Katika kupambana na dawa za kulevya: Wizara kuhoji wenye ukwasi wa mashaka ulivyopatikana
Kasi ya Rais John Magufuli ya kutumbua majipu sasa imeanza kuvunja mtandao wa dawa za kulevya (unga) nchini, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Rais Magufuli ametoa maelekezo mahsusi kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga akielekeza kuwa anataka kuiona Tanzania isiyokuwa na wauzaji na watumiaji ‘unga’.

Rais amenukuliwa akisema haiwezekani wauza unga wakawa na nguvu kuliko Serikali.

Tayari maofisi wa Serikali wameanza kulifanyia kazi agizo hilo kimyakimya na kwa kasi ya aina yake, ambako sasa wanakwenda nyumba hadi nyumba wakihoji wafanyabiashara wenye ukwasi usioelezeka na katika kufanya hivyo wamekutana na ‘maajabu’.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi imeanzisha operesheni ya kukamata wafanyabiashara wote wanaohusishwa na dawa za kulevya jijini Dar es Salaam.

Katika operesheni hiyo, tayari polisi wamekamata ‘mapapa’ wawili wanaoelezwa kuwa miongoni mwa ‘mapapa’ wa biashara hiyo haramu nchini. Mapapa hao wanashikiliwa Kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni.

Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni umeanza msako mkali wa kimyakimya kwa wafanyabiashara hao; operesheni inayoelezwa kuwa inahusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Idara ya Usalama wa Taifa na kitengo maalum kutoka Ikulu.

JAMHURI limethibitishiwa kuwa Hemed Horohoro na Lwitiko Samson Adam, ni kati ya mapapa waliokuwa wakisakwa kwa udi na uvumba na sasa wametiwa nguvuni.

Lwikito ambaye anaelezwa kuwa na makazi nchini Afrika Kusini, alikamatwa nyumbani kwake Magomeni jijini Dar es Salaam. ‘Papa’ huyo, amekutwa kwenye ‘nyumba ya ajabu’.

“Huwezi kuamini. Lwitiko aliishi maisha ya peponi. Ukiiona nyumba yake pale Magomeni, nje si nyumba ya maana, lakini ukiingia ndani utashangaa. Nyumba imejengwa chini ya ardhi (underground). Huko kuna maisha ya peponi.

“Kule chini ya ardhi ana bwawa kubwa la kuogelea huko huko, baa na magari yote ya kifahari yapatayo manane tuliyakuta huko chini ya ardhi, tulistaajabu,” anasema mmoja wa watu waliofanya kazi ya kumkamata.

Magari yaliyokuwa huko chini ya ardhi mengine yana thamani ya hadi Sh milioni 500. JAMHURI limefanikiwa kupiga picha sehemu ya magari hayo katika Kituo cha Polisi Oysterbay, ambayo yamo BMW X6, Lexus, Lumma CLR RS, Cooper na mengine ya kifahari.

Wakati Lwitiko akikamatwa na baadhi ya mali zake, Hemed alikamatwa na gari moja ambalo nalo pia linashikiliwa katika kituo hicho.

Watuhumiwa hao waliokamatwa wanatajwa kuwa wamekuwa wanauza dawa aina ya heroine kutoka Pakistan; cocaine kutoka Brazil, huku wakiishi maisha ya kifahari nchini Tanzania na Afrika Kusini.

Katika kinachohofiwa kuwa taarifa zimevuja ukamataji ulipoanza wiki iliyopita, kundi kubwa la wafanyabiashara waliolengwa lilikimbia nchi.

“Wengi wamekwenda Kenya na Afrika Kusini. Weengine wameikimbia Dar es Salaam, taarifa za kiintelijensia zinaonyesha wako mikoani, lakini kwa vyovyote vile chini ya Rais [John] Magufuli wanapoteza muda. Watakamatwa tu,” amesema mtoa habari wetu.

Kamanda wa Polisi Kanda ya Kinondoni, ACP Christopher Fuime, anasema ukamataji huo ni endelevu, lakini hakutaka kuingia kwa undani zaidi akisema wananchi wasubiri kuona ‘wazungu wa unga’ wote wanapotea mtaani.

Anasema kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya si watu wadogo, bali wana uwezo na wanamiliki mtandao mkubwa, hivyo kukabiliana nao kunahitaji “muda na usiri mkubwa”.

Alipoulizwa ni lini wanatarajia kuwafikisha mahakamani ‘mapapa wawili’ waliokamatwa, amesema hawezi kuzungumzia hilo kwani upelelezi bado unaendelea na kwamba unahusisha taasisi nyingi, hivyo ni vigumu kubainisha hilo.

