[video] Rais Magufuli alipozungumza na watu mbalimbali Ikulu, Alhamisi, 18.02.2016


WM Majaliwa akagua bandari ya Tanga na kutaka maelezo Jumamosi, saa sita!

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkuu wa bandari ya Tanga, Henry Arika (kulia kwake ) na Mhandisi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Felix Mahangwa wakati alipotembelea bandari ya Tanga Februari 19, 2016
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo jioni (Ijumaa, Februari 19, 2016) amekagua bandari ya Tanga na kumtaka Mkuu wa Bandari ya Tanga (Port Master), Bw. Henry Arika amletee maelezo juu ya ukiukwaji wa manunuzi ya tishari ifikapo kesho (Jumamosi) saa 6 mchana.

Waziri Mkuu ambaye aliwasili Tanga leo mchana ili kushiriki mazishi ya baba mzazi wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu yaliyofanyika kwenye makaburi ya Mchukuuni, Tanga, aliamua kuzuru bandari hiyo kabla ya kuelekea uwanja wa ndege akiwa njia njiani kurejea Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikataa kuingia ofisini (bandarini) na akataka apelekwe mahali tishari tatu za bandari hiyo zilipo. Katika maswali aliyoulizwa na Waziri Mkuu, Bw. Arika alikiri kuwa matishari hayo hayafanyi kazi kama inavyotakiwa kwa sababu yanasubiri kusukumwa na tugboat (meli ndogo).

"Nataka kesho saa 6 mchana uniletee barua yenye maelezo ni kwa nini mlinunua tishari tatu ndogo badala ya mbiili kubwa wakati mnajua Serikali ilitenga Dola za Marekani milioni 10.113 kwa ajili ya kununua tishari mbili zenye uwezo wa kujiendesha zenyewe (self propelled) "

“Nataka maelezo ni kwa nini mlizinunua tangu mwaka 2011 lakini zimekaa bila kufanya kazi hadi Novemba mwaka jana? Na kwa nini mnaendelea kutumia hela ya Serikali kwa kukodisha tishari kutoka Mombasa badala ya kutengeneza za kwenu au kufundisha vijana wa Kitanzania? Kwani tunao wahitimu wangapi wa fani hii?" alihoji Waziri Mkuu.

"Taarifa nilizonazo ni kwamba moja ya tishari lilidondoka baharini mkaenda kutafuta huko na kulivuta hadi hapa ndiyo maana yameshindwa kufanya kazi inavyotakiwa," aliongeza.

Katika majibu yake, Bw. Arika alisema wao waliagiza tishari hizo kupitia ofisi ya Bandari makao makuu ambayo iko Dar es Salaam. "Pia wakati zinaagizwa sikuwepo hapa Tanga. Nimekuja mwishoni mwa mwaka jana," alisema Mkuu huyo wa Bandari ambaye inaelezwa alitokea Mamlaka ya Bandari Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bibi Mwantumu Mahiza awaite watu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Bandari na Jeshi la Polisi wakae na kutafuta mbinu za kudhibiti njia za panya zinazotumika kupitisha sukari ya magendo.

"Mkuu wa Mkoa simamia hawa watu, msaidiane kudhibiti uingizaji wa sukari kwa njia za panya. Kuna majahazi yanaleta sukari kutoka Brazil. Mheshimiwa Rais amepiga marufuku uingizaji wa sukari kutoka nje ili viwanda vyetu vya ndani viweze kuongeza uzalishaji. Dhibitini bandari zote ndogondogo hadi Pangani," alisema Waziri Mkuu.

Alisema changamoto inayoikabili Serikali ni kwamba hata Shirika la Viwango Tanzania (TBS) au Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) hawawezi kuzikagua sukari hizo na hazijulikani ubora wake licha ya kuwa zinafika kwa walaji.

Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam leo jioni.

Waziri Mkuu, Kssim Majaliwa akiongozwa na Mkuu wa Bandari ya Tanga , Henry Arika (kulia kwake) kukagua bandari hiyo Februari 19, 2016.

Matishari matatu ambayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametaka apewe maelezo kwa maandishi kuwa ni nani aliyeidhinisha mchakato wa manunuzi yake bila kuzingatia viwango na ubora uliokusudiwa na serikali. mheshimiwa Majaliwa alifanya ziara katika bandari ya Tanga Februari 19, 2016.
  • Taarifa kutoka ofisi ya Waziri MkuuTCU yavifutia vibali vyuo 2 vya Mtakatifu Joseph

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefuta kibali kilichoanzisha vyuo vikuu viwili vishiriki vya Mtakatifu Joseph ambavyo ni Chuo Kikuu kishiriki cha Sayansi ya Kilimo na Teknolojia (SJUCAST) na Chuo Kikuu kishiriki cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (SJUIT) vilivyopo Songea.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za Tume hiyo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Prof. Yunus Mgaya amesema kutokana na mapungufu yaliyobainishwa na Tume ambayo ni matatizo ya ubora wa elimu na ukiukwaji wa Sheria za uendeshaji wa Chuo Kikuu kama ulivyobainishwa na Sheria ya Vyuo Vikuu hii imepelekea Tume kuchukua hatua ya kufuta usajili wa vyuo hivyo.

