Kumbe walijitahidi kumzuia Kitwanga asiingie Bungeni ile siku

[...] Imedaiwa kuwa muda mfupi kabla ya kuingia bungeni juzi asubuhi katika siku anayodaiwa kuingia bungeni akiwa amelewa, (aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles) Kitwanga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi alizuiwa (kuingia) mara tatu na mbunge mwenzake kutoka Mwanza, Richard Ndassa wa Jimbo la Sumve (CCM) lakini hakutaka kusikia ushauri huo.

Akizungumza na Nipashe jana, Ndasa alisema alijaribu kadri alivyoweza kumzuia (Kitwanga) asiingie bungeni na badala yake kuondoka kabisa eneo hilo lakini ilishindikana.

Alisema yeye (Ndasa) alimuona Kitwanga ana kila dalili kuwa amelewa na ndiyo maana alijaribu kumsihi asiingie bungeni, lakini hakuwa tayari baada ya kusisitiza kuwa “yuko sawa kabisa”

Akielezea zaidi, Ndasa alisema alimuuliza Kitwanga kwa lugha ya Kisukuma; “Ole sawa ielelo?" akimaanisha “uko sawa leo”, naye akamjibu pia kwa lugha ya Kisukuma: “Nale sawa gete” akimaanisha yuko sawa kabisa.

“Unajua Kitwanga nakaa naye kiti cha jirani, sasa wakati anaingia asubuhi nikamuona hayuko sawa. Nikamuuliza na alinijibu kwa kifupi, kisha akaenda mbele kukaa tayari kwa kujibu maswali,” alisema Ndassa.

Ndasa alisema hata baada ya kipindi cha Bunge kumalizika asubuhi, alikutana na Kitwanga nje ya viunga vya Bunge na kujaribu kumshika mkono ili kumuondoa na eneo la Bunge, lakini alimkimbia.

Ndassa alisema aliamua kumfuata dereva wa Kitwanga na kumwambia amchukue na kumuondoa kwenye viwanja hivyo vya bunge, lakini Kitwanga hakuwa tayari kuingia ndani ya gari.

“Unajua mimi ni Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM mkoa wa Mwanza, hivyo nilijitahidi sana kumzuia jana (juzi) lakini nilishindwa… na wakati akiwa getini ndipo alipoitwa na Waziri Mkuu ofisini na jioni mkasikia taarifa ya Rais Magufuli,” alisema Ndassa.

[...] Mbunge wa Bukoba Mjini (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, alisema alimpongeza Rais Magufuli kwa kuchukua uamuzi huo haraka, huku akibainisha kuwa bado kuna mawaziri wengine nane ambao anaamini wataungana na Kitwanga kwa kuwa wameonyesha dalili zote kuwa ni 'mizigo'.

"Kitwanga ni sehemu ya matatizo ya serikali nzima ya CCM. Hivyo ndivyo walivyolelewa. Huyu ni mmoja tu, tutaendelea kuwaona wakiwajibishwa kwa sababu Rais ana mtazamo wake, si wa taasisi," alisema.

"Hizi ndizo tabia zao, na alipowanyima semina elekezi aliharibu zaidi. Na bado kuna mawaziri wengine nane hivi wataondoka madarakani kwa utaratibu huu huu,” alisema Lwakatare ambaye aliongeza kuwa alisoma na Kitwanga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) miaka ya 1986-1988 na kwamba kadri amjuavyo, wakati huo hakuwa mnywaji wa kiwango cha kuingia kazini akiwa amelewa.

Taarifa ya habari ChannelTEN Mei 22, 2016


Makonda azipa benki 6 siku 21 zibaini na kurejesha fedha za watumishi bandia

Paul Makonda
Paul Makonda
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amezitaka benki mbalimbali nchini kutoa ushirikiano kwa serikali ili kubaini akaunti zilizokuwa zinatumika kuweka mishahara kwa watumishi bandia, pamoja na kuwabaini wote waliohusika katika malipo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini humo, Makonda amesema kuwa hadi sasa mkoa huo una watumishi bandia zaidi ya 280, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 3 zimekuwa zikitumika kuwalipa.

