Yaliyojiri magazetini leo, Jumatano 24.02.3016


Hali ilivyo katika baadhi ya mitaa ya Dar baada ya usafi wa Desemba 9


Taarifa ya habari ChannelTEN, Februari 23, 2016Polisi Dar yakusanya bilioni 1/= Januari - Februari kwa makosa ya barabarani

ESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetoa taarifa kuwa litaendelea kupambana na uhalifu wa kutumia silaha, kudhibiti dawa za kulevya na kuwatoza faini madereva wanaoendesha kwa uzembe, anaandika Faki Sosi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Simon Siro, Kamishna wa Polisi Kanda Maalimu ya Dar es Salaam, amesema kuwa Jeshi hilo limekamata silaha mbili ikiwemo SMG iliyokatwa mtutu yenye namba 56-1 2803795 ikiwa na risasi 24 na Bastola moja.

Amesema kuwa silaha hizo zimekamatwa baada ya majambazi wawili kukamatwa katika tukio la kupora shilingi 12 Milioni kwa David Isack (32) eneo la uwanja wa ndege.

Isack alikuwa akihamisha fedha hizo kutoka benki ya NMB kuzipeleka Benki ya DTB akiwa njiani majamabazi hayo yakiwa na pikipiki mbili aina ya boxer MC.729, ATZ na MC 557 AZK yalimzingira na kumpora fedha hizo.

Aidha Siro amewaambia waandishi kuwa polisi wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wa ujambazi wanne eneo la Buguruni kwa Mnyamani wanaodaiwa kuwa wamekuwa wakijihusisha na shughuli za ujambazi kwa kutumia silaha ,

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mohamed Hassan (21), Hamiss Ally (20), Adam Salum (23) na Bakari Hamis (19).

Kwa wakati mwengine jeshi la polisi limekamata Gongo lita 160, Bangi kete 250 puli 110 pamoja na watuhumiwa 130

Kwa upande wa makosa ya usalama barabarani Sirro amesema kikosi hicho kimekusanya takribani bilioni moja, baada ya kukamata magari 32528, pikpiki 4046, daladala 23264 na magari mengine ni 9,264 kutokana na makosa ya barabarani kuanzia Januari Mosi hadi Februari 22 mwaka huu.
  • via MwanaHALISI Online

Jengo la posta Dodoma lateketea kwa moto; Vifurushi vya watu ndiyo basi tena


JENGO Posta lililopo katika eneo la sabasaba katika Manispaa ya Dodoma limeteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa, anaandika Dany Tibason, Dodoma.

Akizungumzia kutekeleza kwa jengo hilo Meneja wa Posta Mkoa wa Dodoma, Magreth Mlyomi amesema mpaka sasa kuna hasara kubwa kutokana na kutekeleza jengo hilo sambamba na vifaa vyote vya ofisi.

Mlyomi amesema licha ya kuwa hakuna mfanyakazi hata mmoja aliyepoteza maisha katika jengo hilo lakini mpaka sasa kuna vitendea kazi vingi vya ofisi pamoja na mizigo ya wateja.

“Kuna mizigo mingi pamoja na vifaa vya kazi vyote vimeteketezwa na moto na kwa taarifa nilizopata kulikuwa na mizigo ya watu, niliambiwa kuwa moto umeanza majira ya saa nne asubuhi na inaonesha kuwa chanzo cha moto ni umeme,” ameeleza Meneja.

Akizungumzia kuhusu masuala ya miundombinu ya maeneo husika amesema ni mibovu na kutokana na changamoto hiyo suala hilo lipo katika mamlaka husika ya manispaa.

Kwa upande wake katibu wa wafanyabiashara katika soko la Sabasaba katika Manispaa ya Dodoma, Gergod Lugusi amesema majira ya saa nne asubuhi kulitokea moto mkali ambao uliunguza jengo hilo.

Amesema chanzo cha moto huo inasemakana kuwa ni tatizo la umeme na uongozi ulilazimika kutoa taarifa katika kikosi cha zima moto na bila kuchelewa walifika kwa wakati.

Hata hivyo amesema licha ya kufika kwa wakati katika tukio bado kikosi hicho kilikutana na kikwazo kwa kutokana na miundombinu kuwa mibovu na migumu kupitika.

NECTA yaagiza kusitisha kugawa vyeti kwa wahitimu wa Kidato cha Sita 2015

Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), limeagiza kusitishwa kwa ugawaji wa vyeti vya kidato cha sita kwa wanafunzi waliohitimu mwaka 2015, huku vile vilivyokwisha gawanywa kwa watahiniwa hao vikitakiwa kurejeshwa kwenye chombo hicho.

Hali hiyo imeibua utata mkubwa, huku baadhi ya wadau wakiwamo maofisa elimu, wakihisi hatua hiyo ya Necta huenda inalenga kuvibadili vyeti hivyo kutoka kwenye mfumo wa wastani wa alama (GPA), kwenda kwenye ule wa jumla (division).

