Kurasa za mbele na nyuma za magazeti ya Tanzania leo Juni 4, 2016Mhasibu TANESCO ahukumiwa kifungo jela miaka 425 na faini shilingi bilioni moja

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu kifungo cha miaka 425, aliyekuwa Mhasibu Mwandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lilian Chengula (42) baada ya kupatikana na hatia ya makosa 85 likiwemo la kusababisha hasara ya Sh bilioni 1.3.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi alisema mshtakiwa amepatikana na hatia ya makosa 85 kati 167 yaliyokuwa yanamkabili na katika kila kosa atatumikia kifungo cha miaka mitano jela.

Hata hivyo alisema, Chengula atatumikia adhabu hiyo kwa wakati mmoja ambayo itakuwa ni sawa na kifungo cha miaka mitano jela. Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Shahidi alisema mshtakiwa akimaliza kutumikia kifungo chake, atatakiwa kulipa zaidi ya shilingi bilioni moja.

Aidha aliwaachia huru washtakiwa wenzake watatu, ambao ni mfanyabiashara Salha Salim Saad (57), Salum Saad Ally (65) na Bakary Kinyogoli (65). Alisema anawaachia huru washtakiwa hao kwa kuwa hawajatiwa hatiani katika makosa 82 yaliyokuwa yakiwakabili wote wanne.

Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 13 pamoja na vielelezi ili kuthibitisha mashtaka hayo. Mshtakiwa huyo alikuwa anakabiliwa na makosa ya matumizi mabaya ya madaraka akiwa mtumishi katika Shirika la TANESCO, na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh bilioni 1.3.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Chengula kupitia kwa Wakili wake Alex Mshumbusi, aliomba Mahakama imsamehe kwa kuwa ni kosa lake la kwanza, kesi hiyo ni ya muda mrefu pia ana watoto wanaomtegemea, na muda mrefu hakuwepo kazini.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine. Aidha waliiomba Mahakama itoe amri kwa mshtakiwa huyo kulipa kiasi hicho cha fedha alichosababisha hasara ili kulifidia shirika hilo.

Taarifa ya habari ChannelTEN Juni 3, 2016


Taarifa ya BAVICHA: Rais Magufuli aombe radhi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

RAIS MAGUFULI AOMBE RADHI WANAFUNZI KWA KAULI ZA UPOTOSHAJI

Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) tumeshtushwa na kauli za upotoshaji zilizotolewa jana na Rais John Magufuli alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati alipozindua ujenzi wa jengo la maktaba chuoni hapo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amesikika na kunukuliwa akiwaambia wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuwa wasikubali kutumiwa na wanasiasa na pia waache siasa, badala yake wajikite katika kile alichokiita ni masomo.

Katika hilo, BAVICHA tunamwambia Rais Magufuli kama hakuwa na nia ya kupotosha na kuudanganya umma wa Watanzania na kuwahadaa wanafunzi wa vyuo vikuu, basi akiambie chama chake cha CCM kwanza kifute Idara ya Shirikisho la Vyuo Vikuu, ambacho ni chombo rasmi kilichopewa majukumu na vikao vya juu vya chama hicho kufanya siasa vyuoni.

Rais Magufuli anajua kwa sababu ni mjumbe wa vikao hivyo. Hata DC wa Kinondoni aliyemteua hivi karibuni, ni kiongozi katika idara hiyo.

Kama Rais anajua maana na tafsiri ya alichokizungumza, basi BAVICHA tunamtaka afute masomo ya siasa vyuoni. Kama hajui au amesahau, kuna wanafunzi wanaosoma masomo ya siasa, mfano Shahada ya Sayansi ya Siasa. Kama hataki wanafunzi wafanye siasa, awaambie watafanyia wapi mafunzo kwa vitendo.

Katika muktadha huo wa kauli za kupotosha na kudanganya umma alizotoa jana mbele ya wasomi, BAVICHA tunamtaka Rais Magufuli awaombe radhi wanafunzi wa vyuo vingine nchini kwa kuwaita kuwa ni vilaza huku akiwagawa katika makundi.

Ni aibu na jambo la fedheha kauli kama hizo za kibaguzi kutolewa na Rais wa nchi ambaye hao wote ni vijana wake ambao serikali anayoiongoza inapaswa kuwajibika kuwatumikia.