Makonda amesema:
Kwa hiyo tunazitaka benki zote, na nimeshawaandikia barua, tutawapa idadi ya pesa ambazo tunazidai, karibu benki sita. Kwa hiyo:-
  • Benki zisaidie serikali ya mkoa wa Dar es Salaam kujua ni nani aliyekuwa anaingiza pesa kwenye hizi akaunti

  • Benki iisaidie serikali ya mkoa, ni nani aliyekuwa anachukua hizi kwenye hizi akaunti kwa sababu tunafahamu, hakuna akaunti yoyote ya benki unaweza kuitumia mtu tofauti na mhusika.

  • Kama hakuna aliyekuwa anachukua hizo pesa, maana yake hizi pesa zetu ziko benki. Ninaziomba ndani ya siku 21 nizipate hizo pesa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. 
Makonda amezitaka benki hizo kukamilishwa mambo hayo na amezipatia majina na namba zote za akaunti za watumishi waliokuwa wananufaika na ubadhirifu huo. Amesema kufanya hivyo pia anazisaidia benki kutambua watumishi wa mabenki wasio waaminifu.

Amezitaja benki 6 kuwa ni NMB ambapo zilipitishwa zaidi ya shilingi bilioni 2.8, CRDB milioni 400, NBC milioni 141, DCB milioni 85, Standard Chartered milioni 2 na Community Bank milioni mia moja na tisini na nne.


RC Makonda aagiza kusitishwa ujenzi wa jengo la TALGWU

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemtaka Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sophia Mjema kusitisha ujenzi wa jengo la chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa - TALGWU baada ya kubainika ubadhirifu wa fedha katika ujenzi wa jengo hilo.

Akizungumza baada ya kutembelea jengo hilo Makonda amemtaka Mjema kuwasimamia na kuwachunguza wahandisi wa Halmashauri ya wilaya ya Temeke ili kubaini utata uliopo katika ujenzi wa Jengo hilo.

Makonda ameshauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU ifanye uchunguzi katika ofisi ya wahandisi ya wilaya ya Temeke.

Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sophia Mjema amesema aliagiza ujenzi wa jengo hilo usitishwe tangu mwezi Januari mwaka 2015 lakini agizo hilo halijatekelezwa.
  • Darlin Said, TBC.

Tanga kunani kule? Timu 3 zaaga Ligi Kuu: African Sports, Coastal Union, JKT Mgambo

Klabu ya African Sports imeungana na vilabu vingine vya Tanga (Coastal Union na JKT Mgambo ) kuipa mkono wa kwa heri Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara Msimu huu 2015 / 2016 baada ya kuchapwa bao 2-0 na Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa mwisho wa ligi uliochezwa kwenye uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro.

African Sports na JKT Mgambo zote zilikuwa zikihitaji ushindi kwenye mechi zao za leo,May 22, 2016 huku zikiombea mabaya timu za Ruvu JKT na Kagera Sugarili zenyewe ziwe na uhakika wa kusalia VPL.

Lakini mabo yalikuwa tofauti baada ya Ruvu JKT kuichapa Simba SC kwenye uwanja wa taifa huku Kagera Sugar wakipata sare ya kufungana bao 2 - 2 dhidi ya Mwadui FC.

Kwenye uwanja wa Azam Complex, Mgambo imeshuka daraja kwa kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Azam FC.

Ramadhani Singano ‘Messi’ alianza kuifungia Azam FC dakika ya 60 kabla ya Fully Magangakuisawazishaia Mgambo dakika ya 72.

Mgambo iliyokuwa ikihitaji ushindi kwenye mchezo wa leo imejikuta ikishindwa kupata ushindi kwa mara nyingine mbele ya Azam FC ambao sare hiyo imewafanya wamalize kwenye nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Yanga SC.