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk, Charles Msonde, alipoulizwa na Nipashe jana alikanusha vikali madai hayo, akisema vyeti hivyo havitabadilishwa kutoka kwenye mfumo wake bali vimesitishwa kugawanywa ili baraza lijiridhishe na baadhi ya vitu.

MAOFISA ELIMU, WAKUU WA SHULE

Ofisa Elimu Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda, alipoulizwa na Nipashe jana kama amepokea agizo hilo, alithibitisha kuwa shule zote za mkoa huo zenye kidato cha tano na sita zimepewa taarifa ya kutakiwa kurudisha vyeti hivyo Necta. 

Alisema sababu ya kuvirudisha vyeti hivyo anadhani ni kufanya mabadiliko kutoka GPA na kurudi kwenye divisheni.

Ofisa Elimu Mkoa wa Arusha, Nestory Mloka, alisema amepata barua ya maelekezo hayo kutoka Necta ikimuelekeza kuwataka maofisa elimu wilaya wawasiliane na wakuu wa shule za kidato cha tano na sita wasigawe vyeti vya wanafunzi waliohitimu mwaka 2015.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Matthew iliyoko Kongowe, Mkuranga mkoani Pwani, Abraham Shafuri, naye alikiri kuwapo kwa agizo la Necta la kusimamisha utoaji wa vyeti hivyo kwa wahusika.

Alisema aliambiwa na maofisa wa Necta kuwa vyeti hivyo vinatakiwa kurejeshwa kwenye baraza hilo na kwamba sababu zilizotolewa ni kuwa kuna marekebisho kidogo yanabapaswa kufanyika.

“Nilichoambiwa ni kwamba shule karibu zote za Dar es Salaam zimesharejesha vyeti hivyo na kwamba kwa sisi wa mkoa wa Pwani, maofisa hao watapita kuvichukua lakini hatujui ni lini watakuja,” alisema Shafuri.

Katika Manispaa ya Moshi, mmoja wa wakuu wa shule za sekondari ambaye hakutaka kutajwa jina lake, aliithibitishia Nipashe kwamba wameagizwa na serikali kuvirejesha vyeti hivyo, ikielezwa kwamba vinahitaji kufanyiwa maboresho.

"Ni kweli tumeagizwa hilo na kesho (leo) asubuhi naletewa barua, kwa hiyo nafikiri nitakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia baada ya kuiona rasmi," alisema mkuu huyo wa shule.

Mmiliki mmoja wa shule ya sekondari na chuo cha ualimu binafsi, ambaye aliomba hifadhi ya jina lake, alisema ni kweli wamepata taarifa ya kutotoa vyeti hivyo na kama wamevitoa kuhakikisha vinarejeshwa.
Hata hivyo, alisema kwa taarifa alizosikia ambazo si rasmi ni kwamba vinatakiwa kubadilishwa kutoka GPA na kuwa kwenye mfumo wa Divisheni.

"Lakini serikali inatakiwa kujua kwamba ikifanya hivyo, hilo ni kosa la jinai, kwani hata walivyofanya kwa matokeo ya kidato cha nne kutoka kwa mfumo wa divisheni badala ya GPA, ni kosa la jinai pia kwa kuwa wanafunzi hawakujiandaa kwa mfumo huo," alisema huku akiomba hifadhi ya jina lake na kuongeza:

"Unajua huu ni usumbufu mkubwa, kwani kuna wanafunzi wengine wapo Urusi na kwingineko nje ya nchi wanasoma na huko waliomba kozi zao kwa kutumia 'transcript' ambazo zinaonyesha mfumo wa GPA, sasa baadaye wakipeleka vya Divisheni si wataonekana wanadanganya. Huu ni usumbufu mkubwa hauna maana kwa sasa, ni bora kuacha mfumo uliopita ubaki kama ulivyo."

Mkuu wa Shule ya Sekondari Aruisha, Christopher Malamsha, alithibitisha kupokea maagizo ya ofisa elimu wilaya ya Arusha kumweleza wazuie vyeti kidato cha sita lakini sababu hawajaambiwa.

MZAZI

Kwa upande wake, Audax Rusenene, ambaye ni mzazi wa mwanafunzi aliyehitimu kidato cha sita mwaka jana kwenye Shule ya Wasichana ya Feza, alisema uongozi wa shule hiyo umemtaka mwanaye anayesoma Chuo Kikuu cha Stelenbosch kilicho Afrika Kusini, arejeshi cheti chake.

“Mtoto wangu alienda chuo Januari 17, mwaka huu, lakini nashangaa hivi karibuni kupigiwa simu na msaidizi wa mkuu wa shule aliposoma mwanangu na kutaka arudishe cheti,” alisema na kuongeza:

“Nilipomwambia kwamba mtoto yupo chuo Afrika Kusini, akaniambiwa niwasiliane naye akirudishe kwa sababu hilo ni agizo la serikali.”

“Hiki kitu kinasikitisha kwa sababu kama kuna mabadiliko yatafanywa kwenye cheti wakati alama alizopata ndizo zilizofanya akapata chuo unadhani itakuwaje?.”