Kauli aliyoitoa jana Rais ni ya kuendeleza matabaka, madaraja na baguzi katika elimu ambayo isipokemewa inaligawa taifa.

Kauli hiyo si tu kwamba ni kinyume cha uungwana wa Watanzania bali pia kuendekeza kauli za kibaguzi ni kuvunja Katiba ya nchi.

Katika hali ambayo imetushtua zaidi, Rais Magufuli amepotosha hata sakata la wanafunzi wa UDOM, waliofukuzwa kikatili na Serikali yake kutoka chuoni ndani ya masaa 24 waliodai haki yao ya kufundishwa baada ya kukaa chuoni mwezi mzima bila kufundishwa.

Kama Rais Magufuli hajui au amesahau, BAVICHA tunamkumbusha kwamba wanafunzi hao walikuwa hawasomi masomo ya shahada, bali ilikiwa programu maalum ambayo ipo kwa mujibu wa Sheria iliyopitishwa mwaka 2014 na Bunge.

Sheria hiyo ya mabadiliko ya Sheria namba 4 ya Mwaka 2014 ilisainiwa Disemba 11, 2014 na Rais Kikwete na haijafutwa hadi tunapotoa taarifa hii.

Kama Rais Magufuli ameamua kuwabagua na kuwadhalilisha wanafunzi hao kwa kuwaita vihiyo, awaombe radhi kwa sababu wapo chuoni kwa mujibu wa sheria ambayo ilipitishwa yeye akiwa mbunge na waziri katika serikali hiyo. La sivyo vijana watakuwa na haki ya kutafsiri kuwa serikali iliyopeleka mswada wa sheria hiyo na wabunge walioitunga ni vihiyo?

Kama Rais Magufuli hawaombi radhi wanafunzi hao, tafsiri ya nani kihiyo itakwenda mbele hata kuhoji waliokuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri na Rais aliyesaini sheria hiyo iliyowaruhusu vijana hao kusajiliwa chuoni na kuanza masomo kwa gharama za serikali.

Aidha, BAVICHA inapenda kuhitimisha taarifa hii kwa kuhoji kauli ya Rais Magufuli alipoonekana kuhoji kuwepo kwa barabara hewa alizosema zipo nchini. Tunamtaka asiishie hapo, bali pia awaambie Watanzania barabara hizo zilijengwa na serikali ipi chini ya usimamizi wa waziri yupi, kama si yeye aliyekuwa Waziri wa Ujenzi? Msimamizi huyo naye anastahili kutumbuliwa kwa kusababisha barabara hewa.

Imetolewa leo Ijumaa, Juni 3, 2016 na;
Idara ya Uenezi na Uhamasishaji
BAVICHA-Taifa.

M/Kiti, Katibu Afya, Mhasibu, Mratibu Chanjo, Mganga Mkuu, Mhazini wasimamishwa wakituhumiwa kuihujumu CHF

BARAZA la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora limewasimamisha kazi watumishi watano kwa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh milioni 190, ambazo ni fedha za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) pamoja na fedha za chanjo.

Watumishi hao wanatuhumiwa kughushi nyaraka, kukosekana kwa baadhi ya nyaraka za fedha, kuidhinisha malipo hewa pamoja na kukiuka taratibu na kanuni za utumishi wa umma na kukiuka matumizi ya fedha za umma.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Kiwelle Bundala. Kiwelle aliwataja watumishi waliosimamishwa kazi kupisha uchunguzi kuwa ni Katibu wa Afya Wilaya, Kisasu Sikalwanda, Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya, Denins Gombeye, Mratibu wa Chanjo wa Wilaya, Joel Mjondela, Mganga Mkuu Hospitali ya Wilaya, Emmanuel Mihayo na Mweka Hazina, Stanslaus Kalokola.

Alisema uchunguzi utakapofanyika na kubaini watumishi hao hawana hatia wataendelea na kazi na ikiwa tofauti hatua nyingine za kinidhamu zitachukuliwa.

Mwanri alilipongeza baraza hilo kwa kuchukua maamuzi magumu ya kulinda maslahi ya wananchi na kuongeza kuwa ataendelea kusimamia sheria na taratibu za utumishi wa umma. Aliwataka watumishi wa Serikali kuhakikisha wanasimama katika nafasi zao za kufanya kazi kwa uandilifu na kuepuka ubadhirifu ambao hauna faida ndani yake.

