Waziri aandaa mkataba wa kazi kwa idara; Aonya matumizi ya 'internet kwa matumizi ya hoyo'Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasialino, Profesa Makame Mbarawa, amewaweka roho juu watendaji wa Wizara yake kwa kuwaandalia mkataba wa malengo ya kiutendaji.

Mbarawa amesema Wakuu wa Taasisi na Idara zote za Wizara hiyo wataingia mkataba ikiwa ni hatua ya kuongeza ufanisi wa kazi kwa watumishi wa umma na atakayeshindwa kufikia malengo atafungashiwa virago.

Profesa Mbarawa alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na watumishi na wakuu wa Idara wa Wizara hiyo kutoka taasisi 29 ambapo aliwataka kila mtumishi kutumikia vyema nafasi yake na kuhakikisha anatambua wajibu wake wa kujenga miundominu imara na kufikia lengo la kuwa uchumi wa kati ifikapo 2020/2025.

Alisema kwa kuanza wamekubaliana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kukusanya Sh. trilioni moja badala ya Sh. bilioni 652 walizopanga kukusanya na kwamba Wakuu wa Idara watakaoshindwa kutekeleza malengo hayo watafukuzwa kazi.

Waziri alisema nafasi hizo watapewa watu wengine watakaoonekana kuwa na uwezo wa kumudu majukumu hayo na kufikia malengo hayo.

“Tunataka tuwe na mikataba ya kazi baina ya wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi mbalimbali, ili idara itakayoshindwa kutimiza lengo tumhoji na kama sababu zake hazina mashiko atupishe na nafasi yake apatiwe mtumishi mwingine,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema sekta ya Mawasilino pekee ndio walipeleka mikataba yao ya kazi na alitumia nafasi hiyo kuzitaka mamlaka nyingine kutekeleza agizo hilo mara moja.

Profesa Mbarawa pia aliahidi kuwafukuza kazi mara moja watumishi watakaotumia nafasi zao kutoa maagizo ya kusaidia wazabuni katika wizara yake pindi atakapopata taarifa.

Alisema kuna baadhi ya watumishi wa sekta ya manunuzi wamekuwa wakifuta zabuni zaidi ya mara 10 na kuendelea kuzirudisha hivyo aliahidi kuwa atakayebainika tena atamfuta kazi.

“Tangu nimekuwa Wizara ya Mawasiliano kwa miaka yangu yote mitano sikuwahi na wala sitakaa niwahi kupitisha kimemo kwa wakuu wa idara kwa ajili ya kupitisha zabuni hivyo na mimi nikipokea taarifa za mtumishi anayepitisha zabuni kwa namna yoyote ile bila ya kuzishindanisha nitashughulika naye na sitakuwa na huruma hata kidogo nitaondoka naye,” alisisitiza.

Pia aliwasisitizia watumishi hao kuwa na uadilifu kazi na kila mtu kutekeleza majukumu yake, kuacha tabia ya kutumia huduma za mtandao kwa ajili ya shughuli zao binafsi.

“Hakikisheni mnakuwa waadilifu na muwe na huruma na mali za umma nimepata taarifa kuwa baadhi ya watumishi wanatumia huduma ya mtandao kwa ajili ya matumizi ya ovyo, hakikisheni mnaacha mara moja,” alisema.

Profesa Mbarawa pia alisema ataanzisha utaratibu wa kufanya mkutano na wafanyakazi wote wa wizara hiyo kila baada ya miezi mitatu kwa kutumia televisheni.

Pia alisema wanaandaa utaratibu wa mfumo wa mtandao kwa wakuu wote wa idara utakaowawezesha kupata taarifa za ripoti na mafaili yaliyoko katika ofisi zao ili kuondokana na uzembe wa watumishi wanaokalia mafaili ya watumishi.

Waua mke na mume kwa ujira wa sh 600,000/= za mke mdogoMtu na mkewe, Nyanda Masele na Kwilabya Masasila, wakazi wa kitongoji cha Mawasiliano kijiji cha Mpeta wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma, wameuawa kwa kukatwa mapanga.

Inadaiwa mauaji hayo yalitekelezwa baada ya mke mdogo, Salome Igede, kukodi majambazi kwa Sh.600,000 kuwaua Masele na Masasila.

Akizungumza na Nipashe juzi, mtoto wa marehemu hao, Ngolo Yanda, alisema tukio hilo lilitokea Machi 9, saa 6:00 usiku, katika kitongoji hicho, baada ya watu kadhaa kuvamia chumba cha wazazi wake waliokuwa wamelala na kuwashambulia kwa mapanga hadi kuwaua.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma, Ferdnand Mtui, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema watu watano wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za mauaji, akiwamo mke mdogo wa marehemu na mtoto mwingine wa marehemu.

“Nilisikia mlango unagongwa kwa nguvu na nikasikia kelele na sauti ya mama inaita, Ngolo, Ngolo njoo unisaidie, halafu nikasikia sauti nyingine ikisema tulia wewe na tukawa tunaona tochi zinamulika ndani,” alisema Yanda.

Alisema baada ya muda kimya kikatanda na ndipo akatoka chumbani kwake kwenda chumba cha wazazi ambako alikuta wote wakiwa chini huku damu zimetapakaa kwenye miili yao.

Ndipo alipopiga kelele na kumuita kaka yake Juma Nyanda aliyekuwa amelala nyumba nyingine, alisema.

Naye mtoto wa kiume wa marehemu hao, Nyanda, alisema wakati anaamka baada ya kugongewa mlango na dada yake, alikuta majambazi hao wameshaondoka na akaomba msaada kwa majirani.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpeta, Raphael John, alisema chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina.

Alisema walibaini ni ushirikina baada ya majambazi hao kukamatwa na polisi wa kituo cha Nguruka kisha kukiri kufanya mauaji hayo kwa kukodiwa na mke mdogo wa marehemu kwa Sh.600,000.

“Walijieleza walikuwa wamekubaliana malipo hayo na mke mdogo wa marehemu ambaye alimtuhumu mke mwenzie alikuwa anamloga kwa muda mrefu," alisema John na kuongeza, "Pia walidai aliwahi kuhangaika kubeba mimba ya miaka kumi bila kuzaa.”

