Tofauti ya GPA na GPT; Hatua zinazotumika kupata GPA; Mapendekezo


TANGU serikali ya awamu ya tano iingie madarakani kuna maamuzi kadhaa yamefanywa na kuibua mijadala miongoni mwa jamii, mojawapo ni uamuzi uliofanywa na Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako.

Prof. Ndalichako alibatilisha matumizi ya mfumo wa kupanga madaraja ya ufaulu shuleni kwa kuzingatia wastani wa pointi za daraja ya ufaulu, ambayo kwa Kiingereza ni “Grade Point Average” (GPA).

Badala yake, Ndalichako aliielekeza Wizara kufufua mfumo uliokuwepo hapo awali ili uendelee kutumika shuleni. Mfumo wa awali ulikuwa unapanga madaraja ya ufaulu kwa kuzingatia jumla ya pointi za gredi ya ufaulu, ambayo kwa Kiingereza ni “Grade Point Total” (GPT).

Bila kujali kama umetumika mfumo wa GPT au GPA, bado madaraja ya ufaulu yatatengenezwa, lakini yakiwa na majina tofauti.

Kwa mfano, kwenye mfumo wa GPT wa Tanzania, tunasema Daraja la Kwanza (Division One), Daraja la Pili, Daraja la Tatu, Daraja la Nne, na Daraja Sufuri.

Kwenye mfumo wa GPA, tunasema Daraja la ‘Distinction’ (la tofauti), Daraja la ‘Merit’ (Sifa), Daraja la ‘Credit’ (Stahili), Daraja la ‘Pass’ (Faulu), na Daraja la ‘Fail’ (Kufeli).

Kwa hiyo, sio sahihi kwa mtu kusema, “Dk. Kawambwa alifuta divisheni na Prof. Ndalichako amezirudisha,” kama ambavyo vyombo vingi vya habari vimekuwa vikiripoti. Ukweli ni kwamba, divisheni ziko pale pale siku zote, ila kinachobadilika ni namna ya kuzikokotoa na kuzitamka.

Kuhusu namna ya kuzikokotoa, divisheni za GPT zinapatikana kwa kutafuta jumla ya alama alizopata mwanafunzi, wakati divisheni za GPA zinapatikana kwa kutafuta wastani wa alama alizopata mwanafunzi.

Makala haya ni kwa ajili kuweka bayana mchakato huu wa kutafuta madaraja ya ufaulu shuleni.

Hatua 12 katika mchakato wa kutafuta GPA


Kama walimu wote wanavyofahamu, mchakato wa kutathmini maendeleo ya kitaaluma ya mwanafunzi (academic assessment process) unazo hatua kumi na mbili, kama zinavyojadiliwa katika aya zifuatazo.

Katika hatua ya kwanza, mwanafunzi hufundishwa, kwa kutumia mtaala rasmi. Pili, mwanafunzi hutungiwa mtihani kwa ajili ya kupima uelewa wake.

Tatu, mwanafunzi hujibu mtihani kwa kujibu maswali yaliyoandaliwa na mwalimu wake, na chini ya usimamizi wa mwalimu.

Nne, mwalimu husahihisha majibu ya mtihani kama yalivyoandikwa na mtahiniwa. Hatimaye mwanafunzi hutunukiwa alama za ufaulu kwa mujibu wa skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa asilimia. Katika skeli hii, mwanafunzi anaweza kupata alama kati ya sufuri na mia moja.

Katika hatua ya tano, idadi ya herufi za ufaulu zitakazotumika katika kurekodi ufaulu katika mtindo wa herufi huamuliwa. Herufi hizi kwa pamoja kutengeneza skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa herufi.

Kuhusu idadi ya herufi zinazopaswa kuwemo katika skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa herufi, tunaweza kuwa na skeli yenye herufi mbili [mfano P(Pass), F(Fail)]; skeli yenye herufi tano [mfano A, B, C, D, na F]; skeli yenye herufi sita [mfano A, B, C, D, E na F]; skeli yenye herufi saba [mfano A, B+, B, C, D, E, na F]; na kuendelea. Kwa hapa Tanzania, uamuzi kuhusu idadi ya herufi zinazopaswa kutumika, hufanywa, sio na mwalimu, bali na serikali.

Kwa sasa, idadi ya herufi zilizo katika skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa herufi inayotumika katika vyuo vingi vya elimu ya juu ni saba [A, B+, B, C, D, E, na F].

Skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa herufi inayotumika katika elimu ya sekondari, kati ya kidato cha tano mpaka kidato cha sita, inazo herufi sita [A, B, C, D, E, na F] na skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa herufi inayotumika katika elimu ya sekondari, kati ya kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne, inazo herufi tano [A, B, C, D, na F].

Katika hatua ya sita, skeli ya ufauli ulio katika mtindo wa asilimia (percentage scale) huoanishwa na skeli ya ufaulu ulio katika mtindo wa herufi (letter scale).

Kwa mfano, mchakato wa kuoanisha skeli hizi mbili unaweza kuwa kama ifuatavyo:

Gredi A sawa na ufaulu wowote ulio kati ya 100% na 81%; gredi B sawa na ufaulu wowote ulio kati ya 80% na 61%; gredi C sawa na ufaulu wowote ulio kati ya 60% na 41%; gredi D sawa na ufaulu wowote ulio kati ya 40% na 21%, na gredi F sawa na ufaulu wowote ulio kati ya 20% na 0%.

Nchini Tanzania, uamuzi kuhusu mipaka ya madaraja ya ufaulu kwa kuzingatia herufi yaliyopo kati ya asilimia sufuri mpaka asilimia mia moja, hufanywa, sio na mwalimu, bali na NECTA.

Pia, mipaka ya madaraja ya ufaulu kwa kuzingatia herufi yaliyopo kati ya asilimia sufuri mpaka asilimia mia moja, inatofautiana katika ngazi tofauti za elimu hapa nchini. Kidato cha kwanza mpaka cha nne wanayo mipaka yao; kidato cha tano mpaka cha sita wanayo mipaka yao; na vyuo vya elimu ya juu vinayo mipaka yake kwa kila daraja la kiherufi.

Katika hatua ya saba, kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi hubadilishwa kutoka kwenye gredi ya ufaulu iliyo katika mtindo wa asilimia (percentage score) kwenda katika gredi ya ufaulu iliyo katika mtindo wa herufi (letter score). Kazi hii hufanyika kwa kuzingatia skeli ya ufaulu ulio katika mtindo wa herufi (letter scale) kama ilivyojadiliwa hapo juu.

Nane, uamuzi hufanyika kuhusu utaratibu wa kubadilisha gredi ya ufaulu iliyo katika mtindo wa herufi (letter score) kwenda kwenye gredi ya ufaulu iliyo katika mtindo wa pointi (point score).

Kwa ajili hii, hutengenezwa skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa pointi. Zipo njia mbili za kutengeneza skeli hii. Ama kwa kuhakikisha kwamba skeli hii inaanza na namba kubwa na kuishia na namba ndogo, au kinyume chake.

Katika skeli ya pointi inayoanza na namba kubwa kwenda namba ndogo kazi ya kuoanisha herufi na pointi huweza kufanyika kama ifuatavyo: Gredi A sawa na pointi 4; gredi B sawa na pointi 3; gredi C sawa na pointi 2; gredi D sawa na pointi 1, na gredi F sawa na pointi 0.

Na katika skeli ya pointi inayoanza na namba ndogo kwenda namba kubwa kazi ya kuoanisha herufi na pointi huweza kufanyika kama ifuatavyo: Gredi A sawa na pointi 1; gredi B sawa na pointi 2; gredi C sawa na pointi 3; gredi D sawa na pointi 4, na gredi F sawa na pointi 5.

Hapa nchini, uamuzi kuhusu skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa pointi inayopaswa kutumika, hufanywa, sio na mwalimu, bali na serikali.

Kwa sasa, skeli za kutunuku ufaulu kwa mtindo wa pointi zinatofautiana kutoka ngazi moja ya elimu mpaka ngazi nyingine.

Kwa mfano, shule za sekondari zinatumia skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa pointi inayoanzia pointi 1 mpaka pointi 4 wakati vyuo vya elimu ya juu vinatumia skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa pointi inayoanzia pointi 4 mpaka pointi 1. Hivyo, skeli inayotumika katika ngazi za chini imepinduliwa kichwa chini miguu juu, katika ngazi za juu za elimu.

Tisa, gredi ya ufaulu iliyo katika mtindo wa herufi (letter score) hubadilishwa na kuwa gredi ya ufaulu iliyo katika mtindo wa pointi za ufaulu (point score).

Kumi, jumla ya pointi za ufaulu wa mwanafunzi hutafutwa kwa kujumlisha pointi alizopata mwanafunzi kwa kila somo alilofanyia mtihani. Idadi hii huitwa Jumla ya Pointi za Gredi, ambayo kwa Kiingereza inaitwa “Grade Point Total” (GPT).