Simba SC waliokuwa wakiwania nafasi ya pili wamechapwa 2 – 1 na Ruvu JKT na timu hiyo iliyo chini ya kocha wa zamani wa Simba King Kibadeni imenusurika kushuka daraja ,mabao yake yakifungwa naAbdulrahman Mussadakika ya kwanza na 30, wakati la Wekundu wa Msimbazi limefungwa na NahodhaMussa Hassan Mgosi dakika ya 70.

Kwa matokeo hayo, Azam FC inamaliza na pointi 64, ikifuatiwa na Simba SC inayomaliza na pointi 62 katika nafasi ya tatu.

Yanga SC ambayo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu wiki mbili zilizopita, leo,May 22, 2016 imemaliza kwa sare ya kufungana mabao 2 - 2 na wenyeji Majimaji hivyo kufikisha pointi 73.

Mechi nyingine za kufunga pazia la Ligi Kuu, wenyeji Toto Africanswamefungwa 1 - 0 na Stand UnitedUwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Coastal Union wamefungwa 2 - 0 na PrisonsUwanja wa Mkwakwani, Tanga, Mbeya Cityimelazimishwa sare ya 0 - 0 na Ndanda FC, Mtibwa Sugar wameichapa 2 - 0 African Sport.

Kwa matokeo hayo, timu zote za Tanga, Mgambo JKT, African Sports na Coastal Union zinaipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu, zikizipisha Ruvu Shooting, Mbao FC na African Lyon.

Mgambo JKT imemaliza na pointi 28, African Sports pinti 26 na Coastal Union pointi 22.Taarifa ya Mkenga kupinga ujumbe wa Dk Machuve unaohusu mazishi ya Wilson Kabwe

Familia ya Marehemu Wilson Kabwe imesikitishwa sana na taarifa zilizosambazwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu kauli na msimamo wa familia katika shughuli za maazishi ya mpendwa wao Wilson Kabwe.

Familia inapenda kuchukua nafasi hii kutamka bayana kwamba, Dk. Zawadi Machuve si msemaji wa familia. Kauli yake iliyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba:-
"Sisi hapa hatukaribishi viongozi, huu ni msimamo wa familia kama wao watafanya utaratibu wao sawa, lakini hatuko kwa ajili ya viongozi"
Kauli hiyo ambayo ililenga kutoishirikisha Serikali katika msiba wa mtumishi wake tunaomba ipuuzwe na siyo kauli ya familia.

Familia inatambua na inathamini sana mchango mkubwa wa Serikali katika kugharamia matibabu na huduma zote za mazishi.

Familia inachukua fursa hii kuwakaribisha viongozi wote wa Serikali, ndugu, jamaa na marafiki wanaopenda kushiriki katika shughuli za mazishi ya mpendwa wetu.
Imetolewa na:

PHILIP MKENGA KABWE
MSEMAJI WA FAMILIA.


HABARI YA MSIBA WA WILSON KABWE KWA MUJIBU WA GAZETI LA MWANANCHI


Wakati mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe ukitarajiwa kuzikwa Jumatano ijayo kijijini kwake Mamba, Mpinji wilayani Same, chanzo cha kifo chake kimetajwa kuwa ni saratani ya tezi dume na kuharibika kwa ini.

Kabwe alifariki dunia juzi alipokuwa akitibiwa katika Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mauti hayo yamemkuta ikiwa ni siku 38 baada ya kusimamishwa kazi hadharani na Rais John Magufuli kwa tuhuma za kuingia mikataba iliyosababisha hasara ya zaidi ya Sh3 bilioni.

Mtoto wa marehemu, Geofrey Kabwe, alisema baba yake alianza kuugua maradhi ya tumbo Julai mwaka jana.

Alisema Ilipofika Desemba, alizidiwa na familia iliamua kumpeleka India kwa matibabu zaidi.

“Alipofika India waligundua kuwa alipata hitilafu ndogo kwenye ini, hivyo akafanyiwa upasuaji, madaktari India walisema chanzo cha tatizo hilo ni dawa alizokuwa akitumia,” alisema Geofrey.