Rais Magufuli amebadili protokali ya kuwapokea viongozi

Rais John Magufuli inaelekea amefuta utaratibu wa kupokea marais wenzake ulioonekana kutumiwa mara kadhaa na mtangulizi wake, Jakaya Kikwete, na badala yake ameanza kufuata nyendo za wakuu wa mataifa kadhaa makubwa akiwamo Barack Obama wa Marekani.

Utaratibu unaoonekana kufutwa kwenye awamu hii ya Rais Magufuli ni ule wa kwenda kuwapokea marais wageni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kama ilivyozoeleka wakati wa Kikwete.

Wakati wa awamu yake ya urais, Kikwete alikuwa akienda uwanjani kuwasubiri marais waliokuwa wakiwasili nchini kwa ziara zilizokuwa na malengo mbalimbali.

Baada ya hapo Kikwete aliongozana na wageni wake hao katika msafara hadi Ikulu.

Uchunguzi wa Nipashe wakati wa ujio wa Rais wa Vietnam nchini, Truong Tan Sang, wiki hii umeonyesha kuwapo kwa mabadiliko makubwa katika protokali za kupokea marais.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ndiye aliyemuwakilisha Rais Magufuli kwenda kumpokea Sang.

Hata juzi, Rais huyo alipoondoka baada ya kumaliza ziara yake nchini, Majaliwa ndiye aliyemsindikiza kiongozi huyo kwenda uwanja wa ndege.

Utaratibu huo ni mpya katika protokali za mapokezi ya viongozi wakuu kama Truong, ambaye ni rais wa kwanza kutembelea nchi kwa ziara rasmi ya kiserikali tangu Magufuli aapishwe kuwa Rais Novemba 5, mwaka jana.

Rais Barack Obama wa Marekani amekuwa na utaratibu kama ulioanza kutumiwa na Rais Magufuli ambapo wageni wa kitaifa wa Marekani hupokewa na wasaidizi wake na yeye kuwasubiri Ikulu ya 'White House'.

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, marais wa kigeni ambao wameshakanyaga ardhi ya Tanzania ni pamoja na Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya ambao walikutana naye kwenye mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki uliofanyika mkoani wa Arusha.

Alipoulizwa kuhusu utaratibu huo unaoonekana kuwa mpya wakati wa mapokezi ya marais, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, alikiri kwamba Rais huyo wa Vietnam alipokewa na Waziri Mkuu, Majaliwa na kwamba hakuna tatizo katika hilo kwa sababu ni utaratibu wa kawaida.

“Waziri Mkuu kwenda kumpokea Rais wa Vietnam uwanjani ilikuwa sahihi kabisa kwa sababu ni uamuzi tu nani aende," alisema Msigwa. "Mbona sisi tukienda kwao wakati mwingine Rais wetu anapokewa na Meya au Mkuu wa Mkoa?

"Mapokezi ni mapokezi tu, kule uwanja wa ndege anaweza kwenda yeyote kumpokea isipokuwa hapa Ikulu lazima Rais awepo mwenyewe kumpokea.”

ENZI ZA KIKWETE

Wakati wa utawala wa awamu ya nne ambao pia uliongoza kwa matumizi ya mabaya ya fedha katika kugharimia safari za nje, marais waliokuwa wakiwasili nchini walikuwa wakipokewa na Rais Kikwete kwenye Uwanja wa Ndege, na kuwasindikiza wakati wakiondoka nchini baada ya kumaliza ziara zao.

Ukiacha viongozi wazito kimataifa kama Obama na Rais wa China, Xi Jinping, baadhi ya marais wa mataifa ya kawaida kabisa waliowahi kupokewa na Kikwete walipotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ni pamoja na Rais wa Sri Lanka, Mahinda Rajapaksa, aliyetua nchini Juni 27, 2013.

Wengine ni Rais wa Namibia Hage Gottfried Geingob aliyewasili nchini Oktoba 12, 2015; aliyekuwa Rais wa mpito wa Madagascar, Andry Rajoelina Mei 4, 2013 na Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra Julai 30, 2013.

Mwingine ni Rais Allasane Ouattara wa Ivory Coast ambaye Kikwete alimpokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Mei 29, 2012.

NW aruhusu kuendelea huduma ya 'mortuary' hospitali ya Tumbi baada ya jokofu kutengenezwa
Meya asema Manispaa itaweza kutoa elimu bure bila fedha za serikali ya Magufuli

Taarifa hii iliyonukuliwa kutoka kwenye gazeti la NIPASHE, ilichapishwa katika gazeti la Jumapili, siku ambayo ulisomwa waraka wa Rais Magufuli wa uteuzi wa wakuu wapya wa mikoa, ambapo Said Meck Sadiki amehamishiwa mkoani Kilimanjaro.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, amemtaka Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniphace Jacob, kuacha malumbano ya kisiasa na badala yake ajikite kufanya kazi.

Ushauri wa Sadiki umekuja baada ya Meya Jacob kukaririwa akisema manispaa hiyo ina uwezo wa kukabiliana na uamuzi wa serikali wa kutoa elimu ya bure bila kuhitaji fedha zinazotolewa na utawala wa Rais John Magufuli.

Halmashauri ya wilaya ya Kinondoni inaongozwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao ni mwamvuli unaojumuisha wabunge na madiwani kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF).

Sadiki alisema hahitaji malumbano na kiongozi huyo ambayo hayana tija.

"Mimi sipendi malumbano yasiyo na tija baina ya viongozi," alisema Mkuu wa Mkoa kwa sababu "unapokataa msaada kama huo wa kupunguza mapungufu katika sekta ya elimu, wanaoathirika ni watu waliowachagua."

Serikali imepanga kutumia Sh. Bilioni 137 kugharamia elimu bure katika miezi sita ya kwanza ya Rais wa tano, Magufuli.