Kumi na moja, wastani wa pointi za ufaulu wa mwanafunzi hutafutwa kwa kugawanya GPT dhidi ya idadi ya masomo yaliyofanyiwa mitihani na mtahiniwa. Wastani huu huitwa Wastani wa Pointi za Gredi, ambayo kwa Kiingereza inaitwa “Grade Point Average” (GPA).

Na kumi na mbili, divisheni ya ufaulu ya mwanafunzi hukokotolewa ama kwa kutumia mfumo wa GPT au mfumo wa GPA kulingana na miongozo iliyopo kwa mujibu wa sera za serikali au sera za taasisi nyingine husika.

Hitimisho na mapendekezo

Kutokana na yaliyojadiliwa hapo juu, mambo kadhaa yanafuata kimantiki. Kwanza, kuna skeli tatu tofauti zinazotumika katika kukokotoa kiwango cha ufaulu wa mtahiniwa. Yaani, skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa asilimia, skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa herufi, na skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa pointi.

Pili, taasisi za kielimu zinatofautiana kuhusu idadi ya herufi zilizo katika skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa herufi. Kwa mfano, idadi ya herufi zilizo katika skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa herufi inayotumika katika vyuo vingi vya elimu ya juu ni saba [A, B+, B, C, D, E, na F].

Skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa herufi inayotumika katika elimu ya sekondari, kati ya kidato cha tano mpaka kidato cha sita, inazo herufi sita [A, B, C, D, E, na F].

Na skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa herufi inayotumika katika elimu ya sekondari, kati ya kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne, inazo herufi tano [A, B, C, D, na F]. Kunakosekana ulinganifu (uniformity) hapa.

Tatu, mipaka ya madaraja ya ufaulu kwa kuzingatia herufi yaliyopo kati ya asilimia sufuri mpaka asilimia mia moja, inatofautiana katika ngazi tofauti za elimu hapa nchini. Kidato cha kwanza mpaka cha nne wanayo mipaka yao; kidato cha tano mpaka cha sita wanayo mipaka yao; na vyuo vya elimu ya juu vinayo mipaka yake kwa kila daraja la kiherufi. Kunakosekana ulinganifu (uniformity) hapa pia.

Nne, skeli za kutunuku ufaulu kwa mtindo wa pointi zinatofautiana kutoka ngazi moja ya elimu mpaka ngazi nyingine. Kwa mfano, shule za sekondari zinatumia skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa pointi inayoanzia pointi 1 mpaka pointi 4 na vyuo vya elimu ya juu vinatumia skeli ya kutunuku ufaulu kwa mtindo wa pointi inayoanzia pointi 4 mpaka pointi 1.

Hivyo, skeli inayotumika katika ngazi za chini imepinduliwa kichwa chini miguu juu, katika ngazi za juu za elimu. Kunakosekana ulinganifu (uniformity) hapa pia.

Tano, kuna njia mbili za kukokotoa divisheni ya ufaulu ya mtahiniwa. Yaani, mfumo wa GPA na mfumo wa GPA. Lakini, mfumo wa GPT ukitumika mahali, basi mfumo wa GPA hautatumika, na kinyume chake ni kweli.

Sita, kuna utofauti, kati ya mifumo hii ya GPT na GPA. Kwa mfano, mfumo wa GPT unazo hatua chache zaidi kuliko mfumo wa GPA.

Saba, mfumo wa GPT ni sehemu ya mfumo wa GPA. Yaani, haiwezekani kukokotoa GPA kabla ya kukokotoa GPT. Kwa maneno mengine, mfumo wa GPT unazo hatua chache zaidi kuliko mfumo wa GPA.

Na nane, kwa kuwa akili ya mwanadamu inaelewa haraka namna ya kutafuta “jumla” kuliko namna ya kutafuta “wastani,” inafuata kimantiki kwamba, mfumo wa GPT ni rahisi kueleweka kwa wadau wa elimu kuliko mfumo wa GPA.

Kwahiyo, tatizo lililo mbele yetu sio ama GPT au GPA. Ni tatizo kubwa zaidi kama tukizingatia utata uliomo katika mchakato mzima wa kutathmini maendeleo ya mwanafunzi.

