Taarifa ya habari ChannelTEN Mei 9, 2016Baraza la Madiwani jijini la Dar yabatilisha uuzwaji wa hisa za UDA

Wajumbe wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamebatilisha uuzwaji wa hisa za halmashauri ya jiji, asilimia 51 ya hisa zilizopo katika shirika la Usafirishaji la Jiji la Dar es Salaam (UDA) na kuzirejesha kwenye Mamlaka ya jiji hilo kutoka kwa mmiliki wa sasa hisa hizo, Kampuni ya Simon Group Limited (SGL), baada ya kubaini kuwa mnunuzi wa hisa hizo ambaye ni kampuni ya SGL, hakufuata taratibu katika mchakato wa kuzinunua na kubainika kuwepo kwa udanganyifu mkubwa katika umiliki wake.

Akitangaza mbele ya wanahabari jijini Dar, Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Isaya Mwita amesema hakuna kumbukumbu zozote zinazoonesha kuwa mwanahisa mwenza wa Halmashauri ya Jiji katika UDA, yaani Msajili wa Hazina aliridhia Halmashauri ya Jiji kuuza hisa kwa mtu mwingine. 

Hapo awali, Halmashauri ya Jiji ilikuwa inamilikia asilimia 49 ya hisa huku Kampuni ya Simon Group Limited ikimiliki asilimia 51,

“Sisi kama Jiji tumeona ni busara. Hazina hawafanyi biashara, serikali haifanyi biashara, kazi yake ni kukusanya kodi. Wanaweza kuamua kwa makusudi wakachukua zile hisa 49 ili kuondoa mgogoro huo ambao hauna tija, wakamkabidhi Simon Groups halafu sisi tukabaki na hisa zetu 51 tukaendelea kuwahudumia Wanadaresalam. Ni hatari sana kama shirika, sisi tukajiondoa wakati huo wakati sisi ndiyo tunaosimamia shughuli za usafirishaji jijini Dar es Salaam, ”amesema Mwita.

Mwita ambaye pia nia Diwani wa Kata ya Vijipweni kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema hisa hizo pia ziliiuzwa bila ya kuzingatia sheria ya Manunuzi ya Umma (Public Procurement Act) kutokana na Kampuni ya SGL kutokuwa mwanahisa katika ununuzi wa hisa zisizogawiwa (unallocated shares) jambo analodai ndiyo sababu hisa hizo zilirudishwa, na sasa wanashangaa tena kampuni hiyo kuzipewa.

Sanjari na makosa hayo, pia Mwita ambaye ni meya anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa kutetea katiba ya Wananchi (UKAWA) ameendelea kutaja makosa yaliyofanywa katika uuzaji huo ni hatua ya kutofanyika kwa uthamini wa mali za shirika la UDA kabla ya kuuzwa shirika hilo.

Amesema baada ya Baraza la Madiwani kubaini upungufu huo wajumbe hao waliazimia kuwa fedha zilizolipwa kwa Halmashauri ya jiji na Kampuni ya SGL kwa ajili ya kununua shirika hilo zisirudishwe mpaka pale tathimini itakapofanyika na kujiridhisha kuwa kampuni ya Simon haidaiwi kitu baada ya kubainika kuwa kampuni ya SGL ilitumia mali za UDA kujinufaisha.

Madiwani hao waliridhuia pendekezo la kuundwa kwa kamati ndogo ili ifanye kazi ya uchunguzi wa kina kuhususiana na ubatilishaji wa uuzwaji hisa za Halmashauri ya jiji.

Mwita amewataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Halima Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe, Abdallah Mtolea ambaye ni mbunge wa Kinondoni pamoja na Jummane Mtinangi ambaye ni Mwanasheria wa Jiji.

Mwenyekiti wa Simon Grops Limited, Simon Kisena ameiambia TBC kuwa atatolea ufafanuzi suala hilo mbele ya wanahabari wakati mwingine.

