Makala ya Mwalimu: Ni njia gani itakayokuhakikishia usalana na usiri wako wakati wa mawasiliano?

NI NJIA GANI ITAYOKAYOKUHAKIKISHIA USALAMA NA USIRI WAKO WAKATI WA MAWASILIANO?


Utangulizi:

Usiri (confidentiality) na usalama (security) ni dhana na bidhaa mbili zenye umuhim mkubwa sana kwenye mawasiliano kwa njia za kielekroniki kama simu, ujumbe mfupi wa maandishi, na baruapepe (emails). Moja, ni uhakika kwamba nikiongea na mtu kwa simu au kwa ujumbe wa maandishi (SMS au programu zingine zinazoruhusu kuchati) au kwa baruapepe (emails) hakuna mtu mwingine asiyehusika ambaye anaweza kuyasikia au kuyaona mawasiliano yangu (confidentiality). Mbili, ni uhakika kwamba ninapofanya mawasiliano, mtu au watu wenye lengo la kufuatilia mawasiliano yangu hawataweza kufanya hivyo kwa kuwa nina ulinzi dhidi ya kuingiliwa (kusikiliza sauti au kuona ujumbe) mawasiliano yangu (Security). Haya mambo mawili ni mahitaji makubwa kwa mteja yeyote wa huduma ya mawasiliano duniani kote.
https://3.bp.blogspot.com/-MLjGkiohEvQ/WHpc58uWM1I/AAAAAAAAB3Y/yavbXoO4ns0qS0M5dlp4aiKweSupDIWpACEw/s640/simu1.jpg
Jinsi mawasiliano ya simu yanavyoweza kuingiliwa.  Chanzo: mtandao wa Internet 

Sio lengo la makala hii fupi kukuchosha kwa kuongea kwa undani utaalamu na teknolojia za mawasiliano na jinsi zinavyofanya kazi bali nataka tu kumishirikisha elimu kidogo kwa wale wasio na uelewa wa kutosha na hivyo kumisaidia mambo kadhaa: moja, kujua njia sahihi ya kutumia kulingana na aina ya mawasiliano; mbili, kujua njia gani sio sahihi kuwasiliana wakati gani; tatu, kujua jinsi ya kujilinda na kujihakikisha usalama na usiri kwenye mawasilinao; na nne, kuwa na ujasiri au kujiamini unapowasiliana kwamba uko salama. Hali kadhalika, inaweza kumisidia baadhi ya watu kujua ni aina gani ya simu au vifaa vingine wanavyohitaji kulingana na asili ya mawasiliano yao. Hata hivyo, makala hii haina lengo la kumshawishi au kumsaidia mtu kufanya uhalifu na kuvunja sheria zihusianazo na makosa ya mawasilinao ya kimtandao.
https://2.bp.blogspot.com/-IWM1ObdNDdc/WHpetcCOW-I/AAAAAAAAB3o/yPoYsI92P18lrG28vAsLHUSqd3KAU2c1gCLcB/s640/simu3.jpg
Rais wa Marekani na mshauri wake mkuu wa mambo ya usalama wa taifa wakiongea kwenye chumba maalumu cha mawasiliano ya simu yenye usiri na usalama wa hali ya juu (CHANZO)
https://2.bp.blogspot.com/-M1Jm-ivudyo/WHpc5zLoGsI/AAAAAAAAB3c/a4aeX6tsom4DU8hHCanL3KScVxX1Ib_uwCEw/s640/simu%2B2.png
Kielelezo cha ulinzi wa mawasiliano kati ya pandde mbili. Cahnzo: kutoka kwenye Internet