Hata hivyo, amekiri kukamatwa kwa Horohoro na Lwitiko na anasema: “Hapa tunafuatilia mambo mengi. Tunavyopeleleza kesi za dawa za kulevya tunaangalia umiliki wa mali, utakatishaji wa fedha, na mambo mengine mengi. Ila kwa sasa tumeamua ingawa wengine wanakimbia baada ya kubonyezwa, lakini hiyo siyo tatizo,” anasema Kamanda Fuime.

Katika eneo la kutakatisha fedha za dawa za kulevya, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanamiliki mabasi yanayofanya kazi ya daladala jijini Dar es Salaam na mengine yanakwenda mikoani.

“Mabasi haya mengi yanatoka Mbagala kwenda Posta, yameandikwa jina la moja ya taasisi kubwa za uzalishaji mafuta duniani, na pembeni yameandikwa majina yao kwa kuongeza herufi mbili mwishoni tu zisomekazo ‘so’. Huyu anaingiza hadi kilo 500 ze heroine kutoka Pakistan, na fedha anazopata anazitakatisha kwa kuonyesha anafanya biashara ya daladala na mabasi ya mikoani,” amesema mtoa habari wetu.

“Wiki iliyopita, Wapakistani sita wameingiza kilo 500 za heroine, wakahifadhi robo Segerea jijini Dar es Salaam, nyingine zimehifadhiwa Pemba, nyingine Zanzibar na nyingine zipo kwenye boti majini hazijaingia nchini,” kiliongeza chanzo chetu.

Ukiacha magari, wanaouza dawa za kulevya wanajenga majengo makubwa katika miji ya Dar es salaam, Zanzibar, Arusha, Mwanza, Tanga na Mbeya, kisha wanatumia majengo hayo kudanganya umma kuwa fedha zao zinatokana na kodi ya pango.

Kamanda Fuime, alipoulizwa mkakati wa kupambana na wauzaji waliotajwa kuikimbia nchi, amesema kuzungumzia hilo ni sawa na kuanika mipango ya polisi; jambo ambalo si sahihi.

Miezi miwili iliyopita polisi nchini walifanya uhamisho kwa askari wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni na Tanga kuvunja mtandao wa uhalifu, hususan dawa za kulevya ndani ya Jeshi hilo.

Asilimia kubwa ya ‘mapapa’ wa biashara hiyo haramu wapo jijini Dar es Salaam, hasa maeneo ya Kinondoni, Magomeni na Mbezi Beach.

Waziri Kitwanga ameshakabidhiwa orodha ya polisi wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ambako majina hayo aliyakabidhi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Inspekta Jenerali Ernest Mangu.

Baada ya IGP Mangu kukabidhiwa majina hayo, aliwataka askari wa Oysterbay kumkabidhi orodha ya majina ya wauza ‘unga’ haraka.

Mpango huo ulienda sambamba na kuwapangua baadhi ya polisi walioonekana kushindwa kuukabili mtandao wa wauza ‘unga’.

Maofisa waliohamishwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Kinondoni Camillius Wambura, aliyepelekwa Manyara na Mkuu wa Utawala Kinondoni, pamoja na baadhi ya askari wa kitengo cha upelelezi na wengine kutoka idara mbalimbali.

Kuhamishwa kwao kulitokana na kushindwa kwao kudhibiti mtandao wa dawa za kulevya nchini, kiasi cha kuifanya Tanzania kuwekwa kwenye orodha ya nchi zinazojihusisha na biashara hiyo kwa kiwango cha juu.

Awali, kabla ya matukio hayo, Tanzania ilikuwa ikitumiwa kama njia ya kupitishia dawa za kulevya kwenda Afrika Kusini, Ulaya na Amerika, lakini kadri siku zinavyokwenda inakuwa soko la dawa hizo.

Kinachotokea vijana wengi mitaani wanaoitwa mateja, ndiyo wenye kufanya kazi ya kuiba na kupora vitu vya watu mbalimbali. Fedha wanazopata wanazitumia kununua ‘kete za dawa’ na kuzitumia.

Kundi hili limeongezeka, na inaelezwa kuwa wafanyabiashara vijana wa kundi la kati wengi sasa wanatumia dawa za kulevya na hilo ndilo linachangia magari mengi kuwekewa ‘tinted’, kwa nia ya kuficha maovu.