Alisema mtoto wake huyo alihitimu kidato cha nne mwaka 2012 kwenye Shule ya St. Francis na kukumbwa na kufutwa kwa matokeo yake na sasa anatakiwa tena arudishe cheti chake cha kidato cha sita.

NECTA YANENA

Akifafanua jambo hilo, Dk. Msonde alisema: “Baraza halijaagiza vyeti virudishwe ili vibadilishwe mfumo (GPA), baraza lilichokielekeza ni utaratibu wa kawaida wa baraza la mitihani kuangalia uhalali wa vyeti vyake, serial namba ya vyeti vyake na kujiridhisha kama vyeti hivyo vimetawanyika sawasawa.

“Vyeti hivi baraza limevigawa hivi karibuni na lilichofanya sasa limezuia kwanza shule zisigawe mpaka litakapotoa maelekezo mengine, msingi huo wa kuzuia uko kwenye hoja ya kuhakikisha tu kwamba linajiridhisha kwenye takwimu zake kama zimekaa sawasawa katika vyeti vilivyokwenda kila shule.”

“Baadhi ya vyeti kwenye mkoa wa Dar es Salaam vipo Necta, lakini kwenye mikoa mingine yote viko shuleni,” alisema Dk Msonde.
Aliongeza kuwa, “Kama mkuu wa shule alikuwa amegawa vyeti viwili, vitatu kabla havijarejeshwa baraza ni suala jingine, lakini kiujumla kinachofanywa na baraza hapa ni kuhakiki cheti hiki, kama vimekaa kama utaratibu wetu ulivyo.”

Alisema suala la kubadilisha kutoka kwenye GPA kwenda kwenye divisheni halipo na kwamba matokeo yaliyotangazwa kwa utaratibu wa GPA vyeti vyake vitaendelea kuwa katika mfumo wa GPA na matokeo yaliyotangazwa kwenye utaratibu wa divisheni vyeti vyake vitabaki kuwa kwenye divisheni.

Alisema kwa wale ambao tayari wako nje ya nchi, hakuna atakayeathirika na kama baraza likihitaji cheti chake litafanya utaratibu wa kukipata.

Habari hii imeandaliwa na Fredy Azzah, Dar, Agusta Njoji, Dodoma, Godfrey Mushi, Moshi, John Ngunge, Arusha.

CHANZO: NIPASHE

Kauli na wito wa CUF kuhusu Eddy Riyami

Mohamed Ahmed Sultan Al-Mugheiry (Eddy Riyami)
Mohamed Ahmed Sultan Al-Mugheiry (Eddy Riyami)

Wiki iliopita, mnamo tarehe 16 Februari, 2016, aliyekuwa mjumbe wa Timu ya Kampeni ya Chama Cha Wananchi (CUF), Ndugu Mohamed Ahmed Sultan Al-Mugheiry (maarufu kwa jina la Eddy Riyami), alipokea barua ya wito kutoka kwa Jeshi la Polisi Zanzibar ikimtaka kufika Makao Makuu ya Polisi, Ziwani, Zanzibar siku inayofuata, yaani tarehe 17 Februari, 2016, saa 2 asubuhi kwa kile kilichoelezwa kwamba “kuna mambo muhimu yanayomhusu” ambayo walitaka kuzungumza naye.

Bila ya kukosa, Eddy Riyami aliitikia wito huo na kufika Makao Makuu ya Polisi, Zanzibar na kuonana na SSP Simon S. Pasua wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID). Hata hivyo, hakuhojiwa na badala yake alipewa simu na kutakiwa azungumze na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Bw. Salum Msangi ambaye alimwambia arudi tena Jumatatu, tarehe 22 Februari, 2016.

Eddy Riyami, akiwa raia mwema, alirudi tena jana kama alivyoagizwa. Alipofika hapo alihojiwa na Polisi na baadaye mwanasheria aliyefuatana naye akatakiwa kutafuta wadhamini wawili watakaomdhamini hadi atakapoitwa tena. Wakati mwanasheria wake aliporudi na wadhamini, akaelezwa kwamba Polisi imebadili uamuzi wake na imeamua kumuweka ndani hadi leo, tarehe 23 Februari, 2016. Mwanasheria na familia yake wakatakiwa kwenda tena Makao Makuu ya Polisi hiyo leo, saa 3 asubuhi. Walipofika leo asubuhi, wakaambiwa kwamba DCI kaacha maagizo kuwa suala la Eddy Riyami liachwe kwanza na wao warudi tena saa 6 mchana.

Hadi tunapotoa taarifa hii, hakujapatikana maelezo yoyote ya msingi juu ya kinachoendelea na wala Eddy Riyami hajafikishwa Mahkamani kusomewa mashtaka yoyote.

La ajabu zaidi, ni kwamba hata mke wake alipofika kituo cha polisi cha Madema anakoshikiliwa kwa ajili ya kwenda kumuona, hakuruhusiwa kumuona.

