ambapo wamepata uzito wa 7,400 mbele na nyuma 11,100.

Awali walipotakiwa kupima tena walikataa na kuwa wamekwisha pima inatakiwa kulipa faini hadi pale alipofika askari na mwandishi wa habari hizi ndipo walipopima na kukuta uzito wa GVM 7,750 na nyuma GVM 11,000.


Baadhi ya abiria wa Basi la Newforce walioibua tafrani kwenye Kituo cha Mzani Uyole jana asubuhi


Basi la Newforce likiwa katika kituo cha mizani Uyole jana


Kituo cha Mizani Uyole jijini Mbeya


Kipimo cha Mzani wa Uyole kikisomeka 3500 baada ya shinikizo la kurudia kupima mara ya pili ambapo awali ilisomeka 7750


Msimamizi wa kituo cha Mizani Uyole ambaye aligoma kuwaonesha kipimo wafanyakazi wa Basi la New Force ambao walidai kipimo kilichoelezwa na msimamizi huyo hakisemi ukweli • via Rashind Mkwinda blog

Taarifa ya Wizara: Idadi ya raia wa kigeni waliokamatwa na nchi wanakotoka

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga amesema zoezi linaloendelea sasa la kukamata raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi hapa nchini bila vibali halitawagusa wageni wenye vibali halali.

Mheshimiwa Kitwanga ameyasema haya mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na jumuiya ya raia toka nchini China wakati wa sherehe zilizoandaliwa na raia hao katika Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam.

Katika sherehe hizo ambazo ziliandaliwa mahsusi kuukaribisha mwaka Mpya wa Kichina, Mheshimiwa Kitwanga alisema uhusiano wa Tanzania na China ulianzishwa na marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kiongozi wa China, marehemu Mao Zedong zaidi ya miaka hamsini iliyopita.

Amesema uhusiano huo umeendelea kuimarishwa hadi katika nyanja za kiuchumi ambapo hadi sasa kuna zaidi ya Kampuni 500 za Kichina ambazo zinafanya shughuli za kibiashara hapa nchini ambazo zimetoa zaidi ya nafasi 100,000 za kazi kwa Watanzania.

Mheshimiwa Kitwanga alitumia fursa ya sherehe hizo kuwahakikishia wawekezaji wote waliopo hapa nchini kuwa Serikali ya Tanzania italinda biashara zao kufuatana na sheria za nchi.

Kuhusu zoezi linaloendelea hapa nchini la kukamata wageni ambao wanaishi na kufanya kazi bila vibali halali alisema kumekuwa na taarifa za uzushi zinazoenezwa hapa nchini na nje ya nchi kuwa Serikali ya Tanzania inawafukuza wageni kwa vile haihitaji raia wa kigeni hapa nchini.

Amesema taarifa hizo ni za uongo zinazolenga kuichafua Tanzania katika jumuiya ya kimataifa na kusema raia wa kigeni wanaokamatwa ni wale tu wasio na vibali halali vya kuishi na kufanya kazi hapa nchini.

Amesema zoezi hilo ni la kawaida na linafanywa kufuatana na Sheria za Uhamiaji lakini halitawahusu wageni wenye vibali halali vya kufanya kazi na kuishi nchini.

Kati ya mwaka 2014 na Januari 2016 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetoa vibali vya ukaazi kwa jumla ya wageni 40,765 toka mataifa mbalimbali na idadi hiyo inaendelea kuongezeka siku hadi siku.

Wageni waliofukuzwa kwa sababu mbalimbali mwaka 2015 ni 1,642.

Aidha, kati ya 08 Desemba, 2015 na 14 Januari, 2016 raia wa kigeni waliokamatwa kwa kuishi na kufanya kazi nchini bila vibali halali ni kama ifuatavyo:
 1. Burundi 284
 2. Kenya 26
 3. Uganda 13
 4. Somalia 7
 5. Ethiopia 157
 6. DRC 34
 7. China 285
 8. India 41
 9. Zambia 40
 10. Nigeria 08
 11. Lebanon 01
 12. Ivory Coast 10
 13. Madagascar 05
 14. Malawi 27
 15. Korea 09
 16. Zimbabwe 01
 17. Ghana 01
 18. Rwanda 03
 19. Afrika Kusini 01
 20. Wenye uraia wa utata 11.
Kati ya hawa, wengine wamemepelekwa katika kambi za wakimbizi, hasa raia waliotokea Burundi, wengine wamepewa amri ya kuondoka nchini na wengine kesi zao ziko katika hatua mbalimbali mahakamani.

