Mkutano wa majadiliano ya mandeleo ya tafiti, tiba, elimu na mafunzo ya ugonjwa wa seli mundu (sickle cell)


Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sikoseli Tanzania (SCFT), Prof. Julie Makani akizungumza katika mkutano wa wadau kujadili maendeleo ya tafiti, elimu, matibabu na mafunzo kuhusu ugonjwa wa sikoseli nchini katika kipindi cha miaka 10 katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Profesa Makani pia ni Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Damu ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS). Sikoseli ni ugonjwa wa kurithi kutoka kwa wazazi wenye vinasaba vya ugonjwa huo.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya (kulia) akizungumza na baadhi ya wadau walioshiriki mkutano kujadili maendeleo ya tafiti, elimu, matibabu na mafunzo kuhusu ugonjwa wa sikoseli nchini katika kipindi cha miaka 10 katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sikoseli Tanzania (SCFT), Prof. Julie Makani ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Damu ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sikoseli Tanzania (SCFT), Prof. Julie Makani (wa pili kushoto), ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Damu ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) akiwa na baadhi ya wadau walihudhuria mkutano kujadili maendeleo ya tafiti, elimu, matibabu na mafunzo kuhusu ugonjwa wa sikoseli nchini katika kipindi cha miaka 10 jijini Dar es Salaam jana. Kutoka kushoto ni, Prof. Japhet Killewo, mhadhiri kutoka MUHAS, Dk, Namala Mkopi, daktari bingwa wa watoto na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Watoto (PAT) na Promise Mwakale, Ofisa Uhusiano katika taasisi ya sikoseli.

Mratibu wa matibabu ya Sikoseli katika kitengo ugonjwa huo kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Deogratius Soka (katikati) akibadilishana mawazo na wadau. Kushoto ni Promise Mwakale, Ofisa Uhusiano katika taasisi ya sikoseli na kulia ni Dk, Namala Mkopi, daktari bingwa wa watoto na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Watoto (PAT). Imeelezwa Tanzania ni moja ya nchi yenye inadadi kubwa ya wagonjwa wa sikoseli ikikadiriwa kuwa watoto kati ya 8,000 na 11,000 huzaliwa kila mwaka wakiwa tatizo hilo.

Mmoja wa watu wanaosumbuliwa na tatizo la sikoseli, Hadija Abdallah (20) akitoa ushuhuda wake jinsi anavyoweza kuishi maisha ya kawaida licha ya kugunduliwa na ugonjwa huo akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu.

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sikoseli Tanzania (SCFT), Prof. Julie Makani (wa pili kushoto), ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Damu ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) akiwa na baadhi ya wadau walihudhuria mkutano kujadili maendeleo ya tafiti, elimu, matibabu na mafunzo kuhusu ugonjwa wa sikoseli nchini katika kipindi cha miaka 10 jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dk. Neema Rusibimayila na Dk Sarah Maongezi mkurugenzi masuala ya afya wa Mfuko wa Wanawake na Maendeleo (WAMA).

Ofisa Mtendaji wa Mkuu wa Benjamin William Mkapa Hiv/Aids Foundation, Hellen Mkondya-Senkoro (kulia) akizungumza na Mkurugenzi wa Deloitte, Zahra Nensi huku Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sikoseli Tanzania (SCFT), Prof. Julie Makani akiangalia wakati wa hafla hiyo. Imeelezwa ugonjwa wa sikoseli unatibika kirahisi endapo utagundulika mapema katika umri mdogo.

Waziri Ndalichako asitisha mkataba wa Mkurugenzi Bodi ya Mikopo na kusimamisha Wakurugenzi 3 HESLB

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amevunja mkataba wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) nchini, George Nyategi na kuwasimamisha kazi wakurugenzi wengine watatu huku akitaka uchunguzi ufanyike haraka.

Mkataba wa Bw. Nyageti uliopaswa kuisha tarehe 31/08/2016 umevunjwa leo na kuamriwa alipwe mshahara wa mwezi mmoja kwa mujibu wa kifungu namba 50,03,a cha kanuni za kudumu.

