"Whistle blower" amtonya RC kuhusu maofisa 2 TRA, TPA walioficha "flat screen" tv 288

MAOFISA wawili, mmoja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na mwingine wa Mamlaka ya Bandari (TPA) wilayani hapa, wanatuhumiwa kuhusika na tukio la kuficha televisheni zenye muundo bapa (flat screens) 288. Walitajwa kuwa ni Hadji Nyagawa wa TRA, Idara ya Forodha na Hamis Yusufu wa TPA.

Televisheni hizo zilifichwa juzi kwenye vyoo tayari kusafirishwa kwa kutoroshwa kupitia bandari ya Kilwa Masoko, wilayani humu. Mkuu wa Mkoa wa Lindi na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, Godfrey Zambi, Meneja wa TRA Mkoa, Emmanuel Makwaba na maofisa wengine walitembelea juzi bandari hiyo hadi vyooni zilikofichwa televisheni hizo.

Ilielezwa kuwa zilikuwa katika choo namba 3 na 4 na sasa zimepelekwa katika kituo cha Polisi cha Wilaya. Zambi, baada ya kujiridhisha na tukio hilo aliamuru Polisi mkoa kuwakamata maofisa hao Nyagawa na Yusufu na kuwashikilia kwa uchunguzi zaidi kutokana na tuhuma hizo.

Aliyetoa taarifa ya tukio hilo kwa Mkuu wa Mkoa huo ni msamaria mwema. Imeelezwa kuwa, kumekuwa na mfululizo wa matukio ya kufichwa bidhaa huku nyingine zikisafirishwa kwa magendo na kukwepa kulipa kodi. Hivi karibuni ilikamatwa sukari kutoka India, Brazil na mafuta ya kula kutoka Malaysia.

Serikali yazungumzia hoja za MV Dar es Salaam

Serikali imejibu hoja za upinzani kuhusu uuzwaji wa nyumba za Serikali na kutetea ununuzi wa kivuko cha MV Dar es Salaam ambacho kilitakiwa kufanya safari zake kati ya Dar na Bagamoyo.

Hoja hizo ziliibuliwa katika hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, James Mbatia akitaka kutekelezwa kwa azimio la Bunge la urejeshwaji wa nyumba hizo serikalini lililotolewa Aprili 2008.

Pia, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilibainisha upungufu katika kivuko cha MV Dar es Salaam ambao ni kutolipiwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kutokuwa na kasi kadri ya mkataba na kutokuwapo hati ya makabidhiano.

Hoja hizo za upinzani zilijibiwa juzi jioni na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ambaye alisema hakuna taratibu zozote zilizokiukwa wakati wa ununuzi wa kivuko hicho ambacho kwa zaidi ya mwaka hakijaanza kazi.

Alisema wizara ilipata taarifa ya CAG ambayo ilibainisha upungufu kadhaa ikiwa ni pamoja na kivuko hicho kununuliwa kwa Dola za Marekani 4.9 milioni (Sh7.9 bilioni) bila kulipiwa VAT, lakini akasisitiza kwamba hakukuwa na ukiukwaji wowote wa taratibu za ununuzi.

“Ni kweli kivuko kina mapungufu ikiwamo kasi ndogo, lakini hakuna ukiukwaji wowote wa taratibu wakati wa ununuzi. Temesa ilitangaza zabuni na baada ya maombi kupitiwa, kampuni ya MS Jones Gram Hansen ilishinda zabuni hiyo kwa kuwa na bei nafuu,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema baada ya kivuko kuletwa nchini Desemba 2014, kilifanyiwa majaribio na kubainika kwamba hakikuwa na kasi ya kuridhisha. Alisema makubaliano yalikuwa ni kujenga kivuko chenye kasi ya nots20, lakini hicho kilikuwa na kasi ya nots 15.7.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali ilimtaka mkandarasi kurekebisha kasoro hiyo kwa gharama zake na kuwa ameshawasilisha andiko juu ya namna atakavyoifanya kazi hiyo.

“Mpaka sasa mzabuni huyo hajalipwa asilimia 10 ya malipo yaliyokubaliwa mpaka pale atakapokamilisha kazi hiyo. Kwa hiyo, taratibu zote zilifanyika kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Kuhusu nyumba, Profesa Mbarawa alisema Serikali iliidhinisha mpango huo Aprili 24, 2008 baada ya kupata ridhaa ya Bunge ilipopeleka suala hilo kujadiliwa.

