Mwl. Mndeme: Ushauri kwako Mhe. Paul Makonda

USHAURI KWAKO MH PAUL MAKONDA
C:\Users\User\Desktop\makonda.jpg

Jana nimesikiliza sehemu ya mazungumzo yako kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na wadau wa usafiri wa Taxi jijini DSM hasa kutokana na kile ambacho kimeonekana kama “uvamizi wa kampuni ya Uber” kwenye soko la Taxi. Katika jumla ya niliyojifunza kwenye kikao kile, inaonekana wadau wa Taxi (madereva na wamiliki ) wanalalamikia Kampuni hii juu ya utaratibu wanaotumia kufanya biashara na gharama wanazotoza kutokua halisia (kidogo sana ukilinganisha na viwango vyao vya kawaida) na hivyo kuathiri sana soko lao.
Katika kikao hiki nilivutiwa na mtizamo wako kuhusu tatizo hili kwani nilelewa mambo kadhaa toka kwako: kwamba kwanza umegundua kuna tatizo; pili ulifanya utafiti wako kidogo na usio rasmi; tatu ukataka kuwasikiliza wahusika na kupata maelezo na ushahidi wa kutosha kuhusu tatizo; na mwisho ukataka kupata mapendekezo ya kutatua tatizo toka kwa wanaoathirika. Kwanza niseme hii ni hatua na mtizamo mzuri sana kwa kiongozi wa watu. Kama kiongozi ni vema kuchukua muda unapokabiliana na tatizo kubwa la kijamii na kupata maelezo sahihi kabla ya kufanya maamuzi au kutoa maelekezo. Pili, umeonesha busara kama kiongozi kuwashirikisha waathirika katika kutafuta suluhu na majawabu ya matatizo kabla ya kufanya maamuzi maana kuwa kiongozi hakumaanishi unajua kila kitu. Huu ni mtazamo mzuri na ninakupongeza.
Nimeona umewapa wadau wiki moja wakatafakari na wakupelekee mapendekezo yao. Kwa kuwa wiki hiyo haijaisha nimetamani nami kama mdau wa mkoa wako na zaidi sana kama raia wa Tanzania, nitoe mchango wangu kushauri jambo hili ili kama itakupendeza wewe na wasaidizi wako, muchanganye na mapendekezo yatakayoletwa wadau kupata suhuhisho na majawabu ya kusaidia. Nitajaribu kufupisha sana mawazo yangu:
 1. Moja, mimi sijawahi kutumia usafiri wa Uber DSM lakini nimeutumia nje ya Tanzania. Ni ukweli usio na kificho kwamba mfumo wao wa uendeshaji biashara ya Taxi una faida nyingi kwa mtumiaji hasa kuokoa muda, kupata huduma mahali ulipo,na wakati mwingie gharama ni ndogo kidogo ukilinganisha na wato huduma wengine. Hili halipingiki hasa unapofananisha na huduma zetu za taxi ambazo ziko kizamani sana.
 2. Pili nimesikitika kwamba nchi yetu imefikia mahali pa kuruhusu hadi biashara ya Taxi imfanywe na makampuni ya nje. Uber ni kampuni ya Kimarekani yenye Makao yake makuu katika Jiji la San Fransisco na ilizianzishwa mwaka 2009 jamaa wawili Garrett Camp na Travis Kalanick. Ndani ya maiaka michache ya uhai wake imejitahidi kujipanua kwa haraka kwenye nchi kadhaa. Nchini Uingereza ina maika kama 2 sasa na inapanuka kwa kasi huku kukiwa na mambo kadhaa ambayo yameshaleta migogoro.

Nchi zote makini duniani na hasa za kimagharibi (zilizoendelea) zinajitahidi sana kutoruhusu kila kazi/biashara kufanywa na watu wa nje ya nchi yao. Wanalinda soko lao na wanalinda ajira na vipato vya watu wao. Ndio mana unaweza kuingia kwao ukiwa hata na PhD au umeipata kwao na ikawa ngumu sana kuajiriwa kwa kuwa wanatoa kipaumbele kwa watu wao. Kwa kifupi hawakupi ajira iwapo kuna mtu wao anaihitaji na hana kazi. Tunapoongelea habari ya kukuza uchumi wa watanzania kama taifa na kwa mtu mmoja mmoja ni lazima tuwe na mikakati ya kulinda baadhi ya ajira na biashara kwa ajili ya watu wetu hasa zile zinazofanywa na watu wa kipato kidogo na zisizohitaji utaalamu na elimu kubwa. Ninashawishika kwamba kuruhusu wageni na makampuni ya kigeni kuwekeza usafiri wa taxi, mabasi, bajaji, mama lishe, na zingine zinazofafa na hizo sio kitu sahihi na tutapoteza mwelekeo. Tutunze ajira hizi kwa ajili ya watu wetu kwa nguvu zetu na makampuni ya kigeni tuwasukumize wakawekeze kwenye biashara na shughuli zinazohitaji mitaji mikubwa, utaalamu wa hali juu, na teknolojia ambazo hatuna kama vile usaifiri wa ndege, treni, viwanda vya uzalishaji, nk.