Nauli zilizotanganzwa na SUMATRA kwa mabasi ya DART yanayoanza usafirishaji kesho

Mamlaka ya udhibiti na usafiri wa nchi kavu SUMATRA, imetangaza nauli za mabasi yaendayo haraka, DART, ambayo yataanza shughuli kesho kuanzia saa 11 alfajiri mpaka saa 6 usiku.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salam, Mkurungenzi Mkuu wa SUMATRA Gilliard Ngewe ametaja rasmi leo 09/05/2016 kuwa nauli hizo ni:
  1. Wanafunzi 200/=
  2. Feeder (Njia za Pembeni) 400/= 
  3. Trunk (Njia Kuu) 650/=
  4. Trunk/Feeder (Muunganiko kwa njia za pembeni na njia kuu) 800/=
TAFSIRI

1. Wanafunzi (inaeleweka).

2. Trunk sh. 650/= Ni pale utakapokuwa umepanda Basi la DART linalopita kwenye njia maalumu. Mfano kuanzia Kimara - Kivukoni, Kimara - Kariakoo, Morocco - Kivukoni, Morocco - Kariakoo. Hii haijalishi unapita vituo vingapi au unashukia kituo gani kama ilivyo kwenye daladala.

3. Feeder sh. 400/= Ni pale utakapopanda Basi la DART ambalo linafanya kazi nje ya mfumo (barabara maalum za DART). Mfano Kimara - Mbezi.

4. Trunk/Feeder sh. 800/= hapa ni pale utakapo tumia aina zote za usafiri kwa kuunganisha, mfano Mbezi - Kimara halafu Kimara - Posta.

Mkurugenzi Mkuu wa DART, Ronald Lwakatare amesema huduma hiyo itatolewa bure kwa muda wa siku mbili mara baada ya kuanza kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi na kuzungumzia usalama wao wakieleza kuwa suala la milango kuwa upande wa kushoto badala ya kulia, limeangaliwa.

Leseni ya mwaka mmoja ya magari hayo kuanza kufanya kazi imeteolewa na Ngewe kwa UDA ili kufuatilia utendaji kazi wa mabasi hayo.Sababu zinazochochea wabunge kujiingiza kwenye rushwa

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ametaja sababu zinazochochea wabunge kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa, ni presha kutoka kwa wananchi inayotokana na kutakiwa kuchangia masuala mbalimbali katika majimbo yao.

Spika huyo pia amewatangazia rasmi wabunge kuwa Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatarajia kuwasilisha bungeni muswada wa sheria utakaotenganisha uongozi na biashara.

Aliyasema hayo wakati akizungumza katika uzinduzi wa Chama cha Wabunge wanaopambana na Rushwa (APNAC), mjini hapa. Aliwataka wabunge hao kujiepusha na vitendo vya rushwa licha ya kuwa na maslahi madogo.

Pia aliwataka wajiandae na sheria hiyo kutokana na ukweli kuwa katika bunge hilo wabunge wengi pia ni wafanyabiashara. Presha za rushwa Alitaja sababu za wabunge wa Tanzania kujiingiza kwenye rushwa ni presha za wananchi wao kuwataka wachangie kila inapotokea msiba, sherehe, madawati, madarasa, barabara hadi ada.

Alisema kutokana na kipato kidogo cha fedha, wabunge wengi hutafuta mbinu mbadala za kupata fedha kumudu gharama hizo. Mishahara ya wabunge na marupurupu yake kwa mwezi yanakadiriwa kufikia zaidi ya Sh milioni 11 kwa mwezi.

Sababu nyingine ni mikopo yenye riba kubwa ambayo wabunge wengi wameichukua ikiwa ni pamoja na maslahi madogo wanayopata wabunge hao. “Kutokana na hali hii wakati mwingine humfanya kiongozi ahangaike kutafuta fedha na ndipo wengine hujiingiza katika vitendo hivi vya rushwa.

Nawatahadharisha ninyi kama wabunge mnao wajibu wa kudhibiti rushwa na kuwa mfano katika jamii,” alisema. Spika alilia maslahi Alisema katika eneo la maslahi, ofisi ya Bunge inatambua kuwa bado maslahi wanayopata wabunge hao ikilinganishwa na kazi wanayofanya ni madogo hivyo, wanaendelea kuangalia namna ya kuyaboresha.

Ndugai alisema wabunge wa Tanzania wana wajibu na jukumu kubwa la kudhibiti rushwa kwa kutunga sheria zinazopaswa kutumika katika kuunga mkono au kuleta miswada itakayosaidia kutokomeza rushwa. Alisema pia moja ya kazi ya wabunge ni kushauri na kusimamia Serikali.

Alisema ni vyema pale ambapo kuna viashiria vya rushwa wakatoa ushauri huo bila kukubali kushawishiwa kwa rushwa. “Vilevile katika kupitisha bajeti za serikali, hapana budi kuhakikisha vyombo vinavyohusika na mapambano dhidi ya rushwa vimetengewa fedha za kutosha,” alisema.