“Suala la uuzwaji wa nyumba za Serikali, pia taratibu zilifuatwa. Serikali ilileta mpango huo bungeni na kupata ridhaa ya wabunge wote. Kwa hiyo, niwaambie tu wabunge kwamba suala hili lilipata baraka zao,” alisema waziri huyo.

Uuzwaji wa nyumba za Serikali na ununuzi wa kivuko cha Mv Dar es Salaam vilifanyika wakati Rais John Magufuli akiwa waziri wa ujenzi kwa nyakati tofauti.

Kambi ya upinzani imekuwa ikisisitiza kwamba kuna ukiukwaji wa sheria uliofanyika wakati wa uuzaji wa nyumba na ununuzi wa kivuko hicho. Hata hivyo, Serikali imeshikilia msimamo wake kwamba sheria zilifuatwa.

 • via Mwananchi

Walionusurika katika mauaji ndani ya msikiti Mwanza wazungumza


MAUAJI ya watatu, akiwamo Imamu wa Msikiti wa Rahmani Ibanda, mtaa wa Utemini, Kata ya Mkoloni, Nyamagana jijini Mwanza, ambayo yana viashiria vya ugaidi,, yalichochewa na kisasi baada ya washirika wa wauaji hao kuwa wamekamatwa na polisi siku moja kabla, habari za uhakika ambazo Nipashe imezipata zinasema.

Imam huyo na wafuasi wake, waliuwawa na kundi la watu wanane waliokuwa na bunduki moja, mapanga, mashoka na majambia, kwa kuchinjwa ndani ya msikiti na watu wanaosemekana ni washirika wa Kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu (IS), ambalo linaendesha harakati zake katika nchi mbalimbali za Mashariki ya Kati.

Waliouawa katika tukio hilo ni Imamu Feruz Elias (27), mkazi wa Ibanda Relini, Mbwana Rajab (40), mkazi wa Ibanda na Khamis Mponda (28) mkazi wa Mkolani.

Habari kutoka ndani ya duru za uchunguzi mkoani Mwanza, zilizopatikana jana, zilisema polisi ilikuwa ikifuatilia mienendo ya kikundi kinachoonekana kuwa cha kigaidi na kufanikiwa kukamata wafuasi kadhaa kabla ya kutokea mauaji hayo juzi.

Uwezekano wa kuwapo kwa uhusiano baina ya wauaji hao na kikundi cha kigaidi kinachosakwa na polisi, unatokana na ukweli kuwa kabla ya kufanya mauaji hayo, watu hao walihoji kuwapo kwa ibada hiyo wakati "(Waislamu) wenzetu wamekamatwa na polisi."

Imam wa msikiti na wafuasi hao katika barabara ya kwenda Shinyanga, waliuwawa wakati wa ibada ya saa 2:00 usiku na watu hao waliokuwa na bendera nyeusi yenye maandishi meupe ya Kiarabu kama bendera ya IS na pia wakiwa wameficha nyuso zao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema hawezi kuliita tukio hilo la kigaidi kwa kuwa bado wanaendelea na uchunguzi ili kufahamu kama linahusiana na ugaidi au la.

Habari za kiuchunguzi zinadai polisi ilishtushwa na kuwapo kwa mauaji ya watu yanayodaiwa kuwa ya ujambazi, lakini bila kuwapo kwa ulazima wa majambazi kuwaua watu hao walioporwa mali zao pia.

Chanzo kimoja cha habari kutoka duru za uchunguzi kilisema kwa kawaida, jambazi huwa haui mtu kama hapakuwa na ubishi katika kusalimisha mali au fedha zinazoporwa.

Pamekuwa na matukio ya mauaji ya wafanyabiashara ya mara kwa mara, katika maduka ya simu na kutuma na kupokea fedha, ambayo yamegharimu maisha ya takriban watu wanne tangu kuanza kwa mwaka huu mkoani Mwanza.

Katika kufuatilia mauaji hayo, ndipo vyombo vya usalama vilipogundua kuwapo kwa kikundi cha kigaidi mkoani humo.

MASHUHUDA WASIMULIA
Mashuhuda walionusurika katika tukio hilo, wakizungumza na Nipashe jana eneo la msikiti huo, walisema majira ya saa 3.00 juzi usiku baada ya kumaliza swala, waliingia watu wapatao 10 wakiwa wameshika mashoka, mapanga na majambia na kuwaamuru waumini wote kulala kifudifudi.