Alisema mwishoni mwa Januari, mkurugenzi huyo alirejea nchini akiwa na afya njema na alianza kwenda kazini Februari huku akihudhuria kliniki katika Hospitali ya Apollo nchini India.

Lakini kadri siku zilivyozidi kwenda, hali yake kiafya ilianza kuzorota na ilifikia hatua familia ilitakiwa kukutana ili kushauriana kuhusu hali hiyo.

“Wiki mbili zilizopita nilipigiwa simu nikiwa Arusha nikaelezwa kwamba hali yake kiafya siyo nzuri, tulimwona daktari wake na akabainika kuwa na Pneumonia (homa ya mapafu), akapewa dawa na sindano,” alisema Geofrey na kuongeza:

“Baadaye tulimpeleka TMJ kwa ajili ya kipimo cha CT-Scan, jana mchana majibu yalitoka yakionyesha kuwa ini lilikuwa limeharibika na tayari mwili ulikuwa umeanza kuvimba. Ilipofika saa mbili usiku hali ilibadilika akawa anakoroma na saa tatu usiku akafariki dunia,” alisema Geofrey.

Taarifa zilizopatika jana zimeeleza kuwa Kabwe amekuwa nje ya ofisi yake tangu alipoanza matibabu na siku ya kwanza kurejea kazini ilikuwa Aprili 19 ambako alikutana na rungu la Rais John Magufuli.

Mazishi 

Msemaji wa familia, Dk Ez Machuve alisema mipango ya mazishi inaendelea: “Atasafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwake Jumanne jioni baada ya kuagwa hapa nyumbani kwake. Mazishi tunatarajia kufanya kijijini Mamba Mpinji Jumatano.”

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema katika kipindi chake cha kufanya kazi, hakubahatika kushiriki kazi yoyote na Kabwe kutokana na hali yake kiafya. “Sikubahatika kufanya naye kazi, baada ya Rais kufanya uamuzi mgumu, aliondoka hivyo sikuwahi kushiriki naye,” alisema Mwita.

Kilichomwondoa kazini 

Makosa yaliyosababisha Kabwe kusimamishwa kazi ni madai ya kusaini mkataba kwa kutumia sheria ndogo ya mwaka 2004 kutoza magari yanayotoka kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) Sh4,000 huku akidaiwa kusaini mkataba mwingine wa Sh8,000 chini ya sheria ndogo ya mwaka 2009.

Pia, madai ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa UBT hasa kwenye utaratibu wa kutoa magari na kukodisha vyumba vya kupangisha kinyume na taratibu na kuongeza muda wa mzabuni iliyeingia mkataba na jiji wa maegesho ya magari kinyume na taratibu.

Viongozi 2 CHADEMA Iringa waliomtuhumu Meya kuwa mshurutishi, upendeleo wasimamishwa

HALI si shwari ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Iringa Mjini baada ya juzi kamati tendaji yake kufanya maamuzi magumu yaliyomsimamia, mwenyekiti wa chama wa jimbo hilo, Frank Nyalusi kuendelea na wadhifa wake huo.

Pamoja na Nyalusi, kamati hiyo inayoundwa na wajumbe 21 iliyohudhuriwa pia na mbunge wa jimbo hilo, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Suzan Mgonakulima imetengua uteuzi wa Diwani wa Kata ya Gangilonga, mjini hapa, Dady Igogo kuendelea kuwa mjumbe wa kamati hiyo.

Wawili hao, wamesimamishwa kuendelea na nyadhifa zao hizo ikiwa ni siku kadhaa tangu kuripotiwa na chombo kimoja cha habari wakimtuhumu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe anayetokana na chama chao kuendesha vikao vya baraza la madiwani kibabe na kwa upendeleo.