Serikali ya Awamu ya Nne, iliamua kupambana na dawa za kulevya kwa kubadili sheria na ikaelekeza kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, lakini hadi leo chombo hicho hakijaundwa.

Ukiacha kutoundwa kwa chombo hicho, wafadhili walikuwa wakitoa fedha za kununulia dawa ya methodine kwa ajili ya vijana walioathirika na dawa za kulevya, lakini maofisa waliopo katika Tume ya Dawa za Kulevya wakaishia kuzifuja na hivyo mradi ukafutwa.

Matumaini makubwa ya Watanzania sasa yapo mikononi mwa Rais Magufuli, kwani inaelezwa kuwa yeye hana ushirika na wafanyabiashara ambao baadhi yao wanafanya biashara ya dawa za kulevya.

“Tunachosema, Rais sasa achunguze wanaomiliki mabasi, majumba makubwa na biashara zisizoelezeka mitaji yake ilipatikanaje, kisha kuanzia hapo atajua kina nani wanafanya biashara haramu na kina nani wanatumia biashara kutakatisha fedha za dawa za kulevya,” ameshauri mtoa habari wetu.

Gazeti la JAMHURI limekuwa miongoni mwa vyombo vya habari vilivyo mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Mwezi uliopita lilichapisha orodha ya wauza unga 560 wanaofanya biashara hiyo nchini, na ambao wengi wao wapo mikononi mwa dola kwa sasa.

Hata hivyo, kumekuwapo madai kuwa wanaokamatwa wengi ni wachuuzi wa chini na wa kati, lakini wahusika wakuu wanaogharimia biashara hiyo, wakiwamo viongozi serikalini na katika vyombo vya dola, wakiwa hawajakamatwa.


Taarifa ya habari ChannelTEN, Februari 27, 2016


Watendaji 3 wa Bodi ya Taasisi ya Elimu Tanzania wasimamishwa kazi


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Ufundi, Maimuna Tarishi ameiagiza Bodi ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), kuwasimamisha kazi watendaji wake watatu kwa kushindwa kusimamia uchapaji wa vitabu vya Darasa la Kwanza.

Tarishi ametoa agizo hilo kwa niaba ya Waziri wa izara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, wakati akitoa tamko la serikali kuhusu kupokea vitabu vya kiada darasa la kwanza vilivyokopeshwa na kampuni ya Yukos Enterprises Limited ambavyo vimebainika kuwa na kasoro.

Waliosimamishwa -- Peter Bandio, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Vifaa vya Kielimu, Pili Magongo, Mwanasheria wa TET na Jackson Mwaigonela, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi -- wanatuhumiwa kushindwa kusimamia sheria ya manunuzi na kazi ya uchapaji wa vitabu hivyo imelazimika kuwasimamisha ili kupisha uchunguzi.

“Mnamo tarehe 22 Januari mwaka 2016 bodi hiyo ilishauriwa kusitisha uchapaji wa vitabu uliokuwa ukifanywa na kampuni ya Yukos Enterprises Ltd baada ya kubainika kuwa na mapungufu, lakini haikusitisha,” amesema Tarishi na kuongeza: “Serikali iliamua kusitisha uchapishaji wa vitabu hivyo ili isiendelee kupokea vitabu vyenye mapungufu, hata hivyo taasisi ya elimu haikusitisha uchapishaji wa vitabu hivyo, badala yake kampuni hiyo ilichapisha vitabu vyote ilivyopangiwa,” amesema Tarishi.

Tarishi amesema ufuatiliaji uliofanywa na wizara katika bohari ambayo ilikuwa inapokea vitabu hivyo, ulibaini kuwa vitabu vilivyowasilishwa na kampuni ya Yukos vilikuwa na kasoro.

“Kutokana na kasoro hizo, Taasisi haikutekeleza wajibu wake wa kusimamia uchapaji wa vitabu na uzingatiaji wa sheria ya manunuzi kikamilifu,” amesema.

Kutokana na mapungufu hayo, Wizara imetoa maagizo ya kuondolewa kwa baadhi ya vitabu vilivyowasilishwa kwenye bohari ya serikali ifikapo tarehe 29 Februari mwaka huu.

“Taasisi ya Elimu iwasimamishe kazi mara moja watumishi wafuatao ambao walikuwa na jukumu la kusimamia sheria ya manunuzi na kazi ya uchapaji wa vitabu ili kupisha uchunguzi,” amesema.