Aliwaasa wabunge kujiepusha na vishawishi vya rushwa kwa kuwa nafasi waliyonayo ni nyeti. Alisema pia kutokana na mwenendo wa umakini wa Serikali ya Awamu ya Tano, inawezekana wakawepo watu wanaoona umakini huo kama maslahi yao na kutumia njia pekee ya kuwarubuni wabunge.

“Nawaasa msishawishike,” alisisitiza. Alisema kwa mujibu wa Jumuiya ya Vyama vya Wabunge Wanaopambana na Rushwa Afrika (GOPAC), takribani dola za Marekani bilioni 50 hutoroshwa Afrika kutokana na rushwa. “Hizi ni fedha nyingi sana za walalahoi zinazotumika kwa maslahi ya wachache,” alisema.

Pia amehamasisha wabunge hao kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kile alichosema, katika awamu hii ya serikali ya awamu ya tano, yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo lazima aingie matatani. Sheria ya maadili “Muda si mrefu nitawaalika waje watoe semina kwenu kuhusu undani wa sheria hiyo ili wote muielewe vyema.

Nawashauri muisome vizuri sheria hii ikija kwa sababu wengi wetu pamoja na ubunge tunafanya biashara ili tujiendeshe vizuri,” alisisitiza Ndugai. Alisema sheria hiyo ikipitishwa, haitakuwa ya kwanza Tanzania kuitekeleza kwani nchi nyingi duniani zimekuwa na mfumo unaotenganisha viongozi wake na biashara.

“Wenzetu ni kawaida ukiingia kwenye siasa unakabidhi biashara yako mpaka pale utakapomaliza uongozi wako ndio unaruhusiwa kuendelea, naomba mjiandae kuipokea sheria hii, ni sheria nzuri na ina malengo mazuri,” alisema. Akizungumzia rushwa, alisema kila bunge lina sababu zake za wabunge kujiingiza katika vitendo vya rushwa .

Wabunge; sheria hiyo ni mwiba Baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili baada ya mkutano huo kumalizika, walisema sheria itakayotenganisha viongozi na biashara ni mwiba kwa wabunge wengi na itakapowasilishwa bungeni itazua tafrani.

“Sikufichi, wabunge wengi sisi hapa mnavyotuona ni wafanyabiashara, ukituvua tu nafasi ya biashara hatuna kitu, hili kwa kweli kwetu ni mtihani haya tusubiri tuone,” alisema mmoja wa wabunge hao aliyekataa kutaja jina lake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, aliwataka wabunge kujiepusha kuhusishwa na rushwa akisisitiza kwamba, kutokana na nafasi yao katika jamii, wanapaswa kuwa mstari wa mbele kudhibiti tatizo hilo na kuwa mfano mbele ya jamii hiyo.

“Niwaambie ukweli kwa nafasi hii tuliyonayo wabunge wenzetu hatutakiwi hata kutuhumiwa kwa rushwa. Sisi ndio tunatakiwa kuwa mstari wa mbele kupambana kwa vitendo na walarushwa nchini mwetu,” alisema.

Aidha alizungumzia suala la malalamiko ya adhabu kwa walarushwa kuwa ndogo na kukiri kwamba adhabu zinazotolewa kwa watu wanaothibitika kufanya vitendo vya rushwa ni ndogo ikilinganishwa na hasara iliyotokana na rushwa hiyo.

“Nawaahidi hili tumelipokea la adhabu na tutawasilisha mapendekezo kwa ajili ya kuifanyia kazi sheria yetu ya rushwa. Naomba wabunge wenzangu mtuunge mkono kwa hili,” alisema Waziri Kairuki.

APNAC yapongeza kupunguza rushwa Akiwasilisha mada ya kuhusu tathmini ya shughuli za APNAC katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Mhadhiri wa Siasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Davis Mwamfupe, alisema chama hicho kimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kueneza uelewa wa tatizo la rushwa hususan kwa wabunge.

Hata hivyo, alisema changamoto kubwa iliyopo katika kutatua tatizo la rushwa, ni kutokana na mara zote rushwa kufanyika kwa siri na hufanywa na watu wenye nafasi kubwa katika jamii wakiwemo wanasiasa na wachumi hivyo kuwa vigumu kuwakamata.

