Mahabusu wa Pakistani nchini Tanzania waliokamatwa na dawa za kulevya waomba watupwe baharini

RAIA watatu wa Pakistani na wanane wa Iran wanaokabiliwa na kesi ya kuingiza nchini dawa za kulevya, juma lililopita waliiomba Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam iwatupe baharini.

Watuhumiwa hao walimwomba Warialwende Lema, Hakimu Mkazi Kisutu watupwe baharini kutoka na hali ngumu wanayokutana nayo gerezani na kwamba, hawana ndugu hapa nchini.

Watuhumiwa hao walikamatwa tarehe 4 Februari, 2014 wakiwa na dawa za kulevya aina heroin kilo 200.5 zenye thamani ya Sh. 9.02 bilioni wakiziingiza nchini kupitia Bahari ya Hindi.

Watuhumiwa hao wakati wanakamatwa walikuwa 12 ambapo wamebaki 11 kutokana na mmoja kati yao kufariki dunia. Aliyefariki ni Kapteni Ayoub Mohamed.

Wanaoendelea na kesi hiyo ni Buksh Mohamed, Fahiz Dauda, Khalid Ally, Abdul Somad, Saeed Sahury, Bashir Afraz, Morad Gwaram na Hazir Azad Rais wa Iran.

Raia wa Pakistani ni Buksh Mohamed, Rahim Baksh na Abdul Bakashi ambapo kesi hiyo imeghairishwa hadi tarehe 4 Aprili mwaka huu.

Alivyoeleza mzee Mkinga namna wizi wa mapato unavyofanyika katika sekta ya bandari

Aliyewahi kuwa Naibu Mkugurugenzi wa Uhamiaji, Mshindi wa shilingi milioni 100 za shindano la Vodacom, Mjumbe na mbunge wa Bunge la Katiba 2015 ambaye pia ni mwanaharakati na mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linalopigania haki za kibinadamu na utawala bora ndugu Renatus Gervas Mkinga alizungumza mwaka jana na Albert Kilala katika kipindi cha "Mada Moto" cha ChannelTEN kuhusu ubadhirifu wa mapato unaofanyika katika sekta ya bandari.

Maofisa misitu na wafanyabiashara wakamatwa na magogo, mbao na mikaaMaofisa wawili wa wakala wa huduma za misitu nchini, TFS, pamoja na wafanyabiashara watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyerembe Mnasa Sabi, baada ya kuwakamata shehena ya magogo, mbao na mkaa ambayo inadaiwa kuandaliwa kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi kinyume cha sheria.

Taarifa ya habari ChannelTEN, Aprili 11, 2016Rais Magufuli apokea hundi kutoka Ofisi ya Bunge kwa ajili ya madawati ya wanafunzi

Rais Magufuli ameipongeza Ofisi ya Bunge kwa kubana matumizi na kufanikiwa kuokoa fedha ambayo zitatumika kutengeneza madawati ya wanafunzi wa shule.

Rais Magufuli amezitaka ofisi na taasisi nyingine za serikali kuiga mfano huo.

Ameagiza fedha hizo zipelekwe katika Idara ya Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili vyombo hivyo vifanye kazi ya kutengeneza madawati yanayotarajiwa kuwa zaidi ya 120,000 ambayo yatasambazwa katika shule mbalimbali ili kukabiliana na tatizo la wanafunzi wanaokaa chini kwa kukosa madawati.

Hundi mfanyo ya fedha hizo imekabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais Magufuli na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Akson, ambaye amesema Ofisi ya Bunge imetekeleza wito wa serikali wa kubana matumizi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 6 kimepatikana ndani ya takribani nusu mwaka.


RAIS DK. MAGUFULI AAGIZA BILIONI 6 KUTOKA BUNGE ZIKABIDHIWE KWA MAGEREZA NA JKT ILI KUTENGENEZA MADAWATI 120.000


Rais Magufuli ameipongeza ofisi ya Bunge kwa kubana matumizi na kufanikiwa kuokoa shilingi Bilioni 6, ambazo zitatumika kutengeneza madawati ya wanafunzi wa shule na amezitaka ofisi na taasisi nyingine za serikali kuiga mfano huo.

Ameagiza fedha hizo zipelekwe Idara ya Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili vyombo hivyo vifanye kazi ya kutengeneza madawati yanayotarajiwa kuwa zaidi ya 120,000 ambayo yatasambazwa katika shule ili kukabiliana na tatizo la wanafunzi wanaokaa chini kwa kukosa madawati.

Hundi Kifani ya fedha hizo imekabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Akson, ambaye amesema Ofisi ya Bunge imetekeleza wito wa serikali wa kubana matumizi ambapo kiasi hicho cha shilingi Bilioni 6 kimepatikana kwa kipindi kifupi cha takribani nusu mwaka.

Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilila ametaja maeneo ambayo Bunge limebana matumizi kuwa ni Safari za nje ya nchi, Mafunzo nje ya nchi, Machapisho na ununuzi wa majarida, Shajala, Chakula na Viburudisho, Mtandao, Malazi hotelini, Matibabu ya wabunge na familia zao nje ya nchi, Umeme, Maji, Simu na Uendeshaji wa Mitambo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pia ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Anne Kilango Malecela na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Abdul Rashid Dachi, kufuatia mkoa huo kutoa taarifa zisizo sahihi kuwa hauna watumishi hewa.

Rais Magufuli ametangaza kutengua uteuzi wa Viongozi hao wa Mkoa wa Shinyanga leo tarehe 11 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam, mara baada ya kupokea Taarifa ya Mwaka 2014/2015 ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na kupokea hundi kifani ya shilingi Bilioni 6 kutoka Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizotokana na kubana matumizi.

Dkt. Magufuli ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa kuwa Mkoa wa Shinyanga hauna watumishi hewa, aliamua kutuma timu ya ukaguzi iliyokwenda kufanya uchunguzi ambapo hadi kufikia jana tarehe 10 Aprili, 2016 imebaini kuwepo watumishi hewa 45 huku zoezi likiwa linaendelea katika wilaya mbili za Ushetu na Shinyanga Vijijini.

“Na wale wote wa Shinyanga ambao walisemekana ni zero, hakuna mtumishi hewa, walikuwa tayari wameshalipwa shilingi milioni 339.9, nimejiuliza sana, na nikajiuliza sana na kwa kweli nimejiuliza sana na kwa masikitiko makubwa, kwa nini Mkuu wa Mkoa alisema hakuna mtumishi hewa?” Amesisitiza Rais Magufuli

Rais Magufuli amesema baada ya kutengua uteuzi wake, Anne Kilango Malecela atapangiwa kazi nyingine.