Taarifa za kusimamishwa kwa viongozi hao ambazo viongozi wa chama hicho wamesema hawawezi kuzizungumzia kwa kina kwasababu zinahitaji maamuzi ya mwisho ya mkutano mkuu wa jimbo, zilisambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii hii leo.

Akizungumza na mtandao huu huku akikwepa kutoa taarifa ya maamuzi hayo moja kwa moja, Mgonakulima ambaye pia ni katibu wa chama wa jimbo hilo alisema; “Juzi Mei 21 tulikaa kamati tendeji iliyojadili mwenendo wa chama katika jimbo letu na kufanya maamuzi yatakayopelekwa kwenye mkutano mkuu.”

Mgonakulima alisema maamuzi hayo hata kama yapo kwenye mitandao ya kijamii yataendelea kuwa siri ya chama hicho hadi pale mkutano mkuu utakapokutana na kuyabariki au kuyakataa.

“Mimi ni katibu kweli lakini siwezi kutoa taarifa yoyote ya kikao hicho cha kamati kwasasa kwenye vyombo vya habari mpaka nipate ridhaa ya chama,” alisema huku akisisitiza maamuzi yaliyofanywa na kikao hicho ni ya siri.

Akizungumzia taarifa ya kusimamishwa kwake uenyekiti, Nyalusi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mivinjeni mjini Iringa alisema; “nimepata taarifa hizo kupitia kwa baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho ambacho sielewi kilikuwa ni kikao gani kwasababu hakikuitishwa na mimi kama mwenyekiti baada ya kushauriana na sekretarieti yangu ya chama.”

Nyalusi alisema katika mazingira ya kushangaza alialikwa katika kikao hicho ambacho hakujua kama ni cha kamati tendaji kwa njia ya ujumbe wa maandishi mafupi kwa kupitia simu yake ya kiganjani.

“Nilipofika katika chumba cha mkutano, nikakaribishwa ili nifungue kikao hicho, nikauliza hiki ni kikao gani, nikaelezwa ni cha kamati tendaji. Nilishangaa na kuuliza kinawezaje kuitishwa bila kufuata taratibu, sikupata jibu la kueleweka,” alisema.

Alisema baada ya kukosa jibu alikataa kukifungua kikao hicho alichokiita ni cha uasi ndani ya chama na kuondoka zake bila kusaini daftari la mahudhurio ili kujiepusha na uvunjaji wa katiba.

Nyalusi anayefahamika mjini hapa kwa ujasiri mkubwa wa kusigana na viongozi wa serikali na vyombo vya dola alisema atachukua hatua za haraka kwa mujibu wa katiba ya chama chao pindi atakapopewa rasmi barua ya kusimamishwa madaraka yake hayo.

Kwa upande wake Igogo aliyetenguliwa kuendelea kuwa mjumbe wa kamati tendaji hakuweza kupatikana kuzungumzia taarifa hizo pamoja na kuwepo kwa taarifa zisizo rasmi katika mitandao ya kijamii zinazoonesha alikwishajiuzulu nafasi hiyo kutokana na kutingwa na majukumu yake mengine.

Siku moja kabla kikao hicho hakijafikia maamuzi ya kuwaadhibu viongozi hao, Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Taifa alisema baadhi ya madiwani wa chama hicho wana utovu wa nidhamu unaohatarisha maslai ya chama na wananchi wa jimbo hilo.

Msigwa aliyasema hayo alipokuwa akizungumzia taarifa za baadhi ya madiwani kumtuhumu mstahiki meya wa manispaa ya Iringa kwa ubabe na upendeleo.

“Kwenye chama chetu hakuna mtu aliye juu ya chama. Ni lazima viongozi waliochaguliwa waheshimiwe, ni kosa kiongozi akamtukana kiongozi mwenzake hadharani halafu akavumiliwa, ” alisema.

Alisema kuna watu wengi walijaribu kuwa juu ya chama wakashughulikiwa na wengine kufukuzwa hadi uanachama kwasababu huo ni uasi ndani ya chama.
  • via Frank Leonard blog