Kuna haja ya kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhusu sera yetu inayoongoza mambo haya, ambao utazalisha mwafaka wa kitaifa katika sekta ya elimu. Lakini pia, mjadala wa aina hiyo utazalisha maarifa sahihi ndani ya jamii kuhusu namna wanafunzi wetu wanavyopimwa kitaaluma.
  • Imeandikwa na Deusdedit Jovin

NW, Dk Kigwangalla aagiza kufungwa chumba cha upasuaji hospitali ya Sanitas


Naibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameagiza kufungwa mara moja Chumba cha upasuaji cha hospitali ya Sanitas ya Mikocheni Jijini Dar es Salaam baada ya kubaini kuwa na kasoro mbalimbali ikiwemo mfumo na ramani yake kimefungwa kwa kutokidhi vigezo vya kimataifa vya namna chumba hicho kinavyotakiwa kuwa.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo mapema jana Februari 29.2016, alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye hospitali hiyo majira ya saa nane na nusu mchana ambapo baada ya kutembelea hospitali nzima na kushuhudia namna ya utolewaji wa huduma, hakuridhishwa na hali aliyokutana nayo kwenye chumba hicho na kutoa maagizo kwa Msajili wa Hospitali Binafsi, Dkt. Pamela Sawa kufunga chumba hicho mpaka uongozi wa hospitali hiyo utakapofanya marekebisho ya mapungufu yaliyopo.

“Chumba cha upasuaji hakiko sawa, siwezi kuvumilia kuacha chumba hiki kiko chini ya kiwango cha kimataifa. Rekebisheni chumba hiki kwa kutumia mfumo wa ramani wa wizara,” alieleza Dkt. Kigwangalla wakati wa kutoa maagizo kwa mmoja wa Ofisa wa Hospitali hiyo.

Aidha uongozi wa hospitali hiyo umepewa siku saba wawe wamewasilisha maelezo ya kutowalipa mishahara kwa kipindi cha miezi minne watumishi wake pamoja na jinsi wanavyoteketeza taka hatarishi za hospitali hiyo.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri huyo alipata malalamiko kutoka kwa watumishi hao ambao wamelalamikia kukatwa kwa makato ya mafao pasipo kupelekwa mahali husika kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu.

Dkt. Kigwangalla alivitaja viwango vya chumba cha upasuaji kuwa kinatakiwa chumba cha kubadilishia mavazi,kunawa mikono,sehemu ya alama maalum zenye rangi nyekundu, meza ya upasuaji, ukanda wa usafi, chumba cha mapunziko baada ya kutoka kwenye upasuaji na chumba cha kusafishia vifaa vya upasuaji na kuna mashine maalum kwa kuwa kila upasuaji una idadi ya vifaa vinavyotumika.

Aliongeza kuwa viwango hivi vinawekwa ili kuepuka maambukizi.

Kwa upande wake Meneja Uendeshaji wa hospitali hiyo, Bi. Gean Cabral alisema watarekebisha mapungufu yaliyobainika pamoja na kufanya yale yote waliyoagiziwa baada ya tukio hilo.

Tazama MO tv, kuangalia tukio hilo hapa:

Imeandaliwa na Magreth Kinabo, (MAELEZO), Andrew Chale, Modewjiblog/MO tv)


Naibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla (katikati) akipata maelezo machache kutoka kwa Meneja uendeshaji wa Hospitali ya Sanitas, Bi. Gean Cabral wakati walipowasilia katika ziara hiyo.
Dk Kigwangalla akikagua baaadhi ya sehemu katika hospitali hiyo.
Dk. Kigwangalla akizungumza na baadhi ya wagonjwa (hawapo pichani) namna Serikali ya Rais Magufuli inavyofanya kazi kwa kusimamia haki na usawa ikiwemo kufika katika maeneo yenye kero na kuchukua hatua ilikumuokoa Mwananchi katika kupata haki yake na huduma bora anayostahiki.

Dk. Kigwangalla akitoa maagizo hayo kwa Meneja uendeshaji wa hospitali hiyo, Bi. Gean Cabral

Dk. Kigwangalla akimuonesha moja ya 'karatasi' iliyoandikwa ujumbe mbalimbali dhidi ya madai kutoka kwa wafanyakazi wa Hospitali hiyo.

Meneja Uendeshaji wa Hospitali hiyo Bi. Gean Cabral akifafanua jambo pamoja na Naibu Waziri wakati wa ziara hiyo..