WALIONUSURIKA

Kijana aliyenusurika katika tukio hilo, Abubakari Makabwa (19), alisema baada ya swala kumalizika, watu hao waliingia na kuwaamuru kulala chini huku wakitoa bendera nyeusi na maandishi ya meupe ya Kiarabu kisha kumtaka Imamu wa msikiti kujitokeza mbele. Bendera hiyo inafanana na ile inayotumiwa na Kundi la IS.

“Imamu alipojitokeza huku tukiwa tumelala chini, watu hao walisikika wakisema 'Kwa nini mnaswali wakati wenzetu wamekamatwa na polisi, wengine wanapigana jihad’…hali hiyo ilitushtua zaidi baada ya Imamu kuanza kuchinjwa kwa panga,” alisema Makabwa.

Alisema baada ya Imamu kukatwa kwa panga shingoni, wauaji hao walianza kuwachinja wengine waliolala kabla ya amri ya kutoka kwa mmoja wa wauaji hao, kuwaamuru watoto kuondoka ndani ya msikiti huku wakiendelea kuwachinja wengine.

Makabwa alisema baada ya kutoka akiwa anakimbia na wenzake wanne kupitia mlango wa nyuma, walikutana na mtu mwingine akiwa ameshika bunduki akilinda usalama nje, hali iliyowatia shaka zaidi.

“Tulisikia sauti ya yule mwanamke aliyekuwamo ndani akisema wapige risasi hao. Tulilala vichakani na wala hatukuonekana kutokana na wauaji hao walipofika msikitini walizima taa zote, lakini mshika bunduki hakuweza kurusha risasi yoyote,” alisema.

Aidha, alisema baada ya kufanikiwa kukimbia, watu hao walirusha bomu la mafuta ambalo lililipuka huku lingine likishindwa kulipuka ndani ya msikiti huo.

Naye manusura mwingine, Abeid Gati, alisema awali baada ya watu hao kuingia ndani ya msikiti huo, alidhani ni askari polisi hivyo kumfanya akae chini.

“Ghafla wakatuamuru kulala kifudifudi na kudai wao ni IS wamekuja kufanya kazi yao, kisha wakaanza kutushambulia na kujeruhi. Mwenzangu niliyekuwa naye pembeni alikatwa panga na kuangukia juu yangu, hali hiyo ilinifanya nionekane kama nimekufa,” alisema Gati.

Alisema baada ya tukio, alikaa kwa muda mrefu kama mfu hadi waliporusha chupa ya mlipuko na kuunguza ndoo kubwa ya plastiki na nyingine ilishindwa kulipuka, ndipo alikimbia nje kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa.

MWENYEKITI WA MTAA

Mwenyekiti wa mtaa wa Utemini, Jukaeli Kiula, alisema alipata taarifa za tukio hilo saa 3:20 usiku kutoka kwa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Said, aliyekuwa mmoja wa waumini wa msikiti huo.

“Baada ya taarifa hizo, tulikusanyana kama 'wananzengo' (wanajamii) na kwenda msikiti hapo, tuliwakuta watu watatu wakiwa wamepigwa mapanga na kujeruhiwa vibaya sana, nilipiga simu polisi nao walifika eneo la tukio muda mfupi baadaye,” alisema Kiula.

Kiula alisema msikiti huo una waumini zaidi ya 20 wanaoswali hapo, hivyo baada ya kuvamiwa na watu hao walishindwa kujitetea kwa lolote kutokana na mazingira yaliyopo kwenye msikiti huo.

Katika hatua nyingine aliwaomba, wananchi wa mtaa huo kutoa ushirikiano ili watu hao waweze kupatikana kwani ni sehemu ya watu waliopokelewa na kuhifadhiwa na jamii ya eneo ulipotokea uhalifu huo.

MCHUNGA NG’OMBE
Eneo lililotokea mauaji hayo kuna misikiti miwili huku mmoja ukimilikiwa na dhehebu lililopo chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na mwingine uko chini ya Aswar al Sunn.

Mchunga ng’ombe anayechunga maeneo karibu na msikiti wa Sunn, Mussa Masanja, alisema kuna eneo ambalo linamilikiwa na msikiti huo, huwa anawashuhudia vijana wakifundishwa mchezo wa ngumi na karate karibu na mlima.

“Nilikatazwa na mtu mmoja wa msikiti wa Sunn kuchungia ng’ombe kwa madai nitaharibu miti, lakini baada ya kuchungulia kwa mbali niliwaona watu wazima wawili wakiwafundisha ngumi na karate vijana hali iliyonitisha,” alisema Masanja.