Pamoja na hatua hiyo, Dkt. Magufuli ametaka wakuu wa mikoa yote wawafichue watumishi hewa wote ili waondolewe mara moja, na ameagiza timu iliyofanya uchunguzi Mkoani Shinyanga itumike kufanya uchunguzi katika mikoa mingine kwa lengo la kukomesha upotevu mkubwa wa fedha za umma.

Katikati ya Mwezi Machi, 2016 Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kusimamia zoezi la kuwaondoa watumishi hewa wote katika orodha ya malipo ya mshahara, ambapo mpaka tarehe 31 Machi, 2016 Jumla watumishi hewa 5,507 walibanika.

Kati ya shilingi Bilioni 583 ambazo serikali imekuwa ikitumia kila mwezi kwa ajili kulipa mishahara, kati ya shilingi Bilioni 53 na 54 zimekuwa zikipotea kutokana na kulipa mishahara ya watumishi hewa.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam

11 Aprili, 2016


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akionesha mfano wa hundi aliyokabidhiwa na Ofisi ya Bunge leo Ikulu, Jijini Dar es Salaam ambapo fedha hizo ameelekeza zitumike kutengenezea madawati ya shule hapa nchini(kulia)ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson.


Muonekano wa Madawati ambayo yanatarajiwa kutengenezwa na yaliyoidhinishwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kama yanavyoonekana katika picha.

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, CGP John Casmir Minja(kushoto) akiwa na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Bregedia Jenerali, Michael Isamuhyo(katikati) wakifuatilia hotuba ya Rais Magufuli (kulia) ni Mtendaji Mkuu wa SUMA - JKT, Bregedia Jenerali C.Yateri.

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, CGP John Casmir Minja akiongea na Wandishi wa Habari kuhusu namna Jeshi hilo lilivyojipanga kutekeleza jukumu lililopewa.

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, CGP John Casmir Minja akisalimiana na Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilila wakipokutana katika Viwanja vya Ikulu, Jijini Da es Salaam(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

Na; Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza,

JESHI LA MAGEREZA nchini pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa limepewa jukumu la kutengeneza madawati yenye thamani ya Bilioni 6 ambayo yatasambazwa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Jukumu hilo kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama limetolewa leo Aprili 11, 2016 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, katika hafla fupi ya makabidhiziano ya mfano wa hundi ya Bilioni 6 za pesa ya kitanzania kutoka Sekretarieti ya Bunge ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pesa ambazo zimepatikana kufuatia kubana matumizi ya uendeshaji wa Ofisi hiyo.

Rais Magufuli amesema kuwa Ofisi ya Bunge pamoja na Watendaji wake wameonesha moyo wa kizalendo kwa Taifa lao kwani wametekeleza kwa vitendo maelekezo ya kubana matumizi ya fedha za Serikali hivyo kuokoa kiasi hicho cha Bilioni 6 ambazo wamezikabidhi ili zitumike katika kutatua changamoto ya uhaba wa Madawati katika shule nyingi hapa nchini.

“Nikupongeze sana Dkt. Thomas Kashilila, Watendaji wote wa Ofisi ya Bunge kwa moyo wenu wa upendo, uzalendo mkaamua kiasi hiki cha fedha Bilioni 6 zikafanye kazi ya maendeleo kwani mngeweza kuzitumia fedha hizi katika matumizi mengine hata Mhe. Spika asingejua". Alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amewataka Makatibu Wakuu wote wa Wizara pamoja na Watendaji Wakuu wote wa Taasisi za Umma/Serikali kuiga mfano huo wa kizalendo aliouonesha Katibu wa Bunge,
Dkt. Thomas Kashilila kwani huo ndio mwelekeo anaoutaka katika Serikali yake ya Awamu ya Tano.
Awali akiongea kabla ya Makabidhiano ya hundi hiyo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kimepatikana kufuatia kubana matumizi katika maeneo mbalimbali ikiwemo kupunguza safari za nje, gharama za machapisho mbalimbali, gharama za viburudisho na chakula, matibabu kwa wabunge, mafuta na uendeshaji wa mitambo nk.

Akizungumzia utekelezaji wa jukumu la utengenezaji wa madawati hayo Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, John Casmir Minja amesema kuwa Jeshi la Magereza lipo tayari kutekeleza agizo la Rais na amejipanga kutumia nguvu kazi ya Wafungwa waliopo magerezani pamoja na Maafisa na Askari wa Jeshi hilo ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

"Mhe. Rais ametoa maelekezo ya kwenda kufanya kazi hiyo kama operesheni maalum hivyo sisi kwa upande wa Jeshi letu tupo tayari kuifanya kazi hiyo kama ilivyoelekezwa kwa kuzingatia maelekezo ya Mhe. Rais". Alisema Jenerali Minja.

Jeshi la Magereza Tanzania limepiga hatua kubwa ya Maboresho juu ya utengenezaji wa bidhaa bora za Samani hivyo kupelekea kuibuka mara kwa mara Mshindi wa kwanza katika Maonesho mbalimbali ya Kibiashara hapa nchini.

Waziri apendekeza kuondoa VAT kwa nyumba za NHC zinazouzwa chini ya milioni 40/=

Wizara ya Ardhi imependekeza kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kwa nyumba zisizozidi Sh40 milioni zinazouzwa na taasisi za umma.

Waziri wa Ardhi, William Lukuvi aliieleza Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuwa ameshapeleka pendekezo kwa Baraza la Mawaziri kuondoa kodi hiyo kwenye nyumba zinazouzwa na Shirika la Nyumba (NHC) na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) iwapo zitauzwa kwa gharama isiyozidi Sh40 milioni ili kuwapatia wananchi unafuu.

“Nilipowauliza wataalamu wangu kikomo cha nyumba ya bei nafuu ni shilingi ngapi, walinitajia Sh49.9 milioni, lakini niliona haiwezekani. Ndiyo maana nilipendekeza serikalini VAT iondolewe kwenye nyumba zisizozidi Sh40 milioni,” alisema Lukuvi. 

Wajumbe wa kamati hiyo kwa umoja pia waliikomalia wizara hiyo kuisimamisha kwa muda Mamlaka ya maendeleo ya mji wa Kigamboni (KDA), kwa sababu haipatiwi fedha za kutosha na mradi husika unasuasua.