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkoa wa Tabora, Mohamed Msangi alisema sababu za watumishi hao kusimamishwa kazi ni kughushi nyaraka za malipo, kukosekana kwa baadhi ya nyaraka pamoja na kufanya malipo hewa.

Alisema taarifa ya CAG inaonesha kukiuka taratibu nyingi za matumizi ya fedha za umma.

Prof. Tibaijuka: Kuna mbunge mwenzetu alipata fedha za escrow, ameondoka bungeni, hakuna mtu anajua

Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka amelaumu utaratibu uliotumika kuwashughulikia watu waliotuhumiwa kuchota shilingi bilioni 306 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Profesa Tibaijuka ambaye alipoteza Uwaziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi katika Serikali ya Awamu ya Nne) kwenye kashfa hiyo baada ya kubainika kuwa aliingiziwa fedha kupitia Benki ya Mkombozi, zinazoonekana zilitoka kwenye akaunti hiyo iliyokuwa inamilikiwa kwa pamoja na TANESCO na kampuni ya kufua umeme ya IPTL, akizungumza katika Semina maalum iliyoandaliwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Ufisadi (ACFE), kwa lengo la kuwajengea uwezo wabunge kupambana na ufisadi, alisema kuwa anashangaa kutuhumiwa kupokea fedha wakati aliyempa fedha hizo hakuguswa.

Aidha, Profesa Tibaijuka alisema kuwa ingawa fedha hizo zilitolewa kupitia Benki mbili tofauti (Stanbic Bank na Mkombozi Bank), watuhumiwa waliotoa pesa Mkombozi Bank ndio walianikwa huku majina ya waliochukua fedha kupitia Stanbic yakigeuka siri.

Mbunge huyo alionesha kutokuwa na imani na Tume ya Maadili inayohoji watuhumiwa wa masakata ya Ufisadi akidai kuwa haiko makini kwani kuna watuhumiwa wengine ambao hawakutajwa Bungeni hawakugushwa na Tume hiyo.
“Watu waliotajwa kwenye sakata hilo ni wale waliopewa fedha zilizopitia benki ya Mkombozi, lakini hadi sasa wale waliopewa fedha zinazodaiwa kuwa ni taslimu kutoka Stanbic hawajatajwa.”
“Mie nimeshawahi kushtakiwa Tume ya Maadili, najua kuwa kuna mbunge mwenzetu hapa alipata fedha za Escrow, lakini kwa sababu hakuwa mzungumzaji ameondoka bungeni wala hakuna mtu anajua kama alipata. Unaona jinsi ambavyo hawa watu hawako makini,” alisema.
Profesa Tibaijuka alisema wakazi wa jimbo lake walimchagua kwa mara nyingine licha ya tuhuma za Escrow kwa sababu hawakuziamini.

Profesa Tibaijuka aliinyooshea mkono Takukuru akidai kuwa imekuwa ikichagua kesi za rushwa na ufisadi inapotaka kufanya uchunguzi.

Alisema sheria pekee yake haiwezi kufanya lolote katika mapambano dhidi ya ufisadi na hakubaliani na wabunge wanaosema kuwa hata kama mahakama imeshindwa kuthibitisha ufisadi, watuhumiwa wataifishwe mali zao.
“Sisi wabunge hatukuja kufanya kazi hiyo, tumekuja kutunga sheria ili zisaidie katika kutuongoza,”
“Ni vyema kuzungumzia unyofu wa watu kwa kuanzia katika shule, makanisa, misikiti na wabunge.”alisema.
Aliituhumu TAKUKURU kuwa inakubali kutumiwa kwa kuchagua kesi za kuchunguza.
“Tume ya Maadili ndio usiseme,”
“Mie nimeshawahi kushtakiwa Tume ya Maadili, najua kuwa kuna mbunge mwenzetu hapa alipata fedha za Escrow, lakini kwa sababu hakuwa mzungumzaji ameondoka bungeni wala hakuna mtu anajua kama alipata. Unaona jinsi ambavyo hawa watu hawako makini,”alisema.
Mbunge wa Hanang (CCM), Dk Mary Nagu alilia na watu aliowaita wazushi kwamba wanawazushia wenzao kuchukua rushwa wakati si ukweli.