MWISHO

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi – 24 Januari, 2016

Mbunge atoa vitabu 20 elfu kwa shule zilizomo jimboni mwakeMBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini,na Waziri wa Nishati na Madini,Profesa Sospeter Muhongo ametoa vitabu elfu 20 vya masomo mbalimbali kwa shule za msingi na sekondari katika kusaidia kuinua kiwango cha elimu mashuleni.

Katuni: Tumekosea kuingia...
Membe ajibiwa na Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania

KUSAFIRI NJE YA NCHI

Ndugu Membe anapotosha ukweli anaposema Tanzania sio kisiwa na kwamba Raisi na waziri wake wa mambo ya nje lazima wasafiri nje ya nchi watake wasitake.

Tunapenda kumfahamisha ndugu Membe kuwa, mh. Raisi Dr. John Magufuli hajatoa kauli kuwa yeye au wasaidizi wake hawatosafiri nje ya nchi katika safari za muhimu na zenye tija. Isipokuwa, muongozo wa mh. Rais kuhusu safari za nje unalenga kupunguza safari zile ambazo hazina ulazima na tija kwa taifa.

KUHUSU MGOGORO WA UCHAGUZI WA ZANZIBAR

Katika maelezo aliyonukuliwa na gazeti la Mwananchi, ndugu Membe alieleza kupinga kufutwa kwa matokeo yote ya uchaguzi wa Zanzibar yakiwemo ya wawakilishi, na kwamba jambo hili limeihuzunisha dunia.

Kauli hii ya ndugu Membe inatushangaza na kutusikitisha sana. Kwanza tunajiuliza, Je, ikiwa sehemu kubwa ya uchaguzi iligubikwa na udanganyifu na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi kinyume na sheria za uchaguzi wa Zanzibar, ni kwanini ndugu Membe ashangae uchaguzi wote kufutwa na tume ya uchaguzi ZEC?

Tunamtaka ndugu Membe atueleze, ni dunia ipi hiyo inayotushangaa?

Ni kwanini dunia hiyo anayoitetea ndugu Membe haijashangaa kumuona maalim Seif Shariff Hamad akijitangaza kuwa mshindi kinyume cha sheria za uchaguzi?

Ndugu Membe anapaswa kushangaa, ni kwanini hadi leo hii maalim Seif Shariff Hamad hajakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kujitangaza kuwa mshindi kinyume cha sheria.

KUHUSU VIKAO VYA MARIDHIANO

Kuhusu vikao vya maridhiano vilivyokua vinaendelea, ndugu Membe amekosoa kitendo cha Raisi wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na maalim Seif Shariff hamad kuachwa wakazungumza wenyewe wawili.

Kwanza tunasikitika kuwa ndugu Membe huenda ama hajui kinachoendelea Zanzibar au ameamua kupotosha umma kwa makusudi. Hii ni kwasababu mazungumzo yaliyokua yakiendelea Zanzibar, hayakuwahusisha Dr. Shein na maalim Seif Shariff peke yao. Bali yalishirikisha marais wastaafu wa Zanzibar, Raisi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar.

Pili, katika muafaka wa kisiasa wa Zanzibar wa mwaka 2009/2010 uliopelekea kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, kwa kiasi kikubwa ni maalim Seif Shariff hamad na Rais wa Zanzibar wa wakati huo mh. Amani Abeid Karume pekee walioshiriki mazungumzo.

RAI KWA NDUGU MEMBE

Mosi, tunapenda kumkumbusha ndugu Bernard Membe kuwa yeye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa amewahi kuwa mjumbe wa kamati kuu ya CCM. Hivyo anajua utaratibu wa Chama na anayo nafasi ya kuyasema mawazo yake juu ya uendeshaji wa serikali ndani ya vikao halali vya chama. Aidha, ndugu Membe kwa nafasi yake kama mjumbe wa NEC na waziri wa zamaniwa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, anayo nafasi ya kutoa ushauri na maoni yake moja kwa moja kwa Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mh. Dr. John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM taifa Dr. Jakaya Kikwete au kwa Katibu Mkuu wa CCM ndugu Abdulrahman Kinana.

Kutotumia fursa hizo kutoa maoni yake ni kujishushia heshima mbele ya jamii.

Pili, tunamkumbusha ndugu Membe kuwa yeye sasa ni mstaafu aliyeitumikia nchi yake kwa muda mrefu na nafasi mbalimbali. Ni vema sasa akatoa fursa kwa viongozi wengine walioko madarakani kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia watanzania. Muda wake umekwisha na sasa ni busara akakaa kimya na kuchunga maneno yake.