Lukuvi aliomba kupatiwa Sh61.83 bilioni katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo, ikiwa ni ongezeko la Sh7.2 bilioni kutoka kwenye bajeti ya mwaka 2015/2016.

Aliwaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa kati ya Sh61.83 wanazohitaji, Sh16.35 bilioni zitatumika kulipa mishahara ya watumishi wa wizara hiyo. Wizara hiyo inaomba kutumia Sh25.48 bilioni kutoka katika fungu hilo kwa ajili ya matumizi mengineyo, ambayo yanajumuisha Sh10 bilioni za kuziwezesha halmashauri kusimamia upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashasta Nditiye alisema baada ya kusikiliza mapendekezo hayo wataanza kuijadili leo kwa kina kuona iwapo ni halisi au la.

Wezi wa kimtandao waiibia Standard Chartered Bank ya Tanzania

Wahalifu wa mitandao wamedaiwa kuingilia akaunti za wateja wa Benki ya Biashara ya Standard Chartered na kuiba fedha kiasi ambacho hakijajulikana.

Mkuu wa Uhusiano na Masoko wa benki hiyo, Joanita Mramba alisema wamechukua hatua ikiwamo kuzuia kadi za kutolea fedha na kuanza mchakato wa kutengeneza kadi mpya ili kudhibiti wizi huo.

“Kwanza kabisa nawahakikishia wateja wetu fedha zao ziko salama na wasiwe na wasiwasi waendelee kufurahia huduma ya benki yetu.

Alisema tukio hilo lilianza kujitokeza mwanzoni mwa wiki iliyopita na benki iliwataarifu wateja wake kwa simu kuwa kuna jaribio la kuingilia akaunti zao ili kuibiwa fedha zao.

Mkazi wa Kimara, Method Makumvi aliyekumbwa na mkasa huo alisema alibaini kuwa ameibiwa baada ya kukosa fedha kwenye akaunti yake jana.

“Nilifika katika moja ya mashine za ATM, iliyopo Mwenge, kutoa fedha ya mafuta ya gari langu. Bahati mbaya sikukuta kitu na akaunti ilikuwa na kiasi cha Sh800,000,” alisema Makumvi.

Aliongeza kuwa baada ya kubaini tukio hilo alikwenda moja tawi la benki hiyo maeneo ya Shoppers Plaza na kuwaelezea mkasa huo.

“Wahudumu wa benki waliniambia siyo mimi pekee niliyekumbwa na mkasa huu. Wakanishauri nijaze fomu kwa ajili ya kuzipata fedha zangu zilizokuwa katika akaunti,” alisema.

Kutokana na tukio hilo, Makumvi alielezwa na wahudumu wa benki hiyo kuwa wameamua kuzuia kadi za ATM za wateja wote na kuamua kutoa kadi mpya lengo likiwa ni kupambana na

Alisema alijaza fomu benki kwa ajili ya kupata fedha hizo zilizochotwa katika akaunti yake.

Acacia: Tutaweza kulipa kodi ya zaidi ya bilioni 40/=, nusu tayari imeshapelekwa TRA


Baada ya kutuhumiwa kukwepa kodi kwa miaka mitatu mfululizo, kampuni kubwa ya uchimbaji madini ya Acacia imesema inatarajia kulipa kodi ya zaidi ya Sh40 bilioni mwaka huu wa fedha.

Mwishoni mwa Machi, Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT) iliitaka African Gold Mine (kwa sasa Acacia) kuilipa Serikali kodi ya Dola za Marekani 41.25 milioni (zaidi ya Sh89 bilioni), lakini kampuni hiyo ilikata rufaa na shauri hilo linasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa Tanzania.

Acacia inayomiliki Kampuni tatu ndogo za Bulyanhulu Gold Mining, North Mara na Pangea Minerals zinazoendesha shughuli zote za mapato ya mchimbaji huyo mkubwa kuliko wote nchini ambaye anaelezwa kukwepa kodi ya zuio la malipo ya gawio kwa wanahisa wake.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bradley Gordon ambaye aliwasili jana ili kutembelea miradi hiyo na kuzungumza na wafanyakazi wake, alisema Acacia bado haijaanza kutengeneza faida za kulipa kodi ya Mapato ya Kampuni kwa kuwa bado haijarudisha mtaji wake wa awali.

“Pamoja na kwamba tunatengeneza faida kwa jumla, hiyo haitozwi kodi kwa sababu bado hatujarudisha mtaji wa Dola za Marekani 3.8 bilioni. Mkataba wetu na Serikali ya Tanzania unaonyesha kuwa tutatakiwa kuanza kufanya hivyo kuanzia mwaka 2018,” inasomeka sehemu ya taarifa iliyotolewa na Gordon.

Makamu wa Rais wa Acacia, Deo Mwanyika alisema kuwa kampuni hiyo inaanza kulipa kodi ya mapato mwaka huu baada ya kurejesha mtaji wake iliyowekeza kupitia kampuni yake ya North Mara.

“Tumerudisha mtaji wetu na makadirio yanaonyesha tunaweza kulipa kodi ya Dola 20 milioni za Marekani (zaidi ya Sh40 bilioni). Nusu ya kiasi hicho tayari kimeshapelekwa TRA,” alisema.

Hotuba ya Maalim Seif aliyoitoa Jumapili, Aprili 10, 2016Ndugu zangu Waandishi wa Habari,

Ndugu Waalikwa,

Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima tukaweza kukutana hapa leo.

Namshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kuijaalia nchi yetu kwa kiasi kikubwa kubaki katika hali ya amani na utulivu licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na baadhi ya watu za kuivuruga amani yetu.

Naendelea kumuomba Mola wetu aendelee kuibariki nchi yetu na watu wake, aijaalie kuwa nchi ya amani na atujaalie hekima na busara katika kuendesha mambo yetu.

Nichukue fursa hii pia kukushukuruni nyinyi waandishi wa habari kwa kuitikia wito wetu na kuja kutusikiliza. Shukrani maalum zije kwenu wale ambao mmesafiri kutoka Dar es Salaam na kuja Zanzibar makhsusi kwa ajili ya mkutano huu.


Tunathamini sana mashirikiano yenu nyote tukitambua nafasi na mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika maendeleo ya nchi yoyote ile.

Mtakumbuka kwamba siku saba zilizopita tulizungumza nanyi ambapo tuliwasilisha kwenu maazimio 13 ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama Cha Wananchi (CUF) kuhusiana na msimamo wa Chama chetu dhidi ya ubakaji wa demokrasia Zanzibar uliofanyika tarehe 20 Machi, 2016 na ambao ulipewa jina la uchaguzi wa marudio.