Aliwataka wabunge hao kutotumia nafasi zao ndani ya Bunge na kukemea rushwa kwa mdomo pekee bali waoneshe dhahiri kuichukia na kupambana nayo kwa vitendo. Mbunge wa Nkasi, Ally Keissy, wakati akichangia mada hiyo ya rushwa, alisema tatizo la rushwa litamalizika endapo Mahakama na vyombo vya dola vitachunguzwa kutokana na ukweli kuwa kesi nyingi za rushwa zimefunguliwa, lakini hazishindi.

Taasisi zatii agizo la serikali na kuachana na benki za kibiashara

MASHIRIKA na taasisi zote za serikali zimetii agizo la serikali la kufunga akaunti zake katika benki za biashara na kuhamisha fedha zilizoko katika akaunti hizo kwenda akaunti walizoamriwa kufungua Benki Kuu (BoT).

Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki kuwa baada ya kutoa agizo hilo na kuwapa muda kukamilisha kufunga akaunti hizo, mashirika na taasisi zote zaidi ya 200 walianza mchakato ndani ya muda husika.

Alisema mpaka sasa kuna taasisi au mashirika chini ya 50 ambayo hayajakamilisha uhamishaji wa akaunti hizo kwa sababu mbalimbali ikiwemo zilizo katika mikoa ambayo hakuna tawi la BoT.

Alifafanua kwamba si rahisi kwa mashirika yote kufanikisha hatua zote ndani ya muda waliopewa, kwa kuwa baadhi ya mashirika, ufunguzi wa akaunti ni lazima ufanyike kwa uamuzi wa bodi ya wakurugenzi.

Mafuru alisema akaunti nyingine za mashirika na taasisi hizo, ziko katika akaunti za muda maalumu katika benki hizo za biashara, hivyo kabla ya kuzifunga na kuhamisha fedha husika, kutahitajika majadiliano kati ya shirika au taasisi husika na benki yake.

Februari mwaka huu ambao ulikuwa muda wa kukamilisha kuhamisha akaunti, Msajili wa Hazina aliwataka watendaji wakuu wote wa mashirika na taasisi za serikali kufuata maelekezo matano ya kufunga akaunti zao katika benki za biashara na kuhamishia fedha hizo BoT.

Katika agizo la kwanza, watendaji hao walitakiwa kufungua akaunti ya mapato yao kwa aina ya fedha za mapato wanayopokea; Kama ni za kigeni au shilingi za Tanzania, katika tawi la karibu yao la BoT haraka iwezekanavyo.

Baada ya kufungua akaunti hizo, watendaji hao wametakiwa kuelekeza makusanyo yote ya fedha za ofisi zao ikiwemo fedha za ruzuku zinazotoka serikalini kwenda katika akaunti mpya zilizofunguliwa katika matawi ya BoT.

Agizo la tatu la Serikali kwa watendaji hao ni kuhamisha fedha zote zilizobakia katika akaunti zao zilizoko katika benki hizo za biashara na kupeleka katika akaunti mpya zilizoko BoT.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uhusiano pekee kati ya mashirika hayo na benki za biashara itakuwa akaunti itakayohifadhi fedha za uendeshaji ambayo imetakiwa kuwa na fedha zinazotosha uendeshaji wa shughuli za taasisi zao kwa mujibu wa matarajio ya matumizi yao ya kila mwezi.

TWPG yatoa tamko Bungeni kuhusu kudhalilishwa wabunge wanawakeMwenyekiti wa Chama cha wabunge wanawake Tanzania (TWPG), Magreth Sitta, amelaani vikali vitendo vya kutolewa kwa lugha za matusi na udhalilishaji dhidi ya wabunge wanawake bungeni na kusema hakiwezi kumvumilia mbunge yeyote atakayetoa lugha hizo.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa chama hicho leo bungeni baada ya kipindi cha maswali na majibu Bi.Magret ametoa maelezo binafsi kuhusu kitendo kilichotokea Mei 5 mwaka huu, ambapo Mbunge wa Ulanga Mashariki, Goodluck Mlinga alitoa lugha ya kudhalilisha dhidi ya wabunge wanawake wa upinzani kwa kusema kuwa waliingia katika bungeni baada ya kuitwa 'baby' wa mtu. 

Amesema kuwa chama hicho kimejikita katika kuhakikisha haki za wanawake ndani na nje ya Bunge zinafuatwa, ikiwa ni pamoja na kupinga ukatili na udhalilishaji dhidi yao.

Pia amesema katika kutetea na kuangalia haki za wanawake, hakuangaliwi tofauti za kiitikadi za kisiasa bali kinachoangaliwa ni haki za wanawake wote kwa ujumla wao.