Mapungufu yaliyoonekana kwenye vitabu hivyo ikiwemo upungu wa mwingiliano wa rangi, upungufu wa kurasa katika vitabu, ukataji usiozingatia vipimo, vitabu kuchakaa kabla ya matumizi na mpangilo mbaya wa kurasa.


Baba wa kambo na mama wanusurika kuuawa baada ya kumwua mtoto

Wanandoa wawili Juma Selemani (28) na Suzana Elias (24) wakazi wa Mtaa wa mji wa zamani Manispaa ya Mpanda wamesurika kifo kutoka kwa kundi la wananchi waliotaka kuwauwa kwa kuchoma motonyumba waliokuwa wakiishi baada ya kukasirishwa na kitendo chao cha kumua mtoto wao aliyejulikana kwa jina la Justina Laurent (3) kwa kumchoma na moto kichwani na mikononi na kasha kuuficha mwili wa marehemu ndani ya chumba walichokuwa wakiishi kwa muda wa siku tatu.

Tukio hilo la kusikitisha la mauwaji ya mtoto huyo lilitokea hapo jana majira ya saa moja na nusu usiku katika mtaa huo wa mji wa zamani mjini hapa na lilisikitisha watu wengi wa Manspaa ya mji wa Mpanda.

Mwenyekiti wa Mtaa huo Magreti John alimweleza mwandishi wa gazeti hili aliyekuwepo kwenye eneo hilo la tukio kuwa alipata taarifa za kuuawa kwa mtoto huyo ambae alikuwa akiishi na baba wake wa kambo aliyekuwa amemuowa mama yake Suzana Elias.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa wangaji wa nyumba hiyo alifika kwenye nyumba hiyo na ndipo walipomweleza kuwa kuna mtoto ameuawa na wazazi wake na wamemfungia ndani wakiwa wameuficha mwili huo wa marehemu kwa muda wa siku tatu.

Mwenyekiti huyo wa mtaa alieleza wapangaji hao walishitushwa baada ya kuona mtoto huyo kutoonekana kwake kwa muda wa siku tatu na chumba walichokuwa wakiishi wanandoa hao kuanza kutowa harufu ya kitu kilicho oza na kila walipoulizwa mtoto wao yuko wapi walionekana wanandoa hao kuwa na mashaka na walijibu kuwa mtoto wao anaumwa.

Ndipo walipoamua kutowa taarifa kwa mjumbe wa serikali ya mtaa anaeitwa Matha Idd ambaye naye alitowa taarifa kwa kwake yeye Mwenyekiti wa mtaa ambae aliwapatia tarifa jeshi la Polisi na waandishi wa Habari .

Polisi walifika kwenye eneo hilo na kukuta kundi la watu huku wakiwa na silaha za jadi mawe na fimbo wakiwa wameizingira nyumba hiyo kwa lengo la kutaka kuwashambulia wanandoa wengine huku wengine wakiwa wamshika mafuta ya taa kwa lengo la kutaka kuchoma nyumba hiyo .

Askari polisi ambao walikuwa na silaha za moto walifanikiwa kuwatawanya wananchi hao na kasha waliingia ndani ya chumba na kuwachukua wanandoa hao wawili na kuwapeleka kituo cha polisi cha Mpanda mjini huku wananchi hao wakiwasindikiza kwa kuwarushia mawe.

Kisha polisi waliokuwa wamebaki hapo pamoja na mwenyekiti wa mtaa walifnya uchunguzi wa awali wa kuukagua mwili wa marehemu mtoto huyo na waliweza kuukuta ukiwa umechomwa na moto kichwani na mikononi huku ukiwa umeanza kuharibika na ukiwa unatowa maji mwilini.

Mmoja wa wanandoa hao aliyejitambulisha kwa jina la Maria Komba alieleza kuwa kabla ya tukio hilo amekuwa akisulisha ugomvi wa mara kwa mara ambapo Juma Selemani alikuwa akipinga kitendo cha mke wake kuishi nyumbani kwake marehemu na alikuwa akimtaka mkewe ampeleke kwa baba yake mzazi kwani yeye alikuwa akidai hawezi kukaa na kumtunza mtoto ambae sio wake .

Kaimu Kamanda wa jeshi la polisi wa Mkoa wa Katavi Mohamed Rashid I amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la kusikisha .

Alisema wanandoa hao wote wawili wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi utakapo kuwa umekamilika.
  • Taarifa ya Walter Mguluchuma - Katavi Yetu blog

Mmiliki wa mabasi ya Ngorika, Mberesero agongwa na gari na kufariki dunia


Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ngorika Bus Service, yenye makao yake makuu Kisangara mkoani Kilimanjaro, bwana Stephen Mberesero amefariki dunia baada ya kugongwa na gari aina ya Land Cruiser wakati akizungumza na simu.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Tanga, Mihayo Msikhela amesema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 2;30 usiku katika barabara kuu ya Segera-Njia Panda ya Himo mjini Korogwe.