Leo hii tumekuiteni ili kutimiza agizo nililopewa na Baraza Kuu lililonitaka nizungumze na wananchi wa Zanzibar ili kuwaeleza kwa kina mwelekeo wa hali ya kisiasa ya Zanzibar na hatua zinazochukuliwa na CUF kuhakikisha maamuzi halali ya kidemokrasia ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 yanaheshimiwa.

UCHAFUZI WA TAREHE 20 MACHI, 2016

Nilieleza kwa urefu katika mkutano wangu na waandishi wa habari wa tarehe 11 Januari, 2016 nilioufanya Dar es Salaam juu ya nini kilitokea baina ya tarehe 25 Oktoba 2015 hadi tarehe 28 Oktoba, 2015, siku ambayo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alitoa tangazo batili na haramu la kufuta uchaguzi huru na wa haki uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015. Nilieleza pia hoja za kikatiba na kisheria za kwa nini tangazo lile ni haramu na batili na hoja zile hadi leo watawala wameshindwa kuzijibu.

Kwa hoja hizo hizo, nikaeleza kwamba hakuna vifungu vya Katiba wala Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984 vinavyozungumzia kitu kinachoitwa uchaguzi wa marudio ukiondoa pale inapotokea wagombea wanapopata idadi sawa ya kura.

Sikusudii kurudia yale ambayo nilishayaeleza siku ile maana hayo sasa yanaeleweka na kila mtu ndani na nje ya nchi.

Leo hii nataka niwapongeze kwa mara nyengine tena wananchi jasiri na shupavu wa Zanzibar kwa kuitumia tarehe 20 Machi, 2016 kukifedhehesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mara ya pili ndani ya miezi sita mbele ya macho ya Watanzania na mbele ya macho ya jumuiya ya kimataifa.

Wananchi wazalendo wa Zanzibar wanaoipenda nchi yao waliwakataa watawala waovu wa CCM na sera zao mbovu zinazoidhalilisha Zanzibar yao kupitia sanduku la kura tarehe 25 Oktoba, 2015.

Watawala waovu wa CCM wakaamua kutumia mabavu na uvunjwaji wa katiba na sheria kuyapindua maamuzi ya Wazanzibari, kwa sababu tu maamuzi hayo yalikuwa ni ya kuwakataa watawala hao.

Kwa miezi mitano kuanzia Oktoba 2015 hadi Machi 2016, watawala waovu wa CCM wakawaingiza wananchi watulivu na wanaopenda amani wa Zanzibar katika idhilali na hilaki kubwa kwa kuwazuilia haki zao za msingi za binadamu ili wasiweze kuonesha hisia zao dhidi ya watawala.

Kwa namna ya pekee na ya ustaraabu wa hali ya juu na wa kupigiwa mfano, wananchi wa Zanzibar wakaisubiri tarehe 20 Machi, 2016 na wakapeleka ujumbe wao kwa watawala hao na kwa dunia nzima kwa njia za amani za kuususia uchafuzi ulioitishwa siku hiyo.

Hali halisi iliyoonekana na kila aliyetaka kuona ni kwamba zaidi ya asilimia 80 ya Wazanzibari hawakwenda kupiga kura siku hiyo ili kuonesha hisia zao na kuthibitisha tena maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba, 2015.

Kituo cha televisheni cha ITV kilichokuwa kikirusha matangazo ya moja kwa moja kutoka katika mikoa mitano ya Unguja na Pemba kilionesha vile vilivyoitwa vituo vya kupigia kura vikiwa havina watu kabisa au vikiwa na watu wachache sana.

Walipowahoji wale walioitwa maofisa uchaguzi na walioitwa mawakala kila mmoja alikuwa akija na majibu yake na takwimu zake zinazopingana na za mwenzake.

Vituo vya televisheni vya kimataifa hasa kile cha Al-Jazeera na CCTV ya China vilionesha na kuripoti vituo vikiwa vitupu. Hata televisheni ya watawala ya ZBC ilikuwa ikipata kigugumizi kuonesha hali ilivyokuwa katika vile vilivyoitwa vituo vya kupigia kura hadi kuamua kukatisha matangazo ya moja kwa moja. Magazeti ya Tanzania na ya nje ya nchi yaliripoti na kuchapisha picha zilizoonesha kususiwa kwa uchafuzi huo ulioitishwa na watawala wakidhani wanajihalalishia haramu yao.

Mitandao ya kijamii nayo ilijaa maelezo na vielelezo kutoka watu na taasisi za kimataifa zinazoheshimika vikionesha hali halisi ilivyokuwa na ujasiri wa Wazanzibari wa kuususia uchafuzi huo.

Na hatimaye nchi 16 zikatoa taarifa yao tarehe 21 Machi, 2016 wakieleza kwamba uchaguzi huo haukuwa wa kuheshimika kwa sababu haukuwa shirikishi na wala haukuwakilisha matakwa ya wapiga kura wa Zanzibar.

Nitumie fursa hii kwa mara nyengine tena kuwapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa ujasiri, uzalendo na ari kubwa walioionesha kwa kuitikia kwa kiasi kikubwa wito wa chama chao cha CUF wa kuwataka wasishiriki katika uhuni na ubakaji wa demokrasia uliopewa jina la uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016, na hivyo kuudhihirishia ulimwengu kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina ridhaa ya wananchi wa Zanzibar.

Naungana na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kuwapongeza waliokuwa wagombea wenzangu wa CUF kwa nafasi za Uwakilishi na Udiwani kwa kusimama na wananchi wa Zanzibar na kutoshiriki katika uchaguzi huo haramu na batili wa marudio, jambo ambalo limethibitisha kwamba hawapo kwa ajili ya kutaka nafasi na vyeo binafsi bali wanachotaka ni kuleta mabadiliko ya kweli kwa maslahi ya watu wote wa Zanzibar.

Pongezi zangu za dhati kabisa zinakwenda kwa wagombea Urais, Uwakilishi na Udiwani wa vyama vyengine vya upinzani ambavyo ni NRA, DEMOKRASIA MAKINI, SAU, UMD, JAHAZI ASILIA, CHAUMMA, UPDP, DP, na ACT-WAZALENDO, na vile vinavyoshirikiana kupitia UKAWA ambavyo ni CHADEMA, NCCR na NLD kwa kuungana pamoja na Wazanzibari kutetea demokrasia yao.