Kiasi cha Sh. bilioni 18.77 kilitumwa kwenye akaunti za shule za Msingi na Sekondari za halmashauri zote hapa nchini na vyombo vya usimamizi wa mitihani kwa kila mwezi wa Januari na Februari, kwa ajili ya wanafunzi kusoma bure.

Pesa zilizogawanywa kwenye akaunti za shule za Msingi na Sekondari katika halmashauri zote ni Sh. bilioni 15.7 kila mwezi na Sh. bilioni 3 kila mwezi kwenye akaunti vyombo vya usimamizi wa mitihani katika Halmashauri zote hapa nchini.

Mkuu wa Mkoa alisema fedha hizo zitapelekwa katika Manispaa zote na amdetoa agizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kutumia fedha hizo katika matumizi yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

Sadiki alisema kwa sababu Rais Magufuli ni kiongozi wa wote, ana haki ya kutoa kwa wote bila kuzuia wala mipango yake kukataliwa.

"Yule ni mkuu wa nchi, hata kama wanakusanya fedha za kutosha, zipo taratibu za matumizi ya fedha hizo," alisema Sadiki.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mipango wakati akitoa taarifa ya kuanza kwa utumaji wa fedha za elimu bure Januari 6, mwaka huu, walimu wakuu wa shule zote za Msingi na Sekondari katika halmashauri zote hapa nchini wanatakiwa kuweka wazi matumizi ya fedha hizo katika mbao za matangazo kwa kila shule, ili kila mzazi aweze kujua kiasi gani kimetumika.

Sadiki alikuwa akizungumza wakati akipokea msaada wa ahadi ya ujenzi wa madarasa 12 katika mkoa wa Dar es Salaam kutoka kwa Wamiliki wa Malori Tanzaznia (TATOA), yenye thamani ya Sh. milioni 300.

Mkoa wa Dar es Salaam, alisema Sadiki, una upungufu wa vyumba vya madarasa 7,223, lakini pia uhitaji wa madawati 66,000.

"Yapo maeneo mengi ya kujenga shule, nawaomba wadau wetu muendelee kuhamasisha kupata shule nzima kwani shule nzima inahitaji madarasa kuanzia 22," alisema.

Taarifa ya habari ChannelTEN, Machi 13, 2016

Waziri aagiza Makatibu Wakuu wa Wizara kuweka daftari la kusajili zawadi

MAKATIBU Wakuu wameagizwa kuanzisha daftari la kusajili zawadi kwenye wizara zote, kuhakikisha utumishi wa umma unakuwa na uadilifu. Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki kwenye semina ya watendaji hao iliyofanyika jana Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye ufunguzi, Kairuki alisema kusajili zawadi kutasaidia kufanya tathmini ya zawadi ambazo mtumishi wa umma anapokea kutoka kwenye jamii na kuangalia kama ziko ndani ya sheria au la.

Semina hiyo ya siku moja ya maadili kwa makatibu na manaibu wao, iliandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Umma ikilenga kuwajengea uwezo katika suala zima la maadili na uwajibikaji.

Alisema baadhi ya watumishi waandamizi bado wanashawishi kupokea au kukubali, kuhamishiwa mali zenye maslahi ya kiuchumi zaidi ya kiwango kinachokubalika kinyume na Kifungu cha 12 cha Maadili ya Viongozi wa Umma ambacho kinaelekeza kiwango kinachokubalika ni Sh 50,000.

“ Hali hii inaweza kutatuliwa kwa kuanzisha daftari la kusajili zawadi ambalo litasaidia kubainisha viongozi ambao wanapokea zawadi au kitu kidogo na kuona kama zawadi hizo zinatangazwa kwa maofisa masuuli kama inavyotakiwa kisheria,” alisema.

Alisisitiza kwamba, Sheria iko wazi kuwa kiongozi wa umma, anayepokea zawadi yenye thamani inayozidi Sh 50,000, anatakiwa kuitangaza na thamani na kuwasilisha kiapo hicho kwa ofisa masuuli ambaye ataamua matumizi yake.

Kamishna wa Sektretarieti ya Maadili ya Umma, Jaji mstaafu Salome Kaganda alisema tangu ateuliwe, hakuna kiongozi yeyote kutoka serikali, Bunge au Mahakama ambaye ameshatangaza zawadi aliyopokea.

“Hakuna kiongozi yeyote aliyetangaza zawadi alizopokea, ingawa tumekuwa tukishuhudia viongozi wengi wakipokea kitu kidogo, zawadi na kuhamishiwa mali za kiuchumi,” alisema.

Jaji Kaganda aliwataka makatibu na manaibu wao kuchukua hatua za kuzuia wanapofanya kazi na watu mbalimbali, hususan wanasiasa. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi amewataka makatibu na manaibu wao kuhakikisha wanazingatia kanuni za maadili.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi ambao wana utovu wa nidhamu. “Sitakuwa na furaha kuona mtu yeyote kati yenu anakuwa wa kwanza kumtumbua jipu, kwa wewe kuwa salama unapaswa kufanya kazi zaidi na kuhakikisha unazingatia maadili na uadilifu,” alisema.

USA Presidential Election Politics 2016: Why is March 15 a big deal?

March 15th, 2016 could be decisive for both parties - Republican (GOP) and Democratic Party. 

More than 1,000 delegates are up for grabs — and the results will be pivotal.

It's also the day when the contest rules change for the Republicans. States can start to pick how they want to award their delegates. For both Florida and Ohio, that means winner-take-all - the biggest prizes on the GOP side are the winner-take-all states. On the Democratic side, which still awards delegates proportionally, it's Florida and Illinois, followed by Ohio.

The NPR puts it this way...

What's at stake for Republicans?

If Donald Trump sweeps the winner-take-all states of Ohio and Florida, it could be a wrap party for his nomination as the Republican standard-bearer.
To be clear, Trump won't mathematically clinch Tuesday even with wins in both places. But the odds that anyone else could go into the convention with a majority — or even most — of the delegates would be almost impossible. It will mean the only way Trump wouldn't be the nominee is if he's stopped at a historic and chaotic brokered convention.