"Chama chetu kinatazama umoja wetu wanawake wote humu bungeni na nje ya Bunge, na kupinga udhalilishaji unaoelekezwa kwa wanawake," anasema.

"Kutokana na malengo ya chama chetu tumeona tutoke tamko hili, kwa kuwa kuna wabunge walitoa maneno ya kudhalilisha utu na hadhi ya mwanamke..tunalaami vikali na hatukubaliani na vitendo vya hivi kwa wabunge wanawake iwe humu ndani ya Bunge na hata nje ya bunge"anasisitiza Magreth.

Hata hivyo chama hicho kilikitaka kiti cha Spika kuchukua hatua ya haraka ya kinidhamu dhidi ya mbunge atakayerudia kutoa lugha za namna hiyo dhidi ya wabunge wanawake.

Aidha chama hicho pia kilitoa wito kwa wabunge wote kujiheshimu na kuwaheshimu wabunge wengine ili kuendelea kulinda hadhi na heshima ya Bunge hilo.

"Wabunge tunapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii yetu. Tunaamini kuwa hili litakuwa tukio la mwisho. Tunapaswa kuheshimiana bila kujali tofauti ya kijinsia pamoja na tofauti za kiitikadi za vyama. Pia wabunge wanawake tunapaswa kuendelea kuwa pamoja na tusikubali kugawanywa kutokana na maneno mbalimbali yanayoelekezwa kwetu.'

Rais Magufuli azindua jengo la kitega uchumi la PPF jijini Arusha


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, akihutubia wakazi wa arusha na wadau wa Mfuko wa Pensheni wa PPF wakati alipozindua rasmi, Jengo la Kitegauchumi la Mfuko huo (PPF) lililopo Mtaa wa Korido Jijini Arusha leo, Mei 9, 2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, akikata utepe kuzindua rasmi, Jengo la Kitegauchumi la Mfuko wa Pensheni (PPF) lililopo Mtaa wa Korido Jijini Arusha leo Mei 9, 2016. Wa pili (kushoto) ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenister Mhagama, (kushoto) ni Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro (wa kwanza kutoka kulia) ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya PPF, Ramadhan Kijjah, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, akikata utepe kuzindua rasmi, Jengo la Kitegauchumi la Mfuko wa Pensheni (PPF) lililopo Mtaa wa Korido Jijini Arusha leo Mei 9, 2016. Wa pili (kushoto) ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenister Mhagama, (kushoto) ni Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro (wa kwanza kutoka kulia) ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya PPF, Ramadhan Kijjah, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, akimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, William Erio, baada ya kuweka Jiwe la Msingi la uzinduai wa Jengo la Kitegauchumi la Mfuko huo lililopo Mtaa wa Korido Jijini Arusha leo Mei 9, 2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPF, Ramadhan Kijja, wakati alipowasili kwenye Viwanja vya Jengo la Kitegauchumi la Mfuko wa Pensheni PPF lililopo Mtaa wa Korido jijini Arusha kwa ajili ya uzinduzi wa jengo hilo leo Mei 9, 2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio, wakati alipowasili kwenye Viwanja vya Jengo la Kitegauchumi la Mfuko wa Pensheni PPF lililopo Mtaa wa Korido jijini Arusha kwa ajili ya uzinduzi wa jengo hilo leo Mei 9, 2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, akisalimiana na baadhi ya Wadau wa Mfuko wa Pensheni PPF, wakati alipowasili kwenye Viwanja vya Jengo la Kitegauchumi la Mfuko wa Pensheni PPF lililopo Mtaa wa Korido jijini Arusha kwa ajili ya uzinduzi wa jengo hilo leo Mei 9, 2016. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, akisalimiana na Meneja wa PPF Kanda ya Arusha, Onesmo Ruhasha, wakati alipowasili kwenye Viwanja vya Jengo la Kitegauchumi la Mfuko wa Pensheni PPF lililopo Mtaa wa Korido jijini Arusha kwa ajili ya uzinduzi wa jengo hilo leo Mei 9, 2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, akisalimiana na Meneja Uhusiano na Masoko wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Lulu Mengele, wakati alipowasili kwenye Viwanja vya Jengo la Kitegauchumi la Mfuko wa Pensheni PPF lililopo Mtaa wa Korido jijini Arusha kwa ajili ya uzinduzi wa jengo hilo leo Mei 9, 2016.
Picha ya pamoja.
  • Picha zote kutoka Mafoto Blog

RC Dar asimamisha kazi Mganga Mkuu na Afisa Utumishi Mkuu kwa kutokurishidhwa na utendaji kazi wao

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewasimamisha kazi Mganga Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Dk Sylvia Mamkwe Afisa Mkuu wa Utumishi wa Wilaya ya Ilala, Francis Kilawe kutokana na kutorishidhwa na utendaji wao wa kazi ikiwa ni pamoja na kushindwa kubaini wafanyakazi hewa 11 waliokuwepo katika Wilaya hiyo.