MJANE WA MBWANA RAJAB

Zena Ismail ambaye kwa sasa ni mjane wa watoto watatu, wawili kati yao wasichana wa marehemu Mbwana Rajab, alisema msiba huo umemwachia simanzi kubwa pamoja na familia.

Alisema baada ya kupokea taarifa za kuuawa mume wake, hakuamini kutokana na muda mfupi nyuma aliaga kwenda msikitini kwa ajili ya swala ya usiku.

“Nashindwa kuzungumza chochote, lakini kikubwa tumepoteza baba wa familia,” alisema Zena.

KAMANDA WA POLISI

Akizungumzia tukio hilo, Msangi alisema juzi saa 2.30 usiku, katika msikiti huo, watu wasiozidi 15 wakiwa wamevalia ‘kininja’ huku wakiwa na silaha mbalimbali kama mashoka, mapanga na bendera nyeusi yenye maandishi meupe, waliingia ndani ya msikiti huo na kuzima taa.

“Watu hao walisikika wakiwaambia waumini hao, kwanini wanaswali wakati wenzao wamekamatwa na kushikiliwa na polisi, hali iliyowafanya waanze kuwashambulia papo hapo,” alisema Kamanda Msangi.

Msangi alisema watu hao waliwashambulia kwa silaha hizo watu wanne msikiti hapo na kuwajeruhi vibaya kichwani na shingoni, lakini kati yao watatu walifariki dunia na mwingine mtoto wa miaka 13, kujeruhiwa.

Hata hivyo, alisema baada ya tukio hilo, polisi mkoani hapa inawashikilia watu watatu huku msako mkali wa kuwasaka wengine ukiendelea maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

TAMKO LA SERIKALI
Kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge cha kujadili makadirio ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/17 bungeni mjini hapa jana asubuhi, Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema vyombo vya ulinzi na usalama vitafuatilia kwa kina chanzo cha tukio hilo.

Waziri huyo alitoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali, kuomba mwongozo wa Spika akitaka kauli ya serikali kuhusu tukio hilo, huku akiomba lijadiliwe na Bunge zima.

"Jana (juzi) usiku mkoani Mwanza kwenye eneo linaloitwa Mkolani, kuna watu watatu waliokuwa wamevalia kininja waliingia msikitini wakati waumini wakisali na kuwakata mapanga watu watatu akiwamo imamu wa msikiti huo na watu wote watatu waliokatwa mapanga, wamefariki dunia.

"Naomba mwongozo wako Mheshimiwa Spika na kama unaona inafaa kwa mujibu wa Kanuni ya 47, naomba jambo hili lijadliwe ili tuone, inawezekana serikali ikatupatia majibu ya kina juu ya suala hili kwa sababu ni suala ambalo lime'create tension' kubwa hasa kwa waamini wa Kiislamu," alisema Bobali.

Akitoa mwongozo wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema tukio hilo halifanani na mazingira ya Tanzania.
"Habari ambazo ametupatia Mheshimiwa Bobali, ni za ghafla, lakini pia za kusikitisha sana," Ndugai alisema.
"Natumaini kwa niaba ya Bunge zima, tutoe salamu za rambirambi kwa wote waliopatwa na tukio hili, tuombe Mwenyezi Mungu azipokee roho zao mahali pema peponi.

"Linavyosimuliwa kama vile si tukio la Tanzania hapa. Eeh, hatuwezi kufanya mjadala kwa sababu hata tukiruhusu mjadala, tutajadili nini sasa kwa sasa hivi?

"Tuchukulie kama ni taarifa kwa serikali, acha serikali ijipange iangalie ni jambo gani linaloendelea kwa kuwa limetokea usiku wa kuamkia leo (jana), naamini kabisa vyombo vya ulinzi na usalama viko 'on', watakapokuwa tayari, watatutaarifu kuhusiana na jambo hili kadri linavyoendelea."

Baada ya maelezo hayo ya Spika, Jenista alisimama na kumpongeza Bobali kwa kulitaarifu Bunge kuhusu tukio hilo na kueleza kuwa vyombo vya dola vitalifanyia kazi.

"Kwanza nimshukuru mheshimiwa mbunge kwa taarifa hiyo. Wakati mwingine ni jambo jema Bunge hili likawa linapokea taarifa mbalimbali za matukio mbalimbali yanayotokea katika nchi yetu," alisema.

Jenista aliongeza: “Mheshimiwa Spika umetoa maelekezo na sisi, serikali tutafuatilia tuweze kujua nini kilichojiri kule na chanzo chake nini na mwongozo wa kiti chako, basi tutaona ni namna gani tunaweza tukapeana habari na kujua kabisa kwa dhati jambo gani lililotokea na hatua zilizochukuliwa."