M/Kiti TFF ajitoa kuratibu mchakato wa uchaguzi Yanga kwa sababu hizi 6...

MWENYEKITI wa kamati ya uchaguzi ya TFF Wakili Aloyce Komba ameamua kujitoa katika kuratibu na kusimamia mchakato wa uchaguzi wa klabu ya Yanga uliopangwa kufanyika tarehe 25 June 2016 na zaidi ametoa sababu 6 zilizomfanya aamue kujiweka pembeni kwenye mchakato huo.

Sababu zilizomfanya Wakili huyo kuachia ngazi ni kama ifuatavyo;
  1. Katika mchakato huo nimetuhumiwa kupanga kumhujumu kwa kukata jina la mmoja wa wagombea nafasi ya uenyekiti Bw. Yusuf Manji. Tuhuma ambazo zilitolewa tarehe 2 June kwa waandishi wa habari.
  2. Kutokana na tuhuma hizo, Yusuf Manji amesema ni moja ya sababu zilizomfanya achukue fomu za kugombea uchaguzi utakaoratibiwa na Yanga.
  3. Tuhuma hizo ambazo ni kubwa kwangu binafsi na zikigusa taaluma yangu ya sheria zimetolewa wakati klabu ya Yanga inahitaji amani, utulivu na mshikamano mkubwa wa wanachama, wapenzi na washabiki wake, hivyo mimi kutokuwa chanzo chochote cha vurugu zinazoweza kutokea.
  4. Tuhuma hizo zinahusu mimi kupewa fedha za hongo au rushwa (kiasi hakijulikani) ili nishawishi wajumbe wenzangu wa kamati ya uchaguzi ya TFF kukata jina la aliyekuwa mgombea mtarajiwa, Bw. Yusuf Manji kwasababu ambazo hazijaelezwa.
  5. Napaswa kupisha uchunguzi wowote huru wa tuhuma hizo nzito kama zimeshafikishwa katika vyombo vya uchunguzi wa masuala ya rushwa ili mimi nipate fursa ya kujitetea kwa uhuru zaidi.
  6. Kwa kuzingatia ushauri wa watu mbalimbali ninaowaheshimu na kuwapenda sana ndani na nje ya klabu ya Yanga hususani wanasheria wengine nguli wa masuala ya michezo kama vile Wakili Sais Hamad El-Maamry, Wakili Sam Mapande, Wakili Alex Mgongolwa na waandishi wa habari waandamizi wa michezo, nimeona nisishiriki mchakato huu kwa kusimamiwa na TFF au hata ukisimamiwa na klabu ya Yanga yenyewe.
Kwa kuwa mimi ni muumini mkubwa wa utawala wa sheria na hasa masuala ya katiba na demokrasia katika vilabu na vyama vya michezo, napaswa kuanzia sasa kutoshiriki vikao vyote vinavyohusu mchakato wa klabu ya Yanga nikiwa kama Mwenyekiti au Mjumbe.

Nawaomba Rais wa TFF, Bw. Jamal Malinzi na Katibu Mkuu Selestine Mwesigwa na wajumbe wenzangu wa kamati ya uchaguzi ya TFF, nimemuachia madaraka ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa klabu ya Yanga, Wakili Domina Mideli, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Watakaovunja sheria na kusababisha ajali mabasi ya UDART: Chombo kushikwa + Kifungo + Faini kuanzia sh 300,000/=

Madereva wa magari, bodaboda na bajaj wanaovunja sheria na kuyasababishia ajali ya mabasi yaendayo haraka (UDART) watatozwa faini.

Meneja Uhusiano wa UDART, William Gatambi alisema wamewasilisha maoni ya kupitishiwa sheria ndogondogo kwa ajili ya barabara zinazotumiwa na mabasi hayo katika Wizara husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
“Sheria hizo zitawabana madereva ambao wamekuwa wakipuuza taratibu na matumizi sahihi ya miundombinu, suala ambalo limekuwa likisababisha ajali za kila siku na usumbufu kwa madereva wa mabasi hayo,” alisema Gatambi.
Aliongeza kuwa mchakato huo uko katika hatua za mwisho kukamilika na baadhi ya sheria hizo zinaambatana na adhabu ya faini ya kuanzia Sh 300,000/= na kuendelea, kushikiliwa kwa chombo kilichosababisha ajali kwa muda na kifungo gerezani.