“ kutokana na yaliyobainishwa hapo awali tunapenda kutaarifu umma kwamba ,Tume imejiridhisha kuwa hivi vyuo vikuu vishiriki viwili havitoi elimu ya Chuo kikuu ya viwango stahiki na ukizingatia wanafunzi katika Vyuo hivi ndio waathirika wakubwa wa matatizo yaliyopo”Alisema Prof Mgaya.

“Napenda kufafanua kwamba Vyuo vikuu vishiriki tuliyovifutia usajili ni tawi la Songea na Vyuo vingine vishiriki vya Mtakatifu Joseph vilivyopo Dar es Salaam na Arusha vitaendelea kufanya kazi kama kawaida”Alisema Prof Mgaya.

Prof Yunus Mgaya amesema wanafunzi wote wanaosoma katika vyuo vishiriki vilivyofutwa usajili wanaarifiwa kuwa watahamishiwa kwenye vyuo vikuu vingine vinavyofundisha programu za masomo zinazofanana na masomo wanayosoma hivi sasa chini ya utaratibu uliopangwa.

Amevitaja vyuo ambavyo watapelekwa wanafunzi walipo katika vyuo vishiriki vilivyofutwa usajili kuwa ni Chuo Kikuu cha kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge(MWECAU) na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha(RUCU).

Amesisitiza kuwa orodha ya majina ya wanafunzi na vyuo watavyohamishiwa yatawekwa kwenye tovuti ya Tume hivi karibuni na wale wote wanaonufaika na Mikopo toka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, mikopo yao itahamishiwa katika vyuo watakavyokuwa wamehamishiwa.

Vyuo vikuu vyote chini vinakumbushwa kufata Sheria na kuzingatia utoaji wa elimu inayokidhi viwango vya ubora vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, hivyo Tume haitasita kuchukua hatua stahiki kwa chuo kikuu chochote kitakachobainika kutoa elimu isiyokidhi viwango vya ubora kwa kisingizio cha aina yoyote.
  • Taarifa ya Nyakongo Manyama - MAELEZO.

Ushauri wa Dk Ndugulile (Mb) wa mbinu za kutatua msongamano Muhimbili hospitali

Kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka iliyoanzisha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imeainisha moja ya majukumu ya taasisi hii ni kuwa hospitali ya rufaa ya Taifa.

Taasisi hii ina uwezo wa kulaza wagonjwa 1500 (bed capacity). Takwimu zilizopo kwenye tovuti ya taasisi hii zinaonyesha kuwa hospitali hii inapokea wagonjwa wa nje (outpatients) wapatao 1000-2000 kwa siku na wanalaza wagonjwa 1000-1200 (inpatients) kwa wiki.

Kwa muda mrefu tumeshuhudia hospitali hii kuzidiwa na wagonjwa. Wagonjwa wengi wakiwa ni wagonjwa ambayo wangeweza kutibiwa kwenye hospitali za pembezoni. Hali ambayo imesababisha msongamano na baadhi ya wagonjwa kulala chini.

Kumekuwa na kauli kuwa msongamano wa Muhimbili unatokana na huduma za afya zinazotolewa kuwa nzuri. Hoja hii sio sahihi sana. Tatizo la msongamano katika hospitali ya Muhimbili ni la kimfumo. Pamoja na juhudi za Mhe. Rais la kutaka kuondokana na wagonjwa kulazwa chini, bado ongezeko la vitanda halitaondoa matatizo ya msingi. Vitanda vitajaa na bado mahitaji ya vitanda vya ziada yataendelea kuwepo.

Matatizo ya kimfumo ya msongamano ni yapi?
  1. Mfumo wa rufaa in dhaifu. Hospitali ya Muhimbili ilipaswa kupokea wagonjwa ambao wameonwa kwenye hospitali za pembezoni na ambao wanahitaji vipimo au matibabu mahsusi ambayo hayapatikani kwenye hospitali hizo. Kinyume chake, wagonjwa wenye magonjwa ya kawaida ambayo yangeweza kutibiwa pembezoni na kina mama wenye ujauzito usio na matatizo ndio waliojaa Muhimbili. “Chujio” la kuwachuja wagonjwa halipo. Kwa mfano, kuna vituo vya Afya vya Mnazi Mmoja, Ilala na Round Table, Mbagala ambazo zina huduma za msingi za uzazi lakini havitumiki kikamilifu badala wagonjwa wake kupelekwa Muhimbili. 

  2. Hospitali na vituo vya Afya vya pembezoni kutokuwa na vifaa and wataalamu wa kutosha-Huduma za Amana, Mwananyamala, Temeke, Rangi Tatu na Vijibweni zilipaswa kuwa vyumba vya upasuaji, vyumba vya kuzalia, vifaa na wataalamu kutosha. Hakuna sababu za msingi kwanini mwanamama atoke PembaMnazi, Kivule, Mabwepande au Chamazi akajifungulie Muhimbili. Hata pale ambapo vifaa vipo na madaktari wapo mzigo husukumiwa Muhimbili. Tujiulize not operesheni ngapi za uzazi (Caesarean section) zinazofanyika kwenye hospitali hizi za pembezoni ukilinganisha na Muhimbili? 