Raisi mstaafu wa awamu ya tatu mh. Benjamin William Mkapa aliwahi kusema (nanukuu):-
"Siku moja mtoto mdogo aliwahi kuniuliza. Nani ni bingwa wa kuendesha shughuli za serikali? Nikatafakati sana swali lile, kisha baada ya muda nikamjibu…Ni mwanasiasa aliyestaafu kisha akachunga ulimi wake…"

MWISHO

Tunamshauri ndugu Membe kuuchukua ushauri huu wa Raisi mstaafu Benjamin Mkapa, utamsaidia. Aidha tunamtaka afahamu kwamba watanzania wana imani kubwa na juhudi zinazofanywa na serikali katika kupunguza matumizi, kuziba mianya ya rushwa, ukwepaji kodi na ubadhirifu wa mali za umma. Wakati huu si wa kupika majungu, fitina wala ubabaishaji. Ni wakati wa kuungana pamoja kama taifa na kuchapa kazi tu.

Asanteni.

Imetolewa na ndugu

ALLY S. HAPI
KATIBU WA IDARA,
ELIMU, UTAFITI NA UONGOZI,
SHIRIKISHO LA VYUO VYA ELIMU YA JUU TANZANIA

TRA yakamata maboksi 294 ya StarTimes yenye simu na vifaa mbalimbali

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imedai kukamata maboksi 294 yenye simu 2,744, na vifaa mbalimbali vya simu katika ghala la Kampuni ya StarTimes.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya StarTimes, Clement Mshana alisema yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa wiki na hajapokea taarifa yoyote kutoka TRA kuhusu kukamatwa kwa mizigo hiyo.

“Nimesikia kwenye gazeti lenu sijui chochote,” alisema.

Juzi, mamlaka hiyo ilikamata maboksi hayo ambayo thamani yake haijajulikana baada ya kutilia shaka nyaraka za mizigo hiyo iliyoingizwa nchini ikiwa haionyeshi ni ya nani.

Pia, TRA ilitilia shaka mizigo hiyo ilikotoka na kuwa na taarifa zenye utata kuhusu idadi ya mizigo hiyo. Mkurugenzi wa Huduma ya Elimu kwa Mlipa Kodi (TRA), Richard Kayombo alisema walipokea taarifa za utata wa mizigo iliyodaiwa kuingizwa na kampuni hiyo jambo lililowalazimu kwenda kuikamata kwa ajili ya uchunguzi.

“Tulikamata maboksi yaliyokuwa na simu na vifaa mbalimbali kama vile betri, chaji za simu, powerbank na kava za simu,” alisema Kayombo.

Alisema baada ya kuikamata waligundua kulikuwa na udanganyifu wa idadi ya maboksi yaliyokuwa kwenye nyaraka, kwani zilisomeka kuwa kuna maboksi 211, lakini katika uchunguzi walikuta 294.

Alisema mizigo hiyo ilikuwa haionyeshi ni ya nani na kama imelipiwa kodi, hivyo bado iko mikononi mwao hadi pale watakapojiridhisha na uchunguzi.

“Boksi hizo ziko chini ya TRA, bado tunaendelea na uchunguzi ili kujiridhisha na kujua mizigo hiyo ni ya thamani kiasi gani, imelipiwa kodi na kufuata taratibu zote za usafirishaji au la,” alisema.

Alisema endapo watabaini kuwa mizigo hiyo haijalipiwa kodi hatua za kisheri a zitachukuliwa kwa wahusika.

Balozi wa Tanzania amwakilisha Waziri mkutanoniBalozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Eng. John W.H. Kijazi akimwakilisha Mhe. Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini katika Mkutano wa Nne (4) wa “India – Africa Hydrocarbons Conference”ulioandaliwa na Wizara ya Petroli na Gesi ya Serikali ya India. 

Mkutano huo ulianza tarehe 21 na kumaliza tarehe 22 January 2016, mjini New Delhi, India.


Siku 100 za Rais Magufuli madarakani: Wajiandaa kwa ‘hapa kazi tu’ Half Marathon

Kocha wa timu ya taifa ya Riadha ,Francis John akiwa na wanariadha ,Alphonce Felix na Said Makula waliofuzu viwango vya kushiriki mashindano ya Olyipiki ,walipotamburishwa mbele ya wanahabari. 
SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT) limeandaa mbio fupi kwa ajili ya kuhitimisha siku 100 za rais Dk. John Pombe Magufuli kuwa Ikulu zitakazotimua vumbi jumamosi hii januari 30 mwaka huu mjini Dodoma.