Makonda amechukua hatua hiyo leo katika kikao chake na Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwemo maafisa wote wa Mkoa

Suala la watumishi hewa linaendelea kugonga vichwa vya wakuu wa wilaya na viongozi wa serikali tangu agizo kutoka kwa Rais, Dkt. John Magufuli la kuwabaini watumishi hewa katika halmashauri za wilaya na serikali kuu kutolewa.

Hadi leo katika Mkoa wa Dar wamefikia watumishi hewa 248 wamebainika Dar, waleta hasara ya shilingi bilioni 3.7.

Mei 2, mwaka huu, Makonda aliwapa kiapo cha kazi wakuu wa Idara zote za jiji la Dar pamoja na maafisa Utumishi wa halmashauri za jiji wasaini kiapo cha kazi mbele ya Mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya baada ya kubainika kutoa taarifa zisizo za kweli dhidi ya kuwepo kwa watumishi hewa katika idara zao baada ya kubainika watumishi hewa wengine 209 katika uchunguzi wa siku chache zilizopita.

Miongoni mwa masharti yaliokuwapo katika kiapo hicho ni kwamba iwapo ikigundulika kuwapo kwa watumishi hewa katika idara husika baada wiki moja, Afisa utumishi au mkuu wa idara hiyo atalipa gharama za mishahara iliyopotea, kushitakiwa kwa uhujumu uchumi, kuachishwa kazi lakini pia kufikishwa mahakamani.

Hatua ya kusaini na kula kiapo inatokana na baadhi ya wakuu wa idara pamoja na maafisa Utumishi katika jiji la DSM kudaiwa kutoa taarifa za uongo kwa Mkuu wa mkoa Paul Makonda na wakuu wa wilaya za jiji hilo baada ya kutoa idadi ndogo ya watumishi hewa kwa mkoa wa Dar es Salaam ambao walikuwa 74 tu, huku uhakiki wa sasa uliofanywa na tume maalum ukibaini watumishi hewa 209 ambao wametafuna kiasi cha takribani shilingi bilion 2.7.
  • via blogu ya Frank Leonard

Mbunge wa Moshi Mjini akagua Kata zilizoathiriwa na mvua
Mbunge wa Jimbo la Moshi mjini ,Jafary Michael (mwenye suti) akiwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya (kulia) wakizungumza na Diwani wa kata ya Ng'ambo, Genesis Kiwelu walipofika katika kata hiyo kujionea athari za miondombinu iliyotokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni.

Sehemu ya miondo mbunu ya maji ikiwa imeharibika.

Mbuge Jafary Michael na Mstahiki Meya, Raymond Mboya pamoja na Diwani wa kata ya Ng'ambo Genesis Kiwhelu wakiangalia eneo la daraja lililopo katka kata hiyo namna lilivyoharibika kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni.

Sehemu ya daraja hilo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi,Raymond Mboya akiwa katika moja ya kivuko kilichopo kata ya Ng'ambo akiangalia athari ya mvua zilizonyesha hivi karibuni.


Diwani wa kata ya Msaranga,Anna Mushi akimueleza jambo Mbunge wa Jimbo la Moshi mjini, Jafary Michael alipofanya ziara ya kujionea athari ya mvua zilizonyesha hivi karibuni na kuharibu miundombinu.

Sehemu ya Korongo lililopo katika kati hiyo lililotokana na mvua.


Mbunge wa jimbo la Moshi Mjini, Jafary Michael akisaidia kupalia mahindi wakati akiwa katika kata ya Msaranga akitembelea kujionea athari ya mvua iliyosababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu.

Mstahiki Meya wa manispaa ya Moshi, Raymond Mboya akisadia kaika palizi la Mahindi katika moja ya shamba lililopo kata ya Msaranga.

Diwani wa kata ya Mji Mpya Abuu Shayo akimueleza jambo Mbunge wa jimbo la Moshi mjini Jafaryy Michael alipofika katika kata hiyo kujionea athari ya mvua iliyosababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu.