CCM WANAPENDA NAMBA LAKINI HAWAJUI HESABU

Jambo moja ambalo CCM wamejifedhehesha wenyewe ni lile la kutangaza kile walichokiita matokeo ya uchafuzi wao bila ya kuzingatia kwamba takwimu zina sifa moja, huwa hazisemi uongo.

Vijana wana msemo wao siku hizi; wanasema CCM wanapenda namba lakini hawajui hesabu. Matokeo ya tarehe 20 Machi, 2016 waliyoyatangaza ni kwamba eti jumla ya watu waliopiga kura walikuwa 341,865 na kwamba Dk. Ali Mohamed Shein eti alipata kura 299,982 sawa na asilimia 91.4.

Takwimu za uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 zilionesha kwamba jumla ya wananchi waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni 402,354 na Dk. Ali Mohamed Shein alipata kura 182,011 sawa na asilimia 46.28.

Wakati huo huo kwa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia, wapiga kura kwa upande wa Zanzibar walikuwa 417,882 ambapo mgombea wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli alipata kura 194,317 sawa na asilimia 46.5.

Kwa hivyo, kwa kutumia takwimu hizi, mtu anapochukua takwimu hizi na kulinganisha wapiga kura 402,354 waliojitokeza tarehe 25 Oktoba, 2015 na wale wanaodai eti walijitokeza tarehe 20 Machi kwamba ni 341,865 watawala wa CCM walichotaka kutuaminisha ni kwamba tofauti ya waliokuwa hawakujitokeza kupiga kura ilikuwa ni 60,489 tu. Suala la kujiuliza ni kwamba iwapo hilo ni kweli kwa nini vituo vionekane vitupu kabisa tarehe 20 Machi, 2016?

Lakini kwa upande mwengine, mtu anapokosa hata tahayuri na kudai Dk. Ali Mohamed Shein amepata kura 299,982 anachotaka kutwambia ni kwamba ndani ya miezi mitano ya idhilali na mateso aliyowapatisha Wazanzibari ameweza kuongeza kura 117,971.

Kufedheheka kwa CCM kunakuja zaidi kwamba walisahau kwamba waliyakubali matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa tarehe 25 Oktoba 2015 kwa upande wa Zanzibar ambapo kama tulivyokwisha onesha waliopiga kura walikuwa wengi zaidi wakiwa ni 417,882 (na hilo ungetegemea lingeinufaisha CCM) na bado mgombea wa CCM akapata kura 194,317 sawa na asilimia 46.5. Kwa kutumia idadi waliyotangaza ya kura 299,982 walizompa Dk. Shein wanataka kutwambia kwamba yeye amepata kura 105,665 zaidi kuliko Dr. Magufuli kwa Zanzibar.

Kama takwimu zao zingekuwa sahihi ina maana pia wapiga kura waliomuunga mkono mgombea wa CUF ambao hawakwenda kupiga kura ni 60,489 tu (sawa na asilimia 15 tu). Hivi nani utamdanganya kwamba Maalim Seif Sharif Hamad anaungwa mkono na asilimia 15 tu ya wapiga kura wa Zanzibar? Nani utamdanganya kwamba ndani ya miezi mitano, CCM imeongeza kura 105,665 zaidi ya alizopata mgombea wake Dk. Magufuli kwa upande wa Zanzibar?

Kutokana na ubabe na kiburi cha utawala walicho nacho CCM, wameishia kujifedhehesha kwa takwimu zao za kupika wenyewe. Ndiyo vijana wakasema, CCM wanapenda namba lakini hawajui hesabu.

NINI MWELEKEO WA CUF NA WAZANZIBARI BAADA YA UBAKAJI HUU WA DEMOKRASIA?

Wazanzibari walio wengi wamekuwa wakituuliza nini mwelekeo wa CUF baada ya ubakaji huu wa demokrasia? Wanatuuliza viongozi wao na hasa mimi tunatokaje katika hali hii ambayo imedumu miaka nenda miaka rudi kila pale Zanzibar inapofanya uchaguzi?

Kabla sijalieleza hilo, nataka niweke wazi leo kwamba tulipofanya uamuzi wa kuususia uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016 tuliamua kusimama juu ya uamuzi unaoheshimu misingi ya kikatiba ambayo watu wa Zanzibar tumeamua ndiyo inapaswa iongoze na iendeshe nchi yetu. Tulijua kwamba uamuzi huo utakuwa na athari kwa CUF na kwa Zanzibar lakini tulijua na tuliamini pia kwamba athari hiyo haiwezi kuwa kubwa zaidi kuliko gharama ya kuikanyaga Katiba na Sheria za nchi yetu na gharama za kupiga teke demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.

Tulipima na tukatafakari kwa kina na kuona ni kheri kumeza machungu ya athari binafsi kwetu lakini tusimame kidete na kifua mbele katika kutetea maamuzi ya watu wa Zanzibar waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015, na pia kulinda misingi ya Katiba na Sheria za nchi yetu na misingi ya demokrasia na haki za watu. Tuliona hayo ni kheri kwa huko twendako badala ya kushiriki katika haramu ya ubakaji wa demokrasia na matumizi ya nguvu za kijeshi kulazimisha watawala wasio na ridhaa ya watu.

Tulifanya maamuzi yale pia kwa lengo la kuepusha shari katika nchi yetu. Leo Wazanzibari na dunia nzima ni mashahidi kwamba uamuzi ule ulikuwa sahihi na wa busara. Maana mateso na vitisho walivyokumbana navyo Wazanzibari wakati tumewaachia uchaguzi ule watawala waovu peke yao vilikuwa vya kiasi kile kilichoshuhudiwa.

Je, tungeliamua kushiriki na kusimama kulinda na kutetea ushindi wetu hali ingekuwaje? Bila shaka nchi ingetumbukia katika machafuko ambayo watawala waovu walikuwa tayari yatokee kuliko kuridhia maamuzi halali ya wananchi wa Zanzibar.

Maamuzi yale yamethibitika pia kwamba ni sahihi kwa jinsi watu wa Zanzibar walivyoudharau na kuupuuza uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016. Watawala waovu wa CCM waliwadharau watu wa Zanzibar na watu wa Zanzibar wakaamua kuwadharau wao tarehe 20 Machi 2016.