Tangazo la JKT kwa waliohitimu Kidato cha Sita 2016


TANGAZO MUHIMU KWA VIJANA WALIOMALIZA KIDATO CHA SITA MEI 2016

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), limechagua vijana waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita kwa mwaka 2016, kutoka shule zote za Tanzania Bara kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria.

Sanjari na uchaguzi huo, JKT limewapangia makambi watakayokwenda kupatiwa mafunzo kwa muda wa miezi mitatu na wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia tarehe 01 - 05 Juni 2016.

Vijana waliochaguliwa, wamepangiwa katika Kambi za JKT Rwamkoma – Mara, JKT Msange – Tabora, JKT Ruvu – Pwani, JKT Makutupora – Dodoma, JKT Mafinga – Iringa, JKT Mlale – Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba – Tanga, JKT Bulombora, JKT Kanembwa na JKT Mtabila – Kigoma.

Aidha, wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (physical disabilities) wanatakiwa kuripoti Kambi ya JKT RUVU, iliyopo Mlandizi mkoani Pwani, ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo.

JKT linawataka vijana hao kuripoti makambini wakiwa na nguo za michezo kama vile ‘track suit’, bukta, raba pamoja na nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa kwenye makambi yenye baridi kama JKT Makutupora, JKT Mafinga, JKT Mlale, JKT Kanembwa na JKT Mtabila.

Mkuu wa JKT anawakaribisha vijana wote waliochanguliwa ili waweze kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, uhodari, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa letu.

BONYEZA HAPA KUONA VIKOSI WALIVYOPANGIWA VIJANA KWA MUJIBU WA SHERIA 2016

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya JKT

Tarehe 20 Mei 2016


************************

MAJINA YA WANAFUNZI 1500 KIDATO CHA 6 WALIOCHAGULIWA JKT, BONYEZA MAJINA YA KAMBI MBALIMBALI ZIFUATAZO...


 1. JKT Rwamkoma – Mara
 2. JKT Mafinga-Iringa
 3. JKT Kambi ya Makutopora- Dodoma
 4. JKT Mtabila- Kigoma
 5. JKT Kanembwa- Kigoma
 6. JKT Bulombora-Kigoma
 7. JKT Ruvu- Pwani
 8. JKT Mgambo- Tanga
 9. JKT Maramba-Tanga
 10. JKT Mlale- Songea
 11. JKT Msange -Tabora

Prof. Gastorn kutoka Tanzania achaguliwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kisheria Asia na Afrika

Profesa Kennedy Gastorn, Katibu Mkuu mpya AALCO 
Mkurugenzi wa masuala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kennedy Gastorn amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Mashauriano ya Masuala ya Kisheria katika nchi za Asia na Afrika-‘Asian-African Legal Consultative Organisation-AALCO’.

Profesa Gastorn alichaguliwa kwa kauli moja wakati wa Mkutano wa 55 wa Jumuiya hiyo yenye jumla ya nchi wanachama 47 uliofanyika Mjini New Delhi, India tarehe 17 Mei, 2016 na kuhudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Baraka Luvanda.

Aidha, Profesa Gastorn ambaye alikuwa ni mgombea pekee wa nafasi hiyo baada ya kupendekezwa na Tanzania na kupitishwa na Umoja wa Afrika, anachukua nafasi ya Katibu Mkuu anayemaliza muda wake Profesa Rahmat Mohamad wa Malaysia ambaye muda wake unamalizika rasmi ifikapo mwezi Agosti, 2016 na Profesa Gastorn anatarajia kukabidhiwa madaraka hayo mwanzoni mwa mwezi Agosti, 2016.

Mkutano wa Jumuiya ya AALCO ulifanyika kuanzia tarehe 16 Mei na kumalizika tarehe 20 Mei, 2016.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 20 Mei, 2016.

Gazeti la Raia Mwema la Mei 18, 2016 lilichapisha, "Magufuli awatisha mawaziri wawili"

RAIS Dk. John Magufuli ameonyesha kukerwa zaidi na utendaji kazi wa mawaziri wawili kiasi cha kuwafokea katika kikao maalumu cha mawaziri cha hivi karibuni, Raia Mwema, limeelezwa.
Mawaziri hao ambao katika utawala wa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete walikuwa katika wadhifa wa naibu mawaziri, walijikuta katika mtihani huo mbele ya mawaziri wenzao wengine kadhaa waliobaki vinywa wazi.