 1. Tatu, tunaporuhusu makampuni ya kigeni kuwekeza kwenye biashara za kawaida kama hizi ni wazi kwamba unazidi kuondoa fedha kwenye mzunguko wa watu wa kawaida. Hata kama kampuni hiyo inalipa kodi, tujue kwamba faida wanayoipata kwa sehemu kubwa haibaki nchini maana inakwenda kwenye nchi zao. Hata kama ikibaki haibaki kwa watu ambao fedha hiyo imetolewa (watu wa kipato na maciha ya chini). Hii bado inanipa ushawishi wa kutoruhusu wageni kuwekeza kwenye maeneo kama haya.
 2. Nne, ni kweli tunatakiwa kuboresha huduma ya taxi DSM na miji mingine iondokane na uzamani, ulanguzi, uhatari, na ulaghai. Tunaweza kuboresha huduma hii ikawa ya kisasa, ya kuheshimika, salama, na isiyo na ulanguzi bila kuitafuta wawekezaji au wataalamu wa nje. Mambo kadhaa yanaweza kufanyika:
  1. Tuachane na mfumo wa kuendesha biashara ya taxi kwa mtu mmoja mmoja na badala yake iendeshwe kikampuni. Inaweza ikaundwa kampuni moja au zaidi ambayo kila mwenye taxi anajisajili huko na biashara inakua ni kati ya wateja na kampuni badala ya dereva na mwenye taxi. Kwa mfano, Chama cha Madereva Taxi DMS kinaweza kuondokana na kuwa chama ikawa kampuni. Kila mwenye Taxi anaingia mkataba na kampuni hiyo na kampuni inaweka viwango vya gharama inayoeleweka kwa umbali (kimometa) badala ya ilivyo sasa. Pia kampuni itahakikisha kila taxi inafungwa kifaa cha kuhesabu umbali na kukokotoa gharama hivyo mteja anaona kabisa kasafiri umbali gani na ni gharama kiasi gani bila kuibiwa na kulanguliwa. Vifaa hivi sio ghali na vinapatikana
  2. Kwa kutumia wataalaamu wetu wa ndani na hasa vyuo vikuu, kampuni hizi watengeneze mifumo ya kompyuta ambayo itazisajili taxi zote na kuziratibu zinapokua barabarani ili kutoa huduma kwa wakati. Hii itapunguza uzamani uliko sasa hivi wa taxi kutoka Posta au Mbagala kumfuata mteja Bunju kwa kuwa ndio anaijua wakati kuna Taxi ziko barabarani nyingi kuanzia Mwenge hadi Bagamoyo. Mfumo wanaotumia Uber hautofautiani sana na huu lakini hiki ndicho nchi nyingi za wenzetu zinatumia kwa sasa. Hii itasaidia huduma ya Taxi ipatikane njiani lakini pia mtu aweze kupiga simu kwenye ofisi ya kampuni na kutumiwa taxi iliyokaribu na alipo. Hii tapunguza sana gharama kwani kwa sasa madereva wanatoza gharama kubwa ikisababisha na safari ndefu ya kwenda na kurudi (round trips) kutoka alipo hadi anapompeleka mteja na kurudi tena maskani ake. Najua bado tunachangamoto ya anuani sahihi za makazi lakini bado tunaweza kufanya tafakuri fikirishi na tukapata namna nzuri tu ya kukidhi mahitaji.
  3. Mara nyingine ninahisi viongozi wetu na taasisi za maamuzi serikalini hazina taarifa sahihi/za kutosha juu ya ujuzi na utalaamu wetu uliolala kwenye vyuo vikuu na hivyo kujikuta wanashiwika kirahisi na makampuni ya nje kwenye mambo yahusuyo teknolojia hasa kwenye TEHAMA. Hili laweza kuchangiwa pia na wataalamu wetu hasa vyuo vikuu kujifungia ndani na jamii kutokujua wanaweza kuisaidiaje, lakini tuna wajuzi na wataalmu wengi wanaoweza kuboresha huduma kama hizi. Ninakuomba nenda pale Bamaga kwenye kampasi ya elimu za TEHAMA ya Chuo Kikuu cha DSM (UDSM) wakishirikiana na Shule yao Kuu cha Biashara waambie wakusaidie kukubunia mfumo wa kuratibu Taxi kwenye mkoa wako na mupeane muda. Kwa kufanya haya utakua umeshiriki kukuza tafiti, kuendeleza ubunifu wa ndani, na utakua umepata suluhisho na majawabu unayotafuta kwa mkoa wako. Pia utagundua kwamba Uber au wengine wa nje hawana miujiza sana katika wanachokifanya kwani yanaweza kufanywa vyema na watanzania wenyewe. UDSM kukimba mbali mkoa wako una vyuo vingine kama IFM na DIT ambavyo vina wataalamu wengi wa mifumo ya TEHAMA
  4. Biashara ya Taxi irasimishwe. Kwa utaratibu maalumu na kwa awamu tuachane na mtindo kufanyika biashara hii kienyeji na chini ya wamiliki binafsi ili  kuboresha na kuhakiki usalama wake, kufanikisha ukusanyaji wa kodi, kuongeza ufanisi kwa watumiaji wa huduma, na kupunguza ughali usio wa lazima.

Kama ukipenda kujiridhisha unaweza kupata taarifa ya kitaaalmu kuelezea changamoto ya kukumbatia kampuni za nje kama Uber kwenye soko dogo na linalotegemewa na watu wa chini kama wa nchi yetu ili ikusaidie wewe na wasaidizi wako kufanya maamuzi yenye ushahidi zaidi. Ni muhim sana katika kukabiliana na changamoto za kijamii kama ambazo ziko nyingi, ninyi viongozi mutumie pia wataalamu/wasomi/watafiti ili majawabu na suluhisho munalotoa au linalopatika liwe la kimkakati zaidi, endelevu, na linaloangalia mambo mengi katika mtambuka wa jambo husika.
Nakutakia kazi njema na bidii zaidi katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii yetu ya Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla wake.
Ni mimi mwananchi wako wa Dar esSM, Mathew Mndeme (Mwalimu MM)
Napatikana kupitia barua pepe: mmmwalimu(at)gmail.com