Mbio hizo zimepewa jina maalumu la Dodoma ‘hapa kazi tu’ Half Marathon ambazo zitashirikisha washiriki mbali mbali wakiwamo waheshimiwa wabunge,mawaziri,wanafunzi,walemavu na wanariadha wakongwe nchini.

Akizindua mbio hizo mjini Moshi mwishoni mwa wiki zinazodhaminiwa na Kampuni ya GSM Foundation, Rais wa shirikisho hilo,Anthony Mtaka alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa mbio hizo ambazo zimeandaliwa na kuendeshwa na shirikisho hilo ni kufufua michezo hapa nchini.

Pia alisema mbio hizo zitatumika kwa ajili ya kumpongeza Rais Dk. John Pombe Magufuli kutimiza siku 100 tangu aingie maradakani ambazo zitakuwa februari 14 mwaka huu.

Kwa mujibu wa rais huyo wa RT,mbio hizo zimegawanywa katika makundi matatu ambako mbio za kwanza ni za kilomita 2.5 ambazo zitashirikisha wabunge,mawaziri,walemavu,wanafunzi ,wazee na watu mbalimbali.

Mbio za kilomita 5 ambazo ni za kujifurahisha zitashirikisha wakimbiaji wote na mbio za nusu marathon ambazo zitakuwa ni mbio za ushindani washindi watapata zawadi .

Akitangaza zawadi kwa washindi,Mtaka alisema mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaumme na wanawake atapata zawadi ya piki piki yenye thamani ya sh milioni 2.8,mshindi wa pili akipata bati 100, wa tatu bati 40, mshindi wa nne akipata sh 200,000 huku mshindi wa tano akiondoka na sh100,000.

Mshindi wa sita hadi wa kumi watapata kifuta jasho cha sh 50,000 kila mmoja huku waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa ndiye atayakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mbio hizo na atashiriki mbio za kilomita 2.5.

Wanafunzi waatakaopenda kushiriki mbio hizo watasajiliwa kwa sh 500, huku vwasio wanafunzi wakisajiliwa kwa sh 1,000 na wingine ambao hawakutajwa ni kundi gani wakisajiliwa kwa sh,5,000 na fedha hizo kwa mujibu wa Mtaka zitasaidia kambi ya wanariadha watakaoshiriki michuano ya Olimpiki.

Uzinduzi huo pia ulitumika kuwatambulisha wanariadha wawili ambao wamekidhi vigezo vya kushiriki michuano ya Olimpiki itakayofanyika nchini Brazil mapema mwezi Agosti mwaka huu ambako nchi zaidi ya 216 kutoka kila kona ya dunia zitashiriki.

Wanariadha hao ni Alphonce Felix ambaye ana wastani wa muda wa kukimbia wa saa 2:12.01 na Said Makula ambaye muda wake wa kukimbia ni saa 2:13.27 na watatumia mbio hizo mjini Dodoma kama majaribio yao ya kitaifa kati ya majaribio sita ya kitaifa kabla ya kwenda Brazil.

Julai 6 mwaka jana,Felix alishiriki mbio za Gold Coast Marathon nchini Australia na kumaliza nafasi ya sita huku Makula akishiriki mbio za Casablanca Marathon oktoba 25 mwaka jana na kumaliza katika nafasi ya nne.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania ,Anthony Mtaka akiwa na Mwe3nye3kiti wa Chama cha riadha mkoa wa Kilimanjaro,( KAA) Liston Methacha wakati wa uzinduzi rasmi wa mbio za Dodoma Hapa Kazi tu Half Marathoni 2016 zinzotarajia kufanyika January 30 mwaka huu mjini Dodoma.

Baadhi ya wadau wa Riadha wakifuatiia mkutano wa uzinduzi wa Mbio za Dodoma Hapa kazi tu Half Marathon 2016 uliofanyika katika Hotel ya Nyumbani mjini Moshi.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) Anthony Mtaka akizungumza na wanahabari (hawako pichani ) wakati wa uzinduzi rasmi wa Mbio hizo.Raisi wa RT, Mtaka kifanya mahojiano na Mwandishi wa habari, Enos Masanja wa Azam TV.
 • Imeandaliwa na Charles Ndagulla,Rodrick Mushi na Dixon Busagaga.