Polisi yaangiza wenyeviti SM na wenye nyumba kupiga picha na kuwekeana mkataba na wapangaji

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewataka wenyeviti wa serikali za mitaa kushirikiana na wenye nyumba kuhakikisha wapangaji katika nyumba wanaingia makubaliano ya mkataba na kuwa na picha zao.

Hatua hiyo imetokana na kuwepo kwa watu wanaofanya uhalifu katika maeneo mbalimbali na kushindwa kupatikana pindi polisi wafanyapo operesheni kutokana na kupanga kwenye nyumba hizo lakini wakati akiondoka hawaagi na wenye nyumba wanakosa kuwa na taarifa za watu katika nyumba zao.

Akizungumza na waandishi habari jijini Dar es Salaam leo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina (CP), Simon Sirro amesema kuwa wenye nyumba ambao watashindwa kufanya mkataba bila picha likitokea tukio dhidi ya mpangaji, msalaba utamuangukia mwenye nyumba kuhusika katika uhalifu uliofanywa.

Kuna la kujifunza hapa: Moshi - Watalii "wavamia" vyakula kwa "Mama Ntilie"


Ujio wa watalii wengi wanaoingia mjini Moshi kwa ajili ya kupanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea vivutio vya utalii, imegeuka shubiri kwa wamiliki wa hoteli, baada ya watalii kwenda kula kwenye vibanda vya mamantilie.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini watalii wengi wanaolala Moshi Mjini na maeneo ya jirani, hawali vyakula na vinywaji katika hoteli hizo.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, hoteli nyingi zimeishia kuona idadi kubwa ya watalii wanaolala katika hoteli hizo, lakini hawaoni wakitumia migahawa yao kwa ajili ya chakula.

Vyanzo hivyo vimedokeza hali hiyo inajitokeza baada ya watalii kugundua vyakula wanavyouziwa kwenye hoteli hizo ni ghali, wakati chakula kama hicho wanakipata mitaani kwa bei ya chini.

Mathalan, baadhi ya hoteli za kitalii, vyakula huuzwa kati ya dola nane za Marekani (Sh17,000 za Tanzania) hadi dola 20 za Marekani (Sh43,000), lakini wanapata chakula hicho mitaani kwa Sh5,000 hadi Sh6,000.

Pia, baadhi ya watalii wanakwenda kunywa pombe kwenye baa za mitaani, ambako bia huuzwa kati ya Sh2,000 na Sh4,000 wakati katika hoteli hizo huuzwa kati ya Sh4,000 na Sh8,000.

Mkurugenzi wa Hoteli ya Leopard ya mjini Moshi, Priscus Tarimo, alisema hali hiyo imechangiwa na hoteli nyingi kupika aina zile zile za vyakula ambavyo watalii wanavipata nchini kwao.

“Kosa kubwa ni kutoweka vyakula vya asili. Unapomuekea vyakula kama wanavyokula kwao halafu ukampigia kwa standard (viwango) vya chini moja kwa moja ataikimbia hoteli yako,” alisema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya King of Kilimanjaro Expedition, Shatiel Mhina, alisema tatizo ni hoteli kujikita kupika vyakula vya kizungu.

“Hao watalii wanakuja wakiwa na information (taarifa zote). Anakuambia anataka kula pilau au mtori au machalari (ndizi nyama) na atakuambia na bei ya huko mitaani. Hotelini hawapiki,” alisema.

Mamalishe Mwajuma Hamisi, alisema japo hafahamu Kiingereza, lakini watalii wanaofika kwenye kijiwe chake hutaka vyakula vya asili ambavyo havijawekwa kwenye friji muda mrefu.