Dk Kigwangalla akiangalia namna hali ya maabara ya hospitali hiyo licha ya kuwa na vifaa vya kutosha, lakini imeshindwa kuweka mpangilio mzuri unaotakiwa kutumika katika mahabara. ikiwemo suala la usafi


Naibu Waziriwa Afya, Dk. Kigwangalla (kushoto), Msajili wa Hospitali Binafsi pamoja na maafisa wengine akiwemo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dk. Aziz (kulia) wakijadiliana jambo muda mfupi baada ya kumalizika kwa ziara hiyo ya kushtukiza kuangalia namna ya uendeshaji katika huduma za Sekta za Afya, zikiwemo za Serikali na zile za watu binafsi. 
  • Imeandaliwa na Andrew Chale, MODewji blog/MO tv

Taarifa ya habari ChannelTEN, Februari 29, 2016
Halima Mdee akosa dhamana


Mbunge wa Kawe, Halima Mdee akiwasili katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tuhuma za shambulio, mbunge huyo alikosa dhamana na anashikiliwa na Jeshi la Polisi. (Picha na Francis Dande)

Halima Mdee (katikati) akiwa na mbunge wa Bunda, Ester Bulaya (wa pili kushoto) pamoja na wafuasi wa Chadema wakati akielekea mahabusu.


Mbunge wa Kawe, Halima Mdee akisindikizwa na Ofisa wa Polisi aliyeshika faili kuelekea mahabusu baada ya kukosa dhamana katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam leo.

Mwanasheria wa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Prof. Abdallah Safari akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, baada ya mbunge huyo kukosa dhamana.

Tangazo la kupotea Said Abdallah Ismail: Ombi la maalbino kwa Bunge na Serikali


Taarifa ya EWURA kwa umma kuhusu ombi la TANESCO kurekebisha bei


TAARIFA KWA UMMA: MAOMBI YA TANESCO YA KUREKEBISHA BEI ZA UMEME- WITO WA KUKUSANYA MAONI YA WADAU

FEBRUARY 26, 2016

Mnano tarehe 24 Februari 2016, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ilipokea ombi toka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) la kutaka mabadiliko ya bei ya umeme kwa miaka miwili kuanzia tarehe 1 Aprili 2016.

Kwa mujibu wa kifungu Na. 19(2) (b) cha Sheria ya EWURA, Sura Na. 414, Mamlaka inaanzisha mchakato wa kupata maoni ya wadau ili kujua uhalali wa maombi ya nyongeza ya bei za huduma iliyoyapokea kutoka TANESCO.

Kwa taarifa zaidi, soma nyaraka zifuatazo;
Chanzo cha taarifa ni tovuti ya EWURA

Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam - Yaliyojiri katika "Mada Moto" ya ChannelTENLalamiko la Bi Tatu lasababisha WM Majaliwa aagize Daktari mtuhumiwa asimamishwe kazi

Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akizungumza na Waganga, Wauguzi na wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara wakati alipoitembelea Februari 29, 2016.
  • Ni baada ya kudai rushwa ya sh. 100,000/- kumfanyia upasuaji mgonjwa
  • Mama alilazimika kuuza shamba ili apate fedha za kumtibia baba yake
  • Aagiza maduka ya dawa nje ya hospitali hiyo yafungwe leo hii
  • Amwagiza RAS aitishe kikao cha watumishi wote leo saa 9 alasiri


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kusimamishwa kazi kwa Dk. Fortunatus Namahala wa kitengo cha upasuaji katika hospitali ya Ligula ambayo ni hospitali mkoa wa Mtwara kutokana na tuhuma za kumdai mgonjwa rushwa ya sh. 100,000/-.

Pia ametoa agizo la kufungwa kwa maduka yote ya dawa yaliyo nje ya hospitali hiyo kuanzia leo na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Alfred Luanda asimamie zoezi hilo mara moja.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Februari 29, 2016) kwenye kikao cha watumishi wa hospitali hiyo alichokiitisha baada ya kutembelea maeneo kadhaa ya hospitali hiyo na kupokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa na ndugu wenye wagonjwa waliolazwa.

Mara baada ya kuwasili, Waziri Mkuu aliamua kwenda mojamoja mapokezi badala ya wodini kama alivyopangiwa na kuuliza maswali ni kwa nini wana dirisha moja la kupokelea wagonjwa wote. "Dirisha la wazee lipo?" akajibiwa hakuna. "Dirisha wa watu wa Bima ya Afya (NHIF) lipo" nalo pia akajibiwa halipo. "Je wazee wana daktari wao", hakupata jibu. 

"Mganga Mkuu ni kwa nini hujatenga dirisha la wazee wakati haya maelekezo yalishatolewa siku nyingi? Tengeni dirisha la wazee na uhakikishe wana daktari wao. Siyo kuwaleta huku ili waje kusukumana na wagonjwa vijana," alisema wakati akimwagiza Mgaga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Shaibu Maarifa. 