As it stands now, Trump is favored in both Florida and Ohio, but Marco Rubio and John Kasich are hoping their respective home states put them over the top. There is some evidence of momentum for Kasich in Ohio, where he's a popular governor. One poll showed him in the lead this past week. Rubio's campaign is even telling people to vote for Kasich in Ohio, following a plan laid out by Mitt Romney designed to try and stop Trump from getting a majority before the convention.

Florida has been trending the other direction, with Trump favored. Rubio is running zero ads, and Ted Cruz has made a late play in the state. If Rubio loses Florida, it's likely lights out for his campaign. If Kasich loses Ohio, his chances of winning the nomination are severely diminished from what's already something unlikely to happen. It could also be the end of his candidacy, considering the next contest where he could contest wouldn't be for three weeks in Wisconsin.

Side note: Don't overlook the contests in Illinois, Missouri and North Carolina, which, combined, actually have more delegates than Florida and Ohio put together. Since they are not winner-take-all, though, no one is going to net the margins there that they could in either Florida or Ohio.

What's at stake for Democrats?

These are the first major contests following Bernie Sanders' surprise win over Hillary Clinton in Michigan. It was apparently the biggest polling upset in history. It also showed Sanders can win in a big, diverse state.

But it didn't change one thing — the math. Clinton remains the favorite for the nomination because of her delegate lead and because Democrats award delegates on a proportional basis. Despite the potentially narrative-changing win in Michigan, Sanders woke up further behind, because Clinton had won such a huge margin in Mississippi. Sanders now needs 54 percent of remaining pledged delegates for a pledged-delegate majority. With superdelegates factored in, he needs 60 percent.

Math aside, Tuesday is important, though. If Sanders can pull off more surprise wins in these big states, Clinton will look vulnerable. Superdelegates could switch their allegiance, and Clinton will have her back against the wall. The last thing she wants is to limp to the nomination. She needs to show strength Tuesday.

Sanders believes, after Michigan, that his message on trade has resonance in the Upper Midwest, meaning states like Illinois and Ohio could line up well for him.

One thing already appears clear, however — no one on either side is going to get a majority of delegates for months.

GSM yadhamini ujenzi wa jengo la upasuaji Mwanayamala

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (katikati), ambaye mchana huu Rais Dk. John Magufuli amemteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa jengo la upasuaji katika Hospitali ya Mwananyamala Dar es Salaam leo. Kutoka kulia ni Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Azizi Msuya, Mwakilishi wa Kampuni ya GSM, Deogratias Ndejembi ambao watajenga jengo hilo na kushoto ni Mhandisi, Hersi Said kutoka GSM ambaye atasimamia ujenzi wa jengo hilo
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amezindua ujenzi wa jengo la upasuaji katika Hospitali ya Mwananyamala ambalo litakuwa maalumu kwa ajili ya utoaji wa huduma za upasuaji kwa wajawazito na wagonjwa wengine wadharura.

Jengo hilo ambalo ujenzi wake utaanza rasmi kesho, litakuwa na vyumba maalumu kwa ajili ya upasuaji, uangalizi maalumu kwa ajili ya wagonjwa wadharura (ICU) na uangalizi baada ya upasuaji na vingine kwa ajili ya utawala na huduma nyinginezo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Dar es Salaam leo mchana DC Makonda alisema kuwa jengo hilo litakuwa mahususi kwa ajili ya kupunguza idadi ya wagonjwa ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji kwenda Hospitali yaTaifa ya Rufaa yaMuhimbili.

“Kupitia jengo hili wajawazito wote na wagonjwa wengine ambao wanahitaji upasuaji watapatiwa huduma hiyo hapa hapa Mwananyamala.

Alisema jengo hilo litakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa 350-360 hivyo kwa kiasi kikubwa tutakuwa tumepunguza msongamano Muhimbili.

Pia utakuwa tumefanikiwa kuokoa maisha ya wajawazito ambayo yameku wa yakipotea kutokana na kuchelewa kupata tiba,” alisemaMakonda.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa yaKinondoni, Dk. Azizi Msuya alisema jengo hilo litasaidia kuokoa maisha ya wajawazito na wagonjwa wengine ambao wamekuwa wakifariki kutokana na kucheleweshewa kupata huduma hizo.

“Katika wajawazito 100,000 wanaojifungua, 447 wanapoteza maisha. Sasa kupitia uwepo wa huduma ya upasuaji katika hospitali hii ya Mwananyamala tutajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kuokoa maisha ya wajawazito hao wanaofariki” alisemaDkAzizi.

Mwakilishi wa Kampuni ya GSM Foundation ambao ndiyo wafadhili wa ujenzi wa jengo hilo, Deogratias Ndejembi alisema kuwa kampuni hiyo imeamua kufadhili ujenzi huo ili kuokoa maisha ya watanzania ambao wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosa huduma ya upasuaji na pia kutokana nakuguswa na juhudi za DC Makonda.

“Kama GSM tumeamua kugharamia ujenzi wa jengo hili la upasuaji ili kuokoa maisha ya wanawake, watoto na jamii nyingine ambayo imekuwa ikipoteza maisha kwa kukosa upasuaji. Pia juhudi na uchapaji kazi wa DC Makonda.

Amekuwaakifanyakazikwajuhudikubwa, hivyo tukaona ni vyema tuka muunga mkono” alisema Deogratias Ndejembi.


Ukataji utepe ukiendelea.


DC Makonda akifungua pazia kuashiria uzinduzi wa ujenzi huo.


DC Makonda akiwa na viongozi wa Kampuni ya GSM Foundation. Kushoto ni Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Azizi Msuya.


DC Makonda akizungumza na wanahabari kuhusu ujenzi huo.


Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Azizi Msuya akizungumza na wanahabari.


Wanahabari wakichukua taarifa za ujenzi huo.


Mwakilishi wa Kampuni ya GSM Foundation, Deogratias Ndejembi akizungumza na wanahabari kuhusu ufadhili wao wa ujenzi wa jengo hilo.


Msingi wa jengo hilo.


Mwakilishi wa Kampuni ya GSM Foundation, Deogratias Ndejembi (katikati), Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na Mhandisi atakaye simamia ujenzi huo kutoka GSM, Hersi Said wakionesha picha ya jengo hilo litakavyoonekana baada ya kukamilika.