Diwani wa kata ya Njoro, Jomba John Koi akionesha sehemu ya uharibifu uliotokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni na kuharibu miundombinu.

Sehemu ya Miundombinu ikiwa imeharibika vibaya.


Taka zikiwa zimekwama katika moja ya daraja na kusababisha maji kushindwa kupita vizuri.


Diwani wa kata ya Njoro Jomba Koi akionesha sehemu ya mto Njoro ambao unategemewa kupitisha maji.


Mto Njoro kama unavyoonekana baada ya shughuli za kibinadamu kufanyika.

Ukuta ukiwa umeanguka kutokana na kupitiwa na maji.


Sehemu ya Miundombinu ikiwa imezidiwa na maji ,hatimaye maji yakatafuta njia ambayo iko jirani kabisa na makazi ya watu katika kata ya Njoro.

Hii ndio hali ilivyokuwa kutokana na mvua hizo.

Sehemu ya Korongo ambalo limekuwa likipitisha maji katika kata ya Pasua eneo la Matindigani.


Diwani wa kata ya Pasua, Charles Mkalakala akionesha sehemu ambayo uharibifu wa miundombinu ilivyoharibiwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni.

Mbunge wa jimbo la Moshi mjini, Jafary Michael akitizama eneo la karavati linalotumika kutisha maji likiwa limeziba.

  • Dixon Busagaga

[UPDATE] Familia ya Michuzi yapatwa na msiba wa Maggid mwanaye Muhidin Issa

UPDATE, Mei 14, 2016

Maggid azikwa!


Mwili wa marehemu ukiingizwa katika msikiti wa Maamur Upanga jijini Dar es salaam leo tayari kwa kuswaliwa kabla ya mazishi.

Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete (kushoto) akimfariji baba wa marehemu Ankal Issa Michuzi.

Mama wa marehemu (aliyevaa nguo nyeupe) akiwa na ndugu wa karibu wakiomboleza.

Baba wa marehemu akiwa na viongozi wa dini wakiombea mwili wa marehemu dua.

Mke wa Rais mama Janeth Magufuli (kulia) akiwa na ndugu wa marehemu.

Baba wa marehemu Ankal Issa Michuzi akipata chakula.

Mke wa Rais mama Janeth Magufuli (kulia) akiwasili msibani Wazo hill akiwa na baba wa marehemu Ankal Issa Michuzi.

Baba wa marehemu akiwa na Balozi Cisco Mtiro na baadhi ya waombolezaji.

Baba wa marehemu (mwenye kofia), Ankal Issa Michuzi akipewa pole na baadhi ya waombolezaji mara baada ya maziko ya mtoto wake Maggid Muhidin Michuzi (18) yaliyofanyika katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam leo.

Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba akimpa pole Issa Michuzi.

Rais Mstaa mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete akimfariji Ankal Issa Michuzi.

Issa Michuzi (mwenye kofia) akifuatiwa na Rais mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, kulia kwake ni Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Mhe Ombeni Sefue. Kulia ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi, Katibu Mkuu Ikulu Mhe. Peter Ilomo wakati maziko.

Waumini wakiomba dua.

Baba wa marehemu Issa Michuzi (katikati) akiwa na huzuni akiwa na Rais mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, kulia kwake ni Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde

Baba mkubwa wa marehemu, Ismail Issa Michuzi akitoa shukrani kwa walioshiriki mazishi ya mtoto wao.

Mroki Mroki ambaye aliyekuwa MC akitoa ya muongozo wakati wa mazishi.

Waombolezaji wakiweka udongo kwenye kaburi la marehemu.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John Kijazi akiweka udongo.

Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba akiweka udongo kaburini.

Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiweka udongo kaburini.

Baba wa marehemu Ankal Issa Michuzi akiweka udongo kaburini.

Mwili wa marehemu ukiwekwa kaburini.

Mwili ukiwasili makaburini.

Rais mstaafu Jakaya Kikwete akimpa pole baba wa marehemu, Ankal Issa Michuzi. Kulia ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi. Picha zote na Francis Dande
______________
UPDATE May 13, 2016

Assalaam Aleikhum,

Updates za familia ya Ankal Issa Michuzi iliyopatwa na msiba wa kuondokewa na Mtoto wa Ankal, Maggid Muhidin (18), aliyefariki Jumapili Mei 8, 2016 huko Durban, Afrika Kusini:

Mwili wa Marehemu umeshawsili nchini jana Ijumaa Mei 13, 2016 majira ya saa tisa mchana kwa ndege ya shirika la Emirates kupitia Dubai (kwa kukosekana kwa ndege za moja kwa moja kuja nchini kutoka Durban). Mwili wa kijana wetu umepokelewa na ndugu, jamaa, majirani na marafiki katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere eneo la Cargo la Swissport, Jijini Dar es salaam.