  3. Kutokuwepo na mfumo mzuri wa mawasiliano na uratibu kati ya TAMISEMI na Wizara ya Afya. Hospitali ya Muhimbili na za rufaa ziko chini ya Wizara wakati zahanati, vituo vya afya, hospitali za Wilaya na Mkoa ziko chini ya TAMISEMI. Kila Wizara inafanya mambo yake bila kuwa na mawasiliano na uratibu wa pamoja. Tatizo la msongamano linasababishwa na Tamisemi kutowajibika kikamilifu. Idara ya Afya ndani ya TAMISEMI bado ni ndogo sana kuweza kuratibu huduma za afya. Kuna mjadala ndani ya Wizara ya Afya wa kutaka kurudisha hospitali za mikoa Serikali. Kwangu, hili sio suluhisho. Tutibu mfumo na sio kutengeneza mfumo mbadala. 
Nini kifanyike?
  1. Mfumo wa rufaa upitiwe upya na kuimarishwa. Kuwe na vigezo vya kumpatia rufaa mgonjwa kwenda Muhimbili. 

  2. Hospitali za pembezoni zijengewe uwezo na kupatiwa Vifaa na wataalamu ili waweze kushughulikia wagonjwa na upasuaji usio na “complications”. Jiji la Dar Es Salaam linakuwa kwa kasi sana, Wizara ya Afya na TAMISEMI zianishe maeneo ya kimkakati ya kujenga vituo vya Afya na hospitali. Kwa mfano, Katika Wilaya ya Kinondoni katika njia ya kuelekea Bagamoyo, zaidi ya hospitali binafsi zaa Rabinisia, Massana na hospitali ya Jeshi Lugalo hakuna kituo kikubwa au hospitali ya umma. Tuangalie huduma za Afya kimkakati. 

  3. Mfumo wa mawasiliano na uratibu wa huduma za Afya uboreshwe na kusimamia vizuri. 
Hitimisho

Bila ya kuliangalia tatizo la msongamano kimfumo tutamaliza ofisi zote za umma na bado wagonjwa wataendelea kulala chini. Tuelekeze juhudi zetu katika kurekebisha mfumo na tatizo la msongamano litapungua.

----
Imenukuliwa kutoka kwenye blogu ya Dk Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni

Waziri Nnauye atengua uteuzi wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametengua uteuzi wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Henry Lihaya baada ya kushindwa kutekeleza wajibu wake.

Nnauye alitengua uteuzi huo katika ziara yake aliyoifanya leo mapema katika ofisi za BMT kuona miundo mbinu ya ofisi hizo na kujua changamoto walizonazo.

“Baraza likirekebishwa vyama vya michezo navyo vitakuwa mguu sawa na kuleta chachu na maendeleo katika michezo,”alisema.

Aliongeza kwa kusema kuwa, miaka saba ambayo Lihaya amekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza imetosha kwani hakuna mabadiliko yoyote aliyoyafanya katika sekta ya michezo tangu alipoteuliwa mwaka 2009.

Kutokana na utenguzi huo Nape amemtaka Mwenyekiti wa BMT Dionis Malinzi kupendekeza jina la Katibu Mtendaji mpya wa BMT ambaye anampendekeza kwa mujibu wa sheria ya BMT kifungu cha 5(1) baada ya kupata idhini ya waziri mwenye dhamana.

Vilevile, amemtaka mwenyekiti kuteua Katibu Mtendaji ambaye atakuwa ni mchapa kazi na mwenye mipango ambayo itaibadilisha BMT na kuleta chachu katika michezo nchini.

Aidha Nnauye amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara ya habari, utamaduni sanaa na michezo kumpangia Lihaya kazi nyingine wizarani.

---------- MWISHO ---------

Baraza la Michezo Tanzania (BMT) limemteua Bwana Said Kiganja kuwa Katibu Mtendaji mpya wa Baraza hilo kuanzia leo, ili kujanza nafasi ya aliyekuwa Katibu Mtendaji Baraza hilo ambaye uteuzi wake umetenguliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Nape Nnauye na kumrudisha Wizarani ili aweze kupangiwa majukumu mengine.
Uteuzi huo ni kwa mujibu wa Sheria iliyoundwa na BMT kifungu namba 5(1) ambacho kinampa mamlaka Mwenyekiti wa BMT kuteua Katibu Mtendaji baada ya kupata idhini ya Waziri mwenye dhamana.

Kabla ya uteuzi huo Bwana Kiganja alikuwa ni Afisa Michezo Mkuu katika ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuanzia mwaka 2015 mpaka uteuzi wake ulipo fanyika. Pia bwana Kiganja aliwahi kufanya kazi kama Afisa Mwandamizi Michezo wa Baraza la Michezo Tanzania na Afisa Michezo Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Bwana Kiganja ana shahada ya kwanza ya elimu upande wa masuala ya michezo na utamaduni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Imetolewa na Mwenyekiti wa BMT
Deonis Mallinzi
19/02/2016