Taswira ya jiwe la msingi baada ya kuzinduliwa.


DC Makonda akiwa na viongozi wa Kampuni ya GSM mbele ya msingi litakapo jengwa jengo hilo.
Wagoma kuchukua barua za kufutwa kazi wakisubiri ushauri wa kisheria

Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) waliofutiwa mikataba ya kazi, wamegoma kupokea barua za kuachishwa kazi wakidai kwamba hawajui kilichoandikwa kuhusu hatima ya madai yao.

Wafanyakazi hao walikutana jana Dar es Salaam na kiongozi wao, Seif Kibangu alisema wamekubaliana kutochukua barua hizo hadi pale watakapopata ushauri kutoka kwa wanasheria.

“Licha ya mishahara ya miezi mitatu tuna madai yetu mengine ikiwamo makato ya mafao yetu yaliyotakiwa kupelekwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, pia tumekuwa tukikatwa bima ya afya asilimia tatu ya mishahara yetu hatujui hatma yake. Sasa leo wanataka tuchukue barua hizo tena kwa kusaini kabla ya kujua kilichoandikwa hapana tuendelee kuvumilia haki yetu tutaipata,” alisema Kibangu.

Aliwakosoa waliochukua barua hizo akisema waliajiriwa kwa makundi, ingawa pia wapo waliopewa kazi hiyo kwa vimemo.

“Hili ni jasho letu, hatuibi cha mtu kwa hiyo tunastahili kupata haki zetu zote, mishahara tunayodai kwa miezi mitatu, acha hayo madai mengine... Tunadaiwa huko tunapoishi kwa kweli tunaomba wahusika waingilie kati jambo hili linatuumiza na kuyumbisha maisha yetu,” alisema. Akizungumza kwa niaba ya madereva wenzake, George Mmari alidai kuna gharama nyingi walizoingia ambazo Nida inapaswa kuzilipa ikiwamo malipo ya kuegesha na kuosha magari waliyokuwa wakiendesha.

Akizungumzia madai hayo, Ofisa Habari Mwandamizi wa Nida, Rose Mdami alieleza kushangazwa na hatua ya wafanyakazi hao kugoma kuchukua barua zao badala ya kuzipokea ili wajue kilichoandikwa ili kama wana madai waandike barua na kuyaorodhesha.
  • via Mwananchi

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambao wamisitishiwa mkataba wa kufanya kazi kutokana na ukata ulioikumba mamlaka hiyo, wamegoma kupokea barua rasmi zinazoonyesha kusitishwa kwa mikataba yao.

Mmoja wa wafanyakazi hao, Mpaji Isaya aliiambia Nipashe jana kuwa, waliambiwa wafike kuchukua barua hizo jana, ili kuthibitisha rasmi kufutwa kwa mikataba yao.

“Baada ya kutangaziwa na Kaimu Mkurugenzi kuwa mikataba imefutwa, walisema tufike leo NIDA kuchukua barua za uthibitisho," alisema Isaya.

"Lakini cha ajabu wanataka tusaini fomu kuthibitisha tumepokea barua na tuondoke, wakati kilichoandikwa ndani ya barua hatukijui.
"Sasa kama stahiki zetu tumepunjwa tutajuaje?”

Isaya alisema NIDA ilitakiwa iwape muda wa kuzisoma barua hizo kama ilivyokuwa awali wakati wa kuajiriwa ambapo walipewa muda wa siku tatu kuusoma na kuuelewa mkataba ndipo wakasaini.

Kaimu Mkurugenzi wa NIDA Modestus Kipilimba, alisitisha mikataba ya wafanyakazi 597 wiki iliyopita kwa maelezo ya ukosefu wa fedha za kuwalipa wafanyakazi hao kwa sasa.

Kaimu Mkuu wa kitengo cha Uhusiano wa NIDA, Rose Mdami, alipotafutwa na Nipashe ili kutolea ufafanuzi suala hilo, alisema waliwapa taarifa wafanyakazi hao kufika jana kwa ajili ya kuchukua baraua zao.

“Taarifa za kuja leo (jana) ofisini NIDA wafanyakazi ni za kweli, walikuja kufuata barua zao lakini kwa maelezo mengine ufike ofisini kwetu,” alisema Mdami.

NIDA ilisema haina fedha za kuwalipa malimbikizo ya mishahara ya miezi miwili wafanyakazi wa 597 waliositishiwa mikataba yao ya muda huku menejimenti ikisema inaendelea kujipanga ili kuhakikisha inawalipa kwa wakati bila usumbufu wowote ijapokuwa ofisi hiyo haina fedha kwa sasa.

NIDA ilisema inaendelea kufanya uhakiki wa mikataba ya wafanyakazi wote 597 na kusubiri pesa kutoka hazina kwa ajili ya kuwalipa kwa mujibu wa sheria.

Katuni: Kwa nini uliacha mabua?

Waajiri na wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu wapewa siku 60; HESLB yatoa namba za mawasiliano

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inatoa siku 60 kuanzia tarehe 14 Machi, 2016 kwa wanufaika wote wa mikopo wanaodaiwa na HESLB kujitokeza na kuanza kulipa madeni yao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, katika muda huu wa siku 60 waajiri pia wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanatekeleza wajibu wao wa kisheria wa kuwasilisha taarifa za waajiriwa wao waliohitimu katika vyuo vya elimu ya juu ndani na nje ya nchi. Taarifa zinazopaswa kuwasilishwa zijumuishe majina kamili ya waajiriwa, vyuo na mwaka waliohitimu.

Itakumbukwa kuwa Sheria iliyoanzisha HESLB (Sura 178) (kama ilivyorekebishwa) inatoa wajibu kwa mnufaika wa mikopo ya elimu ya juu na pia wajibu kwa mwajiri.