Akiwa njiani kuelekea wodi aliyopangiwa kuiona, Waziri Mkuu alikutana na kundi la wagonjwa waliokuwa wakiimba "tuna jambo, tuna jambo" wakiashiria kutaka kusikilizwa. Kati ya wauguzaji watatu aliowasikiliza, Waziri Mkuu alipokea kero za kuuziwa dawa kwa bei za juu kwenye maduka ya dawa binafsi, lugha mbaya za madaktari na wauguzi, uchafu wa vyoo na uhaba wa maji.

Lakini kero ya Bi. Tatu Abdallah aliyelazimika kuuza shamba la baba yake ekari 2.5 ili apate fedha za kulipa gharama za kufanya upasuaji kwenye hospitali binafsi baada ya baba huyo kutimuliwa kutoka hospitali ya Ligula ndiyo ilimgusa zaidi Waziri Mkuu.

"Februari Mosi nilimleta baba yangu hapa nikaambiwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji. Nikaandikiwa ninunuue dawa za sh. 85,000/- hapo nje (pharmacy haikumbuki jina) pia uzi wa kushonea kwa sh. 25,000/-. Lakini pia daktari akasema anataka sh. 100,000/- ya kwake. Lakini hadi Februari 7 hakufanyiwa huo upasuaji."

"Tarehe 12 Februari baba alitolewa wodini na kuambiwa arudi tarehe 16 Februari. Niliumia sababu kijiji tunachotoka ni mbali na hali ya baba ilizidi kuzorota. Ndipo baba akaniambia nirudi kijijini kwetu Kilomba nikauze ekari 2.5 za shamba lake ili tulipie matibabu. Niliuza na kumpeleka baba katika zahanati ya Sajora. Huko nililipa sh. 560,000/- na baba akafanyiwa upasuaji sasa hivi yuko nyumbani".

"Leo nataka huyu daktari aje achukue boksi hili la dawa alizoniandikia na pia anirudishie hela yangu iliyopotea bure. Mie sijazitumia, ni kwa nini aliniandikia wakati baba hajampa huduma yoyote?" 

Alipoulizwa kama anaweza kumtambua akimuona, mama huyo alikiri kuwa anaweza. 

Waziri Mkuu alitembelea pia wodi ya akinamama waliojifungua na kukuta wakiwa wametandikiwa shuka moja na wagonjwa kulazimika kuweka khanga juu ya mipira wanayolalia wodini ambayo pia wanaambiwa wajinunulie kabla ya kwenda hospitali kujifungua.

Akiwa njiani kuelekea theatre, Waziri Mkuu alipata kilio cha wagonjwa wengine ambao walisema hospitali hiyo haina maji, choo kinachotumika ni kimoja na kwamba usafi umefanyika leo waliposikia kuwa atatembelea hospitali hiyo. 

Akiwa katika kikao na watumishi hao, Waziri Mkuu aliwainua madaktari wote ili wajitambulishe ndipo akamuomba mama aliyedaiwa rushwa aende kumshika mkono daktari mhusika.

"Gwaride la utambuzi ni jambo la kawaida. RPC hakikisha huyu mama hasumbuliwi. Lakini leo nitaanza na huyu Daktari kwa sababu rushwa haivumiliki. RAS simamia suala lake lakini pia shirikiana na TAKUKURU na Polisi kufanya uchunguzi wa jambo hili hadi mwisho," alisema. 

Kuhusu madai na stahili za watumishi, Waziri Mkuu amemwagiza RAS, RMO na Afisa Utumishi wa mkoa wafanye kikao na watumishi wote wa hospitali hiyo leo saa 9 alasiri na kisha wamletee taarifa.
Kabla ya kufikia uamuzi wa kumsimamisha Dk. Namahala, Waziri Mkuu alitumia muda mwingi kuwaelezea watumishi hao jinsi walivyo na umuhimu katika huduma zao na kwamba nafasi yao ni nyeti kwa maisha ya binadamu hivyo wanapaswa kuwa na huruma na siyo kuwaumiza wananchi wa kipato cha chini ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu. 

Aliwataka waache tabia ya kuwatoza fedha watoto wanaolazwa hospitalini hapo na wanawake wanaojifungua kwani wanapaswa kutibiwa bure kwa mujibu wa sera ya Serikali.

Sakata la hospitali ya Ligula lilianza juzi (Jumamosi, Februari 27, 2016) wakati Waziri Mkuu akiwahutubia mamia ya wakazi wa Mtwara kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mashujaa ambapo baadhi yao walikuwa wakichomekea kuwa aende hospitalini hapo kwa kuwa kuna majipu ya kutumbua. 

Waziri Mkuu aliwajibu kuwa amesikia ujumbe wao na ataenda huko lakini alishindwa kutokana na ratiba za siku hiyo kumalizika jioni sana. 
 