Zipo sababu nyingi zinazotufanya tulazimike kuhitaji usiri mkubwa (confidentiality) na uhakika wa usalama wa mawasiliano (security) tunayofanya. Sio tu kwa sababu tunaweza tukawa tunapeana taarifa zinazotafutwa, au tunatukana mtu, au tunapanga njama mbaya, bali usiri ni haki na hitaji la msingi la kila mwanadamu. Ndio mana kwenye nchi za wenzetu ambazo kuna kamera za usalama (surveillance cameras) karibu kila mahali, sio rahisi ukute chooni kumeandikwa kwamba kuna kamera. Kwa nini? Ni kwa sababu mwanadamu ana upande wa maisha anayohitaji usiri na akikosa hitaji hili anapoteza haiba na utashi wake na anakua sawa na wanyama wengine wasio na utashi kama wetu. Hakuna mtu mwenye mamlaka na sababu ya kumnyima mwanadamu mwingine hitaji hili la asili ili mradi havunji sheria na taratibu zilizowekwa na jamii. Unahitaji usiri wa mawasiliano na watoto au wazazi wako; usiri na mwenza wako, na rafiki zako, nk. Unahitaji usiri na usalama wa mawasiliano yako ya kibiashara, ubunifu, na mikakati mingine ambayo kuiweka wazi kwa mtu zaidi ya yule unayemkusudia kunaweza kuhatarisha jambo fulani au kukuletea hasara au heshima kwenye jamii. Kuna lugha ya “kijinga na kitoto” mtu anaweza kuitumia na mke/mume/mpenzi wake kama sehemu ya mahusiano yao na ambayo hawezi kuitumia pengine popote katika ulimwengu huu na ni vema awe na uhakika kwamba atakapotumia njia mawasiliano bado itabaki ni siri kati yao.

Mvutano katika ya watawala na teknolojia
Kabla ya kwenda mbali, niseme tu kwamba duniani kote kuna mgogoro mkubwa kati ya wataalamu na watoa hudumu za teknolojia za mawasiliano na watawala/serikali/ vyombo vya usalama. Wakati serikali za mataifa yenye nguvu na maendeleo makubwa ya mawasiliano kama Uingereza, Marekani, Ujerumani, Urusi, na wengine wanawekeza sana kukuza teknolojia hizi na kutengeneza wataalamu wenye ujuzi mkubwa, wamejikuta wanaingia pia kwenye mgogoro na makampuni pale ambapo yanakua na uwezo wa kuwazuia watawala na vyombo vya usalama kuingilia mawasiliano ya watu binafsi. Vyombo vya usalama na serikali vinataka kuingilia mawasilino ya watu kwa madai ya kuhakikisha usalama wa nchi na ulinzi kwa ujumla wake na hivyo vinalazimisha wataalamu wa huduma za mawasiliano waache angalau “mlango au dirisha wazi” katika teknolojia zao ili kuwawezesha kuingia ndani na kufanya watakalo. Kwa kifupi wanawaambia jenga nyumba imara, milango imara, madirisha imara, fensi imara yenye geti kubwa, na weka fensi ya umeme. Ila mwisho wa siku nyumba hiyo muitumie bila kufunga mlango mdogo wa geti la nje na waache mlango mmoja au dirisha wazi muda wote kuwawezesha kuingia ndani muda wanaotaka.


Makampuni ya mawasiliano wamekua wakipingana na matakwa haya ya watawala na vyombo vya usalama kwa nguvu kubwa kwa maslahi ya wateja wao na maslahi mapana ya uvumbuzi wa kiteknolojia. Wakati madai na matakwa haya ya watawala ni ya msingi na yana tija, ukweli unabaki kwamba iwapo wataacha dirisha au mlango wazi kwenye mfumo wa mawasiliano, hutatumiwa na vyombo hivi au watawala pekee kwa maslahi ya kiulinzi na usalama. Mlango au dirisha hilo litakua wazi pia kwa vibaka, wahuni, walanguzi, matapeli, majambazi, wambea, waongo, mafisadi, wapelelezi, wanafiki, na wengine wote wenye maslahi (interest) na vilivyoko ndani ya nyumba hiyo. Hivyo wakati uwazi huo utakua unawasaidia watawala na vyombo vya usalama kurahisisha kazi zao, utamweka hatarini mteja wa huduma hii maana wajanja watamwingilia. Serikali na vyombo vya usalama za nchi hizi zinapata ugumu wa kuyafungia makapuni au kuyalazimisha kutimiza matakwa yao kwa sababu nao ni wateja wa teknolojia hizi na iwapo watawatisha watalaamu na makampuni haya wataua hazina ya uvumbuzi na utaalamu wa kiteknolojia ulio adimu na wenye faida kubwa kwa mataifa yao. Moja ya ngumu za mataifa makubwa duniani sio tu uwezo wa silaha, kivita, na uchumi mkubwa, bali ni uwezo wa gunduzi za kiteknolojia hasa kwenye eneo la mawasiliano. Makampuni ya mawasiliano yamekua yakipinga harakati za serikali kuwa na uwezo wa kuingilia mawasiliano kwa lengo la kuwalinda wananchi dhidi ya serikali zinazokandamiza uhuru wa watu binafsi au watu wanaopingana na watawala. Mataifa haya yanafanya nini kutimiza watakacho?

Nchi na na vyombo vya usalama vya mataifa makubwa, pamoja na mambo mengine ndio wana wataalamu bingwa wa teknolojia za mawasiliano na programu za kielekroniki/ kompyuta kuliko hata makampuni ya kibiashara. Baadhi ya gunduzi kubwa za teknolojia za mawasiliano duniani zimeanzia katika vyombo vya ulinzi na usalama. Mataifa haya badala ya kupambana na makampuni ya mawasiliano na kuwalazimisha kufungua madirisha na milango, wanahakikisha wataalamu wao wana maarifa, uzoefu, na elimu ya kutosha ya kila teknolojia mpya. Wanaposhindwa kukabiliana na changamoto basi inawalazimu kwenda mtaani kutafuta wataalamu na kuingia nao mikataba ya kuwasadia kwa kazi maalumu za kifundi. Hii haijafanya waache kulazimisha makamuni kulala milango wazi lakini wanapokataliwa wanabidi kuwa wapole hasa kutokana na mifumo yao imara ya kitaasisi na kisheria inayotoa uhuru na mamlaka makubwa katika biashara na kazi za kitalamu na kisayansi.

Kwa nchi zetu za ulimwengu wa tatu na zilizo nyuma kiteknolojia na utaalamu, bado safari ni ndefu kufikia hatua hizi. Nchi nyingi maskini hazina hata wataalamu wa kawaida katika vyombo vyao vya ulinzi na usalama wenye uwezo na elimu sahihi kuhusu mifumo ya kielekroniki. Na ndio mana sisi tuna njia zetu wenyewe za kimaskini-maskini za kukabiliana na tishio la kiusalama utokanao na mawasiliano ya kimtandao. Kwa kua sio malengo ya makala hii, sitazitaja wala kuzijadili. Ila niseme tu kwamba kama kuna eneo nyeti la kiusalama duniani kwa sasa ambalo nchi zetu zinatakiwa kuwekeza bila mzaha, siasa, kuchelewa, na kudharau taalamu na wataalamu, ni teknolojia za mawasiliano. Ni lazima nchi zetu ziajiri na kufundisha watu wenye uwezo mkubwa wa kiakili katika eneo hili ili wawe sehemu ya usalama na ulinzi wa taifa badala ya kulichukulia kirahisi na kutumiwa “watu wenye uwezo wa kawaida” kufanya jukumu hili. Tunaona sasa kwamba vita kubwa kati ya Marekani na mataifa pinzani kama Urusi, China, Korea na mengine sio ya silaha, majeshi, wala matisho ya silaha za nyuklia pekee bali imehamia kwenye mawasiliano na taarifa maana ndio habari za mujini kwenye ulimwengu wa dijitali.

Mwaka jana vyombo vya ulinzi vya Marekani viliingia kwenye mgogoro na kampuni kubwa ya simu za mikononi za iPhone na kompyuta aina ya Mac vikiitaka kampuni hii ipunguze ugumu wa kuingilia simu zao (hacking) ili waweze kupenyeza kwa kigezo cha kufuatilia mawasiliano mahususi ya kiusalama dhidi ya ugaidi. Walifanya hivi baada ya wataalamu wao kushindwa kabisa kufanikiwa kuingilia mawasiliano ya simu za iPhone kwa mtu ambaye anazitumia kwa kufuata taratibu za kiusalama ikiwa ni pamoja na kuweka ulinzi wa nywila (password). Walichokua wanataka ni kuwaambia iPhone, “Tumeshindwa kuvunja mlango au ukuta ili tuingie ndani ya nyumba hivyo tunaomba muache mlango wazi au muvunjie ukuta ukae wazi kutuwezesha kuingia ndani”. Kampuni ya Apple iligoma kabisa na ikavilazimu vyombo husika kutafuta mtaalam mtaani (ambaye walimpata nchi nyingine) ambaye alikua na utalaamu husika na wakafanikisha mpango wao.

Kampuni ya Facebook iliyonunua kampuni iliyodungua Whatsap, mwaka jana waliongeza usalama kwenye mawasiliano kwa njia ya programu ya whatsapp yanayozuia mtu kuweza kuingilia mawasiliano. Jambo hili lilileta utata mkubwa hasa kwa serikali ya Uingereza hadi kufikia bunge kutaka kutunga sheria itakayozuia kutumiwa kwa teknolojia za aina hii ambazo zinawanyima wakuu wa serikali na vyombo vya usalama kuingilia mawasiliano hata wanapokua na sababu za msingi.

Wewe unawezaje kujilinda?
Watu wengi wamekua na maswali mengi juu ya usalama na usiri (security and confidentiality) ya  mawasiliano yao wanayofanya hasa kwa njia ya simu za mkononi. Siku za karibuni watu wengi wameingiwa na hofu wakiamini kwamba mawasiliano yao sio salama na yanaweza kuingiliwa na watu wengine wenye nia mbaya, au vyombo vya usalama, au wapita njia, na hivyo kuhatarisha usalama wao na kudhoofisha usiri wao. Hili limetokana na ukweli kwamba kumekua na matukio mengi ya mawasiliano ya watu ambayo yalikua ni ya siri lakini yametolewa hadharani bila idhini yao na wengine kukamatwa na kushtakiwa kwa mawasiliano yalioonekana yanavunja sheria za nchi. Hofu hii inatokana na ukweli kwamba watu wengi wana uelewa mdogo juu ya teknolojia zinazotumika katika njia mbalimbali za mawasilino na hivyo kuwa wepesi kudanganywa, kutishwa, au kupotoshwa juu ya usalama na haki yao ya usiri wa mawasiliano.

Labda nijenge hoja kwa kukuuliza maswali:
1. Ni njia gani salama kuwasiliana kwa sauti kati ya kupiga simu za kawaida kwenye namba ya mtu au kutumia applications/ programs zinazotumia internet kama skype, whatsapp, na zingine?
2. Ni njia ipi salama kutuma ujumbe mfupi wa mkononi kati ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi (SMS text messages) au kutumia program zinazotumia internet kama whatsapp, facebook, skype, nk, kutuma ujumbe wa maandishi?
3. Ni njia ipi rahisi kutuma ujumbe wa siri kati ya ujumbe mfupi wa simu, barua pepe (email), kuchati kwa Facebook, skype, whatsapp, twitter, nk?
4. Je, ni salama kiasi gani kuwasiliana au kushiriki kwenye mijadala ya makundi ya kuchati (alamaarufu kama grupu za whatsaap)?

Sehemu ya pili ya makala hii itajikita kuchambua na kutoa mwanga kwenye maswali haya hivyo usikose kuisoma. Unaweza msaidia mtu mwingine kwa kumshauri kusoma makala hii ili kuongeza ufahamu wake wa mawasiliano anayotumia kila mara.

Mwandishi wa makala hii ni Mwalimu MM ambaye ni Mtafiti wa shahada ya uzamivu katika matumizi ya mifumo ya kielekroniki na simu za mikononi katika huduma za afya. Unaweza kuwasiliana naye kwa barua pepe (mmmwalimu (at) gmail.com )

Mwalimu MM