Wajibu wa Mwajiri

Hivyo basi, taarifa hii inalenga kuwakumbusha waajiri ambao bado hawatimizi wajibu wao kisheria (kifungu cha 20) wa kuwasilisha majina ya waajiriwa wao wote ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu kwa HESLB ndani ya siku 28 tangu waajiriwe. Adhabu ya kutotekeleza wajibu huu kwa mwajiri ni faini ya shilingi milioni saba (Tshs milioni 7) au kifungo au vyote kwa pamoja.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, baada ya HESLB kupokea orodha kutoka kwa mwajiri, itafanya uchambuzi ili kubaini wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu na kumwelekeza mwajiri kuingiza makato ya marejesho kwenye mshahara wa mnufaika na kuwasilisha makato hayo kwa HESLB. Adhabu ya kutowasilisha makato kwa HESLB ni faini ya asilimia 10 ya makato yote ambayo hayajawasilishwa na faini hii inapaswa kulipwa na mwajiri.

Wajibu wa mnufaika wa mkopo na wazazi, walezi, wadhamini

Aidha, pamoja na wajibu wa mwajiri kama ulivyofafanuliwa hapo juu, wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu tangu mwaka 1994, wana wajibu wa kisheria (Kifungu cha 19 cha sheria ya HESLB), pamoja na mambo mengine, kuitaarifu HESLB kwa maandishi mahali alipo na kuandaa utaratibu wa kulipa deni lake la mkopo wa elimu ya juu.

Iwapo mnufaika wa mkopo atashindwa kutoa taarifa hizo, adhabu yake ni kushitakiwa mahakamani.
Aidha, HESLB inapenda kuwakumbusha wazazi, walezi na wadhamini wa wanafunzi walionufaika na mikopo kuwa wana wajibu wa kisheria (chini ya kifungu cha 22 cha sheria ya HESLB) wa kuhakikisha kuwa taarifa muhimu za mnufaika waliyemdhamini zinaifikia HESLB.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, taarifa hizo ni pamoja na mahali alipo mnufaika, majina aliyotumia wakati akipata mkopo, mwajiri wake na kuhakikisha mnufaika aliyemdhamini anarejesha mkopo wake kwa HESLB.

Iwapo mwajiri, mnufaika au mdau yeyote ana swali, awasiliane na HESLB kwa simu zifuatazo: 0754 373481; 0763 459 165 au 022 2772432/33.

Lengo la HESLB ni kuhahakisha madeni yote yanakusanywa ili kuongeza uwezo wa kukopesha watanzania wengi zaidi. Ili kutekeleza hili, wanufaika, waajiri na wadau wengine wote wanapaswa kutimiza wajibu wao wa kisheria ili HESLB itekeleze majukumu yake kama ilivyokusudiwa wakati ilipoanzishwa mwaka 2004.

HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu. Aidha, jukumu jingine la Bodi ni kudai na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kuanzia mwaka 1994 wakati Serikali ilipoanza kukopesha wanafunzi.

Mwisho

Imetolewa na:
Bw. Jerry Sabi,
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji – HESLB
Dar es Salaam – Jumapili, Machi 13, 2016

Mtambo wa kusukuma maji kutoka Ruvu Chini wawashwa kwa majaribio

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Muhandisi Mbogo Futakamba akibonyeza moja ya mashine inayoongoza pampu za kusukuma Majikwenda jijini Dar es salaam kutoka Mtambo wa kuzalisha Maji wa Ruvu Chiniwilayani Bagamoyo mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya majaribio ya mtambo huomara baada kukamilika kwa ujenzi wa bomba la kusafirisha maji lenye urefu
wa kilometa 55.9.

Hatimaye moja ya pampu kubwa katika mtambo wa kuzalisha maji kwenye chanzo cha maji cha Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani imewashwa kwa majaribio kufuatia kukamilika kwamradi wa ujenzi wa bomba kubwa la kusafirishia maji lenye urefu wa kilometa 55.9 kutoka chanzo hicho kwenda jijini Dar es salaam.

Majaribiohayo ni sehemu ya awali ya kupitisha maji yenye msukumo mkubwa kwenye bomba hilokuelekea kwenye matenki makubwa ya kuhifadhia maji yaliyoko eneo la Chuo Kikuu Ardhi jijini Dar es salaam. 

Akizungumza mara baada ya kuwasha Pampu hiyo Katibu Mkuu waWizara ya Maji na Umwagiliaji Muhandisi Mbogo Futakamaba amesema kuwa majaribio hayo ambayo yameonyesha mafanikio yatawawezesha wakazi wa jiji hilo na maeneo ya mkoa wa Pwani kupata huduma ya uhakika ya Maji kufikia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu.

Amesema mradi huo utakuwa suluhisho la tatizo la maji la muda mrefu kwa kuwa kiwango cha maji kitakachozalishwa kwa siku kitafikialita milioni 270 ambazo zitaongezwa kwenye msukumo wa lita milioni 182 zilizokuwa zikizalishwa hapo awali kabla ya kukamilika kwa ujenzi wa bomba hilo.
“Hii ni faraja kwa Serikali na wakazi wa jiji la Dar es salaam na mkoa wa Pwani, sasa tutapata lita Zaidi ya milioni 270 kwa siku haya ni mafanikio makubwa, kulingana na mahitaji tuliyokuwa nayo tutahakikisha tunayasambaza maji haya ili kukidhi mahitaji ya wananchi” Amesema Muhandisi Futakamba.

Muhandis Futakamba amewataka wahandisi na watendaji wanaosimamia uendeshaji wa mitambo hiyo kuwa mahili na makini katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha inafanya kazi kwa ufanisi na kwa maslahi ya umma.

Ameiagiza DAWASA na DAWASCO kuendelea kuwajengea uwezo kielimu Wahandisi wa ndani wanaohusika na utunzaji wa miundombinu hiyo ili miradi ya maji wanayoisimamia iweze kudumu na kuwa endelevu kupitia matengenezo na huduma mbalimbali watakazozifanya.

“Ninyi kama wahandisi na wasimamizi wa miradi na mitambo hii mikubwa hakikisheni mnajenga uwezo wenu wa ndani ili muweze kuiendesha na kuidhibiti mitambo hii pia kuwa na uelewa wa ndani wa mifumo yote iliyotumiwa wakati wa uwekaji wake na mabadiliko ya teknolojia” Amesisitiza.