Vyanzo vya kuaminika vya gazeti hili vimeeleza kuwa Rais Magufuli anataka mawaziri wake wawe mfano wa utendaji bora kwa watumishi wote wa serikali na kwamba, kwa sasa kuna mawaziri, mbali na hao wawili aliowafokea, ambao anaona hawaendi na kasi yake.

“Ni mazingira ambayo mawaziri hawakuyazoea kwamba Rais anawaambia moja kwa moja kwa majina, anafoka akisema anaweza kuwafukuza wakati wowote….mawaziri wamezoea mara kwa mara wanapofanya uzembe au makosa wanaonywa kwa staili tofauti ni kama ya kistaarabu hivi. Sasa huyu bwana mkubwa hana mchezo, aliwataja kabisa,” kinaeleza chanzo chetu cha habari ambacho licha ya kututajia majina ya mawaziri hao, hatutaweza kuwataja hapa moja kwa moja kwa sasa.

Mawaziri hao ambao ni wabunge wa kuchaguliwa majimboni kwa upande wa Tanzania Bara wanaongoza wizara nyeti ambazo zinasimamia sekta mtambuka, wizara ambazo zinagusa sehemu ya ahadi za mabadiliko alizonadi Magufuli wakati akigombea urais katika kampeni za mwaka jana.
Raia Mwema halijaweza kufahamu kwa kina makosa ya kiutendaji yaliyomsababisha Magufuli kuwatisha mawaziri hao na wengine ambao wanaonekana kutomridhisha mpaka sasa.

Chanzo chetu cha habari kinamnukuu Rais Magufuli katika sauti yake ya kufoka akisema; “Wewe (anataja jina la waziri) na mwenzako (anamtaja jina pia) nitawatumbua.” Magufuli aliteua baraza lake la kwanza la mawaziri Desemba mwaka jana katika staili ya aina yake, ambapo baadhi ya wizara zilikosa mawaziri licha ya majina ya wizara hizo kutajwa hadharani, sambamba na naibu mawaziri wake.

“Magufuli anataka atoe mfano kwa mawaziri wengine kwamba wao si watu maalumu sana. Kama wanavyotumbuliwa wengine, nao pia wanaweza kutumbuliwa,” kilifafanua chanzo chetu cha habari.
Miongoni mwa wizara ambazo ziliachwa viporo bila kuwa na mawaziri katika uteuzi huo wa kwanza kwa maelezo kuwa “hawajapatikana/wanatafutwa”, ambazo hata hivyo, mawaziri wake si sehemu ya mawaaziri waliofokewa na Rais Magufuli ni pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango ambayo waziri wake ni Dk. Philip Mpango; Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi inayoongozwa na Profesa Joyce Ndalichako; Wizara ya Maliasili na Utalii inayoongozwa na Profesa Jumanne Maghembe na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inayoongozwa na Profesa Makame Mbarawa.

Tangu aingie madarakani Rais Magufuli, baadhi ya viongozi wanamwelezea mkuu huyo wa nchi kuwa ni msema kweli, asiyetaka unafiki na kwamba pale unapokosea anaweka wazi na hata kama unapofanya vizuri si “mchoyo” wa kupongeza, na moja ya mifano inayotolewa inamhusu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, ambaye Februari mwaka huu, alipongezwa na Rais Magufuli kwa uchapa kazi.

Katika kumpongeza, Rais Magufuli aliweka bayana mbele ya hadhira iliyohudhuria mazungumzo kati yake na wazee wa Jiji la Dar es Salaam kwamba; Makonda anafanya kazi nzuri na isishangaze watu kama atapanda cheo na katika kutekeleza kauli yake hiyo, mwezi mmoja baadaye, yaani Machi mwaka huu, alimteua Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“…Unaweza kuona namna Magufuli anavyotaka mambo yanyooke. Ukifanya kazi atakupongeza kwa moyo wote lakini ukivuruga…hana mchezo na wewe, anakutumbua tu,” alisema mmoja wa viongozi waandamizi serikalini (jina linahifadhiwa).

Mmoja wa viongozi maarufu kukutwa na hasira ya Magufuli ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango-Malecela, ambaye aliondolewa kwenye wadhifa huo baada ya kutoa taarifa zisizo za kweli kuhusu suala la watumishi hewa walioko serikalini.

Kilango ambaye alikuwa ameteuliwa na Magufuli kushika wadhifa huo katika kipindi cha mwezi mmoja tu kabla ya kutumbuliwa, alikuwa amesema kwamba mkoa wake hauna wafanyakazi hewa; jambo lililokuja kubainika baadaye kuwa halikuwa la kweli.