Kwa upande mwengine, uamuzi tuliouchukua na kuusimamia pia ni uamuzi uliosimama juu ya misingi ya heshima na misingi ya utu wa watu, ambayo yalikuwa ndiyo malengo sahihi ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume, malengo sahihi ya Chama cha Afro Shirazi na malengo sahihi ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Kwa hakika, uamuzi wa kuupuuza na kuudharau uchafuzi wa tarehe 20 Machi, 2016 ni ushindi mwengine wa Zanzibar katika historia yake ya kisiasa.

Nimalizie sasa kwa kujibu hoja ya ni upi mwelekeo wa CUF na wa Wazanzibari baada ya ubakaji huu wa wazi wa demokrasia na haki za watu wa Zanzibar?

Kwanza, nirudie na kusisitiza msimamo wetu kwamba hatukubaliani na ubakaji wa demokrasia na haki za watu wa Zanzibar uliofanywa na watawala waovu wakisaidiwa na vyombo vya dola. Kwa msingi huo, Wazanzibari wataendelea kuipinga serikali isiyo na ridhaa ya watu kwa kutumia njia za amani, za kidemokrsia na zinazoendana na misingi ya Katiba na Sheria za nchi yetu.

Jana kumetangazwa kile kilichoitwa ni Baraza la Mawaziri. Msimamo wetu uko pale pale. Kama tusivyomtambua aliyelitangaza Baraza hilo, vivyo hivyo hatulitambui Baraza lake la Mawaziri.

Kwa hakika, kwa sababu msingi wa watawala waliojinyakulia madaraka ni kupitia uvunjwaji wa Katiba, kila kinachofuata kimekuwa kikiendeleza uvunjwaji wa Katiba. Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia Marekebisho ya 10 ya mwaka 2010, Ibara ya 9 (1) inalazimisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Ibara za 39, 39A na 42 za Katiba zimeeleza namna Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa itakavyoundwa. Masharti yote hayo yanaendelea kuvunjwa na mtawala aliyeamua kuyapiga teke maamuzi ya Wazanzibari na kujiweka madarakani kwa nguvu. Kwa hivyo, Serikali yake haiwezi kuwa Serikali inayokwenda na Katiba. Kwa ufupi, si Serikali halali kwa mujibu wa Katiba.

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF katika kikao chake cha tarehe 2 – 3 Aprili, 2016 lilipitisha maazimio yafuatayo miongoni mwa maazimio yake:

“Azimio Nam. 9:
Haliyatambui matokeo ya uchaguzi huo haramu na batili, na kwa msingi huo halimtambui Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa kuwa Wawakilishi na wala haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani. Baraza Kuu linaungana na wananchi wa Zanzibar waliokataa kuwapa uhalali watu hao na kwa hivyo halitoitambua Serikali, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zitakazoundwa na watu hao. CUF haitoshirikiana na Serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na Katiba ya Zanzibar, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu. Kwa vyovyote vile, Serikali itakayoundwa haitakidhi matakwa ya Katiba ya Zanzibar na hivyo CUF haitoshiriki kwenye uvunjaji wa Katiba ambayo inaeleza kwa uwazi kabisa namna ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

“Azimio Nam. 10:
Linawataka wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za amani, za kikatiba na kisheria ambazo zimewahi kutumika katika nchi nyingine duniani kuwakataa watawala waovu na wasio na ridhaa ya watu waliojiweka madarakani kwa kutumia nguvu na ubakaji wa demokrasia kwa kutoipa ushirikiano Serikali itakayoundwa na watawala hao.”

Baada ya maazimio hayo ya Baraza Kuu, kinachofuata sasa ni utekelezaji wake. Hivi sasa tunapanga mikakati madhubuti ya utekelezaji wa maazimio hayo kwa kutumia njia za amani, za kidemokrasia na za kikatiba ili kutufikisha kwenye malengo yetu ya kuona maamuzi ya watu wa Zanzibar yanaheshimiwa.

Nina hakika kabisa kuwa mikakati tunayoipanga itazaa hatua ambazo zitaibana Serikali haramu na hatimaye itasalimu amri kwa wananchi wa Zanzibar ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ndiyo wenye mamlaka ya kuiweka madarakani Serikali wanayoitaka. Katika dunia ya leo, hatuwezi kuongozwa na watawala ambao hawakupewa mamlaka na watu wenyewe.

Pili, naipongeza na kuishukuru jumuiya ya kimataifa na washirika wa maendeleo kwa msimamo waliochukua wa kukataa kubariki ubakaji huo wa demokrasia na haki za watu wa Zanzibar na kukataa kushiriki katika uapishwaji wa mtu asiye na ridhaa ya wapiga kura wa Zanzibar. Napongeza hatua ambazo wameanza kuzichukua dhidi ya Serikali za CCM ambazo ndizo zilizosimamia ubakaji huo wa demokrasia na haki za watu. Natoa wito kwao kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya watawala hawa waovu zikiwemo kuwawekea vikwazo vya kusafiri, kufuatilia akaunti zao za fedha nje ya nchi na hatua za kuchunguza matendo yao ya uhalifu dhidi ya binadamu. Wananchi waliodhulumiwa haki zao wanaziunga mkono hatua hizo wakiamini kwamba CCM ni lazima iwajibishwe kwa matendo yake maovu dhidi yao.

Nitumie fursa hii kwa mara nyengine tena kuwataka wananchi wa Zanzibar kudumisha amani ya nchi yetu na umoja wa watu wetu. Nikiwa kiongozi wao ninayewapenda na ambaye nimejitolea kuwatumikia katika umri wangu wote siwezi kuwaongoza kuelekea kwenye fujo na ghasia au vitendo vitakavyopelekea kuiharibu nchi yetu na kuathiri watu wetu. Nina imani kabisa kwamba njia tunayoifuata ni njia ya haki; na haki siku zote itashinda.

Mwaka 2009, mimi na mwenzangu, Dk. Amani Abeid Karume, tuliwaongoza Wazanzibari katika Maridhiano yaliyoashiria mwanzo wa ujenzi wa mahusiano mapya baina ya watu wema wa Zanzibar kwa kuzika siasa za ubaguzi, utengano, chuki, hasama na fujo na badala yake kusimamisha siasa za maelewano, umoja, upendo, mshikamano na udugu katika jamii yetu.

Tulitegemea kuanzia pale tungeendelea mbele kwa kuchukua hatua za kuyaimarisha maridhiano yetu na kuyazamisha zaidi kwenye nyoyo za Wazanzibari. Binafsi nasikitishwa na kuhuzunishwa sana kuona watawala waovu wasiowatakia mema watu wa nchi hii wameturudisha tulikotoka kwa maslahi yao binafsi.