Pia amewataka watendaji hao kuhakikisha kuwa wanatunza mitambo na miundombinu yote ya majiili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) Muhandisi Archard Mutalemwa akizungumza mara baada ya kukagua mitambo ya kuzalisha Maji ya Ruvu Chini amesema kuwa kukamilika kwa bomba hilo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali kupitia DAWASA za kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya maji safi. 

Amesema DAWASA itaendelea kutekeleza majukumu yakekwa kuhakikisha inaendeleza na kusimamia miradi ya maji ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo na kuhakikisha inawawezesha wakazi wa jiji la Dar es salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani yanapata huduma ya Maji Safi kupitia miradi iliyochini yake.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASCO) Muhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza mara baada ya kuwashwa kwa mtambo huo amesema kuwa DAWASCO imejipanga kuhakikisha inawasambazia huduma ya maji wakazi wengi zaidi wa jiji hilo ambao walikua na miundombinu lakini hawapati huduma hiyo pamoja na kuunganisha wateja wapya kwa gharama nafuu.

“Naishukuru Serikali kwa kuwezesha mafanikio haya sisi kama DAWASCO tumejipanga na tutahakikisha maji yanayozalishwa yanawafikia wananchi, yapo maeneo mengi yaliyokuwa na changamoto ya huduma hiyo hata yale ambayo yalikua yameunganishwa tayari katikati ya jiji nay ale yaliyo pembezoni mwa jiji tutahakikisha tutayafikia” Amesisitiza.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa kudhibiti wa wizi wa maji amesema DAWASCO imeanzisha maeneo 25 (DMA) ambayo yamefungwa mita kubwa katika wilaya za jiji hilo ili kuwawezesha Mameneja wa Zoni husika kuweza kubaini wizi , upotevu wa maji, ubovu wa mita na tatizo la usomaji na kisha kuchukua hatua kwa wale wanaobainika kuhujumu miundombinu hiyo.

Aidha, amesema DAWASCO imeandaa mpango wa kuziondoa mita zoteambazo zimefikia umri wa miaka 10 ifikapo mwezi Juni mwaka huu.

Ikumbukwe kuwa mradi wa ujenzi wa bomba kubwa la kusafirishia maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini wenye urefu wa kilometa 55.9 umejengwa na Kampuni ya JBG Gauff Ingenieure kwa gharama ya shilingi Bilioni 141 ambazo zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania.


Mkuu wa Matengenezo wa Mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini Tumaini Ndosi (aliyepanda juu) akitoa ufafanuzi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Muhandisi Mbogo Futakamba kuhusu moja ya mita inayosoma kiwango cha ujazo wa maji yanayosafirishwa kutoka kwenye Pampu za kusukumia maji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Muhandisi Mbogo Futakamba (kulia) akizungumza jambo na Meneja wa Mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini, Emmanuel Makusa (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO Muhandisi Cyprian Luhemeja mara baada ya kukagua mitambo na pampu za kusukumia Maji za Mtambo wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.
Eneo la ndani la Mtambo wa kuzalisha maji likiwa limekamilika mara baada ya kufungwa pampu mpya zenye uwezo wa kusukuma maji Lita milioni 270 kwa siku kuja jijini Dar es salaam na maeneo ya Mkoa wa Pwani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Muhandisi Mbogo Futakamba (katikati) akieleza namna wakazi wa jiji la Dar es salaam na mkoa wa Pwani watakavyonufaika na huduma ya Maji mara baada kukamilika kwa ujenzi wa bomba la kusafirishia Maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini kuja jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) Muhandisi Archard Mutalemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO Muhandisi Cyprian Luhemeja.
Sehemu ya maungio ya Mabomba yanayoingiza maji ndani ya Mtambo huo kutoka mto Ruvu, chini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASCO) Muhandisi Cyprian Luhemeja akitoa ufafanuzi kwa waandishi namna DAWASCO ilivyojipanga kuwahudumia wananchi wa mkoa wa Dar es salaam kwa kuwafikishia huduma ya Maji Safi kufuatia kukamilika ujenzi wa bomba la Maji kutoka Mtambo wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.
Moja ya maungio ya Bomba kubwa la kusafirishia Maji kutoka mtambo wa Maji wa Maji wa Ruvu Chini, Bagamoyo Pwani lililoko eneo la Tegeta jijini Dar es salaam likiwa limekamilika.
Sehemu ya ndani ya Matenki yanayopokea maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini yaliyoko eneo la Chuo Kikuu cha Ardhi jijini Dar es salaam.
  • Taarifa ya Aron Msigwa –MAELEZO.

WM Majaliwa arejea ahadi ya Rais Magufuli: Tutanunua meli ya kusafirisha abiria katika Ziwa Victoria

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanza kukusanya fedha kwa ajili ya kununua meli mpya kwa ajili ya usafirishaji wa abiria na mizigo kwenye Ziwa Victoria.

“Rais John Pombe Magufuli kasema ununuzi wa meli mpya uko pale pale. Tutanunua meli ya kusafirisha abiria katika Ziwa Victoria kama ambavyo aliahidi wakati wa kampeni,” alisema huku akishangiliwa.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Machi 13, 2016) wakati akitoa maelekezo baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Kagera ambako amewasili leo kwa ziara ya siku tatu kwa ajili ya kukagua masuala ya wakimbizi pamoja na mwenendo wa ranchi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na jinsi zinavyotumika.

Mbali ya ununuzi wa meli hiyo, Waziri Mkuu alisema Serikali pia imejipanga kununua ndege mbili ili kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini. “Tuna dhamira ya kununua ndege walau mbili kwa ajili ya shirika letu la ndege la ATC. Tumelazimika kuwaomba Watanzania wenzetu warudi nyumbani ili kusaidia kuendesha shirika letu,” alisema.

Waziri Mkuu alisema suala hilo limeshafika mbali na utekelezaji wake hautachukua muda mrefu kuanzia sasa.