Hata hivyo, tayari wapo mawaziri wengine kadhaa walioonja adha ya kasi ya Magufuli. Mawaziri hao walikumbana na adha hiyo baada ya kushindwa kuwasilisha fomu za tamko la rasilimali na madeni na kuziwasilisha katika Ofisi za Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kwa agizo la Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa aliwataja hadharani kwa majina mawaziri hao na kuwataka kuwasilisha fomu hizo ndani siku moja, Februari 26, 2016, saa 10 jioni.
“Mheshimiwa Rais ameelekeza mawaziri ambao hawajajaza tamko la rasilimali au hati ya ahadi ya uadilifu wafanye hivyo na kuzirejesha kabla saa 12 jioni na Waziri ambaye atashindwa kutekeleza agizo hili atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye nafasi yake,” alisisitiza Waziri Mkuu katika tamko lake hilo.

Tujikumbushe: Walikotoka Magufuli na Kitwanga na alichokisema wakati akimnadi kwenye kampeni


Waziri Kitwanga akijibu maswali bungeni Mei 20, 2016 na baadaye Rais kutengua uteuzi wake


[Aliyekuwa] Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga jinsi alivyokuwa akijibu maswali leo Bungeni, huku taarifa kutoka Ikulu ikieleza kuwa Rais John Magufuli leo hii hii ametengua uteuzi wake baada ya kugundulika kuwa Waziri huyo aliingia bungeni na kujibu maswali ya Wizara yake akiwa amelewa.

Alichosema Mbunge wa Arusha Mjini na Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhusu Kitwanga...Taarifa ya habari ChannelTEN Mei 20, 2016


Taarifa ya kutenguliwa Waziri Kitwanga kwa kujibu swali Bungeni akiwa ametwanga ulabu


Mtui akamatwa kwa biashara madini bandia huku Jamal akikamatwa na bastola iliyotumika kihalifu

Kamishina (CP) Simon Sirro akionesha baadhi ya vitu walivyokamata kwa Wenceslaus Mtui
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linashikilia mkazi wa Makongo, Wencelaus Mtui anayedaiwa kuhujihusisha na utapeli wa madini kwa kumtapeli mtu na madini bandia.

Akizungumza na waandishi habari leo Ofisini Kwake, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishina (CP), Simon Sirro amesema kuwa mtu aliyetapeliwa kiasi cha fedha hizo alilipa kupitia benki ya CRDB kwa madini bandia ya dhahabu kilogramu 20 zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,000.

Amesema baada ya mtu huyo kulipa fedha hizo alikabidhiwa vipande vitatu vya madini venye uzito wa Kilogram 212 na kugundua kuwa ni madini bandia.

Jeshi la polisi lilipompekuwa ofisini kwake na nyumbani kwake walimkuta ,Chuma cha kuchomea madini,Mashine ya kupima madini, vifaa vya kubania (Seal 53) pamoja na taarifa mbalimbali za malipo ambayo ameweka benki na kutoa.

Mtui ambaye anadaiwa kuwa ni tapeli wa madini bandia anamiliki kampuni ya Crown Logistics and Cargo Handling Limited.

Wakati huo huo jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam linamskilia Waziri Jamal (39) mkazi wa Mbezi Msakuzi ambaye wamemkamata na silaha moja aina ya bastola (Browning 6.35 calibre) yenye namba za usajili A.08416/ Car 90522 na baada ya kumhoji wameweza kubaini mtandao wao wa watu nane.

Aidha jeshi la polisi limesema kuwa askari aliyeuawa jana kwa kupigwa risasi ni wa mkoa wa Pwani na kuahidi lazima watakamatwa wote waliohusika.
 • via Michuzi blog

Mwanachuo ashikiliwa na polisi akituhumiwa kutoa maneno ya kichochezi dhidi ya Rais na Mkuu wa Majeshi

Jeshi la polisi mkoani Arusha linamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Tengeru aliyejulikana kwa jina la Harold Mmbando (23) mkazi wa Arusha kwa kosa la kutoa taarifa za uchochezi dhidi ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein na Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange pamoja na kusambaza ujumbe wa maneno makali juu ya viongozi hao.

Akiongelea tukio hilo, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 17 mwaka huu majira ya saa 3 asubuhi. Alisema kuwa mwanafunzi huyo alitoa taarifa za uchochezi kuhusu mkuu wa majeshi.