Alisema Mberesero ambaye mabasi yake hufanya safari kati ya mikoa ya Arusha, Tanga, Dar es Salaam na Singida, alikuwa amesimama pembeni ya kituo cha mafuta cha Lake Oil  alipogongwa na gari hilo.

Mfanyakazi wa kampuni hiyo, Adam Miraji alisema bosi wake huyo alikwenda Korogwe kuangalia kiwanja kwa ajili ya kununua ili kujenga kituo cha mafuta.
Kama unavyojua bosi wetu pamoja na kufanya biashara ya mabasi, alikuwa anamiliki vituo mbalimbali vya mafuta mkoani Kilimanjaro, Dar es Salaam na Arusha, hivyo alipokuja Tanga alituambia anakwenda Korogwe kuangalia kiwanja cha kujenga kituo kipya cha mafuta,
alisema Adam.

Alisema bosi wake huyo alikuwa ameliweka gari lake katika kituo cha mafuta cha Lake Oil na kwamba alishuka kw aajili yakuelekea katika kiwanja hicho.
Wengi waliokuwepo katika eneo la ajali hawakujua kama ni yeye hadi tulipokwenda kuchukua mwili wake ndipo wakashtuka.
Alisema.

Kamanda Mihayo alisema wanamsaka dereva aliyesababisha ajali hiyo kwa uzembe na kusababisha kifo.

Kwa mara ya nne: Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar waahirishwaVURUGU kubwa zimetokea wakati wa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam mara baada ya uchaguzi huo kuhairishwa tena kwa mara ya nne leo, huku Jeshi la Polisi likivamia ukumbi na kuanza kupambana na Madiwani na Wabunge wa muunganiko unaounda UKAWA (Umoja wa Katiba ya Wananchi).

Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ulipangwa kufanyika leo lakini kutokana na kuendelea kwa mvutano kuhusu washiriki walio na sifa ya kushiriki upigaji kura kwenye uchaguzi huo kutopatiwa ufumbuzi, mgogoro huo umeendelea.

Lililotokea leo katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam mara baada ya mkurugenzi wa Jiji, Sara Yohana, kutangaza kuahirisha uchaguzi huo kwa madai ya uchaguzi kuwekewa pingamizi na CCM mahakamani, liliwachukiza madiwani wa UKAWA ambao walidai kuwa hawajapata barua ya pingamizi hilo, hivyo wakataka waruhusiwe kufanya uchaguzi peke yao kwa kuwa akidi ya madiwani kufanya uchaguzi ilikuwa imetimia.

Wakati UKAWA wakijiiandaa kufanya uchaguzi huo wenyewe, Polisi zaidi ya 15 walivamia ukumbi huo na kuwataka madiwani hao waondoke ukumbini ,jambo lilowachukiza tena na kuibua patashika ndani ya ukumbi.


Kabla ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo, wanachama wa Ukawa walifika mapema na kuingia kwenye Ukumbi wa Kareem Jee huku wanachama wa CCM wakijizoazoa kuingia ukumbini hapo.

Theresia Mbando ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo, alitoka nje na kuwataka wajumbe hao wa CCM kuingia ukimbini ili mkutano huo kuanza.

Baada ya CCM kuingia ndani, Mbando alifuata taratibu zote za kiitifaki katika kufungua kikao hicho ikiwa ni pamoja na kugawa ratiba za mkutano huo.

Wajumbe wakiwa tayari kwenda na ratiba ya mkutano huo, ndipo Sara (Kaimu Mkurugenzi) alisimama ghafla na kutangaza kughairishwa kikao hicho.

Yohana alidai kwenye maelezo yake kwamba, amepokea zuio kutoka Mahakama ya Kisutu iliyomtaka kutoendesha uchaguzi huo.

“Tunaahirisha uchaguzi huu kwa kuheshimu zuio la mahakama ambalo litadumu kwa miezi mitatu hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa ndipo tutaitisha tena uchaguzi,” amesema Sara.