Mfanyabiashara huyo alisema bei za vyakula vyake ni ya chini na kutolea mfano kuwa sahani moja ya pilau huuza kwa Sh2,000, bei ambazo watalii hao huzifurahia kuwa ni za chini tofauti na hoteli.
  • MWANANCHI

Mbinu za kushinda kesi za ufisadi zilizojadiliwa katika semina ya wabunge

SERIKALI imepewa mbinu kadhaa zitakazoiwezesha kushinda kesi za ufisadi zinazohusu watu wenye fedha nyingi, nyadhifa na nguvu ya kudhibiti au kupoteza ushahidi na kuonywa kuwa iwapo haitazitumia, rasilimali za Tanzania zitaendelea kutafunwa na wachache wenye ‘nafasi zao’.
Aidha, Rais John Magufuli amepongezwa kwa jitihada za kuanzisha mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini, akitajwa kuwa kiongozi anayeweza kusimamia vita hiyo na kushinda kwa sababu ana sifa ya uadilifu na unyoofu ambayo kila Mtanzania anatakiwa kuwa nayo ikiwa nchi inataka kutokuwa na ufisadi.

Mbinu hizo zimetajwa kwa nyakati tofauti na wabunge mbalimbali na watoa mada kuu katika semina ya wabunge kuhusu ufisadi iliyofanyika Ukumbi wa Msekwa, ndani ya Viwanja vya Bunge mjini hapa, jana.

Semina hiyo iliandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Ufisadi Tanzania (ACFE) na mada kuu mbili; Hali ya ufisadi nchini (Jitihada za kuuzuia, mbinu za kudhibiti mafisadi na changamoto katika kuukabili), masuala ya kisheria kwa ujumla kuhusu ufisadi. Ilitolewa na wakufunzi wa ACFE, Emmanuel Johannes na Dk Julius Mashamba.

Johannes alisema changamoto ya ufisadi ni kubwa zaidi kwenye mashirika ya umma kutokana na mfumo unaotumika kupata wakurugenzi wa bodi, watawala katika mashirika na kutokuwepo kwa uhuru kati ya bodi, wakaguzi wa ndani na watawala kutokana na njia walizopatikana.

Alisema kwa mtindo wa kupendekezana unaoendelea badala ya kutumia vigezo na sifa, taasisi na mashirika mengi ya umma yamejikuta yakishindwa kuendelea vizuri kwa ufanisi, hivyo kushauri mabadiliko kwa kuangalia uwezo, elimu na sifa nyingine muhimu.

Kwa maelezo yake, ikifanyika hivyo, mwanya wa kutokea ufisadi unakuwa ni finyu na hata mtendaji wa ngazi moja anakuwa huru kumwonya au kumkataza wa ngazi nyingine asiushiriki au kuwa tayari kutoa ushahidi katika kesi ya ufisadi pindi unapobainika katika taasisi.

Alisema kwa anayepata nafasi kwa kuzingatia vigezo hawezi kuwa na woga wa kusimamia utendaji mzuri wala upendeleo wala kuruhusu aliyempendekeza afanye ufisadi na kumfichia siri.

Dk Mashamba, Mhadhiri Mwandamizi wa Shule ya Sheria ya Dar es Salaam, alisema serikali inafungua kesi nyingi za rushwa na kushindwa kwa sababu sheria hazigusi baadhi ya vitendo viovu vinavyohusiana moja kwa moja na masuala ya rushwa.

Alisema; “Ikiwa serikali inataka kufanikiwa katika vita ya ufisadi kwa kushinda katika kesi inazozifikisha mahakamani, ni lazima sheria zinazotumika ziongezewe ‘nyama,’ ili ziguse maeneo mengine ya ufisadi ambayo kwa sasa haziyagusi.

“Pia inabidi irekebishe sheria zilizopo kuruhusu ufisadi mpya kama wa mtandao uweze kupelelezwa na kesi kuendeshwa mahakamani na kuamuliwa,” alisema na kuongeza kuwa, mambo mengine yanayopaswa kuangaliwa upya ni utitiri wa taasisi zinazoshughulikia mambo yanayofanana kama rushwa, ufisadi bila kuwa na mawasiliano. “Pia lazima serikali iweke kiwango cha chini cha elimu ya maofisa wanaopeleleza kesi za ufisadi chenye viwango vya kimataifa ili kuepusha kuwa na wasio na elimu kufanyia uchunguzi wenye elimu na ujanja wa kisheria, hivyo kushindwa kesi,” aliongeza Mashamba.