Waziri Mkuu amerejea Jijini Dar es Salaam mchana huu.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMATATU, FEBRUARI 29, 2016.Wamawake wakiwa wametandika khanga kwenye wodi ya wazazi ya Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Februari 29, 2016.Waziri Mkuu, Kassim majaliwa alitembelea wodi hiyo na kukemea mtindo huo akiwataka wauguzi na waganga kutandika mashuka yahospitali ambayo alisema ana taarifa kuwa yapo ili kuepusha hatari ya wananwake hao kubeba magonjwa kupitia kahanga hizo watokapo hospitalini hapo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea hospitali ya Mkoa wa Mtwara Februari 29, 2016. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Halima Dendego na kulia Ni Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt.Shaibu Maarifa.

Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akizungumza na Waganga, Wauguzi na wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara wakati alipoitembelea Februari 29, 2016.Baadhi ya Wauguzi na Madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao hospitalini hapo Februari 29, 2016. (picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim majliwa akitoa agizo la kusimamishwa kazi Daktari wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Fortunatus Namahala (kulia) baada ya kutajwa kuwa alidai rushwa ya sh.100, 000/= ili aweze kumtibu baba mzazi wa Tatu Abdallah (wapili kulia) wakati alipoitembelea hospitali hiyo Februari 29, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akiagana na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Shaibu Maarifa kwenye uwanja wa ndege wa Mtwara kabla ya kurejea Dar es slaam Februari 29, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim majaliwa akitazama ngoma kwenye uwanja wa ndege wa Mtwara kabla ya kuondoka kurejea Dar es salaam Februari 29, 2016.

NW aagiza Shine Care Pharmacy kufungwa

Naibu Waziri wa Afya Dk. Kigwangalla akitoka katika duka hilo la dawa baada ya kuagiza kulifunga


NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangalla ameagiza kufungwa kwa Duka la dawa za binadamu la Shine Care Pharmacy lililopo Temeke, baada ya kubainika kuendeshwa kinyume cha sharia ikiwemo kutokuwa na kibali cha uendeshaji na mfamasia husika.

Dk. Kigwangalla ambaye aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Mfamasia Mkuu wa Serikali pamoja na msajili wa Baraza la famasia nchini na maafisa wengine, ambapo katika tukio hilo mapema leo Februari 29.2016, walikuta madawa mbalimbali yaliyokwisha muda wake na yale ambayo hayatakiwi kuuzwa katika duka kama hilo.

Aidha, Dk. Kigwangalla akitoa agizo la kufungwa kwa duka hilo, ameagiza kuchukuliwa hatua ikiwemo kupelekwa Mahakamani mara moja il iwe fundishi na kwa maduka mengine yenye kufanya hivyo.

Kwa upande wake, Mfamasia wa Serikali, Bw. Henry Irunde amebainisha kuwa, dawa hiza za binadamu zilizokutwa hazifai kuuzwa katika maduka hayo na pia duka ambalo linaendeshwa bila kuwa na Mfamasia ni kinyume na sharia kwani watumiaji wakitumia dawa bila kuwa na maelezo ya kutosha kutoka kwa mtaalam wa dawa zinaweza kusababisha usugu kwa mwili wa binadamu n ahata kumsababishia matatizo.

Duka hilo la dawa ambalo lipo hatua chacche kutoka Hospitali ya Temeke, ni miongoni mwa maduka makubwa ya dawa za binadamu ambapo pia wachunguzi ha wa madawa ya binadamu walibaini kuwa milango mingi zaidi kinyume na ile inayotakiwa kuwa kwa maduka ya dawa hali ambayo walitilia mashaka huenda vitendo vingine vya kutoa huduma vinatumika licha ya kuwa milango hiyo ilifungwa kwa kile kilichoelezwa kuwa wahusika hawakuwapo.

Dk. Kigwangalla amebainisha kuwa, zoezi hilo la kukagua maduka ya dawa ni la nchi nzima na watazunguka nchi nzima kufanya ukaguzi huo bila kutoa taarifa hivyo kwa yeyote atakaekutwa anaendesha kinyume cha sharia atachukuliwa hatua stahiki.