Mara tu baada ya kauli yake, wajumbe wa CCM harakaharaka walisimama na kutoka nje huku wakicheka wengine wakisema “hahahaaa, wajiju. Shoga kwa heri” huku wakigonganisha mikono.Wakati Mwenyekiti na Kaimu Mkurugenzi wakijiandaa kutoka nje ya ukumbi, wananchi pamoja na viongozi wa wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) waliwazuia wakidai kupewa ufafanuzi zaidi wa zuio hilo.

“Hapa huondoki hadi utuoneshe barua kutoka mahakamani, hakimu aliyetoa hilo zuio, aliyefungua madai na sababu za kuzuia uchaguzi,” mjumbe mmoja wa UKAWA alisikika akisema hivyo.

Si mwenyekiti wala kaimu mkurugenzi aliyeweza kujibu maswali ya Ukawa, wakati huo viongozi hao walikuwa wamezingirwa na ahama pia wajumbe wa UKAWA.

Kwa mujibu wa viongozi wa UKAWA, zuio lililobandikwa lilikuwa ni la tarehe 5 Februari mwaka huu ambalo lilikuwa linazuia uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 8 Februari mwaka huu.

“Kwanza hata hivyo kama kweli uchaguzi haujafanyika kwa sababu ya zuio hilo kwanini mkurugenzi aliitisha uchaguzi? Inamaana hakujua kama kuna zuio? Huu ni wizi na ni njama baina ya CCM na Mkurugenzi” viongozi wa UKAWA walisikika wakilalamika.

Baada ya vurugu kuzidi, polisi zaidi ya 15 waliobeba silaha wakaingia ukumbini na kumtoa mwenyekiti kwa nguvu kwa kumpitisha mlango wa dharura na kupandishwa gari lao kisha kutokomea.

Baada ya vurugu kutulia, UKAWA walikaa kikao ambapo John Mnyika, Mbunge wa Kibamba alitoa tamko ambalo liliazimiwa na vingozi wa Ukawa kwamba, wajumbe watawanyike hadi tarehe 29 Februari ambapo wanatarajia kwenda mahakamani.

“Naombeni tuondoke kwa amani, jumatatu tutawachukua madiwani watatu na mawakili wetu kwenda mahakamani ili tuombe kuingia kwenye hiyo kesi. Tunaimani tutashinda hata wafanye nini Jiji ni letu,” amesema Mnyika.Uchaguzi Mkuu ulifanyika tarehe 25.10.2015 na wananchi wa Jiji la DSM Waliamua kuongozwa na UKAWA na ndio maana walichagua Madiwani na Wabunge wengi kutoka UKAWA. Kati ya Majimbo 10 ya Uchaguzi katika Jiji la DSM CCM ilipata Majimbo 3 tu baada ya kuchakachua na UKAWA ilipata yaliyosalia.

Hali ni hiyo hiyo kwenye kata. Wananchi waliamua kuipumzisha CCM kwa kuwa walikua wamechoshwa na uendeshaji mbaya wa Jiji la Dar es Salaam . Tangu Uchaguzi umalizike mpaka leo wananchi wanakosa huduma za Jiji kwa sababu CCM ilitaka kushinda Umeya wa Jiji kwa staili ileile waliyozoea ya goli la mkono. 

Mara wakaletwa wapiga kura feki kutoka Zanzibar huku Wakijua wazi kuwa TAMISEMI sio jambo la Muungano. Waziri mwenye dhamana na TAMISEMI hajawahi kutoa kauli wala kukemea hali hiyo hata siku moja huku akijua wazi kuwa vitendo hivyo vilikua ni kinyume Cha sheria za Nchi.

Leo tarehe 27.02.2016 tumeshuhudia Uchaguzi ukiitishwa na baada ya wajumbe Kuwasili wakakutana na kilichoitwa zuio la Mahakama la Tangu tarehe 05.02.2016 . Jambo hili limetokea baada ya Taarifa kusambaa jana tarehe 26.02.2016 kuwa CCM walipeleka shauri mahakamani la kuweka zuio na kuwa shauri hilo lilitupiliwa Mbali. Nini kinafichwa Jiji la DSM ? Tuna taarifa kuwa ni Ufisadi mkubwa uliofanywa na viongozi wa Jiji waliopita na wakishirikiana na Viongozi wa CCM kupora Mali za Jiji kama vile UDA, Mali za soko la Kariakoo, Viwanja na majengo ya Jiji. Pili tuna Taarifa kuwa hawataki majipu ya Jiji yatumbuliwe kwani kuna vigogo wakubwa wa CCM watatumbuliwa kutokana na kushiriki kwenye Ufisadi mkubwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam. 

Mipango iliyopo.