Alitaja mbinu nyingine ni kushirikisha Mahakama katika mafunzo ya kutambua ufisadi bila kuingilia uhuru wao wa kuendesha kesi na kuwasisitiza wanasheria kutotumika kupotosha ili kuficha ufisadi.

Hata hivyo, Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Anna Tibaijuka alisema endapo suala la uadilifu na unyoofu kwa wananchi na viongozi halitakuwepo, hata kukiwa na sheria za aina gani ufisadi hauwezi kwisha.

Alisema anampongeza Rais Magufuli kwa kupiga vita ufisadi na anaamini atafanikiwa ikiwa watu wake watakuwa wanyoofu na waadilifu kwa sababu hizo ndio sifa zake na anatembea katika njia ya uaminifu.

Maalim Seif: Tutafanya harakati zetu mpaka Shein aondoke na wala wasidhani tutapigana

Chama cha wananchi CUF kimesema kuwa wao hawana ugomvi na serikali ya Muungano ugomvi wao ni serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa madai kuwa imepora maamuzi ya wananchi katika uchaguzi uliofanyika October mwaka jana.

Kauli hiyo ilitolewa na aliyekuwa katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad wakati akizungumza na viongozi wa wilaya ya Magharibi A na B huko katika ofisi ya chama Kilimahewa Mjini Zanzibar.

Alisema ziadi ya 80% ya wananchi wa Zanzibar waliikataa CCM na viongozi wake na kudai hawawezi kukubali hata siku moja kuongozwa na utawala wa mabavu.

“Mkakati wetu tutahakikisha hatumwagi tone la damu lakini Dk shein ataondoka mara hii,”alisema Maalim Seif.

Maalim Seif ambae ni makamo wa kwanza mstaafu alisema Wazanzibari wana jukumu la kumuondosha Dk Shein kutokana na kukosa ridhaa ya walio wengi.

Hata hivyo alisema ajenda yao kubwa ni kuhakikisha wanaiondoa serikali ya Dk Shein kwani katiba zote ile ya Muungano na ya Zanzibar inasema njia ya kuweka uongozi ni kupitia uchaguzi ulio huru na wa haki.

“Sisi tunasema tutafanya harakati zetu mpaka Shein aondoke na wala wasidhani tutapigana,”Alisema Maalim Seif.

Katika kikao hicho Mkurugenzi wa mipango na chaguzi wa chama hicho Omar Ali Shehe alisema ziara aliyoifanya katibu mkuu wa chama chake imeonyesha wanachi wanataka serikali yao ya halali ambayo waliipigia kura Oktoba mwaka jana.

Aidha Shehe alisema baada ya chama cha Mapinduzi kushindwa kufanya siasa wanatumia njia ya kukidhalilisha chama chake ili kisiweze kufanya shughuli zake za kisiasa.

Nae mkurugenzi wa habari na uenezi wa chama hicho salim Abbdlla Bimani amelishutumu Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kuzuwia mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyike Juni 2 maka huu.

Alisema mkutano huo umezuwiwa kwa madai ya kuwepo kwa ugeni kutoka ndani na nje ya nchi wanaokuja katika Ijitmai ya Kimataifa.

Alisema licha ya RPC wa mkoa Kaskazini Hasina kuwataka kutoa tarifa ya maombi wakati wanapohitaji kufanya mikutano wa hadhara.

“Tuna uthibitishia ulimwengu kuwa jeshi la polisi limendelea na kukandamiza demokrasia na linatumika kisiasa,” alisema Bimani.

Alisema kwa mujibu wa barua waliyoipokea kutoka jeshi la polisi iliyotiwa saini na SP Ali Haji mkuu jeshi la polisi Wilaya ya Kaskazini B imekitaka chacha CUF kusitisha mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyika Juni 2 mwaka huu.

Tarifa hiyo imesema kutokana na shughuli mbali mbali kutoka nje ya nchi kwa ajili ya ijitmai shughuli hizo kama zilivyo shughuli nyengine zenye kujumuisha mikusanyiko mikubwa hulazimisha jeshi hilo la polisi kuwa katika utendaji wa kazi zaidi ya wakati za kuhakikisha kunakuwepo amani na usalama.