Kutokana na mwenendo huu, Chama Cha Wananchi (CUF) kinalichukulia suala hili kwamba ni mwendelezo wa vitendo vya unyanyasaji wa kisiasa dhidi ya wapinzani wa CCM, vitendo ambavyo tunaamini vinafanywa kwa shinikizo la wanasiasa.

Itakumbukwa kwamba kwa muda mrefu tokea wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 tumekuwa tukitoa tahadhari za kuwepo mipango ya kuwakamata viongozi wa CUF na wanaharakati wengine ili kufanikisha malengo ya kisiasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tuna kila sababu ya kuamini kwamba hatua ya kumkamata Eddy Riyami na kumuweka ndani bila ya kumfikisha Mahkamani ni utekelezaji wa mipango hiyo. La si hivyo, ikiwa Eddy Riyami ametenda kosa basi angelishafikishwa Mahkamani ndani ya muda wa saa 24 tokea kukamatwa kama sheria inavyotaka.

Chama Cha Wananchi (CUF) kinalitaka Jeshi la Polisi kuacha kutumiwa na kutumika kisiasa kufanikisha malengo ya kisiasa ya CCM. Tunashangazwa kwamba siku zote wanaoitwa kuhojiwa, kukamatwa na kuwekwa ndani ni wanasiasa wa vyama vya upinzani na wanaharakati wengine lakini hatujawahi kushuhudia viongozi wa CCM kuitwa kuhojiwa, kukamatwa na kuwekwa ndani. CUF imetoa taarifa kadhaa kwa Jeshi la Polisi zinazohusu matamshi na vitendo vya viongozi wa CCM vyenye mwelekeo wa uhalifu lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa. Hizo ni dalili za waziwazi za Polisi kutumiwa na kukubali kutumika kisiasa.

Tunalitaka Jeshi la Polisi iwapo kweli lina kesi dhidi ya Eddy Riyami basi limfikishe Mahkamani haraka ili hatua za kisheria zifuate mkondo wake. Na iwapo hawana kesi, basi wamwachie huru mara moja.

Umefika wakati wa Jeshi la Polisi kufanya kazi zake kitaalamu kama sheria na kanuni zao zinavyoagiza badala ya kuwatumikia wanasiasa wa CCM.

HAKI SAWA KWA WOTE
HAMAD MASOUD HAMAD
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI NA MAWASILIANO NA UMMA - CUF

TRA yakamata vifaa vya kiwanda cha Wachina cha namba bandia za magari


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya msako wa kushtukiza katika kampuni ya Tanzania China Trade and Tourism Development Ltd iliyoko Barabara ya Nyerere Dar es salaam baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema na kukamata vifaa pamoja na malighafi za kutengeneza na kutoa vibao vya namba za pikipiki kinyume na sheria.

Katika msako huo uliofanyika tarehe 19 Februari 2016 katika kampuni hiyo, Maofisa wa TRA waliweza kukamata na kutaifisha vibao vyenye namba za pikipiki 2,500 na vibao 5,600 ambavyo havikuwa na namba. Pia maofisa wa TRA walikamata malighafi za rangi ya vibao katoni tatu, pamoja na mashine ya kupaka vibao rangi yenye uzito wa kilo 155.

Mashine nyingine iliyokamatwa katika msako huo ni ya kutengeneza namba za magari yenye uzito wa kilo 902 ambayo imezuiwa isihamishwe kutoka katika kampuni hiyo pamoja na kompyuta mpakato ambayo imepelekwa katika maabara ya uchunguzi TRA kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Taarifa za kuwepo kwa utengenezaji wa vibao vya magari kinyume na taratibu na sheria zilitolewa na msamaria mwema ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni husika Donglinh Guo, Meneja wa Kiwanda Yong Qing Cheng na Meneja wa ghala Peng Zhan walikamatwa baada ya kutokea fujo wakati wa msako na kufikishwa katika kituo cha Polisi Changombe.

Kampuni ya Tanzania China Trade and Tourism Development LTd ndio waingizaji pekee wa pikipiki za Falcon tangu mwaka 2008 ambapo inatuhumiwa kutoa vibao vya namba za pikipiki kwa wateja wake kwa shilingi 5,000 kinyume na sheria.

Uchunguzi wa thamani ya kodi iliyopotea bado unaendelea.

Vibao vya magari na pikipiki hutolewa na kampuni ambazo zinatambuliwa na TRA baada ya kupewa idhini. Kampuni hizo ni Masasi Sign, Auto Zone, Sign Industry, Kiboko, Budda Auto works, Parkinson Ltd na Next Telecom.

Ili kujiridhisha kuwa kadi za pikipiki zinazotolewa kwa wateja wa kampuni hiyo ni halali, TRA ilifanya uchunguzi na kugundua kuwa kadi hizo zinatolewa kihalali.

TRA inawatahadharisha wananchi kufuata taratibu na sheria ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea endapo watagundulika kujihusisha na vitendo ambavyo ni kinyume na sheria.