Alitumia fursa hiyo kuwaarifu wana Kagera kwamba hivi karibuni Serikali itaanza mradi wa kujenga bomba la kusafirisha mafuta ambalo litapita kwenye mkoa huo na hivyo kutoa ajira kwa wakazi wake. “Bomba litaanzia Tanga, kupitia Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Geita, Kagera hadi Uganda. Na humu njiani litakuwa na vituo vya kusukumia mafuta, kwa hiyo tuna uhakika wa kupata ajira kwa ajili ya watu wetu,” alisema.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MACHI 13, 2016.

Katibu Mtendaji NACTE ajiuzulu

Aliyekuwa Katibu Mtendaji wa NACTE, Primus D Nkwera (kulia) akifafanua jambo
Aliyekuwa Katibu Mtendaji wa NACTE, Primus D Nkwera (kulia) akifafanua jambo

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Vyuo vya Ufundi (NACTE), Dk. Primus Nkwera amejiuzulu nafasi yake.

Uamuzi wa kujiuzulu kwa Dk. Nkwera ulitangazwa katika ofisi kuu za Baraza hilo zilizopo Mikocheni Dar es Salaam juzi na Mwenyekiti wa Bodi,Mhandisi Steven Mlote na kusababisha baadhi ya wafanyakazi kuangua kilio.

Akizungumza katika kikao cha dharura cha wafanyakazi wote wa baraza hilo, Mlote alisema Dk. Nkwera amejiuzulu ili kulinda hadhi ya Nacte kutokana na habari iliyoandikwa na Gazeti la Dira ikimtuhumu mambo mbalimbali.

Gazeti hilo la Dira la Jumatatu tarehe 07/03/2016 toleo no.405 lilimtuhumu Katibu Mtendaji wa NACTE, Dk. Primus Nkwera kughushi vyeti vya shahada ya uzamivu baada ya kusomeshwa na serikali Afrika Kusini na kufeli.

Mlote alisema kwa mujibu wa Dk. Nkwera, nafasi hiyo haipaswi kushikwa na mtu mwenye tuhuma ya aina yoyote, na ametafakari na kuona ajiweke kando na uongozi wa Nacte ili uchunguzi ufanyike akiwa pembeni.

"Tumetumia muda mwingi kutafakari hoja ya Dk. Nkwera na hatimaye tumekubali kujiuzulu kwake kwa shingo upande," alisema Mlote na kuongeza:

"Kazi kubwa iliyofanywa na Dk. Nkwera akiwa kiongozi wa Nacte inafahamika na kila mmoja, vilio na machozi ya wafanyakazi wenzake yanadhihirisha kuwa kujiuzulu kwake kunaacha simanzi kubwa.

"Najua mmepata mshtuko mkubwa, lakini Dk. Nkwera hajafa, yuko hai na huyu bado ni mtumishi wa serikali. Alichofanya ni kuamua kuachana na ukatibu utendaji.

"Tutaendelea kumtumia itakapobidi kwa ushauri.Wakati mwingine lazima mkubaliane na hali hii, lakini pia endeleen kuchapakazi kwa ufanisi kama kawaida kana kwamba bado mko na Dk. Nkwera."

Kutokana na kujiuzulu kwake, Mlote alisema bodi imemteua Mkurugenzi wa Mitaala wa Nacte, Dk Adolf Rutayunga kukaimu nafasi hiyo wakati taratibu nyingine zikiendelea.

Walioteuliwa na Rais Magufuli kuwa Wakuu wa Mikoa ya Tanzania

null

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa wakuu wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara, ambapo kati yao 13 ni wapya, 7 wamebakizwa katika vituo vyao vya kazi, 5 wamehamishwa vituo vya kazi na 1 amepangiwa Mkoa Mpya wa Songwe.

Uteuzi huo umetangazwa na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe leo tarehe 13 Machi, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam.

Wakuu wa Mikoa walioteuliwa ni kama ifuatavyo;

1. Mh. Paul Makonda - Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.

2. Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Elias Kyunga - Mkuu wa Mkoa wa Geita.

3. Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu - Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

4. Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga - Mkuu wa Mkoa wa Katavi.

5. Brigedia Jeneral Mstaafu Emmanuel Maganga - Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

6. Mh. Godfrey Zambi - Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

7. Dkt. Steven Kebwe - Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

8. Kamishna Mstaafu wa Polisi Zerote Steven - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

9. Mh. Anna Malecela Kilango - Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

10. Mhandisi Methew Mtigumwe - Mkuu wa Mkoa wa Singida.

11. Mh. Antony Mataka - Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

12. Mh. Aggrey Mwanri - Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

13. Mh. Martine Shigela - Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

14. Mh. Jordan Mungire Rugimbana - Mkuu wa Mkoa Dodoma.

15. Mh. Said Meck Sadick - Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.

16. Mh. Magesa Mulongo - Mkuu wa Mkoa Mara.

17. Mh. Amos Gabriel Makalla - Mkuu wa Mkoa Mbeya.

18. Mh. John Vianey Mongella - Mkuu wa Mkoa Mwanza.

19. Mh. Daudi Felix Ntibenda - Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

20. Mh. Amina Juma Masenza - Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

21. Mh. Joel Nkaya Bendera - Mkuu wa Mkoa wa Manyara.

22. Mh. Halima Omary Dendegu - Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

23. Dkt. Rehema Nchimbi - Mkuu wa Mkoa wa Njombe.

24. Mhandisi Evarist Ndikilo - Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

25. Mh. Said Thabit Mwambungu - Mkuu wa Mkoa Ruvuma.

26. Luteni Mstaafu Chiku Galawa - Mkuu wa Mkoa wa Songwe (Mkoa mpya).

Wakuu wote wa Mikoa walioteuliwa, wataapishwa Jumanne tarehe 15 Machi, 2016 saa 3:30 Asubuhi Ikulu, Jijini Dar es salaam.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam

13 Machi, 2016

  • Wapya ni 13, waliobakizwa 12 (miongoni mwao, 4 wamebakia katika mikoa yao).

Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Katibu Mkuu TAMISEMI, Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe akitangaza Majina ya Wakuu wapya wa Mikoa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam