Gabo atahadharisha utapeli unaotumia jina lake baada ya simu zake kuibwa


Msanii nguli wa Bongo Movies, Gabo Zigamba, anatoa tahadhari kuhusu matapeli mbalimbali wanaotumia jina lake. Awali, msanii huyo alipoteza simu mbili za mkononi, ambazo baadaye zilikuwa zikitumiwa na matapeli hao kuomba misaada kwa watu mbalimbali wakijifanya kuwa wao ndiyo Gabo.

Kadhalika, majuzi, akaunti ya Facebook ya msanii huyo ilidukuliwa na ikatumika kwa muda na matapeli hao kwa kujifanya wao ndio msanii huyo. Hatimaye alifanikiwa kuirejesha akaunti hiyo katika himaya yake.

Gabo ameeleza kuwa anahisi kuwa yeye ndio msanii anayeongoza kwa jina lake kutumiwa na matapeli kwa sababu amekuwa akipata taarifa mbalimbali kuhusu watu wanaotumia jina lake, kwa mfano binti mmoja aliyejifanya ndiye Gabo na amekuwa akitapeli kwa kudai anauza mabegi.

Msanii huyo ametoa wito kwa Watanzania kuwa makini na watu wanaotumia majina ya watu wengine, hususan watu maarufu, kwa minajili ya kutapeli. Amesema kuwa yupo katika mchakato wa uzinduzi mpya wa akaunti zake mbalimbali za mitandao ya kijamii ili, pamoja na sababu nyingine, iwe rahisi kwa watu kuwasiliana nae pindi wanapokumbana na matapeli hao wanaotumia jina lake.

Hospitali ya Muhimbili kununua helikopta ya wagonjwa


BODI mpya ya wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imetangaza mkakati wake wa kununua helkopta maalumu itakayokuwa inasafirisha wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali nchini hadi hospitalini hapo.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Joseph Komwihangiro aliweka wazi nia hiyo jana mbele ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Waziri alikuwa akizindua bodi hiyo na kupokea magari matatu ya kubebea wagonjwa zilizotolewa na Ubalozi wa Japan nchini.
“Kwa muda mrefu MNH imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo uhaba wa wataalamu, vitendea kazi na kukosa fedha za kujiendesha, tutahakikisha tunajifunza kwa wenzetu waliopita wapi walikuwa wakikwama ili tujinasue kutoka hapo.
“Ukweli tunatamani kuipeleka hospitalki hii mbele kwa kuboresha huduma za ubingwa, tumepokea magari hayo tunashukuru lakini tunapenda MNH iwe na angalau helkopta maana kumsafirisha mgonjwa kutoka Katavi kwa mfano hadi Muhimbili, ni changamoto kubwa,” alisema.
Akizungumza, Waziri Ummy alisema wazo hilo ni zuri kwa vile huduma za msaada wa dharura nchini bado ni changamoto kubwa.
“Tanzania mtu anaweza kufa akiwa njiani kwenda hospitalini, tukiziboresha huduma hizi ni wazi kwamba tutaweza kuokoa maisha ya watu wengi na ulemavu.
“Ni vema pia bodi mkakaa chini na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) mkaandaa mtaala maalumu wa kufundisha wataalamu wa huduma hii ya dharura.
“Nasema hivyo kwa sababu wapo wachache… mkakati wa serikali ni kupeleka ‘ambulance’ katika kila kata lakini changamoto iliyopo ni kuwa hatuna wataaamu wa kutosha,” alisema Ummy.
Naye Balozi wa Japan, Masaharu Yoshida alisema ubalozi huo upo tayari kuendelea kushirikiana na serikali katika kuiboresha sekta hiyo.

Hapa ajali ikitokea watu wafe, labda mdomo mbaya wa mtu tu au mapenzi ya mungu...

Fire extinguisher tunayo, msijali... ufa kwenye kioo si tatizo kwa dereva pia

Tairi ni kwa nje tu linakutisha, ila ndani zima kabisa, msihofu
Si unakaa tu kwa muda? Hapo siyo makochi ya nyumbani, keti tu, kama hutaki shuka
Usukani alimradi unakata kona, isikupe taabu
Kila kitu kipo. Clutch ile. Breki ile. Accelerator ipo. Kila kitu kipo
Basi la kubebea abiria wa safari ndefu Tanzania, hapo ni stendi kuu Ubungo, Dar es Salaam

Maendeleo ya ukarabati wa uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera


Mtaka afafanua taarifa hii "Mkuu wa Mkoa aagiza Walimu Wakuu WOTE wa mkoa wavuliwe madaraka"

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na Maafisa Elimu na Viongozi wa CWT wa Mkoa huo katika kikao maalum cha kutoa ufafanuzi
Imeandikwa na Stella Kalinga, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa ufafanuzi wa agizo la kufanya mabadiliko ya Walimu wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata mkoani humo, ambalo Serikali ya Mkoa ililitoa tarehe 17 Agosti, 2016 katika kikao ambacho alipokea vishikwambi (tablets) 637 kutoka EQUIP Tanzania (Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Nchini) kwa ajili ya Walimu wakuu na Waratibu wa Elimu Kata.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa ufafanuzi huo kutokana na taarifa potofu za agizo hilo kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kuwa, "Mkuu wa Mkoa ametangaza kuwavua madaraka Walimu wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata wote wa Mkoa huo" hali iliyosababisha baadhi ya Walimu Wakuu na Waratibu kukosa ari ya kufanya kazi, kwa kigezo cha kusubiri kuvuliwa madaraka.

Mtaka amesema Mkoa ulipokea taarifa za takwimu za wanafunzi hewa, vyumba vya madarasa, idadi ya walimu na idadi ya madawati, baada ya kupokea taarifa hizo ulionekana utofauti mkubwa wa takwimu hizo ndipo Serikali mkoani humo, ikaahidi kupitia mapungufu ya udanganyifu wa takwimu hizo kwa kila shule na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha Walimu wakuu na Wakuu wa Shule waliodanganya idadi ya wanafunzi.

Aidha, Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu umepata bahati ya kuwa na Mradi wa EQUIP Tanzania ambao umewawezesha waratibu kupata pikipiki na posho, walimu wakuu wamepewa vishikwambi kwaa jili ya utunzaji wa takwimu, hivyo Serikali inao wajibu wa kuangalia mahitaji ya Mkoa katika elimu ambapo alielekeza yafanyike mabadiliko ya Walimu wakuu Msingi, Sekondari na Waratibu wa mkoa mzima.

“Nililisema mwanzo na leo nalirudia tutafanya mabadiliko makubwa kwa Wakuu wa Shule za Msingi, Sekondari na Waratibu Elimu kata kwa kujiridhisha na maendeleo ya shule zetu, idadi ya walimu waliopo,idadi ya wanafunzi, kiwango cha ufaulu wa wanafunzi na mazingira ya shule ; lakini tutatoa upendeleo kwa shule 10 bora katika kila wilaya kwa Mitihani ya Kitaifa ya Darasa la IV, VII Kidato cha II na IV , hiki ni kipimo kimojawapo cha walimu wa kuendelea nao. Nasisitiza hakuna mtu atakayeonewa wala kufedheheshwa”, alisema Mtaka.

Mtaka amesema azma ya Serikali ni kuibua vipaji vipya vya viongozi wa Elimu katika ngazi ya Wilaya ambapo alisema ameshaagiza Maafisa Elimu wa Wilaya kuwasilisha taarifa ya walimu waliojiendeleza katika ngazi shahada ya kwanza na shahada ya uzamili ili watakaokuwa na sifa waweze kuteuliwa katika nafasi za Walimu wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata ambao watafanyiwa upekuzi (vetting) na Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Sanjari na hilo , Mkuu huyo wa Mkoa amesema Walimu wakuu na Wakuu wa shule wa zamani ni tofauti na wale wa sasa, kwa kuwa sasa hivi wamekuwa maafisa masuuli wa shule zao ambapo wanapokea fedha za Elimu bila malipo kupitia akaunti za shule zao, hivyo ni lazima wapatikane watu waadilifu, wenye sifa na uwezo wa kuongoza shule na kusimamia fedha za Serikali.

Akichangia katika kikao hicho Afisa Elimu (Msingi) Wilaya ya Meatu, George Lowasa ameshauri Uchambuzi wa watu watakaoteuliwa ufanyike katika umakini mkubwa ili wapatikane watendaji wazuri na kuhusu utoaji wa takwimu sahihi alishauri kuwe na utaratibu wa kuziboresha kila (robo) baada ya miezi mitatu ili kuwa na takwimu sahihi pale zinapohitajika.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amesema Uteuzi huo utazingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya uteuzi ambapo hakuna mtu atakayeonewa au atakayependelewa.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa amesema atawachukulia hatua Maafisa wale wanaolalamikiwa na walimu kwa kuwatolea lugha mbaya kila wanapotoa huduma kwa walimu hao katika Halmashauri za Mkoa huo.

Naye Katibu wa CWT Mkoa wa Simiyu, Said Mselema ameshauri baada ya mabadiliko ya wakuu wa shule na Waratibu wa Elimu Kata kufanyika wale ambao wataonekana hawana sifa za kuendelea kushika nafasi hizo waondolewe kwa staha, ambapo aliomba Serikali ngazi ya Wilaya na Mkoa ikishirikishe chama hicho katika masuala yote muhimu ya kuendeleza sekta ya Elimu, kwa kuwa wanamsaidia mwajiri katika usimamizi wa utendaji kwa walimu.

Kikao hicho cha wadau kilichofanyika mjini Bariadi na kimewahusisha Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Maafisa Elimu kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu pamoja na Wenyeviti na Makatibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ngazi ya Mkoa na Wilaya.

Baadhi ya Wajumbe wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (hayupo pichani) katika kikao maalum cha kutoa ufafanuzi wa agizo lililotolewa na Serikali Mkoani humo la kufanya mabadiliko ya Walimu wakuu na Waratibu Elimu kata, ambalo liliripotiwa tofauti katika vyombo ya habari na mitandao ya kijamii. kuwa Serikali imetangaza kuwavua madaraka,

Katibu wa CWT Mkoa wa Simiyu, Said Mselema (kulia) akizungumza na Maafisa Elimu na Viongozi wa CWT wa Mkoa huo (hawapo pichani) katika kikao maalum cha kutoa ufafanuzi wa agizo lililotolewa na Serikali Mkoani humo la kufanya mabadiliko ya Walimu wakuu na Waratibu Elimu kata, ambalo liliripotiwa tofauti katika vyombo ya habari na mitandao ya kijamii, kuwa Serikali imetangaza kuwavua madaraka.

Baadhi ya Wajumbe wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (hayupo pichani) wa kikao maalum cha kutoa ufafanuzi wa agizo lililotolewwa na Serikali Mkoani humo la kufanya mabadiliko ya Walimu wakuu na Waratibu Elimu kata, ambalo liliripotiwa tofauti katika vyombo ya habari na mitandao ya kijamii. kuwa Serikali imetangaza kuwavua madaraka.

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini akizungumza na Maafisa Elimu na Viongozi wa CWT wa Mkoa huo (hawapo pichani) katika kikao maalum cha kutoa ufafanuzi wa agizo lililotolewa na Serikali Mkoani humo la kufanya mabadiliko ya Walimu wakuu na Waratibu Elimu kata, ambalo liliripotiwa tofauti katika vyombo ya habari na mitandao ya kijamii, kuwa Serikali imetangaza kuwavua madaraka.

WM Majaliwa afafanua kuhusu kuondolewa Walimu Wakuu wasio na sifa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa halmashauri na Maofisa Elimu nchini kutowaondoa katika nyadhifa zao Waratibu wa Elimu Kata na Wakuu wa shule za sekondari wasiokuwa na shahada, walimu wakuu wa shule za msingi wasiokuwa na diploma badala yake wawahamasishe kwenda kusoma.
“Maofisa Elimu na Wakurugenzi msije mkawaondoa wale walimu wakuu kwa zile sifa nilizosema bado muda ukifika tutatangaza.Msije mkawakurupusha sasa hivi waacheni waendelee na kazi zao tutatoa muda ili wajipange viziri,” aliema.
Agosti 20 mwaka huu Waziri Mkuu alisema Waratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata na Wakuu wa shule za sekondari wanatakiwa kuwa na shahada huku walimu wakuu kwenye shule wanatakiwa kuwa na diploma.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha Mandela katika jimbo la Sumbawanga mjini.

Alisema Mratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata ni lazima awe na shahada ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kusimamia utolewaji wa elimu katika shule za sekondari na msingi.
“Wakuu wa shule za sekondari na waratibu wa elimu kata wasiokuwa na shahada wasiondolewe katika nafasi zao kabla ya kupewa nafasi ya kwenda kujiendeleza kwa masomo ili waweze kuwa na vigezo vya kuendelea kushika nyadhifa hizo,” alisema.
Alisema katika kuboresha maslahi ya walimu Serikali imetenga zaidi ya sh. bilioni tano kwa mweziambazo ni posho ya madaraka. Waratibu Elimu Kata wanapewa sh 250,000 kwa mwezi huku Wakuu wa shule za sekondari na walimu wakuu katika shule za msingi wanapewa sh. 200,000.

Waziri Mkuu alisema badala ya kuwaondoa kwenye nyadhifa hizo ni vema Wakurugenziwakawahamasisha walimu hao kwenda kusoma ili na wao wanufaike na posho ya madaraka iliyoanza kutolewa na Serikali hivi karibuni.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka wazazi na walezi kwenda kuwaandisha watoto wenye umri wa miaka mitano katika shule za awali ambapo watapata fursa ya kujengewa msingi mzuri wa masomo kabla ya kuanza darasa la kwanza.

Pia aliagiza shule zote za msingi nchini zisizokuwa na madarasa ya awali kuhakikisha waanzisha madarasa hayo haraka na kuanza kutoa elimu hiyo.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMIS, AGOSTI 25, 2016.

USC law students help Tanzanian albino sisters get asylum in the USA


LOS ANGELES (KABC) --Targeted in their native Tanzania simply because they are albinos, two teenage sisters have been granted asylum in the U.S. after receiving help from students at the USC Gould School of Law --- ABC7 reports.

Tindi Mashamba and Bibiana Mashamba were born with albinism, a rare genetic condition. In their African homeland, their white skin made them prey. Witch doctors pay for body parts and promote the belief that the limbs of albino children hold magical powers.

At age 9, Bibiana's leg and two of her fingers were cut off and sold.

"In our country, albinos, we are not safe," said Bibiana, now 17. "People are hunting for body parts."

For that reason, the sisters turned to the law school at USC for help as their tourist visas were expiring. They received help from the Los Angeles-based African Millennium Foundation and the Orthopedic Institute for Children, which provided therapy for Bibiana and a new prosthesis.

But the teens' constant worry was the possibility of having to return to Tanzania.

"Spell of the Albino," an award-winning documentary produced by Claudio von Planta, chronicles the violence. One assailant cut off the fingers of a child named Adam, with the permission of the boy's father. Investigators believe the dad allowed the attack because he was driven by poverty.

When a group of USC law students heard the Mashamba sisters' plea to stay in the U.S., the aspiring attorneys filed reams of documents. The sisters recently received a letter approving their petition for asylum. Wednesday at the law school, the teens exchanged celebratory hugs with those who worked on their case.

"We are going to court. We are helping people in community and we are providing real-world experience to our students," said USC's Jean Reisz, the law students' mentor.

"It's rewarding, to not only learn the law but make a profound difference in someone's life," said second-year law student Elena Babakhanyan.

The Mashamba sisters' faces radiated with joyful smiles.

"I am happy to stay here without fear," said Bibiana.

After being granted asylum, the sisters have made a pledge: to fight the ignorance that breeds such violence against children, and to return to Tanzania to help others after receiving an education in the U.S.

Hotuba ya Waziri Mahida ya ufunguzi wa Kongamano la 3 la DiasporaHOTUBA YA MHE. BALOZI AUGUSTINE PHILIP MAHIGA, (MB) WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI WAKATI WA KUMKARIBISHA MHE. DKT. ALI MOHAMED SHEIN, RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI WAKATI WA UFUNGUZI WA KONGAMAMO LA TATU LA DIASPORA (3RD DIASPORA CONFERENCE) ZANZIBAR, 24 AGOSTI, 2016

Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mhe. Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi;

Mhe. Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;

Mhe. Issa Haji Ussi Gavu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;

Mhe. Said Hassan Said, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;

Waheshimiwa Wabunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar;

Waheshimiwa Makatibu Wakuu wa Serikali zote mbili;

Waheshimiwa Mabalozi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi;

Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;

Ndugu WanaDiaspora na Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.

ASSAALAM ALEYKUM,

Napenda kuchukua nafasi hii na kutoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuwa mwenyeji wetu na kukubali kuwa mgeni rasmi katika kongamano hili la Tatu la Diaspora. Uwepo wako katika Kongamano hili ni ishara kubwa ya mapenzi ya dhati uliyonayo kwa Diaspora na kutambua umuhimu wa mchango wao katika kuleta maendeleo ya nchini.

Vilevile, nawashukuru sana waandaji wa Kongamano hili kwa ujumla wao pamoja na wadhamini wetu ambao isingekuwa wao tusingeweza kufanikisha shughuli hii. Shukrani za pekee ziwaendee Kamati ya Mapokezi, kwa mapokezi mazuri tangu tulipowasili hapa visiwani Zanzibar, ninawashukuru sana na kuwapongeza kwa kazi nzuri.
Napenda kuchukua nafasi hii pia kuwapa pole kwa safari ndugu zetu wa Diaspora waliosafiri masafa marefu kutoka kila kona ya dunia kuja kuhudhuria Kongamano hili muhimu. Sina shaka mtafurahia ukarimu wa visiwani na huduma mbalimbali mtakazo zipata katika kipindi chote mtakacho kuwepo hapa Zanzibar. Karibuni sana mjisikie mko nyumbani maana mtu kwao ndio ngao.

Mhe. Rais,
Mabibi na Mabwana,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilianzisha Idara ya Diaspora mwaka 2010 kwa lengo la kuwatambua Watanzania wanaoishi ughaibuni na kuwahamasisha katika kuchangia maendeleo ya nchi kwa kutumia mitaji, ujuzi na elimu wanayoipata wakiwa nje ya nchi kwa manufaa ya Taifa lao.
Tangu ilipoanzishwa Idara, kumekuwa na jitihada mahsusi za kuwahamasisha na kuwashirikisha Diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi. Kwa kuanzia, Wizara yangu imekuwa ikiratibu makongamano ya Diaspora ndani na nje ya nchi, na hatimaye Kongamano hili la tatu linalofanyika hapa nchini.
Kwa ufupi lengo la makongamano haya ni kutengeneza mazingira wezeshi ya kuwakutanisha Diaspora na Taasisi mbalimbali zilizopo nchini ili kutumia nafasi hiyo kubadilishana mawazo, elimu na ujuzi katika kuleta maendeleo nchini. Azma hiyo pia inalenga kuongeza fursa za uwekezaji na kupanua soko la bidhaa la biashara ndogondogo na za kati ndani na nje ya nchi.

Mhe. Rais,
Mabibi na Mabwana,

Kongamano la Mwaka huu lina kauli mbiu isemayo ‘Bridging Tanzania Tourism and Investment : ’A new Outlook” kwa Kiswahili tunasema kiunganishi cha utalii na uwekezaji: mtizamo mpya ikiwa ni azma ya Serikali kuleta mwonekano mpya wa kujenga Tanzania yenye matumaini ya uchumi wa kati. Diaspora wakiwa wadau wa maendeleo wana nafasi kubwa ya kuimarisha maendeleo ya utalii na sekta ya uwekezaji kwa mustakabali wa ukuaji wa uchumi wa nchi yetu tukufu ya Tanzania.

Vilevile, Kauli Mbiu hii imechaguliwa ili kuweka msisitizo wa jitihada za Serikali katika kukuza sekta ya utalii na uwekezaji katika uchumi wa nchi, ili kuongeza nafasi za ajira nchini. Tuna imani kuwa Kongamano hili litakuwa ni chachu ya kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii na uwekezaji hapa visiwani kwa kushirikiana na Diaspora wetu katika nchi wanazoishi.

Mhe. Rais,
Ndugu Diaspora,

Nachukua nafasi hii kupongeza ushirikiano na uratibu mzuri baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; kupitia Wizara yangu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na Ofisi ya Rais –Zanzibar Ushirikiano huo umezaa matunda mazuri na leo hii tunajivunia uwepo wenu Diaspora ambao ni wa kihistoria. Shukran kubwa zitolewe kwa wadau na taasisi zilizoshiriki kutoa ufadhili ili kulifanikisha Kongamano hili.

Mhe. Rais,
Ndugu Diaspora,

Kongamano hili limeambatana na maonesho ya huduma zinazotolewa na Taasisi mbalimbali kwa ustawi wa jamii ya Diaspora. Maonesho hayo yameshirikisha wafadhili na vikundi vya wafanyabiashara, mashirika ya umma na Taasisi binafsi, pamoja na Diaspora wenyewe.

Aidha, katika siku mbili hizi kutakuwa na uwasilishwaji wa mada zitakazotolewa na Watendaji Wakuu wa Wizara, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi. Lengo ni kuwapatia washiriki, hususan Diaspora ufahamu na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya utalii na uwekezaji ambao unachangia katika maendeleo ya nchi yetu kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Ushiriki wa Kongamano hili unajumuisha vikundi vya wafanyabiashara, Taasisi mbalimbali za utalii, Diaspora waliorejea baada ya kuishi ughaibuni kwa muda mrefu na wadau wengine kutoka taasisi za umma na binafsi ziilizopo nchini.

Vilevile, kama ilivyokuwa mwaka jana, Kongamano la mwaka huu limehudhuriwa na maafisa kutoka Ofisi za Balozi zetu nje ya nchi. Lengo la kuwashirikisha maafisa hao ni kuhakikisha kuwa wanafuatilia utekelezaji wa maazimio yatakayopitishwa hapa wakati Kongamano hili. Kwa kutambua kuwa Balozi zetu ndio kiungo muhimu baina ya Serikali na Diaspora.

Mhe. Rais,
Mabibi na Mabwana.

Mwisho, naomba uniruhusu nichukuwe fursa hii kuipongeza Kamati ya Maandalizi kwa kufanya kazi hii kwa ushirikiano mkubwa pamoja na kuwashukuru kwa dhati Taasisi zote zilizodhamini Kongamano hili. Ni malengo yetu tutaendelea kushikamana na kufanya kazi kwa pamoja ili kulisukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa letu.

Bila shaka Diaspora wamehamasika vya kutosha na kuthibitisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawajali na iko tayari kuchukua kila hatua kuwashirikisha katika maendeleo chanya ya nchi yetu.

Baada ya kusema hayo naomba nimkaribishe Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ili aweze kufungua rasmi Kongamano hili na kuzungumza na Diaspora.

Asanteni kwa kunisikiliza.

Karibuni sana Mhe. Rais


Taarifa ya habari ChannelTEN Agosti 25, 2016


Mkurugenzi wa Halmashauri Bunda amsimamisha kazi mtumishi wa Ardhi na Mipango Miji

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara, Bibi. Janeth Mayanja amemsimamisha kazi mtumishi wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji kwa kosa la kujipatia fedha kinyume na taratibu za utumishi wa umma.

Akizungumza leo mjini Bunda wakati wa tukio hilo, Bibi. Mayanja alisema kuwa ameamua kumsimamisha kazi kwa muda, Bw.Eliudi Haonga ambaye ni mtumishi wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji pia ni Mthamini wa Halmashauri hiyo ili kupisha uchunguzi kwa kosa la kujipatia fedha kinyume na taratibu za utumishi wa umma.
“Tarehe 28 mwezi Juni mwaka huu Bw. Eliudi Haonga alipokea fedha kiasi cha shilingi milioni saba kutoka kiwanda cha Olam ikiwa ni kodi ya pango kwa mwaka kodi 2015/2016, lakini mtumishi huyo alihifadhi kwenye akaunti ya Halmashauri ya mji yaani ‘own source’ fedha kiasi cha shilingi milioni mbili tu, na kiasi kilichobaki yaani milioni tano alizitumia kwa masuala binafsi kinyume na taratibu za utumishi wa umma” alisema Bibi Mayanja
Aliongeza kuwa Bw. Haonga aligushi risiti ya Halmashauri ya Mji na ambayo aliikabidhi katika kiwanda cha Olam baada ya kupokea fedha hizo.

Alisisitiza kuwa mtumishi huyo amesimamishwa kazi kwa mujibu wa kifungu namba 38 (1) cha kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003.

Aidha, Bibi Mayanja amewaasa watumishi wa umma wanaofanyakazi katika Halmashauri hiyo kuwa waadilifu kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi. Vile vile ameonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka.

---

Immaculate Makilika

Waliokosa nafasi Programu Maalum ya Ualimu UDom wapangiwa vyuo vya serikali


Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewapangia vyuo wanafunzi wa programu maalum ya ualimu chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) ambao hawakupata nafasi ya vyuo katika awamu ya kwanza, walioagizwa kuomba mafunzo kulingana na sifa zao kupitia Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (NACTE).

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo leo, jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa taarifa kuhusu wanafunzi wanaosoma stashahada maalum ya ualimu wa sayansi chuo kikuu cha Dodoma.
“Mtakumbuka tuliagiza kwamba wanafunzi ambao walikosa sifa za kujiunga na ualimu wa sayansi waliombwa kuomba mafunzo yanayolingana na ufaulu wao kupitia NACTE, Lakini baada ya taarifa hiyo tulipokea maombi mengi kutoka kwa vijana hawa wakiomba kupangiwa vyuo moja kwa moja na Wizara, wizara imetafakari na kuamua nao wapangiwe vyuo vya Serikali,” alifafanua Dkt. Akwilapo.
Aliendelea kusema kuwa, wanafunzi ambao waliachwa awamu ya kwanza na kupangiwa katika awamu ya pili ni wanafunzi 290 ambao walikuwa wakisomea programu ya stashahada ya ualimu wa sekondari na wanafunzi 1,181 ambao walikuwa wakisomea stashahada ya ualimu wa msingi.Dkt. Akwilapo amesema kuwa Wizara imeamua kuwapangia wanafunzi hao vyuo kutokana na kuonyesha nia ya dhati ya kusomea ualimu ambapo wanafunzi hao wamepangiwa vyuo vya ualimu vya Marangu na Tabora.

Aidha, Dkt. Akwilapo ameeleza kuwa wanafunzi hao watajigharamia masomo yao kulingana na viwango vya ada vilivyowekwa na Serikali. Pia amewataka kutembelea tovuti ya wizara ya hiyo ambayo ni www.moe.go.tz ili kuona vyuo walivyopangiwa.

Mnamo tarehe Mei 28, 2016 Serikali iliwarejesha nyumbani wanafunzi 7,805 waliokuwa wanasoma Stashahada Maalum ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Katika mchujo wa awamu ya kwanza wanafunzi 382 ndio waliokuwa na sifa ya kuendelea na masomo chuo kikuu cha UDOM na wengine 4,586 walipangiwa vyuo vya ualimu vya Serikali.

---
Lilian Lundo - MAELEZO

Taarifa ya Ikulu: Uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi NIDA


Taarifa ya NMB kwa umma kuhusu waajiriwa waliofutwa kazi