Taarifa ya kukutana kwa WM Majaliwa na mabalozi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Mhe. Alvaro Rodriguez kabla ya mazungumzo yao Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Februari 23, 2016

WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu kutoka nchi za Uturuki, Ireland na Uswisi pamoja na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na mabalozi hao leo (Jumanne, Februari 23, 2016), ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amewashukuru mabalozi hao kwa kuja kujitambulisha rasmi na kwa pongezi walizokuja kumpatia na kuahidi ushirikiano zaidi pamoja na nchi hizo.

Mapema leo, Waziri Mkuu amekutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez ambaye amemweleza jinsi UNDP imekuwa ikisaidia programu za kukabiliana na maafa (resilience), ukuaji wa uchumi, utawala bora na masuala ya jinsia.

Amesisitiza haja ya Tanzania kuendeleza kampeni ya kupambana na ujangili na kusisitiza kuwa Umoja huo una nia ya kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Naye Balozi wa Uturuki, Bibi Yesemin Eralp alimweleza Waziri Mku nia ya nchi kuleta wawekezaji katika nyanja za kilimo, nishati, afya na ujenzi na kusisitiza kuwa kuna haja ya kufungua ubalozi wa Tanzania nchini kwao ili kuimarisha uhusiano uliopo.

“Tunao uwezo wa kifedha na tunao uwezo wa kitaalamu na kiteknolojia. Tukifungua viwanda hapa nchini, tunaweza kuongeza ajira kwa Watanzania,” alisema.

Naye Balozi wa Ireland nchini, Bibi Fionnuala Gilsenan alimweleza Waziri Mkuu jinsi ambavyo nchi yake imekuwa ikisaidia sekta za kilimo kupitia mpango wa ASDP, bajeti ya Serikali na suala la lishe na urutubishaji wa vyakula (food nutrition and fortification).

“Tulianza na suala la kilimo na bajeti ya Serikali. Hivi sasa tunataka kusaidia kwenye uelimishaji juu ya haki za wanawake, masuala ya uzazi wa mpango, pamoja na kupambana na ndoa za utotoni,” alisema.

“Tumeamua kupigia kelele suala la lishe na urutubishaji wa vyakula kwa sababu lishe duni imechangia kwa kiasi kikubwa udumavu wa watoto wengi. Tulipoanza tatizo hili lilikuwa limeenea kwa asilimia 46 kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano lakini sasa limepungua na kufikia asilimia 36 hadi 38,” aliongeza.

Amemuomba Waziri Mkuu Majaliwa alishikie bango suala hilo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kote nchini kwani mtoto akishadumaa kimakuzi hata akili yake pia inadumaa na tatizo lake haliwezi kurekebishwa kwa tiba yoyote ile.

Naye Balozi wa Uswisi nchini, Bibi Florence Mattli alimweleza Waziri Mkuu nia ya nchi yake kudumisha ushirikiano na Tanzania ambao umedumu kwa miaka 50 ili kukuza viwango vya uchumi na kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Alimweleza Waziri Mkuu jinsi nchi yake imekuwa ikisaidia kundeleza nyanja za kupambana na rushwa kupitia TAKUKURU na kampeni ya kusaidia kujenga uelewa wa wananchi kupitia vyombo vya habari nchini.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez Ofisini kwake jijini Dar es salaam Februari 23, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Uturuki nchini, Mhe. Yosemin Eralp kabla ya mazungumzo yao ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Februari 23, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Ireland nchini, Mhe. Fionnuala Gilsenan, Ofisini kwake jijini Dar es salaam Februari 23, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Switzerland nchini, Mhe. Florence Tinguely Mattli, Ofisini kwake Mkuu jijini Dar es salaam Februari 23, 2016.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri afanya mabadiliko kwenye vitengo vya Idara ya Uhamiaji

Waziri Charles Kitwanga (kushoto meza kuu), Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni (kulia meza kuu) na Watendaji Wakuu wa Idara ya Uhamiaji (kushoto) na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (kulia), wakati wa kikao katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Wa kwanza upande wa kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya, na wa kwanza upande wa kushoto ni Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Victoria Lembeli. 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga ameagiza yafanywe mabadiliko makubwa katika Vitengo mbalimbali vya Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma na kuimarisha uadilifu katika Vitengo hivyo.

Mheshimiwa Kitwanga ametoa maagizo hayo leo wakati alipofanya kikao na Viongozi wa Idara ya Uhamiaji ambapo pia kilihudhuriwa na Viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo vya Wizara. Kikao hicho kilifanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Katika kikao hicho, Mheshimiwa Kitwanga ameagiza watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji walioko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, wahamishwe na kupelekwa maeneo mengine nchini, wakiwemo wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Wengine watakaohamishwa ni kutoka Kitengo cha Pasipoti, Uhasibu, Hati za Ukaazi na Kitengo cha Upelelezi, vyote vya Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.