Mkutano wa Uchaguzi Leo uliitishwa pamoja na kuwepo hicho kinachoitwa zuio la Mahakama kwa lengo la kuwaudhi Madiwani wa UKAWA ili waonekane kuwa wanafanya fujo . Hii ni kutokana na ukweli kuwa kama zuio lipo Tangu siku CCM wanaadhimisha miaka39 ya kuzaliwa kwake ni kwanini Mkurugenzi aliitisha mkutano wakati akijua Mahakama imeweka zuio?. Mpango huu umesukwa ili kuhakikisha kuwa Waziri mwenye dhamana na TAMISEMI anatengenezewa sababu za kuweza kuvunja Halimashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuunda Tume ya kuongoza Jiji. 

Ni vyema tukaweka angalizo mapema kuwa Mafisadi wana mikakati mingi sana ya kuhakikisha kuwa hawatumbuliwi Majipu. Kama Rais ambaye ndio Waziri mwenye dhamana na TAMISEMI hakubaliani na mbinu hizi za Mafisadi, aingilie Kati Mara moja na kuhakikisha kuwa Uchaguzi wa Meya unafanyika na kazi ya kutumbua majipu ya Jiji inaendelea kama ambavyo imeshaanza katika Manispaa za Ilala na Kinondoni zinazoongozwa na UKAWA .

Imetolewa na John Mrema.
Mkurugenzi wa Bunge na Halimashauri CHADEMA.
TANESCO yawasilisha maombi EWURA kuomba kurekebisha bei

SHIRIKA la Umeme (TANESCO) limepeleka maombi kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kuomba kupandisha bei ya nishati hiyo, kinyume na matakwa ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ya kushusha bei hiyo.

Taarifa ya Ewura kwa umma iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa maombi hayo yamepokewa Jumatano ya wiki hii na kutaka wadau kujitokeza kujadili uhalali wa nyongeza hiyo siku mkutano huo utakapoitishwa.

“Mamlaka inaanzisha mchakato wa kupata maoni ya wadau, ili kujua uhalali wa maombi ya nyongeza ya bei za huduma iliyoyapokea kutoka TANESCO,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TANESCO iliwasilisha ombi husika kulingana na Sheria ya Umeme namba 131, inayoitaka Ewura kufanya mabadiliko ya bei zinazotozwa na mtoa huduma mara moja kila baada ya miaka mitatu.

“Pendekezo la wastani wa badiliko la bei za umeme ni asilimia 1.1 kuanzia Aprili mosi 2016 na asilimia 7.9 kuanzia Januari mosi 2017,” limeeleza tangazo hilo.

Mapendekezo hayo japo ya kisheria, lakini yanapingana na msimamo wa Waziri Muhongo, ambaye tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo, alielezea kusudio lake la kutaka bei ya nishati hiyo ishushwe.

Profesa Muhongo alikwenda mbali na kuagiza TANESCO, EWURA na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kumpelekea mapendekezo ya kushuka kwa bei ya umeme kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.

Katika maagizo hayo, Profesa Muhongo alihoji kwa nini bei ya umeme isishuke, wakati gharama za uzalishaji wa umeme wa kutumia mafuta zimeshuka kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Kutokana na maombi hayo ya TANESCO, EWURA imewataka wadau wa nishati wanaopenda kutoa maoni yao kwa maandishi, kufanya hivyo kwa kutuma maoni yao kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, ghorofa ya saba jengo la LAPF Pensions Fund Tower, mkabala na Kijiji cha Makumbusho, Kijitonyama Dar es Salaam.

Kwa watakaotuma kwa njia ya posta, wameombwa kufanya hivyo kwa kutumia Sanduku la Posta 72175, Dar es Salaam, Tanzania, simu namba (+255-22) 2123853-4; Fax namba (+255-22) 2123180; Barua pepe[email protected] au tovuti http://www. energyregulators. org.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mamlaka hiyo pia, itaitisha mikutano ya wazi ili kukusanya maoni kuhusu mapendekezo hayo kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwamo Baraza la Wawakilishi wa Watumiaji wa Huduma (CCC); Baraza la Ushauri la Serikali (GCC) pamoja na wananchi kwa ujumla.

Polisi Zanzibar kuwahoji watumiaji 34 wa mitandao ya kijamii

Salum Msangi
Salum Msangi
Jeshi la Polisi Zanzibar linakusudia kuwahoji watumiaaji wa mitandao ya kijamii 34 kutokana na kuhamasisha vurugu sambamba na kuandika lugha za matusi zinazowalenga viongozi wakuu hapa visiwani.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI) Salum Msangi (pichani) alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Makao Makuu ya Polisi Kilimani Zanzibar.