Natoa wito kwa Wazanzibari wenzangu kuwa tukatae kurudishwa kwenye siasa zile za ubaguzi, utengano, chuki, hasama na fujo na kila mmoja afanye lile liliomo katika uwezo wake kuendeleza maelewano, umoja, upendo, mshikamano na udugu katika jamii yetu.

Wazanzibari tumeamua kuisimamisha tena Zanzibar yetu na Zanzibar itasimama tena Inshallah. Hilo sina wasiwasi nalo kama kiongozi wa Wazanzibari waliyenipa ridhaa yao.

HATIMAYE TUTASHINDA.

WANANCHI JASIRI NA SHUPAVU WA ZANZIBAR WATASHINDA.

Ahsanteni sana.
Wakurugenzi kufutwa kazi wakishindwa kutenga mapato: 5% kwa vijana, 5% kwa wamama

OFISI TA WAZIRI MKUU

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amesema Mkurugenzi yeyote wa Halmashauri nchini atakayeshindwa kutenga asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya wanawake na vijana ataondolewa.

Amesema suala la kila Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi ni la lazima na si hiari.
Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo leo (10 Aprili, 2016) alipokuwa anazungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Kitandi, Mtimbo, Likunja, Nkowe na Namahema ambako lifanya mikutano ya hadhara.

“Halmashauri ambayo itashindwa kutenga asilimia 10 kwa maana asilimia tano kwa ajili ya vijana na tano kwa ajili ya akinamama Mkurugenzi wake atakuwa anatafuta safari,” amesema Waziri Mkuu, Majaliwa.

Waziri Mkuu, Majaliwa yupo wilayani Ruangwa, Lindi kwa ajili ya ziara ya kikazi inayolenga kukagua shughuli za maendeleo, ambapo amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutimiza wajibu wao na serikali haitamvumilia yeyote atakayeshindwa.

Pia Waziri Mkuu, Majaliwa amewataka wananchi hao kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili zitakapofika sh milioni 50 za kila kijiji zilizoahidiwa na Rais, Dk. John Magufuli waweze kunufaika.
Amesema fedha hizo ambazo zitatolewa kuanzia mwezi Julai mwaka huu zitagawiwa katika vikundi mbalimbali vilivyosajiliwa na si kwa mtu mmoja mmoja hivyo amewataka watendaji wa kata na vijiji kuwahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu, Majaliwa amesema serikali imefuta tozo tano kati ya tisa za zao la korosho zilizokuwa kero ya muda mrefu na kufanya wakulima wachukie mfumo wa Stakabadhi ghalani.

MWISHO
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu

Safari ya Wakuu 10 wa Wilaya na Wakurugenzi 10 China yafutwa

Ikulu imefuta safari ya wakuu wa wilaya 10 na wakurugenzi idadi kama hiyo waliotakiwa kwenda China kwa mafunzo ya uchumi wa kimaeneo kuanzia jana, na kuna uwezekano mkubwa ikatangaza uteuzi mpya leo.

Wakuu hao wa wilaya na wakurugenzi wao (majina tunayahifadhi) walikuwa waondoke jana kwa ufadhili wa Serikali ya Watu wa China, lakini habari ambazo Mwananchi imezipata Ikulu iliamua kutotoa kibali, hali inayozidisha ubashiri kuwa uamuzi huo umetokana na kukamilika kwa uteuzi wa wakuu wapya.

Safari hiyo ilishakamilika kwa kiwango kikubwa baada ya kupata visa na wengi wao kuwasili jijini Dar es Salaam tayari kwa safari hiyo, lakini wakalazimika kurejea kwenye vituo vyao baada ya kukosa kibali cha Ikulu ambacho hutolewa na Katibu Mkuu Kiongozi.

Mara tu baada ya kuapishwa Novemba 5 mwaka jana, Rais John Magufuli alitangaza kudhibiti safari za nje za watumishi na viongozi wa umma kwa kuagiza kuwa Ikulu ndiyo itakayotoa kibali baada ya kujiridhisha na umuhimu wa safari hizo kwa Taifa.

Tangu atoe agizo hilo, ni mawaziri wawili tu ambao wameruhusiwa kwenda Vietnam kwenda kujifunza kilimo na viwanda. Mawaziri hao ni Mwigulu Nchemba (Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi) na Charles Mwijage (Viwanda na Biashara).

Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji alikwenda nchini Ethiopia kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa fedha, wakati kwa nyakati tofauto Makamu wa Rais Samia Suluhu na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walikwenda Afrika Kusini na Botswana.

Mpaka sasa, Rais Magufuli amefanya safari moja tu ya nje alipokwenda Rwanda kwenye maadhimisho ya mauaji ya kimbari.

Lakini safari ya wakuu hao wa wilaya ilikuwa ifadhiliwe na China, kwa mujibu wa habari hizo na hivyo isingeisababishia Serikali kutumia vibaya fedha za walipa kodi.

Uamuzi huo unaonekana kuzingatia zaidi uteuzi wa wakuu wapya ambao taarifa zinasema unaweza kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa, wakati wa wakurugenzi wa wilaya unatazamiwa kutangazwa baadaye wiki hii au wiki ijayo.

Juhudi za kumpata Katibu Mkuu Kiongozi John Kijazi kuzungumzia suala hilo, hazikuzaa matunda.

Kuanzia saa 7:00 mchana alitafutwa kwa simu na alikuwa hapokei na mara mbili wakati wa jioni alipokea na kukata bila ya kuzungumza lolote, kuashiria kuwa yuko kwenye kazi nyingine muhimu.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alikiri kuwapo kwa safari hiyo, lakini akasema hajui kama imeidhinishwa na Ikulu kwa kuwa si muhusika.

“Katika hatua za awali nilisaini safari hiyo kuwaruhusu waende China, lakini sijui kama wamenyimwa kibali kwa sababu hilo si suala la ofisi yangu,” alisema Waziri Simbachawene.

Kama ni kweli, alifafanua Simbachawene, inaweza kuwa ni kutokana na umuhimu wao wa kuwatumikia wananchi kwenye maeneo wanayotoka. “Hawawezi kuondoka na kuziacha wilaya zao ilhali wao ndiyo waangalizi,” alisema Simbachawene.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa alisema yupo nje ya ofisi hivyo hana taarifa kamili. “Nilikuwa msibani na hivi sasa nipo safarini natoka Njombe. Nikifika ofisini nitakuwa na majibu sahihi,” alisema Msigwa na kukumbusha kuwa aliyekataza safari za nje ni Rais na hakuna anayeweza kufanya kinyume na hilo.