Aidha ameagiza pia kuwa Wakuu wote wa Vitengo vya Upelelezi vya wilaya zilizopo jijini Dar es Salaam, na pia wale wa Vituo vya Tunduma, Mtukula, Holili na Kasumulo, wahamishiwe maeneo mengine, na pia watumishi wote waliokaa kwa zaidi ya miaka mitatu katika Vituo hivyo.

Amesema hatua hii inayochukuliwa sasa ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa yatakayofanywa katika Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma zinazotolewa na Idara hii ambayo ni moja ya Idara muhimu za Serikali.

Amesema katika kuisafisha Idara hii, uangalifu mkubwa utachukuliwa ili kuhakikisha kuwa hakuna mtumishi anayeonewa wala kupendelewa, lakini lengo kubwa ni kuvunja mtandao wa wapokea rushwa na wale wasiowajibika.

Amesema kufuatana na utafiti uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa matatizo ya rushwa katika Idara ya Uhamiaji yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30, asilimia 20 ni uongozi mbovu na asilimia 20 ni matumizi mabaya ya madaraka. Asilimia 15 inahusisha vitendea kazi wa mifumo hafifu ya kufanya kazi, asilimia 10 huduma mbovu na asilimia 5 ukabila na upendeleo.

Amewataka Viongozi na watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi na waepuke vitendo vya kupokea rushwa na kusaidia wahamiaji haramu na wauza madawa ya kulevya.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
23 Februari, 2016


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto meza kuu) akizungumza na Watendaji Wakuu wa Idara ya Uhamiaji nchini (kushoto) pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (kulia), kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji wa kazi ndani ya Idara hiyo na Wizara kiujumla. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Kulia meza kuu ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni. Wakwanza upande wa kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya, na wakwanza upande wa kushoto ni Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Victoria Lembeli.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Simba Yahya akizungumza jambo katika kikao kazi alichokiitisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto meza kuu) kuzungumza na Watendaji Wakuu wa Idara ya Uhamiaji nchini pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara yake, kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji kazi ndani ya Idara hiyo na Wizara kiujumla. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Kulia meza kuu ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni. Wakwanza upande wa kushoto ni Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Victoria Lembeli.

Kaimu Kamishna wa Idara ya Uhamiaji, Victoria Lembeli (wapili upande wa kushoto) akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto meza kuu) kuhusu masuala mbalimbali ya kikazi ndani ya Idara yake katika Kikao kazi cha Watendaji Wakuu wa Idara ya Uhamiaji pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kilichoitishwa na Waziri Kitwanga na kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Wakwanza upande wa kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, balozi Simba Yahya.

Baada ya marekebisho, kesi ya msingi dhidi ya ubunge wa Msigwa ipo pale pale


CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema kesi ya kupinga matokeo iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wake ubunge jimbo la Iringa Mjini, Frederick Mwakalebela iko pale pale, kikipinga taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii jana na kuchapwa katika baadhi ya magazeti leo kwamba kesi hiyo imefutwa.

Akizungumza na wanahabari hii leo, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisema; “kwa mambo yanayohusu sheria ni kawaida sana hata kwa wanasheria wenyewe kufanya makosa ya kiufundi.”

Mtenga alisema katika shauri lao la awali ambalo wanalifanyia marekebisho hawakumuingiza mwanasheria mkuu wa serikali katika orodha ya wanaoshitakiwa.

“Tumewaiteni wanahabari tuwaambieni kwamba Msigwa hajashinda kesi. Kesi ipo na tungependa wananchi wajue kwamba kesi ya msingi ipo na inaendelea,” alisema.

Alisema; “Msigwa hawezi kushinda kesi kwenye FaceBook, wala kwenye magazeti, kwa mujibu wa sheria atashinda kesi hizo pale tu ambapo mahakama itatimiza wajibu wake kwa kutoa haki.”

Naye Mwakalebela alisema shauri lake la kupinga ushindi wa Mchungaji Msigwa limekuwa likipata mapingamizi mengi.

“Pingamizi lingine ni baada ya mwanasheria wangu kutomuweka mwanasheria mkuu wa serikali na hivyo maahakam kuliondoa ili likarekebishwe,” alisema.

Kuondolewa kwa shauri hilo mahakamani haina maana kwamba limefutwa kama ilivyotasfiriwa na upande wa pilia na ndio maana mahakama hiyo hiyo imewapa fursa ya kulirudisha tena mahakamani.

“Kwa sasa wanasheria wetu wanalifanyia kazi hilo vizuri ili litakaporudi mahakamani kusiwepo na dosari zingine na badala yake lianze kusikilizwa,” alisema.

Alisema kesi hiyo ya kupinga matokeo itamalizwa kwa pande zote kusikilizwa ili haki itendeke na sio kwa maamuzi ya propaganda.

Katika shauri la msingi la kesi hiyo namba 5 ya mwaka 2015 ya kupinga matokeo, Mwakalebela aliwatuhumu Mchungaji Peter Msigwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Iringa Mjini, Ahmed Sawa kwa kukiuka sheria na taratibu za uchaguzi hali iliyopelekea yeye kupata matokeo mabaya yasiyo halali. 

Taarifa ya DAWASCO ya kurejeshwa huduma ya maji ya mtambo wa Ruvu Chini

SHIRIKA LA Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO), imerejesha huduma ya upatikanaji wa Maji katika maeneo yote yanayohudumiwa na mtambo wa Ruvu chini jijini Dar es salaam, pamoja na maeneo ya mji wa Bagamoyo mkoani Pwani kutokana na mtambo huo kuzimwa kwa wastani wa saa 36 kuanzia siku ya Alhamisi 18/02/2016.

Akizungumzia kurejea kwa huduma hiyo, Meneja uhusiano wa DAWASCO, Bi. Everlasting Lyaro, amesema kuwa huduma ya Maji katika jiji la Dar es salaam na miji ya Bagamoyo mkoani Pwani kwa sasa yameanza kwenda kwa wananchi, na maeneo mengi ya jiji ambayo yalikosa huduma ya Maji kutokana na uzimwaji wa mtambo wa Ruvu chini.

“Napenda kuwaambia wateja wetu kuwa huduma ya Maji kwa sasa imerejea kwenye maeneo mengi ya jiji baada ya matengenezo kukamilika na mtambo kuwashwa siku ya Jumapili saa 9:30 alasiri” alisema Bi. Lyaro

Alibainisha kuwa Kuna maeneo mengine yatachelewa kupata Maji kwani mara nyingi kwa kitaalamu huwa mtambo ukizimwa kwa zaidiya saa 24 ndani ya mabomba ya kupitisha Maji hujaa hewa hivyo baadhi ya maeneo kazi ya utoaji hewa kwenye mabomba unaendelea, hivyo tuwahakikishie wananchi kuwa huduma imerejea na wataipata ndani ya muda tuliotarajia.

Awali, mtambo wa Ruvu Chini ulizimwa ili kuwaruhusu wakandarasi kutoka kampuni ya sino Hydro na mafundi kutoka DAWASCO kukarabati bomba la Maji lenye inchi 54 linalosafirisha Maji kutoka Bagamoyo mpaka matenki ya Chuo kikuu cha ardhi, Bomba lililokuwa likivuja maeneo ya Makongo Jeshini, na kusababisha maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam kukosa huduma ya Maji, Mji wa Bagamoyo vijiji vya Zinga, Kerege na Mapinga, Bunju, Boko, Tegeta, Kunduchi, Salasala, Jangwani, Mbezi Beach na Kawe.

Maeneo mengine ni pamoja na Maeneo ya Mlalakuwa, Mwenge, Mikocheni, Msasani, Sinza, Manzese, Mabibo, Kijitonyama, Kinondoni, Oysterbay, Magomeni, Upanga, Kariakoo, City centre, Ilala,, Ubungo Maziwa, Kigogo, Mburahati, Hospitali ya Rufaa Muhimbili, Buguruni, Chang’ombe na Keko.

Taarifa ya TRA: Matumizi ya mashine za EFD katika vituo vyote vya matuta


MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA

TANGAZO KWA UMMA


MATUMIZI YA MASHINE ZA EFD KATIKA VITUO VYOTE VYA MAFUTA NCHINI:


Kufuatia Tangazo kwa Umma lilitolewa kwenye vyombo vya Habari na kuchapishwa kwenye Magazeti, Uongozi wa Chama cha Wamiliki na Waendeshaji wa Vituo vya Mafuta Nchini (TAPSOA) ulikutana na Kaimu Kamishna Mkuu na kufanya majadiliano ya msingi kuhusu matumizi ya EFD na kufunga Mashine za EFD Maalum katika vituo vya mafuta kwa ajili ya kutolea risiti za mauzo. Makubaliano ya pamoja kutokana na majadiliano ni kwamba, agizo la Kaimu Kamishna Mkuu liendelee kutekelezwa katika utaratibu ufuatao;

(a) Wamiliki wote wenye vituo vya mafuta walio katika kundi la Makampuni makubwa wanaoagiza mafuta na kutumia Mawakala kusambaza/kuuza mafuta kwa wateja (CODO) wakamilishe kufunga Mashine za EFD katika vituo vyao vyote Nchini kama ilivyokubalika katika kikao hicho (yaani kufikia tarehe 15 Machi 2016).

(b) Wamiliki wote wenye vituo vya mafuta walio katika kundi la Makampuni wanaoagiza mafuta na kusambaza/ kuuza mafuta kwa wateja wao wenyewe (COCO) walioanza na wanaofunga Mashine za EFD kwenye pampu za vituo vyao waendelee kufanya hivyo wakati Mamlaka ya Mapato kwa kushirikiana na Wasambazaji na Uongozi wa TAPSOA wakiendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazojitokeza za kiufundi na gharama ya Mashine za EFD kwa ajili ya pampu husika.