Wengine waliokumbwa na fagio hilo ni pamoja na Mkurugenzi wa Fedha, Bw. Yusuph Kisare, Juma Chagonja, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo na Bw. Onesmo Laizer na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Yusuf Kisare.

Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kuwepo kwa ukiukwaji wa utoaji wa mikopo pamoja na ucheleweshaji usio na sababu za msingi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Profesa Ndalichako amesema kuwa bodi ya mikopo imekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wanafunzi wanaostahili kupata mikopo na kufanya kwao kuweza kupata mikopo mpaka waandamane wizarani kwa kusababishwa na watu wachache wa bodi hiyo.

Profesa Ndalichako, amesema katika udhaifu wa utendaji huo ni pamoja na ulipaji wa mikopo kwa wanafunzi 23 waliolipwa katika vyuo viwili tofauti kwa miaka mitatu mfululizo kwa chuo cha kwanza zililipwa zaidi ya sh.milioni 653 na chuo cha pili ni zaidi ya sh. milioni 147.

Amesema baadhi ya wanafunzi ambao walikwenda kusoma nchini Algeria wamekuwa wakiendelea kulipwa fedha wakati mkataba wao umekwisha kwa kipindi cha miaka saba.

Profesa Ndalichako amesema wanafunzi 169 walipata mikopo katika vyuo viwili tofauti kwa miaka mitatu mfululizo na kulipa chuo cha kwanza zaidi ya sh.milioni 658 na chuo cha pili zaidi ya sh. milioni 665 na wanafunzi 55 walioacha masomo walilipwa zaidi ya sh.milioni 136 huku wanafunzi 343 wasiokuwa na usajili kwenye vyuo husika walilipwa zaidi ya sh.milioni 342.

Aliongeza kuwa zaidi ya sh.milioni 159 zililipwa kwa wanafunzi 306 zaidi ya kiwango kilichobainishwa kutokana na muongozo wa upangaji na ukopeshaji wa mwaka 2008/2009 na 2009/2010.

Aidha amesema kuwa wanafunzi 77 walipatiwa mikopo kwenye vyuo vya ndani na nje ya nchi kwa wakati mmoja ambapo walilipwa zaidi ya sh.milioni 467 kwa vyuo nje na zaidi ya sh.milioni 123 kwa vyuo ndani pamoja na wanafunzi 19,348 walipata mikopo bila kupitiwa na kamati ya mikopo jambo ambalo ni kinyume na kanuni na 8ya kanuni za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Hatahivyo amesema wanafunzi 54,299 walipangiwa mikopo wakati hawakuwa wameomba ambapo walilipwa zaidi y ash.milioni 207 ambazo zilipelekwa kwenye vyuo sita.

Maendeleo ya ujenzi wa bomba la maji Ruvu Chini, Pwani - Dar es SalaamMafundi wakiendelea na kazi ya kulaza mabomba ya Maji eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam. Mabomba hayo ambayo sasa yamekamilika kwa urefu wa kilometa 54.8 kati ya 55.9 yatatumika kusafirisha maji kutoka mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.

Maneja wa Kampuni ya Gauff Consultants, Thorsten Seitz akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari kuhusu maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa bomba hilo la kusafirishia Maji kutoka Ruvu Chini

Maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa barabara ya Mwenge-Morocco


Kipande cha Barabara ya Mwenge-Morocco kilicho kamilika kwa kiwango cha lami katika eneo la Mwenge-Bamaga kinavyoonekana katika picha.


Sehemu ya Barabara ya Morocco kwenda Mwenge ikiwa katika hatua ya kutolewa tabaka ya udongo wa chini na kuwekwa tabaka ya udongo mpya kama inavyooenekana katika picha leo jijini Dar es Salaam .

Mafundi kutoka kampuni ya Ujenzi ya ESTIM wakiwa kazini katika hatua ya kutoa udongo wa chini kwa ajili ya kuweka udongo mpya ,ambapo ujnzi huo unatarajiwa kumalika mapema Mei mwaka huu.


Mafundi wakijengea bomba la maji eneo la Makumbusho kwa kuliwekea zege na nondo ili kulihakikishia usalama wake wakati wa ujenzi wa barabara ya Mwenge-Morocco inayotarajiwa kukamilika mapema mwezi Mei mwaka huu.

Afisa Habari Mkuu kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Bi.Aisha Malima akipata maelezo kutoka kwa Fundi Mchundo (Civil Technician) wa Kampuni ya Ujenzi ya ESTIM ,Bw. Kano Warema kuhusu maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mwenge-Morocco leo jijini Dar es Salaam. 
  • Picha na Lorietha Laurence –Maelezo

TRA yawahamisha wafanyakazi 104 kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa mingine

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya mabadiliko makubwa baada ya kuwahamisha wafanyakazi 104 waliokuwa Mkoa wa Dar es Salaam na kuwapeleka mikoa mbalimbali nchini.

Mbali na wafanyakazi hao, uhamisho huo umemkumba pia mmoja wa wakurugenzi wake, Aboubakar Kunenge ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala aliyehamishiwa mkoani Rukwa.

Akizungumza kwa njia ya simu Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alithibitisha wafanyakazi hao 104 kuhamishwa.

“Ni kweli wafanyakazi hao wamehamishwa, lakini huu ni utaratibu wa kawaida wa kiutawala na tumekuwa tukiufanya mara kwa mara, kila baada ya muda tunawahamisha baadhi ya wafanyakazi wetu,” alisema Kayombo.

Aidha, Kayombo alithibitisha kuwa ni kweli Kunenge ni mmoja wa watumishi wa mamlaka hiyo waliohamishwa na kukiri amepelekwa Rukwa, ambako ataendelea kushughulikia masuala hayo ya utawala na rasilimali watu.

Katika uhamisho huo, wafanyakazi wanaotoka kituo cha TRA Ilala waliohamishwa ni 43 ambao wamepelekwa mikoa ya Iringa, Kigoma, Mbeya, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Manyara, Tanga, Kilimanjaro, Pwani, Tabora, Morogoro, Lindi na Arusha.

Katika kituo cha Kinondoni, jumla ya wafanyakazi zaidi ya 11 wamehamishiwa katika mikoa Singida, Iringa, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Kagera, Mara, Tabora, Arusha na Tanga. Aidha, katika vituo vya Temeke, wafanyakazi zaidi ya 10 walihamishiwa katika mikoa ya Arusha, Morogoro, Iringa, Tabora, Mara, Kagera, Lindi, Morogoro, Kigoma na Rukwa.

Aidha, pia wamo wafanyakazi wawili kutoka Iringa waliohamishiwa Kinondoni Dar es Salaam, mmoja kutoka Iringa kwenda Ilala, Kisarawe kwenda Shinyanga na Bagamoyo kwenda Ruvuma.

Ingawa mkurugenzi huyo alikataa kuzungumzia sababu za kuhamishwa kwa mkupuo kwa watumishi hao, lakini kwa muda mrefu tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa afanye ziara ya kushtukiza katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Novemba mwaka jana, kumekuwa na msukosuko pia katika TRA.

Baada ya kukuta uozo wa kashfa ya ufisadi wa makontena, Waziri Mkuu huyo aliamuru kusimamishwa kwa Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade baada ya kubaini kupitishwa kwa makontena zaidi ya 300 bandarini bila kulipa kodi na kusababishia hasara Serikali ya zaidi ya Sh bilioni 80.

Pamoja na hayo, maofisa wote wa TRA ambao walihusishwa na sakata hilo walitakiwa kutosafiri nje ya nchi na kukabidhi hati zao za kusafiria mpaka pale uchunguzi dhidi yao utakapokamilika.

Aidha, miongoni mwao tayari wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakihusishwa na uzembe uliosababisha kutoroshwa kwa makontena TPA bila ya kulipiwa ushuru.