Mkutano huo wa Wilaya za Magharibi A na B ni wa mwisho katika ziara za Katibu Mkuu kichama za kutembelea Wilaya za Unguja na Pemba zilizoanza Mei 14 hadi 18 kwa kisiwa cha Pemba na Mei 28 hadi Juni 2 katika kisiwa cha Unguja.
  • Taarifa ya Talib Ussi na Mauwa Muhammed

Taarifa ya LAPF ya zoezi la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa pensheniMFUKO WA PENSHENI WA LAPF WAANDAA ZOEZI LA UHAKIKI WA WASTAAFU WANAOLIPWA PENSHENI NA MFUKO HUO

MFUKO WA PENSHENI WA LAPF UNAWATANGAZIA WASTAAFU WANAOLIPWA PENSHENI NA LAPF KUWA KUTAKUWA NA ZOEZI LA UHAKIKI WA WASTAAFU NCHI NZIMA KUANZIA TAREHE 13.06.2016 HADI TAREHE 24.06.2016 KUANZIA SAA MBILI KAMILI ASUBUHI.

TAREHE KAMILI KWA KILA WILAYA INAPATIKANA KWENYA MAGAZETI YA MWANANCHI YA TAREHE 06.06.2016, 08.06.2016 NA 10.06.2016, DAILY NEWS LA TAREHE 07.06.2016 NA 09.06.2016 NA TOVUTI YA MFUKO www.lapf.or.tz

KILA MSTAAFU ANATAKIWA KUFIKA NA PICHA MOJA NDOGO (PASSPORT SIZE) NA KITAMBULISHO CHOCHOTE.

KILA MSTAAFU ANAYELIPWA PENSHENI NA LAPF UNAOMBWA UJITOKEZE KWENYE OFISI ZA HALMASHAURI ZILIZO KARIBU NAWE.

KWA MAELEZO ZAIDI PIGA 0767-600043 AU 0753-999991.

“STAAFU KWA UFAHARI NA LAPF”

Serikali yazungumzia tuhuma za "The Economist" la Uingereza kwa utawala wa Rais Magufuli

Kaimu Mkurugenzi wa Idara Habari Maelezo, Zamarad Kawawa (kushoto) na Kulia ni Meneja Uhusiano wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TCI), Daud Biganda.
Dotto Mwaibale

SERIKALI imekanusha habari zilizoandikwa na gazeti la Kiingereza linalotpka kila wiki lililodai kuwa Rais Dk. John Magufuli anaongoza nchi kwa msukumo licha ya kuonekana mzuri na kuwa taarifa hiyo imelenga kuupotosha umma.

Habari iliyoandikwa kwenye gazeti hilo ilikuwa na kichwa kilicho andikwa "Government by gesture, A President who looks good but governs impulsively."

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana wakati akitoa ufafanuzi wa habari hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Idara Habari Maelezo, Zamarad Kawawa alisema taarifa hiyo haikuwa na uzalendo na amewataka wanahabari kuwa makini na habari zenye mlengo wa kupotosha taifa.

"Nawaombeni wanahabari wenzangu kuweni makini na taarifa zenye mlengo wa kupotosha umma" alisema Zamarad.

Akitoa ufafanuzi kuhusu suala la uchumi Meneja Uhusiano wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Daud Biganda alisema taarifa hiyo siyo sahihi na imelenga kupotosha na inavuruga ukweli kwani tangu Rais Dk. John Magufuli aingie madarakani kwa kipindi cha kati ya mwezi Desemba 2015 na 2016, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeweza kuandikisha miradi ya uwekezaji ipatayo 551 yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 9,211.88 kati ya miradi hiyo miradi 229 yenye asilimia 42 inamilikiwa na watanzania, miradi 215 yenye asilimia 39 inamilikiwa na wageni na miradi 107 yenye asilimia 19 inamilikiwa kwa njia ya ubia kati ya watanzania na wageni.

Biganda alisema kuwa miradi yote hiyo ya uwekezaji ilitarajiwa kuzalisha ajira zipatazo 55,970 na kuleta matokeo mengine kwa watanzania na kuwa imesajiliwa na TIC.


Meneja Uhusiano wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TCI), Daud Biganda (kulia), akitoa ufafanuzi wa Uchumi tangu Rais Dk. John Magufuli aingie madaraka na miradi iliyosajiliwa na kituo hicho.

Mkutano na wanahabari ukiendelea.
  • Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062