"Mtuhumiwa huyo aliandika maneno haya, 'Mwamunyange pindua nchi haiwezekani wote wawe nje halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile kiti,' hayo ndiyo maneno aliyoyasema mtumiwa huyo," alisema Mkumbo.

Aidha aliongeza kuwa mbali na maneno hayo pia mtuhumiwa huyo alisambaza ujumbe mwingine wenye maneno yafuatayo,"Dr Shein akiuawa kama Karume sitashangaa wala kustuka naomba mungu mauaji ya kisiasa yaliyotokea Zanzibar yawe kwa viongozi wa kisasa hasa watawala na sio wananchi wa kawaida,” hayo ndio maneno aliyoyaandika mtuhumiwa huyo kupitia mitandao ya kijamii wa Faccebook.

Mkumbo alisema kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika, huku akitoa rai kwa watu wote wanaotumia mitandao ya kijamii kuitumia pasipo kukiuka sheria na taratibu. Alitumia muda huo pia kutoa onyo kali kwa yeyote atakayebainika anatumia mitandao vibaya na kusema kuwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Wakati hayo yakiendelea, mshtakiwa wa kesi ya kumtukana Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,  John Pombe Magufuli ndugu Isaac Emily (40), mkazi wa Olasiti jiji Arusha, inatarajiwa kuanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Juni 5 mwaka huu katika mahakama ya hakimu mkazi Arusha.
 • Taarifa ya Woinde Shizza

Wadaiwa 21,721 wajitokeza kurejesha mikopo HESLB

Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo kutoka HESLB, Bw. Robert Kibona akiongea. Kulia ni Meneja Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB
Na FATMA SALUM -MAELEZO

Jumla ya wadaiwa wapya 21,721 wa mikopo ya elimu ya juu wamejitokeza ili kuanza kulipa madeni yao kufuatia agizo la siku 60 lililotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) mnamo Machi 14 mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Robert Kibona wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu tathmini ya agizo lililotolewa na bodi hiyo kwa wanufaika wa mikopo na waajiri ili kutimiza wajibu wao kisheria.

Bw. Kibona alifafanua kuwa jumla ya Shilingi bilioni 151.5 zinatarajiwa kurejeshwa na wadaiwa hao ambao walikopeshwa ili kuwawezesha kupata elimu yao ya juu katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi kuanzia mwaka 1994.“Lengo la agizo lilikuwa ni kuhahakisha madeni yote yaliyoiva yanakusanywa ili kuongeza uwezo wa kukopesha watanzania wengi zaidi na agizo hili limeisha Mei 13 mwaka huu.” alisema Bw. Kibona

Kwa mujibu wa Bw. Kibona, kati ya wadaiwa waliopatikana, wadaiwa 19,528 walipatikana baada ya Bodi kuchambua taarifa za waajiriwa zilizowasilishwa na waajiiri na wadaiwa wengine wapatao 2,007 walijitokeza kwa hiari.“Waajiri wana wajibu wa kisheria wa kuwasilisha taarifa za waajiriwa wao, baadhi yao walifanya hivyo katika siku hizo sitini na tukawabaini wadaiwa hao, tunawapongeza waajiri kwa ushirikiano walioutoa na wanufaika wote waliojitokeza kwa hiari” alisema Bw. Kibona.

Aidha Bw. Kibona aliongeza kuwa Bodi imeongeza siku 30 za ziada kuanzia Mei 20, 2016 kwa wadaiwa waliobaki kujitokeza na uamuzi huo umetokana na tathmini iliyoonyesha kuwa kuna idadi kubwa ya waajiri na wanufaika wanaoendelea kujitokeza. Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo Bw. Cosmas Mwaisobwa alisema kuwa kiwango cha ukusanyaji wa madeni kwa mwezi kinatarajiwa kuongezeka kutoka shilingi bilioni 2.7 zinazokusanywa hivi sasa na kufikia shilingi bilioni 8 ifikapo mwezi Juni 2016.

Katika kipindi cha mwaka 1994/1995 hadi sasa, kiasi cha shilingi trilioni 2.44 kimetolewa kwa wanufaika 378,504 wakiwemo wanafunzi wanaoendelea na masomo yao hivi sasa ambao kwa sasa hawana wajibu wa kulipa hadi pale watakapomaliza au kusitisha masomo yao.


Mkurugenzi Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Cosmas Mwaisobwa (kushoto) akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utaratibu wa urejeshaji wa mikopo kwa wadaiwa ambao mikopo yao imeshaiva. Kulia ni Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Robert Kibona.

PICHA NA FATMA SALUM-MAELEZO