“Inawezekana mamlaka imeona hakuna tija ya kuwaruhusu waondoke hata kama wanalipiwa na Serikali ya China,” aliongeza.

Rais aliwasimamisha kazi watumishi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kosa la kukaidi agizo lake la kutosafiri bila kupata kibali. Watumishi hao ni Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani, Rukia Nikitas na Mary Mosha.

Sakata la wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri limekuja katika kipindi ambacho Rais anasubiriwa kutangaza safu yake mpya kwenye uongozi wa wilaya baada ya kukamilisha wakuu wa mikoa mwezi uliopita.

Akiwa Chato mkoani Geita, Rais aliwataka wakuu wa wilaya kuchapa kazi badala ya kuwa na woga wa kutoteuliwa akisema uchapaji kazi ndio utawafanya waendelee kuwapo kwenye nafasi zao.

Rais pia amekuwa akitoa maelezo kadhaa yanayoonyesha atafanya uteuzi kwa kutumia vigezo hivyo, hasa suala la elimu ambayo inakabiwa na tatizo kubwa la uhaba wa madawati na vyumba na majengo, kipindupindu, njaa, migogoro ya ardhi na watumishi hewa.

Baadhi ya wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuueleza umma jinsi wanavyofanya kazi kutatua changamoto zinazozikabili jamii wanazoziongoza, huku mmoja wao akiwa ameshamuomba Rais asimfikirie kwenye uteuzi mpya.

NW atoa maagizo kuhusu kiwanja cha TBC kilichopo Kimani

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia Wambura amemuagiza Meneja wa Miradi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC ) Bw. Mackselin Chota kuhakikisha kiwanja Na.1 Kitalu “B” kilichopo eneo la Kimani wilaya ya Kisarawe kinapatiwa Hati Miliki ili kuepusha kuvamiwa pamoja na migogoro inayoweza kutokea.

Agizo hilo amelitoa jumamosi wakati alipotembelea kiwanja hicho na kueleza kuwa kiwanja hicho ni lazima kiendelezwe kwa ajili ya kuwasaidia wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo kiwanja hicho kilitafutwa kwa dhumuni hilo.

“Naishukuru Halmashauri kwa kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo,hivyo natoa siku saba kwa idara ya Miradi ya TBC kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha kiwanja hicho kinapatiwa Hati”. Alisema Mhe. Annastazia.

Aidha amewataka kuwasilisha gharama zilizotumika katika ujenzi wa nyumba zilizopo katika eneo hilo na wapi zimetoka na sababu zilizosababisha ujenzi huo kukwama kwa zaidi ya miaka mitatu.

Akitoa maelezo kuhusu Kiwanja hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Bi Mwanamvua Mrindoko amesema kuwa kiwanja hicho kilipimwa na ramani yake ya upimaji ilipata kibali cha Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kusajiliwa kwa namba 68480,ramani namba E 292/83 ya tarehe 22 februari, 2012.

“Taratibu za umilikishwaji zilifanyika kwa kuandaliwa gharama za kulipia kabla hati haijaandaliwa,malipo hayo yalifanywa na TBC kupitia NMB na kuwasilisha fomu ya malipo hayo (Bank pay in slip)”. Alisema Bi Mwanamvua.

Naye Meneja wa Miradi wa Shirika la Utangazaji Tanzania Bw. Mackselin Chota amesema kuwa Shirika hilo lina jumla ya viwanja 55 nchi nzima,ambavyo 19 kati ya hivyo vina Hati miliki ambapo katika mkoa wa Pwani kuna kiwanja kimoja, Dar es Salaam viwanja vitano ambavyo viko Pugu Road, Kunduchi, na TAZARA, Mikocheni na Sinza.
  • Shamimu Nyaki, WHUSM.

Wanakijiji waliozuiwa kulima tangu 1992 wakabiliwa na njaa

Wananchi wa Olbili na mabango yao.
KIJIJI cha Olbili kilichopo kitongoji cha Tilili, kata ya Shambarai wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kinakabiliwa na tatizo la ukosefuchakula cha miongoni mwa familia nyingi hali inayochangia kuzorota kwa hali ya lishe na shughuli za kijamii pamoja na za kiuchumi.

Wananchi wa kijiji hicho Zuhura Salim na Anna Lazaro wamesema kuwa uhaba huo wa chakula unatokana na kunyang`anywa maeneo waliyokua wanatumia kwa kilimo na kutumika kama ardhi ya malisho.

Wananchi hao waliandamana na mabango yao kuzunguka eneo la shamba hilo wameiomba serikali kupitia wizara ya ardhi na wizara ya kilimo kuingilia kati mgogoro huo baina yao na wafugaji wanaogombea eneo hilo ambalo kwa zaidi ya miaka 24 tangu mwaka 1992 hadi mwaka 2013 ambapo walizuiwa kutumia maeneo hayo ambayo walikua wakiyatumia kwa shughuli za kilimo cha kujikimu.

Eliud Jackson ni Mwanakijiji wa Olbili amesema kuwa licha ya kunyimwa maeneo ya kulima pia mwaka huu hawakupata chakula cha msaada kama kata nyingine zilizopata mgao huo hivyo kuteseka na njaa wao na watoto wao ,wamemuomba Rais Magufuli kutazama suala hilo na kulipatia ufumbuzi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tilili Kingi Lomayani Laizer amesema kuwa baada ya kuzuiliwa kulima na Mtendaji wa Kata na Diwani aliyekua madarakani walifika katika ngazi za wilaya bila mafanikio hivyo wanamuomba Mkuu wa Mkoa wa Manyara afike kutatua mgogoro huo ili kuwanusuru na baa la njaa.

“Nimefuatilia suala hili kwa Mwenyekiti, Mtendaji wa kata na Diwani aliyemaliza muda wake bila mafanikio kwani wao ndio walitoa zuio la kutuzuia kulima katika maeneo haya, inaonekana jambo hili linashikiliwa na wafugaji wenye fedha wanatumia fedha zao kuwanyanyasa wakulima” Alisema Laizer. Aliiomba serikali kupitia wizara ya kilimo, ardhi kufika katika kijiji hicho na kutatua kero hiyo ya muda mrefu kwani wamekua wakishindwa kuendesha familia zao kutokana na kutegemea kilimo kama shughuli ya kuwapatia chakula na kipato.
  • Na Woinde Shizza, Simanjiro.

Taarifa rasmi ya kutenguliwa uongozini Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala Shinyanga