(c) Wamiliki/Waendeshaji wote wenye vituo vya mafuta walio katika kundi la Makampuni ya watu binafsi wanaonunua mafuta kutoka kwa Makampuni mama na kusambaza/kuuza kwa wateja moja kwa moja (DODO) ambao hawajafunga Mashine za EFD kwenye pampu waendelee kutumia Mashine za EFD za kawaida (ETR) wakati changamoto za kiufundi, mtandao na bei za Mashine za EFD zikishughulikiwa.
Mamlaka ya Mapato kwa kushirikiana na uongozi wa TAPSOA kwa pamoja tutaendelea kuhimiza Matumizi ya Mashine za EFD katika vituo vya mafuta vyote Nchini.
Ni vyema kila Mfanyabiashara akatambua wajibu wake na kujenga utamaduni wa kutekeleza matakwa ya sheria kwa hiari bila kushurutishwa.

Pamoja Tunajenga Taifa Letu

KAIMU KAMISHNA MKUU

Waziri Mbarawa awapa makandarasi nchini siku 30 kusaini na wafanyakazi mikataba ya ajira

Mwonekano wa barabara ya Sakina-Tengeru Km 14.1 inayojengwa kwa njia nne kwa kiwango cha lami ili kupunguza msongamano wa magari kuingia na kutoka katikati ya jiji la Arusha

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ametoa mwezi mmoja kwa makandarasi wote nchini kuhakikisha wanasaini mikataba ya ajira na wafanyakazi katika miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea nchini kote.

Akizungumza jijini Arusha mara baada ya kufanya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa Km 14.1 na barabara ya mchepuo ya kusini (Arusha bypass) yenye urefu wa Km 42.4, Prof. Mbarawa amesema mkandarasi atakayeshindwa kutoa mikataba kwa mujibu wa sheria za Tanzania, atanyang’anywa kazi ya ujenzi kwa kuvunja sheria.

“Barabara zinajengwa kwa kodi za wananchi hivyo wajenzi wa barabara nao ni lazima wafuate sheria za nchi ili kuhakikisha Serikali inapata kodi stahili na wafanyakazi wazawa nao wanapata haki stahili kwa mujibu wa ajira zao", amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Amezitaka taasisi za TRA, NSSF na nyingine zinazosimamia ajira za wafanyakazi kufuatilia miradi ya ujenzi ili kuona fursa za mapato ambazo serikali inaweza kupata na kusajili wafanyakazi katika hifadhi ya mifuko ya jamii.

Waziri Prof. Mbarawa amewataka mameneja wa tanroads na maafisa kazi kukagua mikataba ya ajira za ujenzi katika maeneo yao ili kuona haki inatendeka kwa makandarasi na kwa wafanyakazi ili ujenzi wa barabara ukamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amefungua mkutano wa Sita wa Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na kuwataka kuweka mikakati itakayowezesha kulinda hifadhi ya barabara, kudhibiti magari yanayozidisha uzito na kusimamia kasi katika miradi ya ujenzi wa barabara.

“Mmekua mkifanya kazi nzuri, endeleeni kufanya kazi kwa uadilifu, uwazi, weledi na kujiwekea malengo ya kujipima mwaka hadi mwaka ili muendelee kuwa tassisi ambayo watu watakuja kujifunza kwenu”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Patrick Mfugale amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa TANROADS imejipanga kuhakikisha miradi ipatayo 90 ya ujenzi wa barabara inayoendelea nchini kote inakamilika katika ubora unaotakiwa na unao uwiana na thamani ya fedha.

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Majengo nchini (TBA), mkoa wa Arusha, Bw. Victor Baltazar kukusanya madeni yote kwa haraka ili kukamilisha miradi ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na za biashara inayosimamiwa na Wakala huo mjini Arusha kukamilika kwa wakati.

Prof. Mbarawa ambaye yuko katika ziara ya mikoa ya kanda ya kaskazini amezitaka taasisi zilizo chini wa wizara hiyo kuhakikisha zinafanya kazi kibiashara ili kuboresha mapato ya Serikali na hivyo kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akijadiliana jambo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Fadhili Nkurlu jijini Arusha.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifafanua jambo kuhusu ukusanyaji madeni ambayo Wakala wa Majengo nchini (TBA) inadai wapangaji wake.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kulia) akikagua ripoti ya biashara inayofanywa na Kampuni ya Simu nchini (TTCL), jijini Arusha. Wa tatu kulia ni Meneja Kanda ya Kaskazini TTCL Bw. Peter Lusama.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (katikati) akiimba wimbo wa mshikamano daima na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS kabla ya kufungua rasmi mkutano wa sita wa Baraza hilo. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Patrick Mfugale na kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Fadhili Nkurlu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza kufanya kazi kwa malengo yanayopimika katika kikao chake na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya wizara yake, jijini Arusha.Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mkandarasi M/S Hanil Jiangsu J/V anayejenga barabara ya Sakina-Tengeru Km 14.1 na barabara ya mchepuo wa kusini Arusha bypass Km 42.4 jijini Arusha.
  • Taarifa hii imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.