Mmoja wa maafisa wa TFDA, akikagua dawa katika duka hilo
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigwangalla akiwaonyesha waandishi wa habari cheti cha Famasia kilichoisha muda wake huku akiendelea na biashara yake hiyo kinyume na sheria.
Baadhi ya maafisa walioambatana na Naibu Waziri wa Afya. Dk Kigwangalla wakimsikiliza kwa makini, Dk. Kigwangalla (hayupo pichani) wakati wa tukio hilo.
Naibu Waziri wa Afya, Dk.Kigwangalla akiongea kwa njia ya simu na mmiliki wa duka hilo la Shine Pharmacy , Abraham Mathayo...ambaye alieleza kuwa yupo Mkuranga, hivyo waliamua kuongea naye kwa njia ya simu kwa nini anaendesha duka bila ya kutokuwa na vibali.
Mfamasia Mkuu wa Serikali Henri Irunde, akitoa taarifa yake ya ukaguzi katika duka hilo kwa wanahabari na Naibu Waziri wa Afya Dk. Kigwangalla (Hayupo pichani).
Naibu Waziri Dk. Kigwangalla akitoa maagizo hayo ya kufungwa kwa duka hilo.
  • Imeandaliwa na Andrew Chale.

Tangazo la msiba wa Dk Kisamo

Dk Kisamo
Mrs Elipina Kisamo Mlaki na Linda Kisamo wanasikitika kutangaza kifo cha baba yao mpendwa Dr Michael Kisamo aliyefariki Jumapili 28/2/2016.

Mipango ya Mazishi inafanyika Nyumbani kwake Kinondoni Mkwajuni/Sokoni Magengeni. na Mazishi yanataraji kufanyika Usangi Jumatano 2.03.2016.

Bwana Alitoa na Bwana Ametwaa jina lake lihimidiwe

Ahsante kwa Ushirikiano.

Taarifa ya Bodi ya Utalii: Olduvai Gorge iko Tanzania


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

OLDUVAI GORGE IKO TANZANIA SI KENYA


BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imekuwa ikifuatilia kwa makini majadiliano yanayoendelea katika mitandao mbalimbali ya kijamii kufuatia video iliyotumwa katika YouTube
https://www.youtube.com/watch?=iveX49WE7fw na imekuwa ikisambazwa kupitia njia mbalimbali za habari ikimuonesha mtu mmoja kutoka nchi jirani akisema kuwa Olduvai Gorge ambayo kimsingi iko Tanzania kwamba iko Kenya.

Video hii imeibua majadiliano katika mitandao ya kijamii baina ya watanzania na watu wengine ambao wanaitakia mema Tanzania na wanaoelewa vizuri kuwa Olduvai Gorge iko Tanzania.

Bodi ya Utalii Tanzania kama taasisi ya Umma yenye jukumu la kuvitangaza vivutio vyetu vya utalii imeshtushwa na video hii iliyojaa upotoshwaji mkubwa ambao tunaamini mbali ya malengo mengine inalenga kuchafua kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na Bodi kwa kushirikiana na wadau wengine katika kutamgaza vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwemo Olduvai Gorge.

Tunapenda kuchukua fursa hii kupinga vikali upotoshwaji huu uliofanywa na mtu huyo wakati akihutubia mkutano ambao tumeambiwa ulikuwa ni wa Vijana wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Amerika mwezi Agosti mwaka jana. Tunapenda dunia ifahamu kuwa kama ilivyo kwa Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Zanzibar n.k Olduvai Gorge mahali panapoaminika kuwa ndipo binadamu wa kwanza duniani aliishi na ambako Dr. Louis na Mary Leakey waligundua fuvu la binadamu huyo wa kale anayesadikiwa kuishi miaka takribani milioni 2 iliyopita iko pia Tanzania na si mahali pengine popote duniani. Eneo hili la Olduvai Gorge liko katika bonde la ufa katikati ya bonde la Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Manyara nchini Tanzania.

Tunatoa wito kwa watanzania mahali popote walipo kuendelea kuunga mkono juhudi za Bodi ya Utalii Tanzania za kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya Utalii kwa kujibu na kusahihisha papo hapo bila woga mara tu taarifa ya upotoshaji kuhusu nchi yetu inapotolewa iwe ni kwenye mikutano ya ndani ya nchi au ya Kimataifa. Tunaamini kuwa ni jukumu la kila mtanzania kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya Utalii badala ya kuiachia TTB kazi hii peke yake.

Yawezekana katika mkutano huo wa vijana ambao mjumbe huyo wa nchi jirani alipata fursa ya kuzungumza na kufanya upotoshaji huzo, wajumbe wa Tanzania pia walikuwepo ambao wangweza kukosoa upotoshaji huo papo hapo na kuelezea ukweli na usahihi wa mahali ilipo Olduvai Gorge.

Imetolewa na:

Ofisi ya Uhusiano

BODI YA UTALII TANZANIA