Mazishi yamepangwa kufanyika leo Jumamosi saa 10 alasiri katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam. Taratibu za kuandaa mazishi zitaanza saa 4 asubuhi leo Jumamosi, nyumbani kwa mama wa marehemu kota za Wazo Hill, Tegeta, ulipo msiba.


Jeneza lenye mwili wa marehemu Maggid baada ya kuwasili Dar es salaam jana Ijumaa

Ankal akiwa na ndugu, jamaa na marafiki mara baada ya kuwasili na mwili wa marehemu katika msikiti wa Maamur, Upanga, Dar es salaam, ambako unahifadhiwa hadi baadaye leo kabla ya kupelekwa Wazo Hill saa nne kwa dua na baadaye kurudi hapo msikitini kuswaliwa na hatimaye kupelekwa makaburi ya Kisutu kwa mazishi saa 10 Alasiri.

Ankal akiwa na ndugu, jamaa na marafiki mara baada ya kuwasili katika msikiti wa Maamur, Upanga, Dar es salaam

Ankal akiwa msibani Wazo Hill na wanahabari wenzie usiku huu. Kutoka kushoto ni Faraja Mugwabati, Maggid Mjengwa na Sufiani Mafoto.

-------------------------------------------------

UPDATE, Mei 12, 2016

Assalaam aleikum,

Familia ya Ankal Issa Michuzi iliyopatwa na msiba wa kuondokewa na Mtoto wa Ankal, Maggid Muhidin aliefariki Jumapili Mei 8, 2016 huko Durban, Afrika Kusini.

Taarifa ya sasa ni kwamba, Ndugu zetu kule Durban wanakamilisha taratibu za kusafirisha mwili, hivyo sote tupo standby kwa hilo na naomba tufanye subira kwani hiki ni kipindi kigumu kwetu sote, na mwili ukiwasili ratiba rasmi ya mazishi itatolewa.

Msiba uko Tegeta Wazo Hill, Nyumbani kwa Mama Mzazi wa Marehemu (likiwa ni ombi maalum la Mama), na taratibu zote zinafanyika huko.

NAMNA YA KUFIKA MSIBANI

Ukitokea Tegeta Kibaoni kama unaelekea Kiwanda cha Cement Wazo, mbele mkono wako wa kulia utaona Kanisa la KKKT na ukienda mbele tena kidogo, utaona uzio wenye rangi ya njano umeandikwa Twiga Cement, unakatisha hapo upande huo huo wa kulia. ukikatisha tu utaona kuna mtaa mwingine unaingia upande wa kulia, uache na usogee mbele, utaona mtaa mwingine unaingia kulia, ingia nao huo na utakuwa umefika msibani.

Innalillah wa inna ilayhi raajiun

-AMIN.

UPDATE: Familia ya Ankal Issa Michuzi iliyopatwa na msiba wa kuondokewa na na Mtoto wa Ankal, Maggid Muhidin kilichotokea jana Jumapili huko Durban, Afrika Kusini.
Msiba sasa umehamishiwa Tegeta Wazo Hill, Nyumbani kwa Mama Mzazi wa Marehemu (likiwa ni ombi maalum la Mama), na taratibu zote zinafanyika huko.

Mipango ya kuusafirisha Mwili wa Marehemu kutoka nchini Afrika Kusini na kuja nyumbani kwa mazishi, inafanyika na taratibu za mazishi zitatolewa mara tu baada ya mwili kuwasili nchini.

Habari ziwafikie ndugu, jamaa, majirani na marafiki popote pale walipo.

Innalillah wa inna ilayhi raajiun!Ankal Issa Michuzi anasikitika kutangaza kifo cha mwanae Maggid Muhidin kilichotokea jana Jumapili huko Durban, Afrika Kusini, alikokuwa masomoni.

Mipango ya kuusafirisha mwili wa marehemu inafanywa, msiba utakuwa Tabata Mawenzi jijini Dar es salaam ambako ratiba ya mazishi itatoka mara tu baada ya mwili kuwasili.

Habari ziwafikie ndugu, jamaa, majirani na marafiki popote pale walipo.

Innalillah wa inna ilayhi raajiun.