Alisema kuwa mara baada ya kufutwa kwa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana, kumejitokeza baadhi ya watu na vikundi mbali mbali vinavyotumia mitandao ya kijamii kwa kuandika maneno ya matusi au kutoa clip za kuongea zenye lugha ya matusi kwa kuwatukana watu mbali mbali hasa viongozi wa kitaifa.

Alisema kuwa uchunguzi wa kitaalamu na kisayansi unaendelea na utakapokamilika jalada la ksi hiyo litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashataka (DPP) ikiwa ni utaratibu wa kupeleka kesi mahkamani.

Alisema kwamba jeshi hilo limepata orodha ya watumiaji hao na hadi sasa Jeshi la Polisi linamhoji mtu mmoja kwa ajili uchunguzi ambae anatuhumiwa kutoa moja ya clip zenye lugha ya matusi dhidi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.

Msangi alitoa tahadhari kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kwani kutumia lugha za matusi ni kosa lililoainishwa kisheria kwenye sheria ya kanuni ya adhabu na yoyote atakaefanya kitendo hicho atakamatwa na kufikshwa mbele ya vyombo vya sheria, bila ya kujali limetolewa mahala gani au wakati gani.

“wasidhani kwamba demokrasia ni kuwatukana vuiongozi hilo wasijidanganye lazima sheria ichukue nafasi yake” alisema Msangi.

Aliwatahadharisha watumiaji wa mitandao kwamba serikali iko macho na matendo yao na kuwataka kuacha mara moja kutumia mitandao kwa kukashifu viongozi au watu wengine.

“kabala mtu hajaandike apime ni kitu gani ambacho anataka kuandika kwani akienda kinyume tutamshuhulikia” alieleza Msangi.

Hivi karibuni aliyekuwa mmoja wa timu ya ushindi ya Chama cha Wananchi (CUF) alikamatwa wiki iliyopita kwa madai ya kutoa clip ambayo anamtukana rais wa Zanzibar.
  • Taarifa ya Talib Ussi, Zanzibar

Taarifa ya IGP ya mabadiliko katika safu ya makamanda wa mikoa


WM Majaliwa ziarani mkoani Mtwara


Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akisalimiana na viongozi wa mkoa wa Mtwara baada ya kuwasil kwenye uwanja wa ndege ea Mtwara kwa ziara ya siku moja mkoani humoFebruari 27, 2016.

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akitembelea bandari ya Mtwara Februari 27, 2016.Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Halima Dendego.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wafanyakazi wa kampuni ya TPDC baada ya kuwasili kwenye mtambo wa kuchakata gesi wa Madimba, Mtwara Vijijini kukagua shughuli za gesi Februari 27, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majliwa na viongozi wengine akikagua mtambo wa kuchakata gesi wa Madimba, Mtwara Vijijini Februari 27, 2016. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Naibu Waziri Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Medadi Kalemani na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio, na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Halima Dendego.

Waziri Mkuu, Kassim Majliwa na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa TPDC baada ya kutembelea mtambo wa kuchakata gesi wa Madimba, Mtwara Vijijini Februari 27, 2016

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na walimu na wakufunzi wa Chuo cha Elimu cha Mtwara baada ya kuzungumza nao chuoni hapo , Februari 27, 2016.
  • Picha na maelezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu

Picha za mkutano wa WM Majaliwa na viongozi wa dini


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa dini kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Februari 26, 2016.

Baadhi ya viongozi wa dini wanaunda kamati ya amani ya Dar es salam na baadhi ya mikoa nchini wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Februari 26, 2016.

Baadhi ya viongozi wa dini wanaunda kamati ya amani ya Dar es salam na baadhi ya mikoa nchini wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Februari 26, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Askofu Mkuu wa KKKT Mstaafu, Elinaza Sendoro baada ya kuzungumza na Viongozi wa Dini kwenye Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Februari 26, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Askofu Mkuu wa KKKT Mstaafu, Alex Molasses baada ya kuzungumza na Viongozi wa Dini kwenye Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Februari 26, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Dini baada ya kuzungumza nao kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyererejijini Dar es Salaam, Februari 26, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Dini baada ya kuzungumza nao kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyererejijini Dar es Salaam, Februari 26, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Dini baada ya kuzungumza nao kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyererejijini Dar es Salaam, Februari 26, 2016.
  • Picha zote zimetoka Ofisi ya Waziri Mkuu